Coronavirus: Hoteli zafungwa Zanzibar, Pigo Kubwa Sekta ya Utalii

Janga la Coronavirus limesababisha kutokuwepo kwa wageni Zanzibar
Maelezo ya picha, Janga la Coronavirus limesababisha kutokuwepo kwa wageni Zanzibar
    • Author, Na Sammy Awami
    • Nafasi, BBC News Swahili
  • Iliyochapishwa

Asilimia 95 ya hoteli za kitalii visiwani Zanzibar zimefungwa na asilimia tano zilizobaki zinatarajiwa kufungwa ifikapo mwishoni mwa wiki ijayo.

Sekta ya Utalii Zanzibar ni moja ya nguzo kuu za uchumi wa visiwa hivyo na Tanzania kwa ujumla, lakini tangu mlipuko wa coronavirus ulipoibuka mambo yamebadilika.

Hassan Omar (34) amekuwa katika sekta ya utalii kwa zaidi ya miaka kumi lakini hajawahi kushuhudia kuyumba kwa sekta hiyo visiwani Zanzibar kama ilivyo hivi sasa.

"Ni kweli kwamba janga hili la Corona limetokea wakati wa msimu wa watalii wachache, lakini hakuna aliyetarajia kwamba watalii visiwani hapa hawataonekana kiasi hichi," anasema Hassan Omar, mfanyakazi katika hoteli ya Shangani.

Jengo la Old Trafford Zanzibar ni moja ya maeneo ya utalii ambayo huenda yasitembelewe na wageni kama kawaida kutokana na janga la coronavirus
Maelezo ya picha, Jengo la Old Trafford Zanzibar ni moja ya maeneo ya utalii ambayo huenda yasitembelewe na wageni kama kawaida kutokana na janga la coronavirus

Hiyo ni kwa mujibu wa Waziri wa Utalii visiwani humo Mohamoud Thabit aliyewaambia waandishi wa habari mwishoni mwa juma kuwa watalii waliokuwa wamebaki visiwani humo ni 506 tu ambao nao walikuwa wanasubiri kuchukuliwa na ndege siku ya jumamosi na jumapili wiki hii.

Hali hii ya kutokuwepo kwa wageni ni sehemu ya madhara ambayo ugonjwa wa Coronavirus umesababisha. Baadhi ya nchi zimepiga marufuku safari za ndege kutoka nchi zilizoathiriwa zaidi na Coronavirus, nchi nyingi zimewataka wananchi kubaki nchini mwao, huku mahali pengine wananchi wamezuiliwa hata kutoka nyumbani kwao.

Maelezo ya video, Coronavirus: Utajuaje kuwa umeathirika na virusi?

Hii imepelekea madhara makubwa kiuchumi hasa katika nchi zinazotegemea sekta ya utalii, kama Zanzibar, kwani hakuna tena mzunguko wa wageni.

Hadi hivi sasa, Zanzibar imetangaza kuwepo kwa mgonjwa mmoja tu wa Coronavirus. Mgonjwa huyo ni raia wa Ghana aliyeingia visiwani humo akitokea Ujerumani.

Kama sehemu ya kudhibiti kusambaa zaidi kwa virusi vya Corona, mamlaka nchini visiwani Zanzibar ilizuia ndege ndogo kutoka Italia na kuweka upimaji wa joto bandarini na uwanja wa ndege kuhakikisha kila anayeingia visiwani humo hana maambukizi ya ugonjwa huo.

Unaweza pia kusoma:

Taarifa kutoka ofisi ya Makamu wa Rais Zanzibar ilitanga hatua zingine za ziada ikiwa ni pamoja na wageni wote na wenyeji watakaoingiua Zanzibar kutengwa
Maelezo ya picha, Taarifa kutoka ofisi ya Makamu wa Rais Zanzibar ilitanga hatua zingine za ziada ikiwa ni pamoja na wageni wote na wenyeji watakaoingiua Zanzibar kutengwa

Leo hii, taarifa kutoka ofisi ya Makamu wa Rais Zanzibar ilitanga hatua zingine za ziada ikiwa ni pamoja na wageni wote na wenyeji watakaoingiua Zanzibar kutengwa katika vituo maalum kwa muda wa siku 14 kwa gharama zao wenyewe chini ya utaratibu maalum ulioandaliwa na Wizara ya Afya.

Wakati hatua kama hizi zinasaidia kuzuia kusambaa kwa maambukizi ya Corona, kwa upande mwingine zinazuia watalii kuingia visiwani humo na kufanya hoteli na biashara zingine zinazotegemea utalii kuathirika kwa kiasi kikubwa.

"Kwetu sisi hapa Shangani wateja watalii wa mwisho walikuwa siku ya Jumanne. Hadi hii leo hatujapokea mgeni yeyote yule, na wale waliokuwa wameweka ahadi ya kuja wameahirisha safari yao. Kiukweli hata hatujui tena ni lini tutapata wageni watalii. Hakuna anayejua hili gonjwa litaisha lini" amesema Omar.

Unaweza pia kutazama:

Maelezo ya video, Serikali ya Tanzania yafunga shule zote nchini kuzuia maambukizi ya virusi vya corona

Kwa wafanyakazi kama Omar, baba mwenye mke na watoto wanne, kuyumba kwa biashara kama hivi maana yake hali ngumu ya kifedha kwa yeye na familia yake.

Baadhi ya wamiliki wa hoteli ambazo zimefungwa visiwani Zanzibar wamelazimika kuwapa likizo ya bila malipo wafanyakazi wao huku hoteli zingine zikiwapa nusu mshahara watumishi wao.

"Maisha lazima yaendelee, huwezi kukata tamaa tu. Lakini wengi wetu inabidi tuanze kufikiria namna ya kupata kipato kupitia aina nyingine ya ajira, ambayo hadi sasa bado sijaipata, lakini bado naendelea kufikiria," amesema Omar

Pigo hili kwa sekta ya utalii haliumizi wamiliki na wafanyakazi wa hoteli na wengine waliomo katika sekta hii, lakini hata serikali ya Zanzibar pia kwa ujumla.

Kwa mujibu wa baadhi ya takwimu, zaidi ya asilimia 60 ya fedha za kigeni na bajeti kuu ya Zanzibar inategemea sekta ya utalii.

Jinsi nchi za Africazinavyokabiliana na coronavirus