Hii ni tovuti ya maandishi pekee ambayo inatumia data kidogo. Tazama toleo kuu la tovuti likijumuisha picha na video zote.

Bofya kuelekea tovuti kuu

Pata maelezo zaidi kuhusu toleo hili la linalotumia kiasi kidogo cha data

Moja kwa moja, Marekani na Iran zafikia makubaliano ya kumaliza vita

Pakistan ambaye amekuwa msuluhishi wa mgogoro baina ya nchi hizi imesema mkataba rasmi utasainiwa Ijumaa kumaliza vita vilivyodumu kwa karibu miezi minne.

Muhtasari

Marekani na Iran zafikia makubaliano ya kumaliza vita

Moja kwa moja

Na Asha Juma

  1. Rais Zelensky ajadili mazungumzo ya amani na Trump

    Rais wa Ukraine Volodymyr Zelensky amesema siku ya Jumapili kwamba amezungumza na Rais wa Marekani Donald Trump na kujadili juhudi za kufikia mwisho wa vita vya zaidi ya miaka minne , kabla ya mkutano wa G7 nchini Ufaransa wiki hii.

    Zelensky, akiandika kwenye Telegram, alisema alikuwa amemtakia Trump siku njema ya kuzaliwa ya 80 na akamshukuru kwa msaada uliotolewa na Washington katika kipindi chote cha mzozo.

    "Nilimtakia Rais Trump mafanikio mema, kwanza kabisa katika juhudi zake za kukomesha vita vya Urusi dhidi ya Ukraine," Zelensky alisema.

    Akizungumza baadaye katika hotuba yake kwa njia ya video iliyotolewa usiku, Zelensky alisema yeye na Trump wamekubaliana kukutana wakati wa mikutano huko Evian-les-Bains.

    Alisema ni muhimu kuhakikisha Marekani inaunga mkono juhudi za Ukraine za kupata amani, pamoja na washirika wa Ukraine wa Ulaya.

    "Hili ndilo jambo muhimu zaidi tunalotaka sote, na ni muhimu kwamba jamii ya Marekani iunge mkono kikamilifu hamu yetu ya Waukraine, hamu ya kupata amani," alisema.

    Mazungumzo yanayosimamiwa na Marekani yanayolenga kukomesha vita yamekwama huku Washington ikiendelea kutoa kipaumbele kwa mzozo nchini Iran.

    Hata hivyo, Zelensky amesema katika wiki za hivi karibuni mabadiliko ya kasi katika vitani kwa upande wa Ukraine yamefungua fursa ya kufikia makubaliano ya amani.

    Soma zaidi:

  2. Wapiga mbizi 11 na rubani wafariki katika ajali ya ndege Marekani

    Wapiga mbizi kumi na mmoja na rubani mmoja wamefariki katika ajali ya ndege jimbo la Missouri nchini Marekani, maafisa wamesema.

    Ndege hiyo, ambayo ilikodishwa na kampuni ya wapiga mbizi, ilipaa karibu 11:20 saa za eneo siku ya Jumapili, kulingana na msemaji wa Usimamizi wa Dharura wa Kaunti ya Bates.

    Baada ya kushindwa kupata kasi ya mwinuko, ilipinda upande wa kushoto na kuanguka umbali wa yadi 200 kutoka uwanja wa ndege wa Butler Memorial, msemaji huyo aliiambia BBC. Watu wote 12 waliokuwemo ndani ya ndege hiyo walikufa, alisema.

    "Tunachukulia hilo ... kama majeruhi ya wengi," Mkuu wa Polisi Kaunti ya Bates Chad Anderson alisema wakati wa mkutano wa wanahabari mchana.

    Aliongeza kuwa ndege hiyo haikuwa ya kibiashara, badala yake ni "ndege ya ndani ambayo ilipaa kutoka uwanja wetu wa ndani."

    Utawala wa Usafiri wa Anga (FAA) ulisema ndege hiyo ilikuwa ya Pasifiki ya Aerospace P750 na ilianguka wakati ikipaa kwenye uwanja huo.

    "Huduma za usafiri wa anga hazikuwa zinatolewa wakati huo," FAA ilisema. Msemaji alieleza kuwa ndege hiyo haikuhitajika kuwa katika mawasiliano kutokana na aina ya anga iliyokuwa ikipaa.

    Vyombo vya habari vya eneo hilo viliripoti kwamba watoa huduma wa kwanza walikagua eneo hilo ili kuona kama kuna wapiga mbizi waliofanikiwa kuruka kutoka kwenye ndege kabla ya ajali hiyo.

    Pia unaweza kusoma:

  3. Ivory coast ushindi wa kwanza Afrika, Ujerumani yaisambaratisha Curaçao 7-1.

    Ivory Coast imeanza vyema kampeni yao ya Kombe la Dunia 2026 kutoka kundi E kwa ushindi wa bao 1–0 dhidi ya Ecuador, ushindi wa kwanza kwa timu za Afrika katika mashindano ya mwaka huu.

    Bao pekee la mchezo lilifungwa dakika ya 90 na nyota wa Manchester United, Amad Diallo, akiipa Ivory Coast ushindi muhimu katika mechi yao ya kwanza ya kundi.

    Ecuador walikuwa na nafasi kadhaa nzuri za kufunga, ikiwa ni pamoja mara mbili mipira yao ikigonga mlingoti katika kipindi cha kwanza, lakini walishindwa kutumia nafasi hizo.

    Wakati huo huo, Ujerumani waliibuka na ushindi mnono wa 7–1 dhidi ya Curaçao katika mechi yao ya ufunguzi, katika mchezo mwingine wa kundi E.

    Curaçao, ambao wanacheza Kombe la Dunia kwa mara ya kwanza, walipata bao la kushtukiza kupitia Livano Comenencia, ambaye shuti lake lilimgonga kipa Manuel Neuer na kuingia wavuni.

    Hata hivyo, Ujerumani walijibu haraka na kuendeleza ubabe wao kupitia mabao ya Nico Schlotterbeck, Kai Havertz (2), Jamal Musiala, Nathaniel Brown na Deniz Undav

    Japan na Uholanzi zenyewe zimeenda sare ya 2-2 katika mchezo wa kundi F.

  4. Bei za mafuta zashuka duniani baada ya makubaliano ya Marekani na Iran

    Bei za mafuta zilishuka katika masoko ya Asia baada ya Pakistan, ambayo imekuwa ikisaidia mazungumzo ya kumaliza vita kati ya Marekani na Iran, kutangaza kuwa makubaliano yamefikiwa.

    Rais wa Marekani Donald Trump alisema makubaliano hayo yatawezesha kufunguliwa tena kwa Mlango wa Bahari wa Hormuz, njia muhimu ya usafirishaji wa mafuta duniani.

    Mafuta ya Brent, ambayo ni kipimo kikuu cha bei za mafuta duniani, yalishuka kwa asilimia 3.8 na kufikia dola 84.02 kwa pipa. Mafuta yanayouzwa Marekani yalishuka kwa asilimia 4.1 na kufikia dola 81.40 kwa pipa.

    Waziri Mkuu wa Pakistan, Shehbaz Sharif, alisema hafla rasmi ya kusaini makubaliano hayo itafanyika Ijumaa, tarehe 19 Juni, nchini Uswisi.

    Baadaye, Trump aliandika kwenye mitandao ya kijamii kuwa "mafuta yataanza kutiririka."

    Mlango wa Hormuz ulikuwa umefungwa kwa kiasi kikubwa tangu muda mfupi baada ya Marekani na Israel kuanzisha mashambulizi ya anga dhidi ya Iran tarehe 28 Februari.

    Iran ilikuwa imetishia kushambulia meli zinazotumia njia hiyo muhimu ya bahari, ambayo kwa kawaida hupitisha karibu asilimia 20 ya mafuta na gesi asilia iliyoyeyushwa (LNG) duniani.

    Masoko ya nishati duniani yamekuwa yakibadilika sana katika miezi ya hivi karibuni, huku bei za mafuta zikipanda au kushuka kwa kasi kutokana na matukio mbalimbali yanayohusiana na vita vya Marekani na Israel dhidi ya Iran.

    Mafuta ya Brent, ambayo yalikuwa yanauzwa kwa takribani dola 70 kwa pipa kabla ya vita kuanza, yalipanda hadi karibu dola 120 kwa pipa wakati wa vita.

  5. Marekani na Iran zafikia makubaliano ya kumaliza vita

    Marekani na Iran zimetangaza kufikia makubaliano ya awali ya kumaliza vita kati yao, kumaliza miezi ya mvutano uliotikisa Mashariki ya Kati.

    Maafisa kutoka pande zote mbili walisema Jumapili kuwa wamekubaliana juu ya mfumo wa makubaliano ambao pia unajumuisha pia kufunguliwa tena kwa Mlango-Bahari wa Hormuz, njia muhimu inayopitisha sehemu kubwa ya mafuta ya dunia.

    Rais wa Marekani, Donald Trump, alitangaza mafanikio hayo kupitia mtandao wake wa Truth Social.

    "Makubaliano na Jamhuri ya Kiislamu ya Iran sasa yamekamilika," Trump aliandika.

    Tangazo hilo lilikuja muda mfupi baada ya Waziri Mkuu wa Pakistan, Shehbaz Sharif, ambaye nchi yake imekuwa mpatanishi katika mazungumzo hayo, kusema makubaliano yalifikiwa mapema Jumatatu kwa saa za eneo hilo.

    Maelezo kamili ya makubaliano hayo hayajatangazwa mara moja. Sharif alisema kupitia mtandao wa X kwamba makubaliano hayo yanataka:

    "Kukomeshwa mara moja na kwa kudumu kwa operesheni zote za kijeshi katika maeneo yote ya mapigano, ikiwemo Lebanon."

    Baraza Kuu la Usalama wa Taifa la Iran nalo lilithibitisha kuwa shughuli zote za kijeshi katika maeneo yote ya mzozo, ikiwemo Lebanon, zitasitishwa kuanzia Jumatatu usiku.

    Trump alisema kuwa Mlango wa Bahari wa Strait of Hormuz, ambao ni njia muhimu ya usafirishaji wa mafuta na gesi duniani na ambao Iran imekuwa ikidhibiti kwa miezi kadhaa, utafunguliwa tena Ijumaa.

    Trump aliandika:

    "Meli za dunia, washeni injini zenu. Mafuta yaanze kutiririka!"

  6. Hujambo na karibu katika habari zetu za moja kwa moja