Wafahamu wanaume watano ambao wake zao wamefanikiwa zaidi duniani

Kama ilivyo kwa wanaume ambao mara nyingi ndio wanaotawala siasa, mambo sasa yameanza kuwa vivyo hivyo kwa wanawake.
Utafiti uliofanywa na Profesa wa chuo kikuu cha Stanford ambaye pia ni mshindi wa Tuzo ya Nobeli, Alvin Roth, unaonesha kuwa haijalishi mmoja amefanikiwa kiasi gani katika ndoa, wanandoa wote wawili wana uwezekano mkubwa wa kuwa na furaha ikiwa watakuwa ni wenye kuridhika moyoni mwao.
Kulingana na utafiti wa Profesa Role, ''Wanaume ni kiungo muhimu katika mafanikio ya wake zao''.
Utafiti huo ulihitimisha kuwa wanaume wanaunga mkono wake zao wanawaongezea fursa za kuwa na mafanikio zaidi katika ujasiriamali na hata uongozi.
Fahamu wanaume watano ambao wamekuwa nguzo muhimu katika maendeleo ya wake zao duniani.
Ikemba Iweala mume wa Ngozi Okonjo-Iweala

Chanzo cha picha, @NOIweala
Dkt. Ikemba Iweala ni daktari kutoka jimbo la Abia na alisomea chuo kikuu cha Ibadan, Nigeria.
Dkt. Iweala amedhihirisha kuwa baba bora kwa familia yake licha ya ratiba yake yenye shughuli nyingi.
Amemuona Dkt. Ngozi Okonjo-Iweala, ambaye amewahi kuwa waziri wa fedha mara mbili na pia amehudumu kama waziri wa mambo ya nje na kuwa mshiriki wa bodi zingine za kimataifa kama Twitter na GAVI.
Na sasa hivi anatarajiwa kuwa mwanamke wa kwanza wa Afrika kama rais wa Shirika la Biashara Duniani (WTO).
Wanandoa hao wamejaaliwa watoto wanne, msichana mmoja na wavulana watatu.

Kamala Harris amekuwa mwanamke wa kwanza mweusi kuwa makamu wa rais wa Marekani.
Hiyo ni historia sio tu kwake lakini hata kwa mume wake Douglas Emhoff ambaye amemuunga mkono mke wake hadi pale alipofikia hatua hii.
Kuwa na akaunti ta Twitter aliyotengenezwa rasmi na serikali ya Biden, Bwana Emhoff naye amekuwa mwanaume wa kwanza ambaye mke wake ni makamu rais.
Kama haitoshi, ni mwenye asili ya kiyahudi. Douglas Emhoff alizaliwa Brooklyn na wazazi wake ni Wayahudi, Barbara na Michael Emhoff.
Amesomea California nchini Marekani ambako alimaliza masomo yake ya shahada ya sheria na kufanyakazi katika mashirika kadhaa ya sheria.
Amebaki kuwa mfano kwa wanaume wengine vile wanavyoweza kusaidia wake zao na wakafanikiwa maishani.
Joachim Sauer mume wa Angela Merkel Chansela wa Ujerumani

Chanzo cha picha, Getty Images
Joachim Sauer ni Profesa wa sayansi katika chuo kikuu cha Humboldt huko Berlin, Ujerumani.
Mwaka 1998, alifunga pingu za maisha na Angela Merkel ambaye pia ni mwanasayansi.
Lakini kabla ya kumuoa Merkel, alikuwa amemuoa mwanamke mwingine na kujaliwa watoto wawili.
Angela Merkel alipokuwa chansela wa Ujerumani mwaka 2005, Sauer alikuwa mwanaume wa pili mwenye nguvu Ujerumani baada ya rais.
Kwasababu ya umaarufu wa mke wake katika ulingo wa siasa, Sauer anaangaziwa sana na vyombo vya habari kuliko vile anavyofanya utafiti wake kisayansi.
Mara kadhaa amesema kuwa hapendi kujitokeza kwenye vyombo vya habari na pia hapendi kujadili masuala ya kisiasa.
Peter Murrell mume wa waziri mkuu wa Scotland Nicola Sturgeon

Chanzo cha picha, Getty Images
Peter Tierney Murrell ni afisa mwandamizi wa chama cha Scottish SNP kinachoongozwa na mke wake Nicola Sturgeon.
Alizaliwa mwaka 1964 Edinburgh, na kusoma katika chuo kikuu cha Glasgow huko Scoland.
Murrel ni mwanasiasa ambaye amewahi kushika nafasi ya mtendaji mkuu wa chama cha Scottish National tangu mwaka 1999, na uongozi wake umesifiwa kwa kumuongoza mkewe hadi akapata ushindi katika uchaguzi wa 2007.
Alimuoa Nicola Sturgeon mwaka 2010 lakini mara ya kwanza kabisa walikutana mwaka 1988 katika mkutano wa vijana wa SNP ambao ulikuwa unaandaliwa na Murrell.
Alimposa Nicola Sturgeon mwaka 2003.
Clarke Timothy Gayford, mume wa waziri mkuu Jacinda Ardern

Chanzo cha picha, Getty Images
Clarke Gayford, 44, ni mwanahabari na mume wa aliyekuwa Waziri Mkuu Jacinda Arde
Alianza masomo yake katika shule ya upili ya wavulana ya Palmerston North.
Mwaka 1995, alihudhuria chuo kikuu cha Otago na kuhitimu.
Pia alisoma katika chuo cha utangazaji cha New Zealand huko Christchurch, New Zealand.
Mwaka 2003 akaanza kufanyakazi kama mtangazaji wa kituo cha channel C4 na kuwakilisha programu ya vijana.
Inasemekana kuwa mwaka 2019, Gayford alimposa Ardern.
Kulingana na taarifa kadhaa za New Zealand, ameandamana na Ardern katika nchi kadhaa ikiwemo mkutano wa wakuu wa Serikali za Jumuiya ya Madola London.













