Uchaguzi Uganda 2021: Upi mustakabali wa Bobi Wine baada ya kushindwa uchaguzi?

mseveni

Chanzo cha picha, Reuters

    • Author, Rashid Abdallah
    • Nafasi, Mchambuzi, Tanzania
  • Iliyochapishwa

Kizazi cha vijana wenye miaka 30 kushuka chini, hakimjui mtawala mwingine katika taifa la Uganda zaidi ya Yoweri Kaguta Museveni ambaye ameliongoza taifa hilo la Afrika Mashariki kwa miaka 35 sasa.

Museveni anaingia katika orodha ya Paul Biya, Rais wa Cameroon, akiwa madarakani tangu Novemba 1982 na Teodoro Obiang Nguema Mbasogo, Rais wa Equatorial Guinea, kakishikilia kiti hicho tangu Agosti 1979. Ni Marais wa Afrika waliopo madarakani kwa muda mrefu sasa. Naye Museveni anaingia mamlakani kwa muhula wa sita baada ya kutangazwa mshindi wa uchaguzi uliomalizika hivi karibuni. Anakishikilia kiti hicho tangu 1986.

Akitangaza matokeo mkuu wa Tume ya Taifa ya Uchaguzi ya Uganda, Simon Mugenyi Byabakama.

Museveni ameshinda uchaguzi wa 14 Januari, 2021, kwa kupata asilimia 58.6 ya kura zote, akifuatiwa na Robert Kyagulanyi, maarufu kama Bobi Wine aliyepata asilimia 34.8.

Katika mataifa ya Afrika Mashariki, upo uraibu wa viongozi kukaa madarakani muda mrefu. Aghlabu hufanyika mabadiliko ya kikatiba ili waendelee kuwepo, na mara nyingi mabadiliko hayo huleta fujo au manung'uniko.

Marehemu Pierre Nkurunziza wa Burundi ni mfano wa watawala hao. Kwa sasa amebaki Paul Kagame wa Rwanda na Yoweri Museveni wa Uganda.

Hawa wawili hakuna ajuaye lini wataviachia viti hivyo, kwa sababu mabadiliko ya kikatiba yanawaruhusu kuendelea kuwepo.

Yapi yametia doa uchaguzi wa Uganda?

Maelezo ya video, Waangalizi wa Afrika Mashariki wasema uchaguzi ulikuwa wa huru na haki

Kundi moja la waangalizi wa uchaguzi lijiitalo EASF kutoka nchi za Afrika Mashariki wameeleza kuwa uchaguzi ulikuwa huru na haki. Ingawa wamekosoa hatua ya kuzimwa kwa huduma ya wavuti.

Bob Wine, mgombea mkuu wa upinzani anasema uchaguzi haukuwa huru na haki. Ameeleza kuwa anao ushahidi wa madai yake na anasuburi muda muafaka ili awaoneshe Waganda kile kilichotokea.

Tukirudi nyuma kuupitia uchaguzi huu, Kulikuwa na kampeni zilizokumbwa na umwagaji wa damu.

Watu wasiopungua 30 waliripotiwa kuuawa katika mji mkuu Kampala, baada ya kutiwa mbaroni kiongozi wa chama cha upinzani cha National Unity Platform (NUP), Robert Kyagulanyi.

Kampeni za uchaguzi uliomalizika, ziligubikwa na kamata kamata ya viongozi wa upinzani na wafuasi wao. Sanjari na kutatizwa kwa shughuli zao za kampeni mara kadhaa na vyombo vya usalama.

Pia Uganda ilifuata nyayo za Tanzania, Ingawa hatua ya Uganda kufunga huduma ya wavuti wakati wa uchaguzi, ilikuwa ni kubwa zaidi ukilinganisha na hatua ya Tanzania kuifungia mitandao ya kijamii katika uchaguzi wake wa Oktoba 2020.

mm

Kupitia ukurasa wake wa Facebook, Bobi Wine ameeleza kwamba nyumba yake imezingirwa na vikosi vya usalama. Huku waandishi wa habari na wanasiasa wa upande wake wakizuiwa kuonana naye.

Mgombea huyo ameendesha kampeni zake kwa kuvaa kizibao na kofia ngumu kwa ajili ya kuzuia risasi.

Baada ya wasindikizaji wake kadhaa kuuwawa. Wine alihofia usalama wake wakati wote akiendesha shughuli za kampeni.

Uhuru wa vyombo vya habari katika kutekeleza majukumu yao umetatizwa mara kadhaa kwa matukio ya waandishi kushambuliwa wakati wakifanya majukumu yao katika kampeni.

Kiasi cha wengine kulazwa hospitali wakiwa katika hali mbaya.

Ugonjwa wa corona ulitumika pia kama silaha dhidi ya harakati za upinzani. Mikusanyiko ya chama tawala yalikuwa halali, lakini baadhi ya mikusanyiko ya upinzani yalikuwa hayaruhusiwi kwa sababu ya corona, Ulikuwa ni undumilakuwili wa wazi wazi.

Linalotia shaka zaidi ni kwamba, uchaguzi wenye mlolongo wa matukio yasiyo rafiki kwa mfumo wa kidemokrasia, yataendelea hadi lini katika taifa lenye miaka 58 tangu kujipatia uhuru kutoka kwa mkoloni?

Kipi kimedhihirika katika uchaguzi huu?

bobi

Bado Uganda kama yalivyo baadhi ya mataifa mengine ya Afrika iko katika demokrasia yenye utata mwingi. Upo uhuru wa watu kuchagua viongozi wao lakini uhuru huo unapita katika misukosuko mingi isiyo ya lazima.

Kinachosemwa na upande wa utawala juu ya uhuru na demokrasia katika siasa, sicho kinachoonekana wakati wa kampeni na uchaguzi. Kuna hadithi tofauti inayoakisi kukosekana usawa kati ya chama tawala na upinzani katika medani ya kisiasa.

Vyombo vya usalama vilidhihirisha kukandamiza upinzani na kusimama na chama tawala. Vilijiingiza katika mizozo kiasi cha baadhi ya maafisa kuonekana katika kamera za wanahabari, wakivutana magwanda wao kwa wao.

Mazingira ya uchaguzi yanaacha swali, kuhusu kilichotangazwa na Tume ya Taifa ya Uchaguzi ya taifa hilo, ndicho kweli kilichoamuliwa na wananchi katika masanduku ya kura!

Lisilohitaji mjadala ni kuwa, Museveni ataiongoza tena Uganda huku kukiwa kumedhihirika kundi kubwa la vijana ambalo halivutiwi tena na utawala wake.

Umasikini na ukosefu wa ajira zikiwa ndizo sababu kuu za kuuchukia utawala huo.

Kipi kifuatacho kwa Bobi Wine?

g

Bobi Wine anayo nafasi ya kwenda mahakamani, ingawa matarajio ya wengi mahakama haitokuja na maamuzi ya kupindua matokeo hayo. Wapo wanaotilia shaka pia, uhuru wa mahakama hiyo.

Kizza Besigye, aliyekuwa mgombea wa Urais katika chaguzi zilizopita. Alikimbilia mahakamani mara kadhaa kupinga ushindi wa Museveni, lakini mahakama haikuwahi kubatilisha kilichohalalishwa na tume.

Kwa kuzingatia historia hiyo, Yoweri Mseveni ana nafasi isiyo na shaka ya kuendelea kuitawala Uganda kwa miaka mengine mitano au zaidi.

Yumkini ndoto ya mpiganaji huyo wa zamani wa msituni mwenye miaka 76, ni kuendelea kuiongoza Uganda hadi pale afya yake itakapo mlazimisha kupumzika au atakapolazimishwa kupumzika.

Bobi Wine bado ana nafasi na muda wa kutosha kuendelea kuwepo katika siasa za Uganda. Ushawishi wake ni mkubwa, na umri unaendelea kumruhusu hata kupambana tena baada ya miaka mitano.

Ingawa kizingiti kikubwa ni kukosekana kwa uwanja safi wa kisiasa hasa kwa upinzani. Na hilo ndilo jambo kubwa anapaswa kulipigania katika hii miaka mitano, kabla ya kurudi tena katika ulingo kupambana na yeyote yule.