Hii ni tovuti ya maandishi pekee ambayo inatumia data kidogo. Tazama toleo kuu la tovuti likijumuisha picha na video zote.
Pata maelezo zaidi kuhusu toleo hili la linalotumia kiasi kidogo cha data
Ukweli kuhusu picha ya mtoto iliyosambaa mtandaoni nchini India
Mtoto mwenye umri wa miaka mitano huko kusini mwa mji wa Hyderabad aliandikishwa kuanza shule baada ya picha yake aliyoonekana akiwa anachungulia watoto wenzake wakiwa darasani kusambaa mtandaoni.
Picha ya hivi karibuni ya mtoto huyo mwenye aibu iliibuka kuwa gumzo, Picha hiyo ya mtoto Divya inayomuonyesha akiwa ameshikilia sufuria mkononi huku akisikiliza kwa makini kile ambacho watoto wenzake wanafundishwa darasani katika shule moja ya serikali.
Picha hiyo ambayo imegusa wengi ilichapishwa katika gazeti la 'Telugu' la tarehe 7 Novemba ikiwa na maandishi yanayosema "macho yenye njaa".
Picha hiyo iliibua hisia za watu kwa haraka, mwanaharakati wa masuala ya watoto aliandika kwenye mtandao wa Facebook, akisema kuwa mtoto mwingine amenyimwa haki ya chakula na elimu.
Kutokana na madai hayo, Divya aliandikishwa shule siku iliyofuata.
Ingawa baba yake bwana Lakshman, analalamikia picha ya mtoto kusambaa mtandaoni kuwa sio jambo la kiungwana kwake au kwa mke wake Yashoda ambaye anafanya kazi ya kufagia.
"Nilisikitika sana nilipoiona picha ya mwanangu gazetini," baba huyo aliiambia BBC. " Divya ana wazazi ambao wanafanya kazi kwa bidii kwa ajili ya maisha yake ya baadae lakini alionyeshwa kama mtoto yatima", aliongeza kusema baba huyo.
Bwana Lakshman anadai kuwa alikuwa anasubiri Divya kutimiza miaka sita ili amuandikishe katika shule yenye hosteli ya serikali ambapo watoto wake wengine wawili wa kike wanaishi.
Wazazi hao wana mtoto mwingine wa kiume ambaye amemaliza sekondari na sasa ametuma maombi ya chuo huku akiwa anamsaidia baba yake kuokota taka.
Divya na wazazi wake wanaishi kwenye chumba kimoja katikati ya mji wa Hyderabad. Katika makazi duni wanayoishi ni kilomita 100 kufika shule ya serikali, eneo ambalo Divya alipigwa picha.
Familia zipatazo 300 zinazoishi katika maeneo hayo huwa wanapokea posho za kila siku na watoto wao huwa wanaenda kusoma shule za karibu.
Nyumba yao imezungukwa namakopo yaliyokatwa , tayari kwa ajili ya kuuza kufanyia uchakataji.Anasema kuwa na mke wa ke huwa wanapata kipato cha dola 139 kwa mwezi, fedha ambayo inanunua chakula chao na mavazi. Elimu ni bure kwa watoto kwa sababu shule ni za serikali.
Bwana Lakshman anajua changamoto anazopitia , yeye mwenyewe alikuwa bila wazazi na kila siku anapambana kupata maisha bora.
"Sikutaka watoto wangu wapitie maisha niliyoishi hivyo nilihakikisha kuwa wote wanaenda shule."
Aliongeza kusema kuwa picha ile ilimuumiza sana kwa sababu amekuwa akiwatunza watoto wengine watano wa kaka yake.
"Kaka yangu na mke wake walifariki hivyo ilinibidi nichukue jukumu la kuwalea kwa sababu sikutaka waishi kama watoto yatima, hivyo niliwaweka wote watano kwenye bweni na kuwatunza."
Alipoulizwa kwa nini Divya alienda shule ya serikali akiwa ameshika sufuria mkononi, bwana Lakshman anaeleza kuwa watoto wengi wadogo huwa wanazurura kutoka makazi duni haya mpaka mengine nyakati za chakula cha mchana ili kupata chakula cha bure ambacho kinatolewa na serikali.
Kuna programu ya serikali inayotoa chakula cha mchana katika shule zaidi ya milioni moja na watoto wadogo wanajua kwa sababu ndugu zao wanasoma huko.
"Divya huwa huwa haendi mara nyingi , ilitokea tu ameenda na mpiga picha akampiga picha.
Maelezo yake yalithibitishwa na walimu wa shule hiyo ambao waliiambia BBC.
"Watoto ni watoto huwezi kuwazuia kufanya kitu na hapa hakuna shule ya awali ili watoto wadogo zaidi waende, alisema mwalimu mmoja ambaye hakutaka jina lake lifahamike.
Bwana Lakshman na jirani zake walisema ukosefu wa shule ya awali hufanya wazazi kushindwa kupata sehemu ya kuwaacha ili waendelee na shughuli zao nyingine.
Walimu na viongozi wa kijiji wana matumaini kuwa picha ya Divya itaweza kuchochea kuboresha mazingira ya shule, kwa kupatikana kwa mahitaji ya shule na lishe bora kwa watoto.
Hata hivyo Divya, amefurahia kuanza kwenda shule baada ya kupewa begi jipya la shule ambalo amekuwa akizunguka nalo kila mahali.
Licha ya kwamba baba wa mtoto hakupenda mtoto wake apigwe picha lakini amekubali kuwa , picha hiyo imeleta matokeo chanya.
"Sasa watoto wengine wenye umri sawa na Divya waliandikishwa shule.Hilo ndilo jambo lililonifurahisha."
Unaweza kusoma pia kuhusu: