Hii ni tovuti ya maandishi pekee ambayo inatumia data kidogo. Tazama toleo kuu la tovuti likijumuisha picha na video zote.
Pata maelezo zaidi kuhusu toleo hili la linalotumia kiasi kidogo cha data
Miaka 60 ya uhuru; Je ushawishi wa Tanzania barani Afrika umepanda au kushuka?
- Author, Markus Mpangala
- Nafasi, Mchambuzi, Tanzania
- Iliyochapishwa
Sifa kedekede ilizopata miaka ya mwanzo ya uhuru wake hususan katika diplomasia ya ukombozi kusini mwa Afrika pamoja na harakati za kushawishi kuunda taifa la Afrika, umoja, mshikamano, miungano ya kikanda, utatuzi wa migogoro na kusimamia sera zake za nje kwa kuziweka karibu nchi zote, kwa sasa zinaonekana kushuka huku baadhi ya mataifa yakiipiga kumbo Tanzania ambayo Desemba 9 mwaka huu itatimiza miaka 60 tangu iliyokuwa Tanganyika kupata uhuru wake mwaka 1961 kutoka kwa Uingereza.
Uwezo wa kushawishi mataifa ya Afrika katika ajenda,sera na mipango mbalimbali ni miongoni mwa sifa zilizoipambanua Tanzania kwa miongo mingi ikiwa imefanikiwa kutoa Katibu Mkuu wa Umoja wa Afrika, Dkt. Salim Ahmed Salim, ambaye pia mwaka 1981 ilibakia kidogo tu achaguliwe kuwa Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa kama si kupingwa na Marekani kwa kura ya turufu.
Katika kilele cha ushawishi uliokuwepo, taifa hilo lilichomoza kupigania haki ya kiti cha China ndani ya Umoja wa Mataifa katika miaka ya 1970 katikati ya wimbi la siasa za vita baridi baina ya mataifa ya Magharibi na mengine.
Duru za kisiasa zinaonesha sasa upepo umebadilika na kwamba katika makundi matatu yaliyoko ndani ya Umoja wa Nchi za Afrika kulingana na historia zao za ukoloni; Nchi zilizotawaliwa na Ufaransa (Francophone), Nchi zilizotaliwa na Uingereza (Anglophone) na zile zilizotaliwa na Ureno(Lusophone), ushawishi wa Tanzania unachechemea kwa sababu ambazo wachambuzi wa kisiasa wanazitaja kutokana na hali yake ya kiuchumi na kubadilika kwa zama za kutoka siasa za diplomasia ya ukombozi hadi diplomasia ya uchumi.
Kuondoka kwenye diplomasia ya ukombozi hadi kuingia nguvu za kiuchumi ni sababu za kushuka ushawishi wa Tanzania katika siasa za Afrika, pamoja na uwekezaji toka nje wa kiwango cha chini, licha ya taifa hilo kuwahi kuwa Mwenyekiti wa Nchi za Mstari wa mbele katika kuunganisha na kupigania ukombozi wa nchi za kusini mwa Afrika, hivyo Dar es Salaam kuwa makao ya kamati ya ya ukombozi chini ya Katibu Mtendaji, Brigedia Jenerali Hashim Mbita.
Katika mahojiano na gazeti moja la kila wiki mwanzoni mwa Novemba mwaka huu, aliyekuwa waziri wa Mambo ya Nje wa Tanzania, Bernard Membe aliibua hoja yenye kuashiria kuporomoka kwa ushawishi wa taifa hilo, baada ya kueleza kuwa ameshangazwa Tanzania kupigwa kumbo na Rwanda kwenye masuala ya diplomasia hususani suala la kulinda amani na kupambana na ugaidi nchini Msumbiji.
Matamshi ya Waziri huyo wa zamani yanaashiria kuwa hicho ni kigezo kimojawapo cha kushuka kwa ushawishi wa taifa hilo miongoni mwa mataifa ya Afrika.
Mambo gani yaliipatia sifa Tanzania?
Yafuayayo ni mambo machache yaliyoipa sifa na ushawishi Tanzania katika kipindi cha miaka 60 ya uhuru wake.
• Utatuzi wa migogoro mbalimbali barani Afrika ikiwemo uchaguzi wa mwaka 2002 wa Kenya na kupambana na waasi wa Comoro na kuongoza upatanishi nchini Zimbabwe kati ya viongozi wa zamani Robert Mugabe na Morgan Tsvangirai
• Kushiriki katika Operesheni mbalimbali za Kijeshi za kulinda amani Darfur,DRC,Lebanon na kwingineko
• Kusaidia na kuhifadhi wapigania uhuru na kuongoza mapambano ya uhuru kusini mwa Afrika; Msumbiji, Afrika kusini,Zambia,Zimbabwe na Namibia na Angola.
• Kupigania umoja wa Afrika kwa kuanza na miungano ya kikanda.
• Kuunga mkono juhudi za Jumuiya ya Maendeleo ya Nchi za kusini mwa Afrika.
• Kuwa sauti ya wanyonge ikiwemo kuunga mkono wananchi wa jimbo la Biafra, Nigeria.
. Kuvunja uhusiano wa kidiplomasia na Uingereza ili kupinga siasa za ukandamizaji Afrika Kusini na Zimbabwe. ya sasa
• Kurejesha Jumuiya ya Afrika mashariki
• Kupokea wakimbizi wa mataifa jirani
• Ushirikiano usio na mashaka kwa mataifa jirani
• Kuwa kimbilio la wanapigania uhuru,wanasiasa na wanaharakati toka mataifa ya Afrika.
. Kuwa mwenyeji wa mazungumzo Amsni ya Burundi kati ya 1996 hadi 2000 uliposainiwa mkataba wa amani.
Je nini kilikwenda kombo?
Kwa kipindi cha miaka sita tangu mwaka 2015 hadi 2020 Tanzania haikuonekana kushiriki katika masuala mengi yanayogusa siasa za Afrika.
Tanzania haikuwa na kauli au matamko ambayo yanatikisa na kuwavutia wanasiasa na viongozi wengine barani Afrika.
Hilo lilitokana na aina ya uongozi ambayo ilijikita katika siasa za ndani huku ikiporomosha misuli yake katika anga za kimataifa tofauti na utawala wa rais mstaafu Jakaya Kikwete (2005-2015).
Katika kipindi cha miaka sita Tanzania haikujitokeza kwenye utatuzi wa migogoro Afrika, ushiriki wake katika masuala ya kikanda umekuwa hafifu.
Ni sababu hizi zinamlazimu rais wa sasa Samia Suluhu Hassan kutembelea mataifa mbalimbali barani Afrika, pamoja kushiriki mikutano ya kimtaifa kama njia na mbinu ya kurejesha ushawishi na kuongeza ushirikiano na mataifa mengine.
Je taifa hilo litaweza kuinua ushawishi wake?
Dkt. Richard Mbunda, Mhadhiri wa Sayansi ya Siasa toka Chuo Kikuu cha Dar es salaam amemwambia mwandishi wa makala haya, "Ushawishi unaendana na kipato.
Nani anataka kusikiliza nchi maskini?
Tanzania iliwahi kuwa Mwenyekiti wa Nchi za Mstari wa mbele wakati wa kupigania uhuru wa mataifa ya kusini mwa Afrika, lakini sasa zama zimebadilika.
Sasa hivi wenye ushawishi barani Afrika ni Nigeria,Afrika kusini na Misri, hawa wana nguvu kiuchumi.
"Sasa katika nukta hii lazima tutafute njia na majibu ya kupandisha ushawishi wa Tanzania ndani ya bara hili. Miaka 1960 aliyekuwa rais wa Ghana, Kwame Nkrumah alishauri Afrika tupate ufalme wa kisiasa kwanza mengine yatafuata, lakini sasa hivi ufalme wa kiuchumi ni muhimu zaidi ya ule wa kisiasa.
Tanzania inatakiwa kujielekeza katika kujenga uchumi wa kujitegemea na kutafuta fursa za uwekezaji wa nje zinazokuza uchumi wetu, kisha nguvu za ushawishi wa kidiplomasia zitakuja zenyewe. Mfano hali tete ya Msumbiji, tusisahau jambo moja muhimu kupeleka majeshi au kusaidia namna yoyote ile kijeshi kunahitaji uwezo wa kijeshi ambao unakutaka uwe na uchumi mzuri,"
Hivyo, Tanzania bado inayo fursa ya kurejesha sauti yake ya ushawishi barani Afrika na hata nje ya bara hilo kama ilivyokuwa enzi za Mwalimu Julius Nyerere, Mzee Ali Hassan Mwinyi, Benjamin Mkapa na Jakaya Kikwete lakini kwa kuzingatia mabadiliko ya nyakati, yaliyojiegemeza katika nguvu ya kiuchumi badala ya nguvu ya kisiasa.
Nje ya hapo jitihada za awamu ya sita chini ya Rais Samia Suluhu Hassan zitazidi kupungukiwa nguvu na kasi iliyokusudiwa, na kubakia na ushawishi wa kawaida au wa wastani bila kujipambanua kama ilivyokuwa awali.