Kingsley Obiekwu :Aliishindia Nigeria dhahabu lakini sasa ni dereva wa basi

Iliyochapishwa

Miaka 25 baada ya kuishindia Nigeria medali ya dhahabu katika Michezo ya Olimpiki, mwanasoka wa zamani Kingsley Obiekwu ameiambia BBC kuwa amelazimika kuwa dereva wa basi ili kutunza familia yake.

Wakati mchezaji huyo mwenye umri wa miaka 47 alipoonekana akiendesha basi wiki hii katika mji wa mashariki wa Enugukisa chake kilisambaa - na kumfanya nahodha wa taifa wa soka Ahmed Musa kumtumia $5,000 (£3,600) kumsaidia.

Obiekwu alisema kuwa kukosa kumaliza elimu yake akiwa kijana kumesababisha kukosa fursa.

"Baada ya kustaafu kutoka soka mwaka 2004 na kumaliza kozi yangu ya ukocha nchini Uingereza, nilirejea Nigeria mwaka 2008, lakini hakuna Klabu ya Ligi Kuu iliyonikubali, walisema sitambuliki kama kocha.

"Rafiki yangu mmoja alinipa nafasi ya kufundisha katika akademi yake ya soka ya mashinani na tangu wakati huo nimekuwa nikiingia na kutoka kazini.

"Ninapata naira 50,000 [dola 120] katika kazi yangu ya sasa kama kocha katika klabu ya soka ya wachezaji wasiokuwa wa kulipwa , [lakini] nina familia yenye watoto wangu wanne katika chuo kikuu, malipo hayatoshi.

"Badala ya kukunja mikono yangu na kulalamika, niliamua kuwa dereva wa basi ili kupata pesa kidogo za kutunza familia yangu."

Alisema alimshukuru sana Musa kwa zawadi yake: "Nina heshima kwamba Nahodha wa Super Eagles Ahmed Musa na Wanigeria wengine wa nyumbani na nje ya nchi walikuja kuniunga mkono kipindi hiki walichokumbuka mashujaa wao."

Musa aliambia BBC kuwa alielewa masaibu ya Obiekwu kwani alitatizika kula alipokuwa akikua.

Aliwashauri wanasoka chipukizi kuwekeza wakati wanacheza soka wanapojiandaa kustaafu.

"Wachezaji wachanga wa soka wanapaswa kujifunza kutoka kwa wachezaji wetu wa zamani, hali waliyonayo sasa ni kwa sababu hawakuwekeza.

"Sahau kuhusu magari makubwa, mtindo wa maisha, mavazi ya kisasa , unapostaafu ndipo maisha huanza."