Mchakato na kura ya maamuzi kuhusu BBI unamweka Naibu Rais Ruto kwenye njia panda

Rutto
    • Author, Hezron Mogambi
    • Nafasi, Mhadhiri, Chuo Kikuu cha Nairobi
  • Iliyochapishwa

Naibu Rais wa Kenya, William Ruto amejikuta katika hali ngumu ya kisiasa kuhusiana na mchakato na kura ya maamuzi inayotarajiwa mwaka ujao kuhusu ripoti ya Mpango wa Maridhiano (BBI) inayolenga kuleta mageuzi ya kikatiba, huku uhusiano wake na Rais Uhuru Kenyatta na kiongozi wa upinzani, Raila Odinga ukiwa njia panda.

Hali anamojikuta Bw Ruto kwa sasa inatokana na hali na mjadala kuhusu marekebisho ya katiba na kile kinachoonekana kama hali iliyotokea mwaka wa 2010 wakati kulipokuwepo na kura ya maamuzi kuhusu katiba ambapo kulikuwepo na kundi na "ndio" na lingine la "hapana".

Makundi mawili pinzani kuhusu BBI

Tayari, kama inavyoonekana, kuna makundi mawili: moja linalohodhi na kudai kusimamia na kuongoza utaratibu wa marekebisho ya katiba na lingine linaloonekana kupinga na kutaka kuwekwa wazi kwa utaratibu wenyewe ili maoni zaidi ya Wakenya yajumuishwe kwenye ripoti ya jopo lililojulikana kama Building Bridges Initiative (BBI).

Jopo hilo lililoundwa na Rais Uhuru Kenyatta na kiongozi wa upinzani Raila Odinga mnamo Machi 2018, lilipaswa kuangazia masuala tisa yakiwemo ukabila, ufisadi na ugatuzi - ikiwa ni miongoni mwa changamoto kuu tangu Kenya kupata uhuru mwaka wa 1963.

Inayoonekana kwa sasa, makundi haya mawili yanajitayarisha kwa mapambano katika kile kinaoonekana kuwa mchuano mkali wa kisiasa wa mwaka ujao.

Ni juma hili tu ambapo kiongozi wa chama cha ODM Raila Odinga aliwasuta kwa maneno makali wale wanaoonekana kupinga ripoti ya BBI kuhusiana na mabadiliko ya kikatiba nchini Kenya.

Huku naibu rais William Ruto, kiongozi wa chama cha Amani National Congress (ANC) Musalia Mudavadi, baadhi ya viongozi wa makanisa, wawakilishi kaunti, magavana na wawakilishi wa makundi mbali mbali wakiwarai viongozi wakuu wa mchakato wa BBI, Rais Uhuru Kenyatta na Raila Odinga, kukubali ripoti ya BBI kufanyiwa marekebisho ya mwisho kabla ya kura ya maamuzi ambayo imepangwa kufanywa mnamo Juni mwaka ujao, kile kinachojitokeza ni kuwa kuna masuala yanayoleta utata kati ya pande mbili husika.

Anayoyapinga Ruto Kwenye BBI

Kenya

Chanzo cha picha, AFP

Hata hivyo, Rais Uhuru Kenyatta na kiongozi wa upinzani Raila Odinga wamekuwa wakishikilia kuwa kutayarishwa kwa ripoti hiyo kumechukua muda wa miaka miwili na kuwa, muda umeyoyoma kwa sasa kwani ripoti imefikia kikomo kutayarishwa kwa kura ya maamuzi wala si maoni zaidi.

Itakumbukwa kwamba katika tangu kuanzishwa kwa jopo la BBI, naibu Rais William Ruto amekuwa akionyesha kupinga shughuli nzima ya jopo hilo.

Wadadisi wengi nchini Kenya wamekuwa wakisema kwamba Bw. Ruto hajakuwa akiunga mkono shughuli au hata ajenda ya jopo hilo wala mapendekezo ya jopo lenyewe.

Hii ndiyo sababu, wakati wa uzinduzi wa awamu ya kwanza wa ripoti ya BBI uliofanyika katika ukumbi huo mnamo Novemba mwaka jana, Bw Ruto alihudhuria japo alionekana kukerwa na kutotosheka na shughuli nzima ya mchakato huo.

Kudhibitisha haya, wakati wa uzinduzi wa ripoti yenyewe mwezi uliopita katika ukumbi wa Bomas jijini Nairobi, akizingumza mbele ya Rais Uhuru Kenyatta na mshirika wake katika mchakato huo Raila Odinga, Dkt Ruto alikosoa baadhi ya mapendekezo ya jopo la BBI yakiwemo kubadilisha Tume Huru ya Uchaguzi (IEBC), pendekezo la kubuni wadhifa wa afisa wa kupokea malalamishi katika Idara ya Mahakama atakayeteuliwa na rais, hatua za kupokonya Seneti jukumu la kuamua mgao kwa kaunti, pendekezo la kubuniwa kwa Baraza la Polisi litakalosimamiwa na waziri wa usalama wa ndani na hatua ya kubuni nyadhifa za waziri mkuu na manaibu wake.

Pia, alikosoa pendekezo la kuunga mkono baadhi ya mapendekezo, akisema yanaweza kutumiwa kuwadhulumu wale wanaoyashinikiza.

bb

Dkt Ruto alitaja hatua ya kubuni wadhifa wa afisa wa kupokea malalamishi kuhusu mahakama kama itakayopokonya idara hiyo uhuru wake na kuifanya ithibitiwe na serikali kuu.

Alieleza kuwa mahakama inafaa kutengewa pesa zaidi kujenga korti nchini ili kuimarisha utoaji wa haki kwa Wakenya.

Kinachobainika kwa sasa ni kuwa kiongozi wa upinzani Raila Odinga na naibu Rais William Ruto huenda wakawa kwenye pande mbili tofauti kuhusiana na suala BBI na labda, uchaguzi mkuu wa mwakwa wa 2022.

Kwa Raila, ripoti ya BBI na kura ya maamuzi itampa nafasi nzuri ya kurudi kwa kishindo kwa shughuli za kisiasa baada ya kushindwa mara nne katika chaguzi za awali pamoja na uchaguzi wa mwaka 2017, matokeo ambayo aliyapinga mahakamani.

Kwa upande mwingine, labda, utakuwa wakati mzuri kwa William Ruto kuondoka kwenye upande wa serikali na kurudia alichokifanya kwenye kura ya maamuzi ya mwaka wa 2010, ambapo alijijengea jina kwa kupinga katiba ya mwaka wa 2010.

Kwa misingi hii, shughuli nzima ya BBI inaonekana kuwa na sifa kubwa sana za kisiasa na kushiriki au kutoshiriki pamoja na matokeo yake kwa wanasiasa wakuu nchini Kenya kuna umuhimu wake kwa uchaguzi wa mwaka wa 2022.

Hii ndio sababu kuna vuta nikuvute kuhusiana na shughuli nzima za mchakato wa BBI.

Hili lina msingi wake kwenye kampeini za BBI ambazo zinatoa nafasi mwafaka kwa wanasiasa wawili wenye ushawishi mkubwa nchini Kenya kuonyesha ni nani mwenye ushawishi zaidi na ni nani hafifu kisiasa. Hivyo ripoti ya BBI itasaidia pande zote-upande wa Rais Uhuru Kenyatta na Raila na upande ule mwingine- ule wa Ruto- kujipima kuhusiana na uchaguzi wa mwaka wa 2022.

Walakini kwa kambi ya Ruto

bbi

Wandani wa naibu Rais wakiwemo Seneta wa Elgeyo Marakwet, Bw Kipchumba Murkomen, Seneta wa Nakuru, Bi Susan Kihika, Mbunge wa Soy, Caleb Kositany, Mbunge wa Kikuyu Kimani Ichungwah na wengineo wameshikilia kuwa watapinga mswada huo wa BBI iwapo marekebishio wanayopendekeza hayatatiliwa maanani.

Aidha, wamekuwa wakidai kwamba mabadiliko kwa katiba kwa sasa si jambo muhimu huku wakisisitiza kwamba masuala ya Covid-19 na uchumi uliodorora yanafaa kupewa kipaumbele nchini Kenya kwa sasa.

Hata ingawa akionekana kutopendezwa na shughuli nzima ya mchakato wa BBI na kura ya maamuzi itakayoandaliwa, kinachomtatiza Bw. William Ruto ni uwezekano wa kushiriki kwenye kampeni mbili za kisiasa; ya kura ya maamuzi kuhusu marekebisho ya katiba na baada ya hapo, uchaguzi Mkuu wa 2022.

Katika siku za hivi karibuni, Bw. Ruto amekuwa akionyesha wazi kwamba huenda asiwe kwenye kundi litakalopinga mabadiliko ya katiba kwa sababu, kulingana na wandani wake na wachanganuzi wengine, hatua kama hiyo inaweza kutatiza lengo lake kwenye uchaguzi wa mwaka wa 2022.

Njia hii panda ya kisiasa imemletea Bw. Ruto mkwaruzo wa mawazo. Lakini Bw. Ruto ameamuaje kuhusu suala hili?

Kulingana na duru za kuaminika, Bw. Ruto anapanga kuendelea na mipango na miradi yake kwenye sehemu mbali mbali nchini Kenya ambayo inayonuiwa kumchora kama mwanasiasa anayewajali wananchi wa kawaida na maskini huku akiendeleza azma yake ya kuwania Urais mwaka wa 2022.

Jambo hili linatokana na ukweli kwamba kushiriki kwake kamili kwenye kampeini ya kupinga ripoti ya BBI huenda iwe kikwazo kwake katika harakati za kujipigia debe na kuwania umaarufu kwenye uchaguzi wa 2022.

Maelezo ya sauti, Je ripoti ya BBI ndio suluhisho la amani na umoja wa kudumu Kenya

"Ni wazi kwetu kwamba yeyote ambaye ana wazo tofauti na yale yaliyo kwenye ripoti ya BBI ambayo yanaweza kuboresha ripoti hiyo sasa anaambiwa kwenda kwenye kundi la "la" ama wanaopinga.Mbona mnataka kulazimisha watu kwenda upande huo ilhali tunaweza kuungana sote kwa maelewano na kuunda nchi yenye umoja?"aliuliza wiki hii alipokutana na wawakilishi wodi kutoka Kaunti ya Wajir huku akieleza kwamba hali iliyoko ni mtego kwake na amefahamu hilo.

Kura ya maamuzi ni "uchaguzi wa mapema"

Seneta wa Bomet Christopher Lang'at aliwashtumu wale wanaopinga kuongezwa kwa mabadiliko kwa ripoti ya BBI kwa kuwa na njama ya "uchaguzi wa mapema" ili kutathmini umaarufu wa Bw Ruto, jambo ambalo "tumelikatalia mbali".

Wanasiasa wengi wakuu wanaomuunga mkono Bw. Ruto wanakubaliana kwamba hakuna haja ya kushiriki kwenye kampeini ya kupinga ripoti ya BBI huku mbunge wa Kimilili Didmus Barasa na mwenzake wa Keiyo Kusini Daniel Rono wakisema hakuna haja ya kupoteza pesa nyingi kupinga ripoti ya BBI ilhali lengo lao ni uchaguzi wa 2022.

Pamoja na walakini huu kwenye kambi ya Bw. Ruto, kuna masuala fulani ambayo ni vivutio kwa wadau wa sekta mbali mbali ambayo huenda yakawafanya Wakenya kuipigia kura ripoti ya BBI, jambo ambalo kambi ya Ruto haitaki kutathmini wakati huu.

Haya ni pamoja na kuongezwa kwa fedha zinazotolewa kwa serikali za kaunti kutoka asilimia 15 ya sasa hadi asilimia 35, kubuniwa kwa hazina ya ustawishaji wa Wadi, vijana wanaoanzisha biashara kupata afua ya kutolipa ushuru kwa kipindi cha miaka saba, nafuu kwa vijana walionufaika na fedha kutoka kwa Bodi ya Mikopo ya Elimu ya Vyuoni (HELB) kuongezewa muda wa kuanza kulipa kwa miaka minne baada ya kuhitimu,

Ili kuwavutia wanawake, ripoti ya BBI na mswada wake unapendekeza kuwa kila kaunti itawachagua maseneta wawili; mwanamke na mwanaume. Suala hili bado linatatiza wadau wengi na inasemekana linashughulikiwa ili kuhakikisha suala la jinsia katika bunge la kitaifa na seneti linashughulikiwa ipasavyo.

IKULU

Chanzo cha picha, IKULU KENYA

Rais Uhuru Kenyatta na Bw Odinga wamekuwa wakipigia debe BBI huku Bw Odinga akisisitiza kuwa mchakato wa kukusanya saini milioni moja za raia utaanza rasmi wiki hii licha ya pingamizi kutoka kwa baadhi ya viongozi wanaotaka pawepo mazungumzo kwanza.

Hata hivyo, Dkt Ruto anasisitiza kuwa taifa litapoteza umoja wake iwapo wanasiasa watagawanyika katika mirengo ya 'Ndiyo' na 'La' ilhali bado kuna muda wa kuhakikisha pande zote zinakubaliana kuhusu yaliyomo kwenye BBI.

Amekuwa akishikilia kwamba licha ya kamati ya BBI kuchukua muda wa miaka miwili kuiandaa, ripoti hiyo haiwezi kupigiwa kura jinsi ilivyo kutokana na masuala mengi ndani yake yanayokinzana.

Aidha, alishikilia kuwa atawaongoza wafuasi wake kuunga BBI iwapo marekebisho yanayohimizwa na kwamba maoni ya mashirika mbalimbali yatajumuishwa katika ripoti hiyo.

Hata hivyo, pendekezo hili limetupiliwa mbali na Raila Odinga akisema muda tayari umepita kwa shughuli kama hiyo. Ilivyo, hali ni tete.

Linalobainika kwenye vuta nikuvute kwenye mchakato wa ripoti ya jopo la BBI ni kuwa siasa za uchaguzi wa mwaka wa 2022 zimezama kwenye mchakato mzima.

Pande zinazohusika zinapania kutumia mchakato mzima kujipigia debe na kujipa umaarufu kuelekea mwaka wa 2022.