Utafiti: Unajua kulala kati ya saa 4 na saa 5 usiku kunapunguza hatari ya magonjwa ya moyo?

Chanzo cha picha, Getty Images
Inaonekana kuna muda muafaka wa kulala - kati ya saa 4 na 5 usiku - ambao unaohusishwa na afya bora ya moyo, wanasema watafiti ambao wamewachunguza watu wa kujitolea takribani 88,000.
Timu maalumu kutoka Biobank ya Uingereza inaamini kwamba kuwa na uwiano sawa wa usingizi na namna mwili unavyotaka kunaweza kufafanua uhusiano uliopo wa uwezekano wa kupunguza hatari ya mshtuko wa moyo pamoja na kiharusi.
Namna ya mwendendo wa asili wa mwili wa saa 24 ni muhimu kwa ustawi pamoja na tahadhari. Kwa sababu kuna uwezekano wa kutokea kwa shinikizo la damu.
Katika utafiti huo, ambao umechapishwa katika Jarida kuhusu masuala ya Moyo la Ulaya, watafiti walikusanya data kuhusu nyakati za kulala na kuamka kwa zaidi ya siku saba kwa kutumia kifaa kinachofanana na saa ya mkono kinachovaliwa na watu waliojitolea.
Walifuatilia kile kilichotokea kwa waliojitolea katika suala la afya ya moyo na mzunguko wa damu kwa wastani wa miaka sita.
Zaidi ya watu wazima 3,000 walipata ugonjwa wa moyo na mishipa. Visa hivi ving kati ya zilizotokea kwa watu ambao walichelewa kulala au walilala mapema kabla ya muda muafaka wa kati ya saa 4 na saa 5 usiku.
Watafiti hao walijaribu kudhibiti vyanzo ama mambo mengine yanayosababisha matatizo ya moyo wa mtu, kama vile umri wao, uzito na viwango vya 'cholesterol', lakini mkazo uliowekwa na utafiti wao ni kwmaba hauwezi kuthibitisha chanjo na athari.

Chanzo cha picha, Getty Images
Mwandishi wa utafiti huo, Dk David Plans, kutoka Chuo Kikuu cha Exeter, alisema: "Ingawa hatuwezi kuhitimisha sababu kutoka kwenye utafiti wetu, matokeo yanaonyesha kuwa kulala mapema au kuchelewa kulala kunaweza kutatiza namna mwili unavyojiendesha kwa saa 24 na kusababisha matokeo mabaya kwa afya ya moyo na mishipa.
"Wakati wa hatari zaidi ulikuwa baada ya usiku wa manane, kwa sababu inaweza kupunguza uwezekano wa kuona mwanga wa asubuhi, ambao huweka upya saa ya mwili ama mwili unavyoanza upya wasaa wake wa maisha ya siku."
Regina Giblin, muuguzi mkuu wa magonjwa ya moyo katoka taasisi ya magonjwa ya moyo ya British Heart Foundation, alisema: "Utafiti huu mkubwa unaonyesha kuwa kulala kati ya saa 4 na saa 5 usiku kunaweza kuwa mahali pazuri kwa watu wengi kuweka mioyo yao kuwa yenye afya kwa muda mrefu.
"Hata hivyo, ni muhimu kukumbuka kuwa utafiti huu unaonyehsa uhusiano tu uliopo wa kulala kati ya saa 5-6 na afya ya moyo na utafiti huu hauwezi kuthibitisha sababu hasa nini ya hilo na athari ni zipi. Utafiti zaidi unahitajika kuhusu wakati wa kulala kama moja ya sababu zinazoweza kuleta hatari ya magonjwa ya moyo na mzunguko wa damu.
Kupata usingizi wa kutosha ni muhimu kwa ustawi wetu kwa jumla pamoja na afya ya moyo na mzunguko wa damu. Watu wazima wengi wanapaswa kulenga kulala kwa angalau masaa saba hadi tisa kila usiku, alisema.
"Lakini usingizi sio jambo pekee linaloweza kuathiri afya ya moyo. Ni muhimu pia kuangalia mtindo wako wa maisha kama kujua hali ya shinikizo la damu na viwango vya cholesterol, kuwa na uzito mzuri, kufanya mazoezi mara kwa mara, kupunguza ulaji wa chumvi na unywaji wa pombe. Pia kula mlo kamili kunaweza pia kusaidia kudumisha afya ya moyo wako." alisema.












