Collins Kibet: Mjukuu wa Rais Moi atimuliwa katika nyumba anayoishi Kenya

Iliyochapishwa

Mjukuu wa rais wa zamani wa Kenya Daniel arap Moi, ambaye alifariki miaka miwili iliopita , amefurushwa kutoka katika nyumba yake kutokana na kukosa kulipa malimbikizi ya kodi ya nyumba ya zaidi ya $2,100 (£1,550) ya miezi sita.

Hatua hiyo inajiri huku kukiwa na kesi mahakamani ambapo familia hiyo inapigamia usimamizi wa mali yake.

Collins Kibet, mwenye umri wa miaka 45, aliambia mahakama kwamba alikuwa hana fedha za kulipia kodi yake ya nyumba na hata kuiangalia familia yake - akiongezea kwamba alifurushwa wiki iliopita.

Aliwashutumu ndugu zake akiwemo mamake wa kambo - ambao ndio wasimamizi wa mali hiyo - kwa kutomuhusisha kurithi mali ya babu yake.

Babake Kibet , Jonathan Toroitich ambaye ni mwana wa Moi , alifariki 2019 bila ya kuwacha wasia.

Mali ya familia hiyo inadaiwa kuwa kubwa.

Bwana Kibet anaitaka mahakama kumzuia mamake wa kambo na ndguye wa kambo kusimamia mali hiyo na kushirikishwa miongoni mwa warithi wa mali ya kiongozi huyo wa zamani wa Kenya.

Bwana Moi ndiye rais aliyehudumu kipindi kirefu zaidi . Aliongoza Kenya kwa miaka 24 hadi shinikizo kali zilipomlazimu kujiuzulu 2002.

Je Jonathan Toroitich ni nani?

Jonathan Moi alizaliwa mwezi Julai tarehe 23, 1954.

Alikwenda katika shule ya msingi ya Timboiywo katika darasa la kwanza na la pili kabla ya kujiunga na shule ya msingi ya St Joseph mjini Nakuru.

Alijiunga na shule ya upili ya Nairobi School na baadaye kusomea katika chuo kikuu cha Delaware nchini Marekani ambapo alipata shahada ya Kilimo.

Alifunga ndoa na Sylvia Cherotich mwezi Agosti tarehe 24 1984.

Mwaka 1986 alijiunga katika mashindano ya safari Rally kabla ya kustaafu 1997 baada ya kushinda mataji 800 ikiwemo taji la kuwa mshindi wa mashindano ya safari Raly barani Afrika.

Alijaribu bahati yake katika siasa 2002 na 2007 alipopigania kiti cha ubunge cha eneo bunge la Eldama Ravine.