Hii ni tovuti ya maandishi pekee ambayo inatumia data kidogo. Tazama toleo kuu la tovuti likijumuisha picha na video zote.
Pata maelezo zaidi kuhusu toleo hili la linalotumia kiasi kidogo cha data
Sanaa ya Mashairi yavuma Mombasa
Sauti tamu za watoto ndizo zinazokukaribisha katika kijiji cha Ujamaa, eneo bunge la Likoni, Mombasa, Kenya
Wakati huu ambapo janga la Corona limerindima na kulazimu shule kufungwa nchini Kenya, watoto hao wananoa makali yao katika sanaa hii ya Kiswahili.
Hili ni wazo la Hamisi Mwagarashi, mshairi mahiri wa Mombasa ambaye anasema kwamba amewaleta pamoja watoto hao ili kuhakikisha kwamba wanakuza vipaji vyao, lakini pia hawajihusishi na tabia potofu wakati huu ambapo shule zimefungwa.
'Watoto hawa wako hapa kwa lengo la kusoma. Wazo hili lilinijia baada ya mimi kupitia changamoto kadhaa maishani, kisha nikajiuliza kama kesho sitakuwepo nani atakayeendeleza sanaa hii ya kughani mashairi?' anauliza Mwagarashi.
Ushairi ni utungo wa kisanaa unaotumia lugha teule na mpangilio fulani wa maneno badala ya kutumia lugha natharia au lugha mfululizo.
Aidha ushairi unaweza pia kutajwa kama kipera cha fasihi simulizi (au nyimbo) na pia katika fasihi andishi kwa sababu mashairi yanaweza kuwasilishwa kwa njia ya kukariri na pia kwa njia ya maandishi. Mashairi yanayoghanwa badala ya kuimbwa huitwa maghani.
Mmoja wa wanafunzi hapa ni Hassani Iddi Chano mwenye umri wa miaka 11 ambaye amepata umaarufu mkubwa mitandaoni baada ya video zake za mashairi kusambaa.
'Mimi nilipomsikia Mwagarashi akiimba mara ya kwanza nilimwambia nataka anifunze. Na mimi sasa nafurahia sana kughani mashairi.'
Lakini umaarufu wa sanaa hii umepungua katika siku za hivi karibuni, kama anavyoeleza Mwagarashi.
'Wale waliowania mashairi na kuweza kutambulika kishairi, hawajafika popote, wala hawakufanyiwa chochote cha maana.
Wamekufa wakiishi kwa nyumba za nyasi, wengine wakilala kwa nyumba za kuku. Sasa washairi wa sasa wameona hakuna faida bali ni hasara tupu.'
Hata hivyo, licha ya taswira hiyo, mwalimu huyu wa Kiswahili anasisitiza kwamba mashairi ni ajira na sanaa hiyo inapaswa kupewa kipaumbele.
Matamshi yake yanaungwa mkono na Mwalimu Mathias Momanyi, mtaalam wa Kiswahili kutoka Nairobi Kenya.
'Mashairi huelimisha, hukosoa, hurekebisha jamii, hususan jamii inapoelekea kupotoka. Lakini sasa hivi kuna uhaba mkubwa wa malenga na washairi wanaoweza kuzungumzia madhila katika jamii yetu.'
Sasa nini kinapaswa kufanywa ili kuhakikisha kwamba sanaa hii ya tangu jadi haitokomei kabisa?
Wasomi wa Kiswahili wanasisitiza ushairi kupewa uzito katika mtaala wa masomo shuleni. Na pia wazazi kuwahimiza watoto wao wenye vipaji vya utunzi na uimbaji wa mashairi kuzingatia kukuza vipaji hivyo.
'Shule zinapaswa kuwa na kitengo maalum cha mashairi kama vile kuna vitengo vya michezo ya Karate, ama Uogeleaji mashuleni.
Hiyo itasaidia katika kukuza vipaji vya watoto ambao wanaipenda sanaa hii ya kughani mashairi,' anasema Bi Fatma Alfan, ambaye watoto wake watatu ni wanafunzi wa kughani mashairi.
Basi wakati wasomi na wataalamu wa elimu wakijikita katika kuhakikisha elimu ya sasa ni yenye manufaa kwa kizazi kijacho, hapa Ujamaa katika eneo bunge la Likoni, Mombasa Kenya, Hamisi Mwagarashi anajitahidi kukuza kizazi chenye sanaa na vipaji, kwa shairi moja kila siku.