Virusi vya corona: Marufuku ya kutotoka nje yatangazwa katika mji mkuu wa Rwanda kutokana na corona

rwanda
    • Author, Yves Bucyana
    • Nafasi, BBC Africa, Kigali
  • Iliyochapishwa
  • Muda wa kusoma: Dakika 2

Rwanda imerejesha sheria ya watu kutotoka nyumbani katika mji mkuu wa Kigali kama mkakati wa kuzuia maambukizi zaidi ya virusi vya Corona.

Shughuli nyingi zimepigwa marufuku zikiwemo biashara , ibada na mikusanyiko huku pia watumishi wote wa serikali na wa sekta binafsi wakitakiwa kufanyia kazi nyumbani.

Kadhalika sheria ya kutotoka nje usiku itatekelezwa kuanzia saa kumi na mbili jioni.

Serikali ya nchi hiyo imesema kwamba uamuzi huo umetokana na idadi kubwa ya maambukizi kuwahi kushuhudiwa ambapo watu zaidi ya elfu nne wameambukizwa ugonjwa huo mnamo kipindi cha siku 50.

Kutoka Kigali ,mwandishi wa BBC Yves Bucyana amesema kikao cha baraza la mawaziri kimetangaza sheria hiyo ya watu kutotoka nyumbani mjini Kigali na kusema kwamba watu wataruhusiwa kutoka tu ili kununua chakula au kwa ajili ya matibabu, vinginevyo ni mtu awe nampaka kibali maalum kinachotolewa na polisi.

Shughuli za ibada zimepigwa marufuku pamoja na mikusanyiko ya kila aina, biashara zote zimeamrishwa kufunga isipokuwa bidhaa za vyakula huku migahawa ikiruhusiwa tu kutoa huduma ya kupelekea watu vyakula majumbani.

Kwa mara ya kwanza serikali imaamuru watumishi wake na watumishi wa sekta binafsi, wakati awali iliruhusu asilimia 30 ya watumishi kufanyia kazi ofisini.

Waziri wa afya Dr Daniel Ngamije amesema hali ya maambukizi inazidi kuwa ya kutisha na serikali haina njia nyingine ya kumudu kasi ya maambukizi ya covid19:

''Hadi kufikia sasa walioambukizwa covid19 ni watu zaidi ya elfu 11, jambo la kushangaza ni kwamba asilimia 46 ya watu hao waliambukizwa mnamo kipindi cha siku 50 zilizopita.

Watu waliokufa ni 142 asilimia 65 yao walikufa mnamo siku 50 zilizopita. Hii ina maana kwamba mnamo kipindi cha siku 50 zilizopita hali imekuwa ya kutisha ndio maana ili tuweze kumudu kasi ya maambukizi kama tunavyoishuhudia tumelazimika kuchukukua hatua kali.

Jumatatu jioni Wizara ya afya nchini humo ilitoa taarifa kuhusu maambukizi , kabla ya tangazo la baraza la mawaziri kutolewa kupitia ukurasa wake wa Twitter:

Ruka X ujumbe
Ruhusu maudhui? (Mitandao ya kijamii)

Mkala hii imebeba madhui yaliyotoka kwenye mitandao ya kijamii. Tunaomba ruhusa yako kabla kitu chochote hakija pakiwa, sababu wanaweza wakawa wanatumia Cookies na tekinolojia nyingine. Unaweza ukasoma sera sera ya kutumia cookies katika mitandao ya kijamii kabla ya kukubali. Kutazama maudhui haya chagua accept and continue

Onyo: Imetoka kwingine na inaweza kuwa na matangazo

Mwisho wa X ujumbe

Tuna wagonjwa wengi hususani mjini Kigali wanaopokea matibabu ya Covid19 wakiwa nyumbani na hivyo kuwataka watu kubaki nyumbani ni hatua itakayosaidia kupunguza kusambaa kwa virusi.''

Shule zote mjini Kigali pamoja na vyuo vikuu vya serikali na vya binafsi zimefungwa.

Baadhi ya Hoteli zitakazotangazwa zitaruhusiwa kupokea wageni kutoka nje ya nchi wanaokaa kwa muda mfupi na kumewekwa marufuku ya kutotembea usiku kuanza kutekelezwa kuanzia saa kumi na mbili jioni hadi saa kumi alfajiri.

Wagonjwa zaidi ya elfu 3,500 bado wanatibiwa covid19.

Serikali imesema mnamo siku mbili itapata madawa ya kusaidia wagonjwa mahtuti kupona ikiwa pia Rwanda iko mstari wa mbele kupata kinga dhidi ya ugonjwa huo.

Ni kwa mara ya pili Rwanda kutangaza sheria ya kutotoka nyumbani kama mkakati wa kuzuiya maambukizi ya covid19,mara ya kwanza ilikuwa mwezi wa nne mwaka jana kabla ya kulegeza masharti hayo mwezi moja baadae.

Baadhi ya wananchi wasio na kipato waliishi kwa mgao wa chakula kutoka serikali lakini kulikuwa na malalamiko ya njaa.