Uchaguzi wa Uganda 2021: Ukabila, Jeshi na Siasa za Uganda katika uchaguzi

    • Author, Ezekiel Kamwaga
    • Nafasi, Mchambuzi
  • Iliyochapishwa

Wakati Uganda inapata Uhuru wake mwaka 1962, akili za wakubwa wawili wa serikali mpya zilikuwa zinawaza mambo tofauti kuhusu muundo wa Jeshi la Uganda.

Rais wa kwanza, Edward Mutesa, kutoka kabila la Waganda na Waziri Mkuu wake, Apollo Milton Obote, walikuwa na picha tofauti kuhusu jeshi litalolinda Uhuru wa Uganda mpya.

Wanajeshi wengi walitoka Kaskazini mwa Uganda ambako alikuwa anatoka Obote. Watu wa kabila la Baganda anakotoka Mutesa hawakuwa na mahaba na kazi ya jeshi.

Kwa hiyo, Mutesa alitaka maofisa wa Kiingereza waendelee kubaki - akijua kwamba endapo wataondoka, nafasi zao zitachukuliwa na wanajeshi kutoka Kaskazini; jambo ambalo lingemwongezea nguvu zaidi Waziri Mkuu wakati huo ,Bwana Obote.

Kwa mujibu wa maandishi mbalimbali ya kihistoria, yalipotokea maasi ya wanajeshi ya mwaka 1964 - yaliyotokea pia Tanganyika na Kenya; askari wakidai malipo zaidi na wakitaka wazungu na watu wa rangi nyingine waliokuwa wakipendelewa na wakoloni kuondoka, Mutesa akawa katika wakati mgumu na Obote akatumia mwanya huo kwa faida yake.

Ni maasi hayo ndiyo yaliyokuwa chanzo cha kupandishwa cheo kwa Jenerali Idi Amini ambaye alikuwa kipenzi cha askari enzi hizo.

Ni huyuhuyu Amin ambaye baadaye alikuja kumpindua Obote, wakati alipokuwa rais wa Uganda. Amin naye akaja kupinduliwa na ushirikiano wa wanajeshi wa Tanzania na vikundi vya kijeshi vya Uganda.

Baadaye Uganda ikaja kuongozwa na Tito Okello aliyempindua mtawala wa kiraia, Godfrey Binaisa. Okello alikuja kupinduliwa na Yoweri Museveni kupitia vita vya msituni.

Hii ndiyo historia fupi ya makabila, jeshi na siasa za Uganda. Kujua hapa tulipo sasa, ni muhimu kurejea nyuma zaidi.

Hiba ya Wakoloni

Uganda ina makabila zaidi ya 20. Miongoni mwa makabila hayo, kabila la Baganda ndilo linaloongoza kwa kuwa na watu wengi, wasomi wengi zaidi na matajiri wengi kuliko makabila mengine ya taifa hilo.

Kabila hilo lina misingi yake katikati ya taifa hilo na liko katika eneo lenye rutuba ya kutosha na shughuli nyingi za kiuchumi.

Hata kabla Uganda haijapata Uhuru wake, watu wa kabila la Baganda tayari walikuwa wanamiliki shule, hospitali na taasisi nyingine za huduma za kijamii.

Wakati huohuo, wakati Waingereza wanaitawala Uganda, wakipendelewa sifa kadhaa za aina ya watu waliotaka wawe askari. Sifa kubwa ilikuwa kwenye maumbile na hawakuangalia sana uwezo wa kiakili.

Aina ya maumbile waliyokuwa wakiyapenda Wakoloni yalikuwa zaidi Kaskazini mwa Uganda kwenye makabila kama Langi (la Obote), Acholi na kabila la Lugbara ambako mama mzazi wa Idi Amin alikuwa anatokea.

Ni sawa tu na namna wakoloni haohao walivyofanya Tanganyika kwa kupendelea watu kutoka mkoani Mara kwa sababu za maumbile na ujasiri wao katika nyakati hizo.

Kwa watu wa kabila la Baganda, kazi ya jeshi haikuwa kazi ya heshima wala fahari. Matokeo yake ni kwamba kabila hilo lina ushawishi mdogo sana ndani ya Jeshi la Ulinzi la Wananchi wa Uganda) hata leo. Hilo nalo ni tatizo.

Mara baada ya kumpindua Idi Amin, Museveni alitumia wadhifa wake wa Waziri wa Ulinzi kuingiza jeshini watu wengi kutoka Magharibi mwa Uganda anakotokea yeye. Wengi wao ni wa asili ya Wahima na alijumuisha pia wakimbizi kutoka Rwanda waliokuwa wa kabila la Watutsi, jamii ya Rais Paul Kagame.

Kama Museveni, kiongozi mwenzake wa kijeshi katika umoja wa UNLA, David Oyite Ojok, yeye aliingiza jeshini watu wengi zaidi wa asili ya kabila lake la Acholi.

Mgogoro ndani ya UNLA mwanzoni mwa miaka ya 1980 ulisababisha kutengana kwa Museveni na akina Ojok. Rais huyo wa sasa wa Uganda akalazimika kuingia msituni na jeshi lake la Popular Resistance Army (PRA) lililojaa askari wengi kutoka Magharibi mwa Uganda.

Hata hivyo, hali haikuwa shwari ndani ya majeshi ya serikali. Ingawa wengi wa wanajeshi walikuwa wanatoka Kaskazini mwa Uganda, kulikuwa na upendeleo wa wazi kwa askari wa kabila la Langi - analotoka Obote, huku wale wa Acholi wakipewa vyeo vya chini.

Mgogoro huo wa ndani kwa ndani wa wanajeshi wa serikali, ndiyo ulikuwa chanzo cha kuanguka kwa serikali ya Tito Okello Lutwa , aliye kuwa rais wa Uganda kwa miezi sita tu kuanzia Julai 29, 1985 hadi Januari 26 , 1986 .Mapinduzi hayo yalitokea baada ya kifo cha Mkuu wa Majeshi Ojok; aliyekuwa kipenzi cha askari wengi. Ojok alikufa kwa ajali ya helkopta.

UPDF na Siasa za Uganda

Mara baada ya Museveni kuingia madarakani mwaka 1986, ilionekana wazi kwamba muundo wa jeshi ulibadilika. Vyeo karibu vyote vya juu vilianza kushikiliwa na watu wa asili ya Bahima - si ajabu kwa sababu ndiyo waliomuunga mkono kiongozi huyo tangu alipoanza harakati za kivita.

Museveni alibadilisha jeshi kutoka kuwa NRA lililokuwa jeshi la msituni na kuunda Jeshi la Ulinzi la Wananchi wa Uganda (UPDF). Kimuundo, likifanana sana na jeshi la Tanzania.

Lugha inayotumiwa zaidi na UPDF ni Kiswahili. Nje ya jeshi kiswahili si lugha inayotumika sana .Na miongoni mwa watu wa kabila la Baganda, lugha hiyo inahusishwa moja kwa moja na vitendo vya ukatili walivyowahi kukutana navyo kutoka kwa wanajeshi.

UPDF imejitahidi kuwa jeshi la kizalendo linaloundwa na Waganda wa makabila yote ingawa bado kuna wanaoamini jeshi hilo liko chini ya watu wa asili ya Wahima.

Akiandika katika mtandao wa Twitter, Timothy Kalyegira; mmoja wa wakosoaji wakubwa wa utawala wa Museveni, aliwahi kuhoji ni kwa vipi tangu mwaka 1986, watu wanaopewa wadhifa wa Msemaji wa Jeshi huwa wanatoka upande mmoja wa nchi hiyo - Magharibi.

Pia, kuondoa Jenerali Katumba Wamala na Jenerali Jeje Odongo, karibu wakuu wote wa UPDF wametoka Magharibi mwa Uganda. Wakuu wengine wa UPDF waliopita ni Mugisha Muntu, James Kazini na Aronda Nyakairima. Mkuu wa sasa wa UPDF ni Jenerali David Muhoozi - naye kutoka Magharibi.

Siasa za kijeshi.

Kwa sababu ya historia hii ya Uganda, inaaminika kwamba itakuwa vigumu kwa mrithi wa Museveni - wakati utakapofika, kuwa raia ambaye hajawahi kutumikia jeshi.

Ndiyo sababu, bado kuna shaka kama mgombea wa chama cha upinzani cha National Unity Platform (NUP), Robert Kyagulanyi maarufu kama 'Bobi Wine', ataweza kushinda kwenye uchaguzi wa mwakani dhidi ya Museveni.

Tangu Uhuru wa Uganda, hakuna kiongozi wa kiraia aliyewahi kukabidhi madaraka kwa njia ya kura kumpisha mwenzake. Hakuna pia mtawala wa kijeshi aliyeachia madaraka kwa mwingine kwa hiari yake.

Kwa sababu ya muundo wa sasa wa UPDF ambako wenye ushawishi zaidi wanatoka Magharibi mwa Uganda, faida iko kwa mgombea mwenye sifa mbili; awe askari mashuhuri na pengine awe anatokea upande huo wa nchi.

Ndiyo sababu ni jina moja tu ndilo linatajwa sana kama mtu ambae anayeandaliwa kumrithi Rais Museveni; iwe kwa njia ya kura au hata kwa njia ya kukabidhiwa madaraka.

Mtu huyo anayesemekana kuandaliwa kuwa rais siku za baadae ni Luteni Jenerali Muhoozi Kainerugaba; Mwanae mkubwa Rais Yoweri Kaguta Museveni.