Vita vya Ukraine: Warusi wanaopigania pasipoti ya Ukraine

Na James Waterhouse
Mwandishi wa BBC Ukraine
Galina alizaliwa huko Ukraine. Anazungumza Kiukreni, mume wake anahudumu katika jeshi la Ukraine, na anaishi katika kijiji kilicho kusini mwa jiji la kati la Ukraine la Vinnytsia.
Lakini Galina ni Mrusi kisheria. Alihamia huko akiwa mtoto ambapo kisha akawa raia.
Inamaanisha kuwa yeye - kama maelfu ya Warusi wengine nchini Ukraine - sasa yuko katika hali mbaya ya kisheria.
"Unapoonyesha hati zako, watu wanadhani wewe ni kitu cha kushangaza," ananiambia jikoni kwake, ambapo hutumia wakati wake kushona fulana za askari wa Ukraine waliojeruhiwa.
Huduma ya uhamiaji ya serikali ya Ukraine inasisitiza kwamba wageni wote nchini Ukraine wana haki sawa kama kila mmoja, na hakuna taifa moja linalobaguliwa.
Lakini wengine wanadai kuwa hii sivyo. Wanasheria wanaofanya kazi na Warusi nchini Ukraine kwa mfano waliambia BBC kwamba wateja wao wanakabiliwa na hatari ya kufungiwa akaunti zao.
Baada ya Urusi kuanzisha uvamizi wake dhidi ya Ukraine,Benki ya Kitaifa ya Ukraine ilizuia huduma za kifedha kwa raia wote wa Urusi na Belarusi, ingawa inasema wale walio na kibali cha kuishi hawaathiriwi.
Galina hakubaliani na kauli hiyo. Anasema kwamba kwa sababu ya pasipoti yake, hawezi kupata kazi, na anahofia akaunti yake ya benki inaweza kuzuiwa.
Ana ujauzito wa miezi saba lakini kwa sababu si raia wa Ukraine kisheria, hawezi kupata huduma za afya za serikali bila malipo.
Galina pia ana wasiwasi kuwa hataweza kusajili kuzaliwa kwa mtoto wake: baada ya kuolewa na mume wake wa Ukraine Maksym kanisani, anasema kwamba maafisa walikataa kutambua ndoa yao kwa sababu ya hali yake isiyoelezeka.
"Walisema, 'Rudi ukiwa na pasipoti'," anaelezea Galina. "Hawawezi kunielewa mimi ni nani." Chini ya sheria ya Ukraine ni marufuku kuwa na uraia wa nchi mbili , ingawa wengine wanafanya hivyo.

Chanzo cha picha, KWA HISANI YA GALINA
Pata habari za kina kutoka BBC News Swahili, moja kwa moja kupitia WhatsApp.
Bonyeza hapa kujiunga
Mwisho wa Whatsapp
Alianza kutuma maombi ya kuwa raia wa Ukraine lakini hakuweza kukamilisha mchakato huo kwa sababu ya uvamizi wa Urusi. Sasa pasipoti ya muda ya Galina ya Ukraine imeisha muda wake, anasema anahisi kama "mateka wa Urusi".
"Kubadilisha hati za kusafiria ilikuwa vigumu hata kabla ya vita - sasa haiwezekani," anasema.
Juu ya Povitroflotskyi Avenue katikati ya Kyiv anakaa anakaa orofa ya tatu ya jengo la rangi nyeupe na bustani inayokuwa. Imezungukwa na uzio mrefu na wenye miba.
Wamekuwa hapo tangu 23 Februari mwaka jana wakati wafanyakazi katika Ubalozi wa Urusi walihamishwa kwa "sababu za usalama". Siku moja baadaye Moscow ilianzisha uvamizi wake kamili, na kile kilichosalia cha uhusiano wa kidiplomasia kati ya Kyiv na Moscow kilisambaratika.
Ina maana maelfu ya watu nchini Ukraine, kama Galina, wanaishi kwa kutokuwa na uhakika.
Hivi sasa kuna zaidi ya Warusi 150,000 wenye vibali vya ukaaji wa kudumu nchini Ukraine. Takriban 17,000 wana za muda.
Ili waweze kuomba kwa mafanikio pasipoti ya Kiukreni au uraia, wanahitaji kwanza kuukana uraia wao wa Urusi. Moscow ilifanya mchakato huo kuwa mgumu: kufanya hivyo, wangelazimika kusalimisha karatasi zao katika ubalozi mdogo wa Urusi nje ya nchi, au Urusi yenyewe.
Hakuna hakikisho kwamba Galina hangekamatwa katika mchakato huo, au kuishia kukwama nje ya Ukraine.

Chanzo cha picha, Getty Images
Watoto wa Galina wanaporudi kutoka shuleni, unaweza kuona uchungu machoni mwake. Wasiwasi anaojaribu kuwaficha watoto wake.
Lakini anakataa kuiwajibisha Ukraine, au kudai ubaguzi.
Anaweka lawama zake zote kwa Urusi kwa hali yake, pamoja na wanafamilia wake wa Urusi ambao wamechagua kuunga mkono nchi yao katika kile kinachoitwa "operesheni maalum ya kijeshi".
"Ninawezaje kumuunga mkono jambazi, mbakaji na muuaji anayevunja nyumba yangu?" anasema.
Baada ya Galina kumaliza kupiga simu ya video na mumewe Maksym, ninamuuliza nini kitatokea kwa familia yake ikiwa atauawa kwenye mstari wa mbele vita
Anaweka mkono wake mdomoni. Wazo ambalo alijaribu kuweka nyuma ya akili yake, ghafla analiweka mbele ya fikra zake.
"Inatisha sana," anasema. "Hata akijeruhiwa, siwezi kumtembelea hospitali, kwa sababu hatujaoana kirasmi'
"Kwa ulimwengu wote sisi ni wageni."
'Nilichagua Ukraine'
Wakati Anastasia Leonova, Mrusi, alipohama kutoka Moscow hadi Kyiv mwaka wa 2015, marafiki zake walimuonya "hataruhusiwa kuzungumza Kirusi" na kwamba "kulikuwa na Wanazi tu huko".
Ilikuwa simulizi ya propaganda ya Urusi ambayo ilimkasirisha, kwa kuwa alikuwa na wajomba na binamu wanaoishi Ukraine

Kuhamishwa kwa Anastasia kulifuatia ukosoaji wake mtandaoni wa kunyakuliwa kwa Crimea na urusi mwaka 2014 na kuungwa mkono na wanamgambo wanaotaka kujitenga, jambo ambalo lilipelekea kupoteza kazi yake nchini Urusi na pia kupokea vitisho vya kuuawa.
Mnamo tarehe 24 Februari mwaka jana, wakati wanajeshi wa Urusi wakielekea Kyiv, Anastasia anasema alikuwa na wazo moja tu akilini mwake - kubaki na kupigana.
"Damu yangu ni sehemu ya Ukraine" anasema. "Nilizaliwa kama sehemu ya Ukraine."
"Nilichagua Ukraine kama nchi yangu; sikuweza kusaliti chaguo hili".
Alijitolea kuwa daktari wa mapigano na vikosi vya Ukraine, kwani walilinda mji mkuu dhidi ya wanajeshi kutoka nchi yake.
Ninauliza ikiwa anatendewa tofauti kwa kuwa Mrusi.
"Hakuna mtu aliyekuwa akiuliza pasipoti yangu nilipokuwa nikifanya kazi," anasema huku akitabasamu.
"Kwa hakika, wenzangu wanajua."

Anakubali kwamba mwanzoni ilikuwa vigumu sana kuwatibu Warusi waliojeruhiwa kwa sababu ya kile walichokuwa wakifanya.
Lakini baadaye, anasema, aligundua kuwa kuwahudumia ilikuwa "njia ya kuwarudisha watu wetu, Waukraine ambao walitekwa na Warusi".
"Tangu nilipokuja hapa kutoka siku yangu ya kwanza, nimekuwa na ndoto ya kuwa na pasipoti ya Kiukreni," anasema.
"Hili ndilo ninalopigania. Sio tu kwa uhuru, lakini kwa pasipoti yangu."
Ni mia chache tu ya Warusi wamepewa uraia wa Ukraine katika muda wa miezi 18 tangu uvamizi huo kamili, kutoka 1,700 mwaka uliopita.
Tofauti na Galina, Anastasia anahisi yuko karibu na ndoto yake. Huenda kutumikia jeshi kumesaidia kazi yake.
Huduma ya kijeshi, ndoa kwa raia wa Ukraine na muda mrefu wa kuishi Ukraine huzingatiwa katika maombi ya uraia. Kama mamlaka zinavyosema, kuwa na haki ya kisheria ya kukaa Ukraine kunahitaji zaidi ya kubadili utambulisho tu.
Vita hivi vimeweka maelfu ya Warusi kama Galina na Anastasia katika hali ngumu ndani ya Ukraine.
Mkuu wa Huduma ya Uhamiaji ya nchi ya Ukraine, Natalia Naumenko, alituambia hakuna taifa linalobaguliwa linapokuja suala la kupata uraia.
Sheria mpya inatayarishwa ambayo itarahisisha maombi ya uraia na ukaazi kwa wale wanaopigania Ukraine.
Lakini Bi Naumenko anasema kwamba kutokana na uvamizi huo kamili, mchakato hakika hautafanywa rahisi kwa Warusi.
"Tayari tumerahisisha kwa wale wanaopigania Ukraine," anasema.
"Kwa nini Ukraine inapaswa kurahisisha kwa Warusi wote kwa ujumla?"
Ripoti ya ziada ya Insaf Abbas, Hanna Chornous, Anastasia Levchenko na Hanna Tsyba.
Imetafsiriwa na kuhaririwa na Yusuf Jumah












