Tshisekedi na Uwenyekiti wa Umoja wa Afrika - Je matatizo bado yatakuwa yale yale?

    • Author, Na Mohammed AbdulRahman
    • Nafasi, BBC Swahili
  • Iliyochapishwa
  • Muda wa kusoma: Dakika 5

Umoja wa Afrika (AU) umemchagua Mwenyekiti mpya wa mwaka. Rais Felix Tshisekedi wa Jamhuri ya Kidemokrasi ya Congo, amechukua wadhifa huo kutoka kwa Rais Cyril Ramaphosa wa Afrika Kusini wakati wa mkutano wa viongozi wakuu na serikali mjini Addis Ababa.

Kikao cha 34 cha kumchagua mwenyekiti huyo kilifanyika siku ya Jumamosi huku kauli mbiu ikiwa ni "Sanaa, Utamaduni na Urathi, lakini masuala sugu yanaendelea kutawala mkutano huo unaokamilika leo Jumapili tarehe 7 mwezi wa Februari 2021.

Tshisekedi alichaguliwa katika kikao cha 2020 kuwa Mwenyekiti wa mwaka 2021, wadhifa unaozunguka miongoni mwa viongozi wa nchi wanachama kwa kipindi cha mwaka mmoja. Tangu mwaka jana Tshisekedi amekuwa kwenye kampeni ya kujijenga kwa kufanya ziara kadhaa barani humo na kujiimarisha kidiplomasia.

Hali ya ndani DRC na suala la usalama

Wakati huo huo tokea mwezi Desemba amejiimarisha nyumbani baada ya kuvunja ushirikiano na Rais wa zamani Joseph Kabila na kuvunja pia ushawishi wake.

Miongoni mwa masuala mazito yanayomkabili nyumbani , kwanza ni Kurejesha usalama na amani ikiwa miongoni mwa ahadi alizotoa alipoapishwa kumrithi Kabila Januari 2019.

Katika suala la usalama ,Congo bado inahitaji kuendelea kuwepo nchini humo, ujumbe wa kusimamia amani wa Jeshi la Umoja wa Mataifa, unaojulikana kama MONUSCO.

Katika taarifa yake kupitia ukurasa wa Twitter, Naibu Katibu mkuu wa Umoja wa Mataifa anayesimamia shughuli za kusimamia amani Jean-Pierre Lacroix, amekiri 2020 ulikuwa mwaka mwengine mgumu katika shughuli za kusimamia amani nchini Congo.

Leila Zerrougui, mjumbe maalum wa Katibu mkuu wa Umoja wa Mataifa Antonio Guterres, amesema lengo kuu pale wakati wa kuondoka utakapowadia ni kuiacha Congo ikiwa na amani na utengamano, iliweza kuanza safari ya maendeleo.

Diplomasia ya Kuzijongelea na nchi jirani

Akitambua kwamba uhusiano mwema na nchi jirani jirani ni muhimu, Tshisekedi amekuwa akijaribu kuimarisha uhusiano na Rwanda na Uganda, zilizosaidia kijeshi kumn´goa madarakani Mobutu Sese Seko.

Nchi hizo mbili zilipigana vita dhidi wa utawala wa Laurent Desire Kabila kuyasaidia makundi tafauti ya waasi na uhasama huo ukaendelea katika utawala wa Kabila .

Vita hivyo 1998-2003 vilivyoitwa "vita vya pili vya Congo", viliyaingiza mataifa sita, huku Angola, Zimbabwe, Namibia na Burundi zikimsaidia Kabila.

Kabla ya kuondoka madarakani kufuatia ushindi wa Tshisekedi katika uchaguzi wa Desemba 2018 ambapo Kabila hakushiriki, tayari Kabila mdogo alikuwa ameshaanza kujongeleana na mahasimu wake Rais Paul Kagame wa Rwanda na Yoweri Museveni Uganda na wakati wote wa mazungumzo suala kuu lilikuwa ni usalama.

Kabila (ibumoso) na Tshisekedi mu muhango wo kurahira kwa Tshisekedi mu kwezi kwa mbere mu 2019

Kagame amekuwa akishinikiza kuyaangamizwa masalio ya kundi la waasi wa Kihutu FDLR walioko ndani ya Congo, huku Museveni akisema tayari kuisaidia Congo kuwafyeka wapiganaji wa Allied Democratic Forces (ADF), ambao bado ni kitisho kwa nchi zote mbili.

Maelewano ya Tshisekedi na Kagame ni mazuri ambapo Rais wa Rwanda aliiizuru Kinshasa Juni 2019, ingawa wengi wa raia wa Congo wangali na machungu ya kujihusisha Rwanda kijeshi nchini Congo mnamo miaka ya nyuma..

Changamoto za Kanda

Wakati Tshisekedi akirekebisha uhusiano wa Congo na Rwanda na Uganda, pia amechukua jukumu la kuwapatanisha majirani zake ambao nao wamekuwa katika mvutano wa kidiplomasia.

Februari 2020, akishirikiana na Rais wa Angola João Lourenço, walifanikiwa kuitisha mkutano wa kilele mjini Luanda Angola uliohudhuriwa na Kagame na Museveni kujadili njia za kuondoa tafauti zao.

Angola inaangaliwa kuwa nguvu ya kutegemewa kijeshi na kiuchumi.

Suala jengine ni uhusiano tete kati ya Rwanda na Burundi tangu lilipofanyika jaribio la mapinduzi dhidi ya Rais wa zamani hayati Pierre Nkurunziza 2015. Inadaiwa baadhi ya wanajeshi waliohusika katika mpango huo ulioshindwa walikimbiliaRwanda ambayo inawapa hifadhi. Rwanda imeyakanusha madai hayo.

Mvutano wa nchi hizo mbili bado ungalipo,licha ya awali kuwepo matumaini kwamba zingeondoa tafauti zao baada ya Rais mpya Evariste Ndayishimiye kuchaguliwa Mei 2020, mwezi mmoja kabla ya kifo cha Nkurunziza aliyetangaza kustaafu.

Septemba 2020, Tshisekedi aliwaalika marais Kagame, Museveni, Ndiyishimiye na Lorenco kwa mkutano mdogo wa kilele mjini Goma, kwa lengo la kujenga msingi wa kuaminiana, lakini rais wa Burundi Evariste Ndayishimiye hakuhudhuria.

Mataifa yote hayo yanatambuakwamba amani na utulivu katika eneo hilo ni muhimu kwa maendeleo yao na kwamba yanahitaji kufungua ukurasa mpya kufanikisha maendeleo ya nchi zao. Tshisekedi pia anatambua umuhimu wa uhusiano mwema na majirani zake ili aweze kuwa na utulivu wa kisiasa.

Mtihani mwengine unaomsubiri

Mwenyekiti mpya wa Umoja wa Afrika, atakuwa na kazi ngumu kuyashughulikia masuala yanayoukabili Umoja huo wakati huu na ambayo mtangulizi wake Rais Ramaphosa wa Afrika Kusini anayaacha kama alivyoyakuta bila kupiga hatua yoyote.

Miongoni mwayo ni mashambulio ya waasi wa Kiislamu wa itikadi katika jimbo la kaskazini la Cabo Delgado nchini Msumbiji. Waasi hao wanasemekana kuwa na mafungamano kundi la Dola la Kiislamu (IS).

Kadhalika kuna mgogoro wa Libya ambao kujiingiza kwa dola za kigeni Ufaransa, Urusi na Uturuki kumezizotesha kabisa juhudi za upatanishi za Umoja wa Afrika na Mali na kipindi mpito kuelekea kurejeshwa demokrasia baada ya mapinduzi ya Agosti 2020 dhidi ya Rais Ibrahim Boubakar Keita .

Jengine ni Somalia na suala la Sahara magharibi ambapo hadi leo Umoja wa Afrika bado umegawika kati ya wanaoiunga mkono Sahara magharibi na haki ya wakaazi wake kujiamulia mustakbali wao na Morocco inayodai ni sehemu yake.

Pamoja na yote hayo, kubwa na suala tete wakati huu ni jinsi ya kukabilianana athari za janga la Corona (Covid-19) ambapo umeibuka mjadala mkubwa barani humo, kuhusu matumizi ya chanjo.

Umoja wa Afrika na hoja ya kutowajibika

Kwa mtazamo wa matatizo hayo lukuki, Mwenyekiti mpya kama ilivyokuwa kwa mtangulizi wake, ataukuta Umoja huo na tasisi zake katika hali ile ile ya kushindwa kuwajibika ipasavyo. Miongni mwazo ni bunge la Afrika , liloasisiwa 2004.

Bunge hilo lenye makao yake makuu Midrand Afrika Kusini lilitarajiwa liwe jukwaa la kuchukua maamuzi kuhusu matatizo yanayolikabili bara hilo na kuhakikisha yanafanyiwa kazi na Halmashauri kuu yenye makuu mjini Addis Ababa na kuongozwa na Rais wake Mussa Faki Mahamat.

Bunge la Afrika lilikusudiwa hatimaye kuwa taasisi yenye madaraka kamili. Kwa bahati mbaya miaka 17 baada ya kuundwa bado halijakamilisha lengo hilo.

Wengi wanaamini Umoja wa Afrika hauna meno ya kuuma, hasa panapohusika na ukandamizaji wa demokrasia na kuzorota kwa utawala bora miongoni mwa nchi wanachama.

Pamoja na yote hayo kwa Tshisekedi kuwa Mwenyekiti mpya atakuwa kwa namna moja au nyengine inairejesha Congo katika jukwaa la kimataifa na kuondoa ile sura iliotawala muda mrefu kuwa taifa lenye misukosuko, utawala mbovu na vita.

Atakuwa anatarajia kwamba angalau mafanikio upande huo, yataweza kumjengea haiba katika siasa za Afrika na Kimataifa.