Mambo gani unahitaji kuhofia kama mtumiaji wa mitandao ya kijamii

Iliyochapishwa

Ulimwengu umeshuhudia ukuaji mkubwa wa matumizi ya teknolojia na pia intaneti hasa wakati huu wa janga la Covid-19.

Lakini watumiaji wengi wa teknolojia hizi wamekuwa wakielezea wasiwasi wao kuhusu uwezo wao wa kudhibiti jinsi taarifa zao katika mitandao zinavyotumiwa.

Katika kipindi cha mwaka mmoja uliopita, kumekuwa na ongezeko la matumizi ya teknolojia ambazo zinawezesha utoaji wa masomo mtandaoni, ununuzi wa bidhaa, mikutano ya kikazi, ibaada na mambo mengine ambayo yanafanyika kupitia mifumo ya kigijitali.

Mifumo hii ya teknolojia inashikilia na kudhibiti taarifa nyingi za kibinafsi za watumizi wake, jambo ambalo limewaweka wasiwasi baadhi ya watu kama vile Abigael Arunga ambaye ni mwanahabari kutoka Kenya. Abigael anasema makampuni ya teknolojia yanafaa yawekewe sheria kali sana kuhusu taarifa wanazochukua kwa watu wakati watu wanajiunga na mitandao hiyo.

"Unajua jinsi wanavyosema - kwamba kama unatumia kitu mtandaoni bila kulipia, basi huenda wewe ukawa ndio bidhaa inayouzwa.

Mimi binafsi kama mtumiaji anayefaa kuwa na uwezo wa kukataa kuwa bidhaa yenyewe. Baadhi ya programu huficha kanuni halisi za matumizi kwa kuweka maneno ambayo hayaeleweki kwa mtu wa kawaida, na huu ni udanganyifu," anasema Abigael.

Awali mwezi huu, mtandao wa kijamii wa WhatsApp ulitangaza kwamba kuanzia Februari, watumizi wake wangelazimika kukubali kanuni mpya za matumizi iwapo wangependa kuendelea kutumia programu hiyo.

Tangazo hili lilizua wasiwasi kuwa taarifa za watu zingetolewa kutoka kwa WhatsApp hadi Facebook, ambayo ni kampuni inayomiliki WhatsApp.

Kufuatia hili, WhatsApp ililazimika kuongeza muda wa kutekeleza hatua hiyo hadi Mwezi Mei mwaka huu. Hata hivyo, watumiaji wa programu hiyo walioko barani Ulaya hawangeathirika na masharti hayo kutokana na sheria kali maarufu kama GDPR ambayo inadhibiti matumizi ya taarifa binafsi za watu.

Barani Afrika, ni nchi 28 tu kati ya nchi 54 ambazo zimeweka sheria za kudhibiti taarifa za watu, hii ni kulingana na Shirika la Umoja wa Mataifa kuhusu Biashara na Maendeleo Duniani, UNCTAD.

Je, nchi za Afrika zinahitaji kufanya nini zaidi?

Andrew Bourne, meneja wa kampuni ya kiteknolojia ya Zoho kutoka Afrika Kusini anasema kuwa suluhu ni kuwepo kwa sheria na pia utoaji wa elimu kwa umma kuhusu matumizi ya teknolojia.

"Wanaotunga sheria wanafaa kulichukulia jambo hili kwa umakini sana. Wanafaa waangalie mfano wa sheria za GDPR, waone ni mambo gani mazuri yanayoletwa na GDPR. Na jambo lingine muhimu ni kwamba wakati sheria hizo zinapopitishwa, kuwepo na bodi au mamlaka ambapo watu wa nchi hiyo wanaweza kutoa taarifa za shughuli za ukiukaji sheria za data zinapotokea," anasema Andrew.