Patrick Kimaro : 'Ni maandalizi ya siku yangu ya kufa'

- Author, Aboubakar Famau
- Nafasi, BBC Swahili
- Iliyochapishwa
Kwa kawaida kila mtu anafahamu kuwa atakufa lakini kuzungumzia au kujiandaa kwa ajili ya kifo ni suala sio la kawaida kabisa.
Hata kama mtu ni mgonjwa mahututi sana, familia au mgonjwa hawezi kuanza kutaka kaburi kuanza kuandaliwa.
Lakini , ukijaaliwa kufika, katika kijiji cha Mbosho, wilayani Machame, katika mkoa wa Kilimanjaro, ambapo ndipo anapoishi Patrick Kimaro, mwenye umri wa miaka 59, ukiingia tu katika nyumba yake, mkono wa kulia utakutana na kaburi.
Kwa haraka haraka, maswali yafuatayo yanaweza kukupitia akilini. Kwanza kabisa, unaweza kuuliza, lini mlivunja matanga, au nani katika familia hii amefariki?
Lakini ukisogea karibu ya kaburi hilo, utakutana na maandishi ukutani yasemayo;
"Kipande hiki cha ardhi kimetengwa na kutayarishwa kwa ajili ya kuhifadhi mwili wa ndugu Patrick Matei Kimaro @Sabasita leo TRH 15/01/2022. Kuzaliwa 02/02/1963."

Baada ya kusoma tangazo hilo, ndio utaelewa kwamba, kaburi hilo halina mwili wa marehemu, bali limejengwa kumsubiri mtu ambaye yuko hai.
Hatua hii ya bwana Kimaro imewashangaza wengi, ndani ya kijiji chake na nje ya mipaka ya kijiji hicho.
Kwa sababu sio jambo lililozoeleka katika jamii za kiafrika hasa jamii ya kichaga anayotoka Kimaro.

Ingawa mwenyewe, anajitetea na kusema, ni sehemu tu ya kujiandaa na maisha ya baadae na kuongeza kusema kuwa amefanya hivyo akiwa na akili timamu bila kushinikizwa, lakini bado, kwa baadhi watu wanaona jambo hilo kwao linatia ukakasi.
Baadhi wanalichukulia kama uchuroau laana kwa misingi kwamba linaweza kuleta kisirani katika familia.
Mama Anna, ambaye ni shangazi wa Kimaro, yeye baada ya kusikia kuwa mpwa wake amejenga karibu, anasema hakuamini, na ilibidi afunge safari kuja kujionea mwenyewe.
"Mimi niliposikia mambo haya, nilisikitika sana, sijaamini kwamba ni kweli, ndio sasa hivi nimekuja, nikasema ngoja niangalie kama ni kweli, amenishangaza sana kuona mambo haya, na sijisikii vizuri," anasema mama Anna.

Naye Wilbard William ambaye ni mwenyekiti wa mila na tamaduni ya eneo hilo, anasema yeye pia alishangazwa kwa sababu haijawahi kutokea.
Ingawa wakati huo huo anakiri kwamba, alichokifanya Kimaro ni kuwapunguzia gharama za kujenga kaburi baada ya kifo chake. Hivyo anamshukuru kwa hilo.
Kwa sasa , kujenga kaburi inaweza kugharimu kiasi cha dola 500 za Kimarekani na kuendelea, na utaratibu huwa ni ndugu, jamaa na marafiki huwa wanachangishana ili kufikia kiwango husika.
Licha ya hatua hii kumpa umaarufu lakini pia imemfanya azongwe na maswali yanayotoka kwa watu mbalimbali. Lakini wakati huo huo, baadhi ya majirani nao, wameingiwa na hofu hata ya kutosogelea boma la bwana Kimaro.
Grace Kimaro anayetoka família moja na Kimaro, lakini pia ndiye mlinzi wa nyumba hiyo anasimulia. "Ni kweli, baada ya kujengwa kwa kaburi hili, baadhi ya majirani wanaogopa kufika hapa, ingawa wengine wameanza kulizoea."

Ujenzi wa kaburi hili mpaka sasa umegharimu kiasi cha shilingi za kitanzania milioni sita, ambazo ni takriban dola za kimarekani elfu tatu.
Waswahili wanasema, siku zote mwanzo ni mgumu.
Likiwa katika hatua ya mwisho ya ujenzi, polepole, ndugu waliokuwa na hofu awali, hivi sasa wanaonekana kuanza kulizoea, na hata wakati mwingine, hukaa pembezoni na kuligeuza kuwa ni sehemu ya kupiga soga.
Kutokana na siri ya kifo aijuae ni Mwenyezi Mungu mwenyewe, hivyo baadhi ya benki nchini Tanzania tayari wameona kuna fursa ya kupata mteja, hivyo zimeanza kumshawishi bwana kimaro, kwenda mbele zaidi na kulikatia bima kaburi lake.
Hii itamsaidia iwapo kutatokea uharibifu wa aina yeyote utakaosababishwa na majanga kama mvua kubwa, basi bima yake itamwezesha kujengewa kaburi kama hilo.
Kimaro anaweza asiwe wa kwanza wala wa mwisho kutengeza kaburi lake mwenyewe.
Ingawa jambo hili ni la kufikirisha.
Lakini mpaka sasa, ni vigumu kujua ni wangapi wameanza kushawishika na hatua aliyoichukua Kimaro ya kujijengea kaburi akiwa bado yuko hai.













