Hii ni tovuti ya maandishi pekee ambayo inatumia data kidogo. Tazama toleo kuu la tovuti likijumuisha picha na video zote.
Pata maelezo zaidi kuhusu toleo hili la linalotumia kiasi kidogo cha data
Zainab Oladehinde: 'Hizi ni hujuma dhidi ya utalii na jeshi la polisi- Polisi Zanzibar
Kamanda wa polisi mkoa wa Kaskazini Unguja, Martin Otieno ametoa taarifa rasmi juu ya tukio la mtalii kutoka Nigeria Zainab Oladehinde aliyedai kunusurika kubakwa na kuibiwa zaidi ya dola 1000 wakati akiwa katika hoteli moja visiwani Zanzibar.
Katika taarifa yake kwa vyombo vya habari, kamanda aliwataja watuhumiwa wa tukio hilo kuwa ni ''Ezekiel Petro Joseph (Muha) na Mohamed Juma Khamis (Mzanzibari)'' ambao waliingia kwa nyakati tofauti.
Watuhumiwa hao wanadaiwa kuingia katika chumba cha Zainab na kutaka kumbaka kisha wakamuibia dola za marekani 1100.
Aliendelea kueleza kuwa baada ya kesi hiyo kufika polisi, Zainab alimshinikiza mkuu wa kituo cha polisi kuhakikisha kuwa analipwa kiasi cha dola za marekani 10,000 na mmliki wa hoteli, jambo ambalo polisi hawakukubaliana nalo.
'Bi Zainab alieleweshwa hivyo, lakini hakuwa tayari kukubaliana na ushauri huo na alielimishwa kuwa kama anataka kulipwa, hivyo ni vyema afungue madai yake mahakamani. Jeshi la Polisi libaki na madai yake ya msingi ya kudhalilishwa na kuibiwa USD 1,100.'' Anasema kamanda Otieno.
Alimtambua vipi mtuhumiwa
Katika taarifa ya Zainab kupitia mtandao wake wa Twitter alisema kuwa alivamiwa usiku chumbani kwake na taa ilikua imezimwa, hivyo hakumuona mtuhumiwa lakini alisikia harufu ya mtu huyo.
Kwa upande wa polisi wanasema kuwa madai ya Zainab ya kumjua mtuhumiwa kutumia harufu yake ulikua ni ushahidi hafifu kuhusu kesi hiyo.
'' Hata alipoulizwa jinsi gani anaweza kumtambua mtuhumiwa aliyetaka kumdhalilisha yeye alisema anamtambua kwa harufu tu ya nywele zake fupi.'' Alisema Kamanda Otieno.
Hata hivyo polisi visiwani humo imemtaka Zainab kurudi na kutoa ushirikiano, na kitendo alichokifanya ni hujuma dhidi ya polisi visiwani humo na utalii.
''Nimuombe Bi Zainab popote pale alipo aje ili tuweze kushirikiana naye katika upelelezi wa shauri hili ili haki iweze kutendeka.''
Katika taarifa ya Zainab, alianisha mambo kadhaa ikiwemo picha na video za hoteli, maafisa wa polisi pamoja na kituo cha polisi eneo la Nungwi.
Taarifa za hoteli bado zina utata kutokana na kubadilika na kufutwa kwa baadhi ya maelezo. Lakini walidai kuwa walishughulika na kesi yake lakini Zainab hakutaka kuendelea na kesi hiyo.
Kwa upande wa Ubalozi wa Nigeria nchi Tanzania bado haujatoa taarifa yoyote kuhusu tukio hilo.
Uchunguzi wa tukio hilo unaofanywa na mamlaka visiwani Zanzibar bado unaendelea.
Zanzibar inategemea sana pato la utalii, kwa mujibu wa mamlaka visiwani humo mwaka 2021 Zanzibar ilikusanya bilioni 69.1 sawa na dola za marekani milioni 29.893 kutoka katika shughuli za kitalii pekee.