Rais wa Marekani, Donald Trump, amesema kuwa makubaliano ya kumaliza mapigano kati ya Marekani na Iran yanatarajiwa kutiwa saini Jumapili, baada ya Tehran kuonyesha mashaka kuhusu muda wa kufikiwa kwa makubaliano hayo.
Katika ujumbe aliouchapisha kwenye mitandao ya kijamii, Trump alisema kuwa Mlango wa Bahari wa Hormuz, njia muhimu ya usafirishaji wa bidhaa kwa meli, utakuwa "wazi kwa wote" mara tu makubaliano hayo yatakapokubaliwa.
Pakistan, ambayo imekuwa mpatanishi muhimu katika mazungumzo hayo, pia ilisema makubaliano hayo yanatarajiwa kukamilishwa ndani ya saa 24 zijazo na kwamba maandalizi ya kutiwa saini kwa njia ya kielektroniki yanaendelea.
Kabla ya matamshi ya Trump, msemaji wa Wizara ya Mambo ya Nje ya Iran, Esmaeil Baghaei, alionyesha tahadhari kuhusu ratiba hiyo akisema:
"Tutalazimika kusubiri na kuona tarehe kamili ya kutiwa saini kwa hati ya maelewano, ingawa haitakuwa kesho."
Katika ujumbe wake kwenye mtandao wa Truth Social, Trump aliandika:
"Makubaliano hayo yamepangwa kutiwa saini kesho(akirejelea leo), na mara tu yatakapotiwa saini, Mlango wa Hormuz utakuwa WAZI KWA WOTE."
Akirejelea kile kinachoaminika kuwa akiba ya urani iliyoboreshwa ya Iran, Trump alisema kwamba "wakati mwafaka, hali ikiwa imetulia kabisa, tutaingia na kuchukua mabaki ya nyuklia," akiongeza kuwa baadaye yataharibiwa.
Kwa miongo kadhaa, Iran imekuwa ikituhumiwa na mataifa ya Magharibi kwa kujaribu kutengeneza silaha za nyuklia. Tehran imekuwa ikikanusha madai hayo na kusisitiza kuwa mpango wake wa nyuklia ni wa matumizi ya amani, ikiwemo uzalishaji wa umeme na shughuli za utafiti.
Trump pia alionya kwamba iwapo mambo hayataenda "haraka, kwa urahisi na kwa utulivu", Washington ina "njia mbadala ya mwisho kabisa", ambayo alieleza kuwa anatumaini haitalazimika kutumiwa tena.
Mapema Jumamosi, Waziri Mkuu wa Pakistan, Shehbaz Sharif, alisema kuwa "tuko karibu zaidi kuliko wakati wowote kufikia makubaliano ya amani."
"Tukiwa na matarajio ya kukamilisha makubaliano hayo ndani ya saa 24 zijazo, Pakistan inajiandaa kwa kutiwa saini kwa njia ya kielektroniki mara tu yatakapokamilika, kabla ya mazungumzo ya kiufundi kuanza wiki ijayo," Sharif aliandika kwenye mtandao wa X.
Ijumaa, Waziri wa Mambo ya Nje wa Iran, Seyed Abbas Araghchi, alisema kuwa makubaliano kati ya Iran na Marekani yako karibu kufikiwa.
Alisema makubaliano hayo yanatarajiwa kujumuisha kusitishwa kwa mzozo kati ya Israel na kundi la Hezbollah nchini Lebanon.
Araghchi aliiambia televisheni ya taifa ya Iran kuwa makubaliano hayo pia yanajumuisha kufunguliwa tena kwa Mlango wa Hormuz pamoja na kuondolewa kwa vizuizi vya Marekani dhidi ya bandari za Iran.
Hata hivyo, alisema mazungumzo kuhusu mpango wa nyuklia wa Iran yataanza katika hatua ya baadaye.
Maafisa wa Marekani wamethibitisha baadhi ya vipengele vya makubaliano hayo, wakisema kuwa manufaa ya kiuchumi kwa Iran yatategemea uwezo wa Tehran kutekeleza wajibu wake chini ya makubaliano hayo.
Ripoti za awali kutoka Marekani zilidokeza kuwa Lebanon huenda isiwe sehemu ya makubaliano hayo, huku Iran ikiripotiwa kusisitiza suala hilo lijumuishwe katika mazungumzo.