Mzozo wa Ukraine: Takriban watalii 1000 wa Ukraine wapatiwa huduma za kibinadamu Zanzibar

- Author, Aboubakar Famau
- Nafasi, BBC Africa, Tanzania
- Iliyochapishwa
Serikali ya Zanzibar imesema inashirikiana kwa karibu na ubalozi wa Ukraine uliopo nchini Kenya kuangalia ni namna gani itawasafirisha watalii wa Ukraine wapatao elfu moja ambao hivi sasa wamekwama kisiwani humo baada ya kuzuka kwa vita kati ya Urusi na Ukraine.
Serikali ya Zanzibar imeiambia BBC kwamba, watalii hao, tayari wanaendelea kupewa huduma za kibinadamu licha ya wengine kuwa wamemaliza siku zao za kutalii.
Baadhi ya watalii kutoka nchini Ukraine, bila kutarajia, wamejikuta wamekwama visiwani Zanzibar punde tu baada ya Urusi kuishambulia Ukraine na kusababisha anga za nchi hizo mbili kufungwa.
Hivi sasa njia pekee ya kuwa karibu na yanayoendelea nchini mwao, ni kufuatia kupitia runinga au hata mawasiliano ya simu. Mmoja wa watalii kutoka Ukraine Katerina Kalatur ambaye amekwama na mama yake anasema;
''Tulikuja kutembea hakuna aliyetarajia hili kutokea tuko kwemye hali ya taharuki hasa kutokana na hali inayoendelea nyumbani tuna hofia usalama wa ndugu na jamaa tulio waacha nyumbani licha ya kuwa hapa sisi tuko salama''

Hamasa kubwa ya wageni hawa ya kutaka kurudi nyumbani licha ya vita vinavyoendelea, ni kwamba baadhi wanakiri kuacha familia zao nyumbani, huku wengine wakisukumwa na sababu za kifedha, hasa baada ya siku zao za kukaa ugenini kama watalii kufikia ukomo.

Hali hii imelazimu baadhi ya hoteli za kitalii kutoa msaada wa kupunguza viwango vya bei huku nyengine zikiamua kuwapa hifadhi wageni bila malipo. Calvin Samuel ni mkurugenzi wa Zanzibar Star Resort iliyopo Nungwi.
''Baada ya janga kutokea wakati mwingine tusiangalie sana fedha, tuangalie na utu kidogo, nilikaa na wageni wangu wao walipewa taarifa kuwa wanapaswa wajilipie nao wanasema hela hatuna na nchi yetu ina vita hatujui tukirudi tunaanza vipi''.
''Nilichofanya nikawaambia wakae bure, wale bure, hakuna chochote wanachonichangia hata shilingi kumi''. Alisema Mkurugenzi huyo.
Kwa upande wake, serikali ya Zanzibar imesema mpango uliopo hivi sasa ni kushirikiana na ubalozi wa Ukraine uliopo nchini Kenya ili kuwaondoa wageni hao na kuwapeleka nchi jirani ya Poland.

''Tumefanya mazungumzo na Balozi wa Ukraine na kesho aliye nchini Kenya na kesho tunatarajia atafika hapa Zanzibar tumefanya mpango atawaondoa, balozi ametuambia wana mpango kwa kuwa ndege ambazo zipo zinatoka moja kwa moja Zanzibar kwenda Poland zipo.'' alisema Waziri wa utalii wa Zanzibar Leila Mohamed Musa.
Zanzibar, kwa miaka mingi, imekuwa ni kivutio cha watalii kutoka maeneo mbalimbali duniani. Katika kipindi cha miaka miwili iliyopita, hasa baada ya kuibuka kwa wimbi la Covid19, na nchi nyingi kuzuia raia wake kusafiri, Zanzibar imekuwa ikiendelea kupokea wageni kutoka Ukraine na nchi nyengine za ulaya ya mashariki.
Kwa siku kadhaa tangu vita hivi vianze, kumekuwa na taharuki miongoni mwa watalii wanaotoka nchi hizo huku wengine wakibaki vyumbani mwao na kutafakari hatma yao.












