Mwanaume alipigwa hadi kufa akijaribu 'kukufuru' kwenye Hekalu la Sikh Golden huko India

Sikh devotees pay respect at the Golden Temple in Amritsar on December 18, 2021

Chanzo cha picha, Getty Images

Maelezo ya picha, Hekalu la dhahabu
Iliyochapishwa

Polisi katika mji wa Amritsar nchini India wamesema kuwa mwanaume mmoja anayeshukiwa kujaribu kufanya kitendo cha kufuru katika hekalu takatifu la Sikhism amepigwa hadi kufa.

Kisa hicho kilitokea wakati wa ibada ya maombi kwenye Hekalu la dhahabu la jiji hilo siku ya Jumamosi, kwa mujibu wa vyombo vya habari vya eneo hilo.

Mwanaume huyo anadaiwa kujipenyeza kwenye ukumbi wa ndani, ambapo kitabu kitakatifu cha Guru Granth Sahib, kinawekwa.

Kisha akajaribu kugusa upanga maalum uliowekwa karibu na kitabu, lakini alizidiwa nguvu na walinzi na waabudu.

Mzozo huo ulifanyika mwendo wa kumi na mbili kasoro saa za huko na alinaswa na kamera huku maombi ya jioni yalipokuwa yakitangazwa kwenye televisheni.

Haijulikani ni nini hasa kilitokea baadaye. Polisi walisema mtu huyo alipatikana akiwa amefariki mara tu maafisa walipofika eneo la tukio, na uchunguzi unaendelea.

Police officials trying to pacify the Sikh activists gathered outside Teja Singh Samundri Hall Shiromani Gurdwara Parbandhak Committee (SGPC) head office after sacrilege attempt at Golden Temple, on December 18, 2021 in Amritsar, India

Chanzo cha picha, Getty Images

Maelezo ya picha, Baada ya tukio hilo wanaharakati walikusanyika nje ya ofisi kuu ya Kamati ya Shiromani Gurdwara Parbandhak (SGPC), ambayo inaendesha eneo takatifu.

Katika ujumbe wa Twitter, Waziri Mkuu wa Punjab Charanjit Singh Channi alisema aliamuru polisi "kuchunguza chanzo cha tukio hilo kutisha".

Tukio hilo linajiri siku chache baada ya mwanaume mwingine kukamatwa kwa madai ya kutupa kitabu kitakatifu cha Sikh, Gutka Sahib, kwenye kisima cha maji kilichotengenezwa na mwanadamu kuzunguka hekalu hilo.

Kudhalilishwa kwa Guru Granth Sahib ni suala la kuhuzunisha sana miongoni mwa jamii ya Sikh.

Udhalilishaji kadhaa ulifanyika mnamo 2014 na 2015, na ikawa suala kuu la kisiasa wakati wa uchaguzi wa Punjab mnamo 2017 na 2019.

Chama tawala cha Congress kilishutumiwa na wapinzani wa kisiasa, kwa kushindwa kuleta haki kwa wahalifu waliopita wa kunajisi.

Balwinder Bhunder, mbunge wa chama cha upinzani Akali Dal, alilaani tukio la hivi punde siku ya Jumamosi, akiambia chombo cha habari cha NDTV kwamba lilikuwa ni jaribio la makusudi "kudhoofisha Punjab, ambayo ni mkono wa upanga wa India".

"Baadhi ya watu wameufanya mchezo wa kisiasa katika kipindi cha miaka mitano iliyopita," aliongeza.