Hii ni tovuti ya maandishi pekee ambayo inatumia data kidogo. Tazama toleo kuu la tovuti likijumuisha picha na video zote.
Pata maelezo zaidi kuhusu toleo hili la linalotumia kiasi kidogo cha data
Fedha za msaada wa corona Tanzania zazua mjadala Bunge la Ulaya
Msaada wa Euro Milioni 27 ambao Tanzania ilipokea mapema mwaka huu kutoka Umoja wa Ulaya (EU) kukabiliana na athari za corona umezua mjadala katika Bunge la Umoja huo.
Mwenyekiti wa Kamati ya Mambo ya Nje wa Bunge hilo Dkt David McAllisster alihoji ni vigezo gani vilitumiwa na uongozi wa EU kutoa msaada kwa Tanzania ambayo ameituhumu kwa kutokuwa wazi juu ya taarifa za corona na kutofuata miongozo ya Shirika la Afya Duniani (WHO).
"Ninapata wakati mgumu kwamba tunatoa fedha kwa Tanzania ambayo haifuati kanuni za WHO, serikali haina ushirikiano...
Nataka kujua vigezo na taratibu zilizotumika kutoa fedha, kufanya nini na zimetumikaje?" alieleza Dk McAllister ambaye alitoa saa 48 (kuanzia jana asubuhi) kupata majibu kutoka kwa maafisa wa EU.
Mwenyekiti huyo pia aligusia juu ya kuminywa kwa haki za binadamu na kutaka EU na washirika wake wahakikishe watetezi wa haki za binadamu wanalindwa Tanzania.
Baadhi ya mitandao nchini Tanzania iliripoti juu ya tukio hilo na kudai kuwa Bunge la EU limepitisha azimio la kuiwekea vikwazo Tanzania, taarifa ambazo zimekanushwa na serikali ya Tanzania.
Taarifa juu ya msaada huo awali zilitolewa Septemba 14 na Wizara ya Mambo ya Nje ya Tanzania.
Taarifa hiyo ilimnukuu Rais wa Baraza la EU Bw. Charles Michel akisema kuwa msaada huo unalenga kujenga miundombinu ya maji na umeme kwenye zahanati na hospitali za serikali.
"Umoja wa Ulaya umesema uko tayari kutoa kiasi cha Euro milioni 27 sawa na takriban shilingi bilioni 70 za Tanzania kwa lengo la kusaidia mipango ya kukabiliana na janga la Covid 19 na madhara yake ya kiuchumi"
Nia ya msaada huu wa Umoja wa Ulaya ulikuja wakati Tanzania ikiwa imekwisha tangaza kumalizika kwa ugonjwa wa Corona nchini humo.
Katika mkutano wa kampeni za uchaguzi, Rais wa Tanzania John Pombe Magufuli alisema kuwa shetani alitaka kuitawala dunia kupitia virusi vya corona lakini hana nafasi nchini Tanzania.
Magufuli alisema kuwa ''haiwezekani kwa uchumi wa dunia kufungwa kwasababu ya ugonjwa''
Akizungumza katika mkutano huo Chato Geita, Magufuli alisema, bahati nzuri, serikali yake haikukubali shinikizo la kufunga shughuli za kiuchumi na kukaa nyumbani ''lockdown''.
Tanzania inasemaje taarifa hii
Balozi wa Tanzania nchini Ubelgiji na EU Jestus Nyamanga amekanusha vikali juu ya ripoti za kupitishwa kwa azimio la Bunge la EU dhidi ya Tanzania.
Ameeleza kuwa kikao kilichoketi kilikuwa cha Kamati ya Mambo ya Nje na si Bunge lote.
"Umoja wa Ulaya haujasitisha misaada ya mikopo Tanzania"