Zainab Oladehinde: 'Zanzibar tulimpatia msaada unaohitajika'-Mamlaka

Chanzo cha picha, ZAINAB/INSTAGRAM
- Author, Munira Hussein
- Nafasi, Reporter
- Iliyochapishwa
Baada ya mjadala mkali kuibuka maeneo mbalimbali Afrika, kutokana na taarifa ya raia mwanamke kutoka Nigeria kudai kuwa alinurusika kubakwa na kuibiwa pesa katika hoteli moja visiwani Zanzibar, Mamlaka ya wilaya imezungumzia tukio hilo.
Mkuu wa wilaya kaskazini A Unguja Sadifa Juma Khamis, ambaye eneo la Nungwi lipo chini ya uongozi wake, amezungmza na BBC juu la tukio hilo.
Sadifa Juma anasema kuwa baada ya kupatiwa taarifa ya tukio la mtalii huyo, jambo la kwanza alilofanya alikwenda na kufanya utaratibu wa kumhamisha hoteli na kumpatia hoteli mpya pamoja na ulinzi wakati wote.
''Katika malalamiko yake alisema amenusurika kubakwa, na akasema kuishi katika eneo lile hana amani, kwahiyo mimi Mkuu wa Wilaya nikiwa muwakilishi wa rais, nilimhamisha eneo lile, lakini pia nilifanya mazungumzo na ile hoteli pia juu ya madai hayo'' anasema Sadifa Juma.
Mkuu huyo wa Wilaya aliongeza pia kwakuwa kulikuwa na kesi ya jinai, polisi iliendelea na uchunguzi na mshukiwa aliwekwa mahabusu na vyombo vya usalama. Mshukiwa huyo hakuachiwa huru hadi siku Zainab anaondoka visiwani humo.
''Mshukiwa alikamatwa na aliwekwa mahabusu, lakini taratibu zinataka kesi kuenda kwa DPP, na faili lake lilirudishwa kwa polisi kwa ajili ya marekebisho, lakini kabla ya kufika mahakamani, Zainab aliondoka nchini hivyo ikawa vigumu kwa yeye kutoa ushahidi wake'' anasema Sadifa.
'Hoteli walikosea'
Sadifa Juma anadai kuwa kwa ushirikiano aliuonesha kwa Zainab, alimshauri yeye pamoja na wanasheria wake kutoka Taasisi ya wanasheria Zanzibar wafungue kesi ya madai dhidi ya hoteli ile, mbali na ile kesi ya jinai ili aweze kupatiwa fidia yake na hukumu itolewe na mahakama.
Ameongeza pia ni kweli hoteli ilikua na makosa ya uzembe kwani usalama wa mgeni uko chini yao na sheria inawabana juu ya hilo.
Anadai pia yeye kama mkuu wa wilaya hakuwa na mamlaka ya kuchukua hatua dhidi ya hoteli ile, hivyo aliachia Wizara ishughulike baada ya yeye kukabidhi taarifa yake.
''Kesi ya jinai ilikua inaendelea, lakini niliwashauri wafungue kesi ya madai juu ya hoteli ile, hoteli ilifanya makosa ya uzembe kwasababu sheria inataka mtu atakayefikia kwao awe salama, lakini hawakufungua kesi hiyo''
Video iliyosambaa akifukuzwa kituo cha polisi
Katika taarifa aliyotuma kwenye mtandao wake wa Twitter, Zainab alituma pia video inayoonesha polisi wakimfukuza eneo la polisi.
Kutokana na tukio hilo Mkuu wa wilaya Sadifa alisema kuwa yeye hakupewa taarifa yoyote juu ya tukio na Zainab, na video hiyo ameiona mara ya kwanza siku ya jana.
''Sikupata taarifa ya tukio hilo na Zainab hakuniambia chochote, angeniambia nigechukua hatua kwasababu polisi ya pale iko chini ya mamlaka yangu''. Anasema Sadifa.

Chanzo cha picha, ZAINAB/INSTAGRAM
Madai ya fidia ya dola za marekani 10,000
Katika taarifa za awali kutoka kwa hoteli aliyofikia Zainab, ilisema kuwa anataka fidia ya dola za marekani 10,000. Na katika taarifa yake Zainab alisema wanasheria wake ndio walishauri kiasi hicho cha fidia.
Sadifa alisema Zainab kupitia wanasheria wake, kweli alitaka fidia hiyo kutoka kwa hoteli tukio lilipotokea, lakini hoteli ilisema kuwa watatuma wanasheria wake ndio wakutane na wanasheria wa Zainab.
''Kwa upande wetu sisi tulimpatia malazi, chakula na ulinzi kwa wakati wote huo'' anasema Sadifa.
'Hatujawasiliana hadi sasa'
Kabla ya Zainab kuondoka Zanzibar, Mkuu wa Wilaya Sadifa anasema alimpa ushirikiano mzuri. Katika taarifa aliyotuma jana kupitia mtandao wake wa Twitter, Zainab alishukuru ushikiano wa mkuu huyo wa wilaya pamoja na taasisi ya wanasheria wanawake Zanzibar.
Lakini Sadifa anasema kuwa baada ya Zainab kuondoka hakuwahi kupokea simu zake tena wala kuuliza taarifa za mtuhumiwa.
''Kwa ubinadamu nilionesha, nilitarajia Zainab akifika nyumbani angalau aseme kuwa amefika salama, lakini hatujawasiliana tena'' anasema Sadifa, mkuu wa wilaya Kaskazini Unguja.
Hoteli inasema nini?
Hoteli inayodaiwa kuwa tukio hilo limetokea, imetoa taarifa kadhaa kupitia mitandao yake ya kijamii, lakini katika utoaji wa taarifa hizo baadhi zimekua zikifutwa na kurudiwa.
Katika taarifa yake ya awali, hoteli hiyo ilieleza kuwa tukio lilitokea mwezi Aprili mwaka jana na utaratibu wa kufikishwa polisi ulifanyika, kisha kwenda Ofisi ya Mkuu wa Wilaya na baadaye Ofisi ya Makamu wa Rais. Lakini mlalamikaji Zainab alikataa kuendelea na kesi.

Tukio kubwa lilongonga vichwa vya Habari kutoka visiwani Zanzibar ni lile la watalii wawili kutoka Uingereza kumwagiwa tindi kali mwaka 2013.
Tukio hilo lilisababisha ulinzi kuimarishwa na vifaa vya CCTV kamera kufungwa katika maeneo mbalimbali ya eneo la Stone town.
Zanzibar inategemea sana pato la utalii, kwa mujibu wa mamlaka visiwani humo mwaka 2021 Zanzibar ilikusanya bilioni 69.1 sawa na dola za marekani milioni 29.893.














