'Mume wangu alinitoroka na kunitapeli mali ya mamilioni ya fedha niliyowekeza'

    • Author, Anne Ngugi
    • Nafasi, BBC Swahili
  • Iliyochapishwa

Mary Miriti ana miaka 32 ni Mama wa watoto wawili akitokea Nairobi Kenya na kama wanawake wengine alitamani kuwa na mume na pia watoto ili kutimiza baadhi ya malengo yake kama binadamu yeyote .

Mary Miriti alizaliwa kaunti ya Meru nchini Kenya ,alipokuwa chuo kikuu alikutana na mwanamume mmoja ambaye walianza urafiki naye . wakati huo urafiki wao ulikuwa tu wa kawaida haukuwa wa kimapenzi ,ni hadi mwaka wa 2010 ambapo wote wawili hao waliamua waanze kuishi pamoja kama wapenzi au mume na mke . Lakini cha ajabu ni kuwa mary anasema ;

" Mpenzi wangu alihamia kwangu , na wala sio mimi nilihamia kwake , kutokana na kuwa yeye hakuwa na chochote , ila mimi nilikuwa na vitu vya nyumba kama kitanda na hata vitu vya kutumia " aliongeza Mary.

Mary anasema kuwa mpenzi wake alikuwa hana chochote katika nyumba yake na kwa kuwa walikuwa wamependana sana walikubaliana yeye (mume) ahamie kwake Mary.

Wakati huo kibarua chake mary kilikuwa kinamlipa karibia 13000/- shilingi za kenya ilhali mume wake alikuwa na kibarua kilichokuwa kinampa 15000/- shilingi za kenya , hii ni kama dola kumi na mbili na tano mtawalia .

Mary anasema kuwa alitoa wazo la kuwa yeye achukue mkopo katika benki kwa lengo la kuanza biashara ya kuuza vyombo ambavyo vimetumiwa iweni ngup aui vyombo vya nyumba

"nilitamani tuanze biashara pamoja ili tujijenge kama jamii , na kwa hio nilikwenda kwenye benki mmoja na nilipoomba mkopo walinipea shilingi laki mmoja za Kenya (Dolla1000)" Mary alisema

Na kwa kweli waliamua kuhamia mji ambao wao pekee yao ndio walikuwa na biashara ya aina hio ya kuuza bidhaa kutoka nje ya nchi ambazo zimetumiwa , biashara ilinoga kwa kiasi sana huku mary akidokeza kuwa walikuwa wanapata faida ya fehda kama zile laki 1 alizozichukua kama mkopo .

Kwa hio walifaulu kulipa mkopo huo katika kipindi cha miezi mitano tu na hawakuchukua mkopo mwengine wa kuwekeza kwa biashara kwani faida ilikuwa inatiririka kila kuchao .

Pia wakati huo Mary alifanikiwa kununua nyumba , baada ya yeye na mume wake wakati huo kukubaliana kuwa wachukue mkopo mwingine ambao ungewawezesha kununua nyumba , Mary anasema kuwa nyumba ilihitaji milioni 13 za Kenya , ilhali wao walikuwa na milioni tano taslimu walirejea kwenye benki na kuchukua mkopo wa shilingi milioni 7, na hapo ndipo walifanikiwa kununua nyumba yao .

"Maisha yalikuwa mazuri , na tuliimarika kama jamii , mimi na mume wangu kila mtu alikuwa na gari lake , na hatukukosa chochote tulichohitaji "Mary aliongeza kusema

Lakini cha ajabu anasema kuwa yeye kama mke mwema alikubali fedha zote ziwe zinawekwa kwenye akaunti ya mume wake , anasema kuwa ile akaunti ilikuwa na zaidi ya milioni 2 , anasema kuwa alikuwa anamuamini sana mumewe

"Mamangu mzazi alikuwa amenishauri kuwa mume kama kichwa cha nyumba alifaa asikizwe na maoni yake yaheshimiwe " Mary alisema

Kwa hiyo hakuona shida yeyote kwa fedha zao zote kuwekwa kwenye akaunti ya mume wake .

Baada ya muda Mary anasema kuwa mumewe alianza kubadilika kwanza saa zake za kufika nyumbani zolibadilika pia alianza kuwa na tabia ya kubugia vileo na kuingia nyumbani usiku wa manane .

Hayakuishia hapo mume wake alianza uhusiano na mwanamke mwingine ambaye alianza kuwasiliana na Mary kumweleza yanayofanyika nje ya ndoa yake .

Mary anasema kuwa alishtuka alipogundua kuwa mume wake alikuwa na uhusiano wa kimapenzi nje ya ndoa na hata kwani alipomuuliza mumewe hakukana chochote na akawa mkali kwake .

Pia Mary aligundua kuwa kwa miezi minne malipo ya nyumba yao ya mkopo hayakulipwa na muda sio muda benki ilichukua nyumba hiyo baada ya wao kushindwa kuilipia . vile vile Mume wake alitoroka na fedha zote zilizokuwa kwenye akaunti na kuanza maisha mapya na mwanamke mwingine .

"Benki ilichukua nyumba yetu kwa kuwa hatukua tumemaliza kuilipa na pia kwa kuwa mume wangu alitoroka na pesa ilibidi mimi na watoto wangu wawili tuhamie makazi ya chini mno,pia Gari langu lilichukuliwa na benki " Mary alisema

Mary anasema kuwa alianza kuishi chumba kimoja tu ambacho kilikuwa ni jikoni , chumba cha kulala na kadhalika .Baada ya hapo alianzia chini tena baada ya rafiki yake kumpa shilingi alfu tatu au dola 30 ambazo alianza biashara ndogo ya kuanza Mboga Nyanya vitunguu na kadhalika

Anasema kuwa karo ya shule ni dadake pamoja na mamake mzazi walikuwa wanawalipia

Baada ya miezi mitatu ya shida na mahangaiko alipata ajira kama ofisa wa mauzo katika kampuni moja , kazi ambayo kwa sasa imemsaidia kujiinua tena na hadi tayari amenunua kiwanja ambacho anapania kujenga tena

Mary husaidia sana wanawake ambao hujipata pabaya baada ya ndoa au uhusiano wa kimapenzi kuisha na pengine wanasalia mafukara , anatoa ushauri kwa wanawake kujiimarisha na kuhakikisha kuwa wanajisimamia kiuchumi ili wawe na uhuru wa kuishi maisha wanayoyataka .