Hii ni tovuti ya maandishi pekee ambayo inatumia data kidogo. Tazama toleo kuu la tovuti likijumuisha picha na video zote.
Pata maelezo zaidi kuhusu toleo hili la linalotumia kiasi kidogo cha data
Uchaguzi Uganda 2021: Mfahamu mgombea pekee mwanamke Nancy Kalembe
- Author, Markus Mpangala
- Nafasi, Mchambuzi, Tanzania
- Iliyochapishwa
Miaka mitano baada ya kuzaliwa Nancy Linda Kalembe ndipo Yoweri Museveni alitwaa uongozi nchini Uganda kutoka msituni akiwa na miaka 42.
Nancy ni mgombea pekee mwanamke anayewania nafasi ya urais akiwa mgombea binafsi.
Kama ilivyokuwa kwa mgombea binafsi mwingine kijana John katumba ndivyo ilivyo kwa Nancy Kalembe mwenye umri wa miaka 40 akiwakilisha vijana wanawake katika taifa hilo wenye nyota hafifu ya kung'ara katika majukwaa ya kisiasa kila unapowadia uchaguzi mkuu.
Duru za kisiasa nchini humo zinaonesha mchuano mkali upo kwa wagombea wawili wenye ushindani mkubwa Yoweri Museveni na Robert Kyagulanyi, lakini kuibuka kwa mgombea mwanamke katikati yao kunafanya kinyang'anyiro hicho kutia fora huku maelfu ya wapigakura wakiwa na hamu na ghamu ya kuamua mshindi siku ya upigaji kura tarehe 14 Januari mwaka 2021.
Je, ni nani huyu Nancy Kalembe?
Kwa mujibu wa mtandao wa gazeti la The Independent limemuelezea Nancy Kalembe kuwa alizaliwa kwa wazazi George Patrick Bageya na Aida Cissy Kubaaza.
Alipata elimu yake hadi kidato cha nne St. Mary's College na kidato cha tano na sita alisoma shule ya Juu ya Mariam.
Shahada ya kwanza alihitimu katika Chuo Kikuu Makerere mwaka 2007.
Awali mwaka 2003 alishiriki mashindano ya urembo, baadaye aliajiriwa na kituo cha redio Sanyu F.M. Januari 8, mwaka 2008 alishiriki kipindi cha runinga cha Apprentice Africa kilichoongozwa na Donald Trump na kushika nafasi ya sita kati ya washiriki 16.
Kipindi hicho kilifungulia njia ya kupata ajira katika Benki ya PHP nchini Nigeria.
Mwaka 2009 alirudi Uganda kufanya kazi na Benki ya Orient hadi alipojiuzulu mwaka 2010 ili kusimamia biashara zake ikiwemo kampuni ya kufanya usafi ya Mbalimbali Limited iliyoweka makao yake huko Nakawa. Amewahi kufanya kazi katika televisheni ya UTV na Shirika la mawasiliano la Uganda.
Mgombea huyo ana sera zipi kwa wapigakura?
Anasisitiza uongozi wa kulinda maadili, kuzalisha ajira kwa vijana, huduma bora za afya kwa wananchi wote, kuboresha mitaala ya elimu, kuboresha sekta ya michezo, kupinga ubaguzi miongoni mwa watoto na watu, kufanya mabadiliko ya mifumo ya vyombo vya dola, kuimarisha umoja wa kitaifa,kulinda uchumi na wawekezaji na kudhibiti ushawishi wa vyombo vya habari vya nje.
Hivi karibuni gazeti la New Vision lilieleza kuwa mgombea huyo alifanya tukio la kipekee kwa kufanya kampeni katika jukwaa moja na wagombea chama cha NUP katika Kata ya Goma Manispaa ya Mukono.
Wagombea hao wa nafasi tofauti alioshirikiana nao ni Mchungaji Peter Bakaluba Mukasa, Hanifer Nabukeera na Betty Nambooze.
Akiwa katika mkutano huo aliwaambia wafuasi wa Bob Wine kuwa hana tatizo na mgombea mwenzake huyo kwa sababu wote wanapigania jambo moja la ustawi wa wananchi na taifa.
Je, 'Mission 56' ni nini?
Ni kauli mbiu ya ilani anayotumia kuwasiliana na wapigakura kote nchini humo. Mission 56 ina maana ya makabila 56 yaliyoko nchini Uganda.
Mission 56 imekusudia kuwaunganisha Waganda bila kujali itikadi zao za kisiasa, na haki sawa kwa wananchi wa makabila yote nchini humo na kuwafanya wafanye kazi pamoja.
Katika kauli mbiu hiyo lipo neno la nyongeza, "Leaving No One Behind", kwamba hakuna atakayeachwa nyuma.
Akizungumza na mwandishi wa makala haya kwa njia ya simu kutoka jijini Kampala mgombea huyo anafafanua sera yake kuwa inalenga kujenga msingi wa umoja miongoni mwa raia wa Uganda.
Anasema akishinda urais suala la umoja litakuwa ajenda nyeti, hivyo kuomba Waganda kuwa naye bega kwa bega.
"Tupo makabila 56 hapa Uganda lakini kwa miaka mingi hatuna umoja. Kwanza zama za ukoloni ziliweka mipaka na kutugawa kijiografia, na kisha tugawanywa kwa misingi ya dini na itikadi za siasa. Masuala ya rasilimali, uongozi na maendeleo vikawa vitu adimu katika makabila yetu na kuendelea kufukarisha watu wetu.
Mipango niliyonayo sasa ni kuhakikisha makabila yote 56 yanasimamia ajenda na mwelekeo mmoja wa kitaifa,kuzikubali tofauti zetu kiitikadi na dini kwa madhumuni ya kuchochea maendeleo ya taifa. Tofauti hizo zisiwe kikwazo cha umoja wetu na kufaidi rasilimali zetu bila ubaguzi,"
Aidha, anasema kampeni zake zilizinduliwa katika uwanja wa Kakiundu jijini Jinja mnamo Novemba 12 mwaka huu wa 2020, kisha akaelekea miji mingine, ambapo anatarajia kufunga kampeni hizo ifikapo Januari 12 mwaka 2021 jijini Jinja nchini humo.
Nani anafadhili kampeni zake?
Anasema kuwa bajeti za kampeni zake zinatokana na michango ya hali na mali kutoka kwa wafuasi,wadau na wapenzi wa mabadiliko ya kisiasa nchini humo.
Hivyo basi kama walivyo wengine naye amekuwa akitoa matangazo kupitia kurasa zake za mitandao ya kijamii kuomba michango ya hali na mali kwa ajili ya kuendesha kampeni zake.
Wachangiaji wanatakiwa kuchangia kwa njia ya akaunti ya benki au simu ya mikononi. Ikumbukwe harambee ni miongoni mwa vitu muhimu kwa mgombea bila kujali mgombea binafsi au anatoka chama cha siasa.
Nafasi za wanawake katika jumuiya
Wakati Tanzania ikifanya uchaguzi wake Oktoba 28 mwaka 2020 ilikuwa na wagombea wawili kati ya 15 wanawake katika nafasi ya urais, Queen Cathbert Sendinga wa chama ADC na Cecilia Augustiono Mwanga kutoka chama cha Demokrasia Makini.
Upande wao Kenya jumla ya wagombea 8 walichuana katika uchaguzi wa mwaka 2017 nchini, lakini hakukuwa na mgombea mwanamke. Mataifa ya Afrika mashariki kama yalivyo mengine ya bara la Afrika ni nadra kwa wanawake kugombea ama kutia nia kwa nafasi za juu za uongozi.
Matarajio ya nchi za kusini mwa Jangwa Sahara ni kuhakikisha usawa katika vyombo vya uamuzi na ushiriki kwenye masuala ya uendeshaji jamii na taifa kwa ujumla. Umoja wa Afrika unasisitiza ajenda ya hiyo na kwamba ifikapo mwaka 2050 bara la Afrika liwe na limepiga hatua kubwa kwenye suala la haki sawa.
Uganda inaonekana kuwa nyuma kwenye ushiriki wa demokrasia, kujitokeza mwanamke mmoja kuwania nafasi ya urais akiwa mgombea binafsi huku vyama karibu vyote vikiwa na wagombea wanaume ni ishara ya suala la jinsia kupigwa teke, licha ya matumaini yaliyopo siku zijazo.
Ingawa matumaini yangalipo kuwainua wanawake, lakini wanasisitizwe na kushiriki kwenye vyombo vya uamuzi na siasa za ushindani kuliko kusubiri nafasi za kuteuliwa.