Yote unayohitaji kufahamu kuhusu makubaliano ya Iran na Marekani

Iliyochapishwa
Muda wa kusoma: Dakika 7

Rais wa Marekani Donald Trump na Naibu Waziri wa Mambo ya Nje wa Iran, Kazem Gharibabadi, wamethibitisha kuwa makubaliano ya kumaliza vita yamefikiwa.

Trump aliandika kwenye mtandao wake wa Truth Social kwamba, "Makubaliano na Jamhuri ya Kiislamu ya Iran yameafikiwa."

Alisema ameridhia kufunguliwa kwa Mlango wa Bahari wa Hormuz na kuondolewa mara moja kwa kile alichokiita zuio la majini la Marekani dhidi ya Iran.

"Mafuta yaanze kutiririka!" aliandika Trump, kabla ya kufafanua baadaye kuwa usafirishaji huo utaanza baada ya makubaliano kutiwa saini rasmi Juni 19.

Baada ya ujumbe huo, vyombo vya habari vya serikali ya Iran vilitangaza, vikimnukuu Waziri Mkuu wa Pakistan Shehbaz Sharif, kwamba Tehran na Washington zimefikia makubaliano.

Baadaye, Naibu Waziri wa Mambo ya Nje wa Iran Kazem Gharibabadi alithibitisha kupitia televisheni ya taifa kuwa makubaliano hayo yamekamilishwa na kwamba hafla rasmi ya kutiwa saini itafanyika nchini Uswizi tarehe 19 mwezi Juni.

"Itatangazwa jioni hii kwamba mapigano na operesheni za kijeshi katika nyanja mbalimbali, ikiwa ni pamoja na Lebanon, zitamalizika mara moja na kudumu," alisema.

Vile vile ameongeza kuwa vikwazo vya jeshi la majini la Marekani dhidi ya Iran vitaondolewa usiku wa kuamkia leo.

Kabla tu ya nchi hizo mbili kuthibitisha makubaliano hayo, Waziri Mkuu wa Pakistani Shahbaz Sharif, ambaye alikuwa akifanya kazi kama mpatanishi, alitoa taarifa kwamba makubaliano yamefikiwa kati ya Marekani na Iran.

"Kufuatia mazungumzo ya kina, tunafuraha kutangaza kwamba makubaliano ya amani yamefikiwa kati ya Marekani na Jamhuri ya Kiislamu ya Iran," Sharif aliandika.

"Pande zote mbili zimetangaza kukomesha mara moja na kudumu kwa operesheni za kijeshi katika nyanja zote, ikiwa ni pamoja na nchini Lebanon," alisema.

Aliongeza kuwa hafla rasmi ya kutia saini itafanyika Uswizi mnamo Juni 19.

Sharif pia aliwashukuru Qatar, Saudi Arabia na Turkey kwa kuunga mkono juhudi hizo.

Vipengele vya makubaliano vinavyoripotiwa

Shirika la habari la Mehr limeripoti kuwa rasimu ya makubaliano ina vipengele 14, ingawa bado havijathibitishwa rasmi na pande zote mbili.

Miongoni mwa vipengele hivyo ni:

• Kusitishwa kwa mapigano kwa kudumu katika maeneo yote, ikiwemo Lebanon.

• Kuondolewa kwa vikwazo dhidi ya mafuta na sekta ya nishati ya Iran.

• Kufunguliwa tena kwa Mlango wa Hormuz ndani ya siku 30.

• Ahadi ya Iran kutotengeneza silaha za nyuklia.

• Kutolewa kwa msaada wa ujenzi na uwekezaji wa zaidi ya dola bilioni 300 kwa Iran.

• Ahadi ya Marekani kutoweka vikwazo vipya wala kuongeza wanajeshi wake katika eneo hilo.

Mehr pia alisema kuwa "mazungumzo ya mwisho hayataanza hadi nusu ya fedha zilizozuiliwa za Iran zitolewe, vikwazo vya mafuta dhidi ya Iran visimamishwe, na kizuizi cha majini kiondolewe."

Ilielezwa kuwa makubaliano ya mwisho yatapitishwa na azimio la Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa.

Dunia yapokea makubaliano hayo kwa matumaini

Waziri wa Mambo ya Nje wa Uturuki Hakan Fidan alisema nchi yake inakaribisha makubaliano hayo na kutumaini mazungumzo yatakayofuata yatafanyika kwa njia ya kujenga.

"Tunatumai kuwa mazungumzo ya nyongeza pia yataendelea kwa njia ya kujenga," Fidan alisema, akisisitiza umuhimu wa nchi zote kufanya kazi kwa busara na wajibu wa kulinda amani na usalama wa kikanda.

Rais Recep Tayyip Erdoğan alisema ana matumaini hatua hiyo itachangia kuleta amani ya kudumu katika eneo hilo, huku akionya dhidi ya matamshi au vitendo vinavyoweza kuongeza mvutano kabla ya makubaliano kutiwa saini.

Viongozi wa Uingereza, Ufaransa, Ujerumani na Italia walisema hatua hiyo ni fursa ya kurejesha utulivu wa kikanda na kusaidia uchumi wa dunia.

Waziri Mkuu wa Uingereza Keir Starmer alieleza makubaliano hayo kuwa hatua muhimu kuelekea mwisho wa vita na kurejesha uthabiti katika eneo la Ghuba.

Waziri Mkuu na Waziri wa Mambo ya Nje wa Qatar Sheikh Mohammed bin Abdulrahman Al Thani alisema, "Tunatazamia mazungumzo ambayo pande zote zitafikia kwa ari chanya na yenye kujenga ambayo itasaidia kuimarisha na kujenga juu ya maendeleo haya."

Rais wa Ufaransa Emmanuel Macron alisema kuwa viongozi wa G7, wanaokutana wiki hii katika mji wa mapumziko wa Ufaransa wa Evian, watajadili kufunguliwa tena kwa Mlango-Bahari wa Hormuz kwa muda mrefu kama sehemu ya makubaliano ya Marekani na Iran.

Katika video aliyoitoa, Macron alisema, "Lengo letu litakuwa kuona matokeo ya makubaliano haya, kutoa msaada kwa Lebanon, kuhakikisha kufunguliwa tena kwa kudumu kwa Mlango-Bahari wa Hormuz, na bila shaka, kufikia makubaliano juu ya mipango ya nyuklia na makombora ya balestiki ya Iran."

Viongozi kutoka Uingereza, Kanada, Ujerumani, Italia, Japan na Marekani wanakusanyika kwa ajili ya mkutano wa kilele wa siku tatu kuanzia Jumatatu, Juni 15.

Je, Mlango-Bahari wa Hormuz unaweza kufunguliwa mara moja?

Mwandishi wa BBC wa masuala ya uchumi Jonathan Josephs anasema kuwa kufuatia makubaliano hayo, huenda ikachukua muda kwa usafiri wa baharini katika Mlango wa Hormuz kurudi katika viwango vya kabla ya vita.

Josephs alisema kuwa makampuni ya meli yangetaka kuona makubaliano hayo yakiendelea kutekelezwa, akiongeza, "Makampuni ya usafirishaji wa baharini yanatarajiwa kusubiri kuona ikiwa makubaliano hayo yatadumu kabla ya kurejesha shughuli zake kikamilifu.''

Ni nini kilifanyika katika masaa yaliyotangulia makubaliano?

Saa chache kabla ya tangazo hilo, mashambulizi mapya ya Israel katika vitongoji vya kusini mwa Beirut yalikuwa yamezua mashaka kuhusu mustakabali wa makubaliano hayo.

Hata hivyo, Trump alisema pande zote zilikuwa karibu sana kufikia amani na kuhimiza kusitishwa kwa mashambulizi yoyote mapya.

Wakati huo huo, Tehran ilisema kwamba mashambulizi ya hivi karibuni dhidi ya Beirut yamedhihirisha kwamba Washington haina nia ya kutimiza wajibu wake.

Trump alisema mashambulizi ya Israel "hayakupaswa kutokea."

Jeshi la Israel lilitangaza mapema Jumapili, Juni 14, kwamba lilishambulia kituo cha kamandi cha Hezbollah katika kitongoji cha Dahiye cha Beirut kufuatia shambulio la kombora la Hezbollah katika ardhi ya Israel.

Mpatanishi mkuu wa Iran, Mohammad Bagher Qalibaf, alisema kuwa mashambulizi ya hivi karibuni ya Israel yalionyesha kuwa Marekani imeshindwa kutekeleza ahadi zake na kukosa nia au uwezo wa kufanya hivyo.

Iran kwa muda mrefu imekuwa ikisisitiza kuwa Lebanon ijumuishwe katika makubaliano ya amani yanayojadiliwa na Washington.

Kalibaf alisema "haikuwa na maana" kuzungumza juu ya kuendelea "kwenye njia hii."

Trump alisema mashambulizi ya Israel "hayakupaswa kutokea," na kuongeza, "Hasa katika siku ambayo tuko karibu sana na makubaliano ya amani na Iran."

Katika ujumbe uliotumwa kwenye mtandao wa kijamii wa Truth Social, Trump alisema kuwa Israel ina "haki ya kujilinda," lakini shambulio ambalo ilijibu lilikuwa "dogo sana na lisilo na maana."

Marekani na Iran "ziko karibu sana na makubaliano ambayo yataleta amani katika eneo hilo, ikiwa ni pamoja na Lebanon, na pande zote zinahitaji kurudi nyuma," aliongeza.

Trump alisema kwamba hakupaswi kuwa na mashambulizi tena kutoka kwa Israeli au "upande mwingine wowote," akiongeza kwamba "unaweza kuwa mwanzo wa amani ya muda mrefu na nzuri," na kuwataka watu "kutoivuruga!"

Jumamosi, Juni 13, Trump pia alichapisha kwenye Truth Social, "Makubaliano hayo yamepangwa kutiwa saini kesho, na mara tu yatakapotiwa saini, Mlango-Bahari wa Hormuz utakuwa WAZI KWA KILA MTU."

Trump pia alisema atahakikisha kuwa Iran haitawahi kutengeneza silaha za nyuklia.

Akirejelea kwa uwazi akiba ya urani iliyorutubishwa ya Iran, Trump alisema: "Wakati mwafaka ukifika na hali ikitulia, tutaenda kuchukua mabaki ya nyenzo za nyuklia," akiongeza kuwa baadaye yataharibiwa.

Kwa miaka mingi, Iran imekuwa ikituhumiwa na mataifa ya Magharibi kwa kujaribu kutengeneza bomu la nyuklia. Hata hivyo, Tehran imekanusha madai hayo, ikisisitiza kuwa mpango wake wa nyuklia unalenga matumizi ya amani, ikiwemo uzalishaji wa umeme na shughuli za utafiti.

Trump pia alisema kuwa Washington ina "chaguo la mwisho" iwapo mambo hayatakwenda "kwa haraka, kwa urahisi na kwa utulivu," akiongeza kuwa anatumaini hatua hiyo haitalazimika kutumika tena.

Mapema Jumamosi, Waziri Mkuu wa Pakistan Shehbaz Sharif alisema kuwa pande husika ziko karibu zaidi kuliko wakati mwingine wowote kufikia makubaliano ya amani.

Katika ujumbe aliouchapisha kwenye mtandao wa X, Sharif alisema makubaliano hayo yanatarajiwa kukamilishwa ndani ya saa 24 zijazo, huku Pakistan ikiendelea na maandalizi ya kutiwa saini kwa njia ya kielektroniki pamoja na mazungumzo ya kiufundi yatakayofanyika wiki ijayo.

Makubaliano hayo yamekuwa yakitarajiwa tangu Ijumaa

Ijumaa, Waziri wa Mambo ya Nje wa Iran, Seyed Abbas Araghchi, alisema kuwa makubaliano kati ya Iran na Marekani yalikuwa karibu kufikiwa.

Araghchi alisema makubaliano hayo yanakusudia kumaliza mzozo kati ya Israel na Hezbollah nchini Lebanon, huku mazungumzo kuhusu mpango wa nyuklia wa Iran yakitarajiwa kuanza baadaye.

Maafisa wa Marekani pia walithibitisha baadhi ya vipengele vya makubaliano hayo na kusema kuwa manufaa ya kiuchumi yatakayotolewa kwa Iran yatategemea utekelezaji wa majukumu yake kwa mujibu wa makubaliano.

Ingawa katika miezi ya karibuni matoleo mbalimbali ya makubaliano hayo yalielezwa kuwa yako karibu kukamilika, hayakuwahi kufikia hatua ya mwisho ya kuidhinishwa.

Vita hivyo vilianza baada ya mashambulizi ya Marekani na Israel dhidi ya Iran mnamo Februari 28.

Baadaye Iran ilijibu kwa mashambulizi dhidi ya Israel na washirika wa Marekani katika eneo la Ghuba, hali iliyosababisha kufungwa kwa Mlango wa Hormuz, njia muhimu kwa usafirishaji wa mafuta na gesi asilia iliyoyeyushwa duniani.

Licha ya pande hizo kukubaliana kusitisha mapigano mwezi Aprili, Marekani na Iran zimeendelea kushambuliana mara kwa mara.

Ripoti za awali zilidokeza kuwa Marekani huenda isijumuishe mzozo kati ya Hezbollah inayoungwa mkono na Iran na Israel katika makubaliano hayo. Hata hivyo, Iran ilisisitiza kuwa kusitishwa kwa mashambulizi dhidi ya Lebanon ni sehemu muhimu ya makubaliano.

Israel si mshiriki wa makubaliano ya Iran na Marekani, na imeendelea kusisitiza kuwa itaendeleza mashambulizi yake dhidi ya Hezbollah kwa kujibu mashambulizi yanayolenga maeneo ya kaskazini mwa Israel.

Imetafsiriwa na Mariam Mjahid