Zelensky amfuta kazi kamanda mkuu wa jeshi la Ukraine - Kunani?

Iliyochapishwa

Rais wa Ukraine amemfuta kazi kamanda mkuu wa jeshi la nchi hiyo Valerii Zaluzhnyi.

Hatua hii inafuatia uvumi kuhusu mpasuko kati ya rais na Jenerali Zaluzhnyi, ambaye ameongoza juhudi za vita vya Ukraine tangu mzozo huo uanze.

Jenerali Oleksandr Syrskyi alitangazwa kuchukua nafasi yake katika agizo la rais.

Ni mabadiliko makubwa zaidi kwa uongozi wa kijeshi wa Ukraine tangu uvamizi kamili wa Urusi mnamo Februari 2022.

Rais Volodymyr Zelensky alisema amri ya juu inapaswa "kufanyiwa marekebisho" na kwamba Jenerali Zaluzhnyi anaweza "kusalia kwenye timu".

"Kuanzia leo, timu mpya ya usimamizi itachukua uongozi wa Vikosi vya Wanajeshi vya Ukraine," Rais alisema siku ya Alhamisi.

Jenerali Zaluzhnyi ni maarufu na anayeaminiwa na wanajeshi wa Ukraine na umma, na amekuwa shujaa wa taifa.

Katika siku za hivi karibuni, makadirio ya kukubalika kwake yamekuwa ya juu kuliko yale ya Bw Zelensky.

Rais alisema yeye na Jenerali Zaluzhnyi walikuwa na "mazungumzo ya wazi" kuhusu mabadiliko yanayohitajika katika jeshi, na kwamba alimshukuru jenerali kwa kuilinda Ukraine dhidi ya Urusi.

Mkuu mpya wa jeshi, Jenerali Syrskyi, ana uzoefu wa vita vya kujihami na vya kushambulia, Bw Zelensky alisema.

Aliongoza kikosi cha ulinzi cha Kyiv katika mji mkuu wa Ukraine, mwanzoni mwa uvamizi kamili wa Urusi mnamo 2022.

Kisha alipanga shambulio la kujibu lililofanikiwa huko Kharkiv majira ya joto, na tangu wakati huo amekuwa akihudumu kama mkuu wa operesheni za kijeshi mashariki mwa Ukraine - moja ya maeneo yenye mashambulizi makuu mawili katika uvamizi wa Ukraine.

"Lazima tufanye mwaka huu kuwa muhimu," Bw Zelensky alisema.

"Muhimu kwa kufikia malengo ya Ukraine katika vita. Urusi haiwezi tu kukubali kuwepo kwa Ukraine iliyo huru - uwepo wa maisha huru katika nchi yetu."

Alisema kubadilisha uongozi wa jeshi "sio kuhusu majina ya ukoo" au siasa, lakini badala yake ni usimamizi wa vikosi vya kijeshi vya Ukraine na uzoefu wa makamanda walio vitani.

"Hatua za jeshi lazima ziwe za juu zaidi kiteknolojia. Kwa ujumla, uongozi lazima ubadilishwe," aliongeza.

Bw Zelensky alisema anatarajia mpango wa kina wa vikosi vya kijeshi mwaka huu, kwa kuzingatia ukweli wa vita na Urusi. Alisema kunahitajika kuwa na mbinu tofauti ya usimamizi, uhamasishaji na usajili wa makurutu.

Mykhailo Podolyak, ambaye ni mshauri wa mkuu wa ofisi ya rais, alisema hatua hiyo inahitajika ili kurekebisha mbinu zilizotumika katika makabiliano ya Ukraine mwaka jana.

Alirejea maoni ya Bw Zelensky kuhusu hitaji la kuzuia mkwamo kwenye mstari wa mbele na kutafuta suluhu za teknolojia ya juu.

Lakini kumekuwa na maoni tofauti hadi sasa kuhusu tangazo hilo, huku wabunge wa upinzani wakiwa wa kwanza kukosoa mtikisiko huo.

Meya wa Kyiv Vitali Klitschko alimshukuru Jenerali Zaluzhnyi kwa utumishi wake kwa Ukraine, akiongeza kuwa anatumai mamlaka itahalalisha mabadiliko hayo.

Oleksii Honcharenko, mbunge kutoka chama cha upinzani kinachoongozwa na Rais wa zamani Petro Poroshenko, alisema hatua hiyo ni "kosa kubwa" la rais. Na kuongeza kwamba itakuwa hatari kwa nchi: "Sote tutalazimika kugharamika kwa kosa hili."

Mbunge mwingine wa upinzani, Valentyn Nalyvaichenko kutoka chama cha Batkivschina, alisema uongozi wa kijeshi wakati wa vita "ni jambo ambalo lazima tulihifadhi, kuunga mkono, sio kukosoa, lakini kusaidia kwa kila njia".

Waziri wa Ulinzi wa Ukraine, Rustem Umerov, alimshukuru Jenerali Zaluzhnyi katika taarifa yake, akisema:

"Jenerali Valerii Zaluzhnyi alikuwa na moja ya kazi ngumu zaidi - kuongoza Vikosi vya Wanajeshi vya Ukraine wakati wa Vita Kuu na Urusi.

"Lakini vita havisalii vile vile. Vita vinabadilika na vinadai mabadiliko. Vita vya 2022, 2023 na 2024 ni ukweli mara tatu uliotofauti. 2024 italeta mabadiliko mapya, ambayo lazima tuwe tayari. Mbinu mpya, mikakati mipya inahitajika.

"Leo, uamuzi ulifanywa juu ya hitaji la kubadilisha uongozi wa Kikosi cha Wanajeshi wa Ukraine.

"Ninamshukuru kwa dhati Valerii Fedorovych kwa mafanikio na ushindi wake wote."

Imefasiriwa na Asha Juma