Wakati Raila Odinga akitokea katika familia maarufu ya kisiasa nchini Kenya, kofia ya urais imekuwa ikimponyoka katika kipindi chote cha miongo kadhaa ya maisha yake ya siasa - kama ilivyomtokea baba yake, ambaye aliwahi kuwa makamu wa rais baada ya Kenya kupata uhuru kutoka kwa Waingereza.
Akiwa na umri wa miaka 77, Bw Odinga atafanya jaribio lake la tano la kuwania urais katika uchaguzi wa Agosti 9, mwaka huu akiwa amewahi kuteuliwa kuwa Waziri Mkuu mwaka 2008 moja ya nafasi za juu za utawala Kenya.
Bwana Odinga ana wafuasi wengi, na mashabiki wake wanaomfuatilia kwa karibu wamempa jina la utani "Baba" , "Agwambo" na "Tinga" - lililotolewa kutoka kwa nembo ya chama chake katika uchaguzi wa 1997.
Mtindo wake wa wa kucheza taratibu nyimbo za reggae wakati wa mikutano yake imepewa jina la "Staili au mtindo wa kucheza wa Raila".
Mfuasi wa klabu ya soka ya Arsenal ya Uingereza, Bwana Odinga anakuja na koti jipya la kisiasa katika kila uchaguzi. Anashiriki uchaguzi wa mwaka huu chini ya bendera ya Azimio la Umoja, huku akijaribu kuwateka wafuasi wa Rais anayeondoka madarakani, Uhuru Kenyatta.
Wawili hao - wanaowakilisha familia kubwa mbili za kisiasa nchini Kenya - walikuwa wapinzani wakubwa katika uchaguzi wa 2017, lakini waliungana pamoja mwaka uliofuata katika hafla iliyotangazwa sana na iliyopewa jina la 'The Handshake'.
Chanzo cha picha, Getty Images
Maelezo ya picha, Bwana Odinga and Rais Kenyatta wakishikana mikono kumaliza uhasama wa kisiasa wa muda mrefu
Bwana Odinga sasa anaahidi kuendeleza hoja ya maendeleo ya Bwana Kenyatta na kuboresha maisha ya Wakenya walio hatarini kwa kuwapa posho ya shilingi 6,000 za Kenya sawa na dola 50 kila mwezi kutoka kwa hazina mpya ya hifadhi ya jamii, iwapo atachaguliwa kuwa rais.
Pesa za mfuko huo, anasema, zitatokana na alichokiita kukabiliana na ufisadi ulioenea nchini humo.
Bwana Odinga pia ameahidi kutoa huduma za afya kwa gharama nafuu kupitia mpango aliouita "Baba Care", akijitangaza kama baba katika taifa hilo lenye watu zaidi ya milioni 56.
Mgombea mwenza mwanamke
Haijulikani ikiwa hili litakuwa jaribio la mwisho la mzee huyo mwenye umri wa miaka 77 katika kuwania urais.
Hapo awali alielezea azma yake ya urais 2017 kama "risasi" yake ya mwisho, kwa maana ya jaribio lake la mwisho. Lakini alieleza hatua yake ya kubadilisha maamuzi hayo katika mahojiano na Sophie Ikenye wa BBC Focus on Africa TV mnamo Machi 2022, kwa kueleza kuwa Wakenya "walimtaka agombee tena urais kwa sababu ya imani kubwa" waliyokuwa nayo kwake.
Nani yuko kwenye kinyang'anyiro cha kuiongoza Kenya ?
Fahamu zaidi kuwahusu wagombea urais wa Kenya
Chagua mgombea ili kutazama wasifu wake
Raila Amollo Odinga
Muungano wa Azimio la Umoja
Mgombea huyo mwenye umri wa miaka 77 ni mhandisi aliyesomea Chuo Kikuu cha Ufundi cha Magdeburg (sasa kinajulikana kama Chuo Kikuu cha Otto-von-Guericke Magdeburg) nchini Ujerumani.
Anawania kiti cha urais kwa tikiti ya Azimio la Umoja One Kenya Coalition Party.
Hili litakuwa jaribio lake la tano baada ya kugombea katika: 1997, 2007, 2013 na 2017.
Bw Odinga alikuwa mmoja wa wapiganiaji wa demokrasia ya vyama vingi nchini Kenya. Alikamatwa, akafungwa na wakati fulani akaenda uhamishoni kwa sababu ya kupigania haki hiyo
Aliwahi kuwa Waziri Mkuu, kuanzia 2008-2013.
Odinga alihusika kufanikisha miradi mikubwa iliyotekelezwa na serikali ya Kibaki, kama vile miradi ya umeme vijijini na barabara.
Kuafikia ukuaji wa uchumi wa tarakimu mbili kupitia uwekezaji katika biashara ndogo ndogo na sekta ya viwanda.
Utoaji wa huduma bora za afya kwa wote.
Utoaji wa vifaa vya michezo na burudani kwa ukuaji wa kimwili, kiakili, kijamii, kimaadili na maendeleo ya watu.
Kufuatia jaribio la mapinduzi ya Agosti 1, 1982, Raila Odinga alikamatwa na kukabiliwa na mashtaka kadhaa, yakiwemo ya uhaini ambayo alizuiliwa bila kufunguliwa mashtaka. Tume ya Ukweli ya Haki na Maridhiano iliambiwa mwaka 2011 kwamba Odinga alikuwa na mawasiliano na mpangaji mkuu wa mapinduzi hayo. Odinga amekana kuhusika kila mara. - Makavazi ya Kitaifa ya Kenya.
William Samoei Ruto
Muungano wa Kenya Kwanza
Mgombea huyu mwenye umri wa miaka 55 ana Shahada ya Uzamifu/PhD katika Ikolojia ya Mimea na BSc katika Botany na Zoology kutoka Chuo Kikuu cha Nairobi.
Anawania kiti cha urais kwa tikiti ya chama cha United Democratic Alliance ( chenye mafungamano na Kenya Kwanza).
Aliongoza Vuguvugu la vijana la Youth for Kanu '92 (YK'(92).
Wizara yake iliorodheshwa kama inayofanya bora zaidi serikalini alipokuwa Waziri wa Kilimo.
Alihudumu kama Naibu Rais wa kwanza wa Kenya chini ya katiba mpya ya 2010.
Alihudumu kama mbunge wa eneo bunge la Eldoret Kaskazini kuanzia 1997-2007.
Kutenga $424 milioni kila mwaka kwa biashara ndogo ndogo za kati.
Kuanzisha mfuko wa elimu wa kitaifa ili kukidhi gharama zisizo za masomo.
Tekeleza kikamilifu sheria ya usawa wa kijinsia ya thuluthi mbili katika uteuzi wa kisiasa na kutenga nusu ya baraza lake la mawaziri kwa wanawake.
Mnamo 2008, Mahakama Kuu ya Kenya iliamuru Naibu Rais William Ruto kusalimisha shamba la ekari 100 na kulipa $ 62,500 kwa Adrian Muteshi, mkulima ambaye alimshtaki kwa kuchukua mali hiyo baada ya uchaguzi wa 2007. - Kenya Law
Mnamo 2011, Bw Ruto alikabiliwa na kesi kwa makosa matatu dhidi ya binadamu: Mauaji, uhamisho wa watu kwa lazima na mateso ya watu katika Mahakama ya Kimataifa ya Uhalifu. Miaka mitano baadaye mahakama ilisitisha kesi hiyo kwa msingi kwamba - ushahidi wa upande wa mashtaka ulikuwa dhaifu. -ICC
George Wajackoyah
Chama cha Roots
Profesa huyo mwenye umri wa miaka 61 ana shahada ya uzamili katika sheria kuhusu maendeleo kutoka Chuo Kikuu cha Warwick na shahada ya uzamili , sheria (sheria za Marekani kutoka Chuo Kikuu cha Baltimore.
Bw Wajackoyah anawania kiti cha urais kwa tiketi ya Chama cha Roots Party.
Alihudumu kama Inspekta katika idara ya usalama ya Special branch wakati wa utawala wa marehemu Rais Daniel Moi kabla ya kulazimika kutorokea ng'ambo ili kuepuka kufunguliwa mashtaka na mamlaka.
Yeye ni mshirika katika kampuni ya mawakili aliyoianzisha mwaka wa 2018.
Alifunnza somo la sheria na uchumi katika vyuo vikuu vya Marekani, Uingereza na Kenya.
Kuhalalisha matumizi ya kiviwanda ya bangi
Badilisha siku za kazi hadi Jumatatu hadi Alhamisi.
Huduma ya afya ya bure na msaada kwa wazee, walio hatarini na wajawazito
David Mwaure Waihiga
Chama cha Agano
David Mwaure anawania kiti cha urais kwa tiketi ya Chama cha Agano.
Ni kiongozi wa Chama cha Agano.
Alihitimu na shahada ya sheria kutoka Chuo Kikuu cha Nairobi na ana Shahada ya Uzamili katika masomo ya uongozi.
Yeye ni wakili mkuu na amehudumu kama mwanasheria kwa zaidi ya miongo mitatu.
Ana kampuni ya uwakili na amewania viti mbalimbali vya kisiasa.
Ilianzishwa chama cha Agano mwaka 2006.
Kupambana na ufisadi uliokithiri.
kuunda nafasi za ajira.
Kurejesha mali ya Kenya iliyofichwa nje ya nchi.
Pata maelezo zaidi kuhusu sera za wagombea urais hapa
Bw Odinga amemchagua aliyekuwa Waziri wa Sheria Martha Karua kuwa mgombea mwenza wake. Hili linaonekana ni jambo la kihistoria - ni mara ya kwanza kwa mgombea urais kumchagua naibu mwanamke.
Timu yao ya kampeni inawalinganisha wawili hao na Rais wa Marekani Joe Biden na Makamu wake Kamala Harris.
Bw Odinga anawekeza nguvu katika maeneo muhimu ya kati, magharibi na pwani ya Kenya ili kumpa zaidi ya 50% ya kura.
Chanzo cha picha, Getty Images
Maelezo ya picha, Disemba 2021, Bwana Odinga alizindua kampeni zake za urais katika uchaguzi mkuu ujao wa Agosti 9, 2022, pamoja na mengine uzinduzi huo ulishereheshwa na ngoma za asili.
Bwana Odinga anaonekana kuwa mrithi wa kisiasa wa baba yake, Jaramogi Odinga. Alikuwa makamu wa kwanza wa rais wa Kenya baada ya uhuru, lakini aliondoka serikalini mwaka wa 1966 baada ya kutofautiana na kiongozi wa wakati huo, Jomo Kenyatta, baba yake na rais wa sasa, Uhuru Kenyatta.
Jaramogi Odinga aliunga mkono ushirika na uhusiano wa karibu na nchi za Umoja wa Kisovieti na China, huku Jomo Kenyatta akiunga mkono ushirika wa Marekani na mataifa mengine yenye nguvu ya Magharibi.
Tofauti zao zilizidi kuwa mbaya, ambapo Jaramogi Odinga alifungwa kwa miezi 18 hadi alipoachiliwa huru mnamo mwaka 1971. Raila Odinga pia ni mfungwa wa zamani wa kisiasa, na anashikilia rekodi ya kuwa mfungwa wa kisiasa aliyetumikia kifungo cha muda mrefu zaidi nchini Kenya.
Mapambano yake dhidi ya udikteta wa chama kimoja yalimfanya awekwe kizuizini mara mbili (kutoka 1982 hadi 1988 na 1989 hadi 1991) wakati wa utawala wa mrithi wa Jomo Kenyatta na Daniel Arap Moi.
Hapo awali alifungwa kwa kujaribu kufanya mapinduzi mwaka wa 1982.
Mhamasishaji na mtaalamu wa mikakati
Baada ya demokrasia ya vyama vingi kuanzishwa muongo mmoja baadaye, alishindwa mara kwa mara katika jaribio lake la kuwa rais, mara kwa mara akisema ulifanyika udanganyifu na kumpokonya ushindi.
Hii ilisababisha mzozo mkubwa zaidi katika historia ya siasa za Kenya, aliposhawishika kuwa kulikuwa na udanganyifu mkubwa wa kura katika uchaguzi wa ,waka 2007 uliompa ushindi rais wa wakati huo Mwai Kibaki.
Katika ghasia za baada ya uchaguzi zilizofuata, watu 1,200 walikufa na zaidi ya 500,000 waliyakimbia makazi yao.
Chanzo cha picha, AFP
Maelezo ya picha, Ghasia za baada ya uchaguzi wa mwaka 2007 zilikuwa ghasia mbaya zaidi Kenya tanguipate uhuru katika miaka ya 1960s
Baada ya mazungumzo ya upatanishi yaliyoongozwa na Katibu mkuu wa zamani wa Umoja wa Mataifa Kofi Annan, alichukua wadhifa wa Waziri Mkuu katika serikali ya mseto, lakini uhusiano wake na Bwana Kibaki ulikumbwa na kile alichokiita "vita vya mamlaka".
Katika uchaguzi wa 2017, alishindwa na Bwana Kenyatta kwenye sanduku la kura, lakini akashinda katika Mahakama ya Juu, ambayo ilibatilisha matokeo kwa sababu ya dosari nyingi alizozitaja. Uchaguzi ukarudiwa.
Bw. Odinga hata hivyo alisusia kushiriki uchaguzi huo wa marudio, akieleza kutokuwepo kwa uwanja sawa wa kisiasia.
Hilo likafungua njia ya kuchaguliwa tena kwa Bw Kenyatta, wakati Bw Odinga - anayejulikana kuwa mtaalamu wa mikakati na mhamasishaji mkuu - alijitangaza kama "rais wa watu" katika mkutano mkubwa katika mji mkuu, Nairobi.
Wafuasi wake walitii wito wake wa kususia idadi kubwa ya biashara zinazomilikiwa na familia ya Kenyatta ili kuonyesha hasira zao kwa kuchaguliwa tena kwa rais.
Ilikuwa ni moja tu ya maandamano mengi waliyokuwa wamefanya kwa miongo kadhaa kuangazia malalamiko yao ya kisiasa na kiuchumi.
Chanzo cha picha, Getty Images
Maelezo ya picha, Wafuasi wa Odinga mara kadhaa wameripotiwa kugoma kushindwa kwake katika chaguzi zilizopita
Lakini tangu maridhiano ya mwaka 2018 kati ya Bwana Odinga na Bwana Kenyatta, Kenya haijaona maandamano makubwa, licha ya hasira iliyoenea kutokana na kupanda kwa gharama ya maisha.
Maelewano hayo yalipelekea watu hao wawili kuzindua mpango wa "Building Bridges Initiative" (BBI) ili kufanya mabadiliko makubwa ya katiba, ikiwa ni pamoja na kufufua tena wadhifa wa waziri mkuu.
Uvumi ulienea kwamba badala ya kuunga mkono azma yake ya urais, Bwana Odinga atamteua Bwana Kenyatta kuwa waziri mkuu, katika hatua ya mwisho ya kumaliza uhasama kati ya enzi hizo mbili za kisiasa.
Lakini mpango wao ulishindikana baada ya Mahakama Kuu kuamua kwamba rais alikuwa ametenda kinyume cha sheria alipokuwa akiongoza mageuzi hayo kupitia BBI.
Hata hivyo, Bw Kenyatta anamuungua mkono Bwana Odinga, badala ya Naibu wake wa Rais, William Ruto.
Bw Odinga amemuoa Mama Ida na kwa pamoja wamfanikiwa kupata watoto wanne - marehemu Fidel, Rosemary, Junior na Winnie.
Fidel alipewa jina la kiongozi wa Cuba Fidel Castro na Bw Odinga aliwahi kueleza kwamba alichagua jina hilo kwa sababu mwanawe alizaliwa wakati wa Vita Baridi, na "Bw Castro alionekana kupinganana Marekani katika vita vya Vietnam".
Kuendeleza utamaduni wa nasaba, baba huyo alionekana akimlea mtoto wake huyo mkubwa kama mrithi wake, lakini Fidel alikufa akiwa na umri wa miaka 41 mnamo 2015.
Mnamo mwaka wa 2017 binti yake Rosemary alitangaza nia ya kugombea ubunge anayewakilisha kitongoji duni na kikubwa zaidi barani Afrika, Kibera, ambacho babake alikiwakilisha kwa miaka 20.
Lakini alijiondoa kwenye kinyang'anyiro hicho, akitoa sababu za kiafya.
Mbali na siasa Bwana Odinga ni tajiri kwa viwango vya Kenya, akimiliki mali kadhaa ikiwemo kampuni ya kutengeneza mitungi ya gesi East Africa Specter.
Anatoka katika kabila la Wajaluo - la nne kwa ukubwa nchini Kenya. Anatumai kuwa atakuwa Mluo wa kwanza kunyakua kiti cha urais ambacho kimewaniwa kwa muda mrefu na ukoo wa Odinga.