Ivan Rakitic: Kiungo wa kati wa Barcelona anasema yeye sio gunia la viazi

Chanzo cha picha, Gettyimages
Soka imejaa nukuu za kufurahisha na nyengine za kushangaza na mfano wa Rakitic sasa unajumuika na mifano mengine maarufu zaidi baada ya kupata njia ya kipekee kuikejeli Barcelona kuhusu jinsi timu hiyo inavyomchukulia kwa sasa.
Kiungo huyo wa kati wa Croatia amekuwa na klabu hiyo ya Barcelona tangu 2014, lakini alipoteza fursa ya kuanzishwa kushiriki mechi msimu huu kufuatia kuwasili kwa mchezaji matata wa Uholanzi Frankie de Jong.
Katika mahojiano na gazeti moja la Uhispania Mundo Deportivo, mchezaji huyo mwenye umri wa miaka 32 alifichua kwamba alikataa kuhamia PSG mwaka uliopita kama makubaliano ya kumrudisha Neymar katika klabu hiyo ya Nou Camp.
Alipoulizwa kuhusu hatma yake alijibu: Naelewa hali lakini mimi sio gunia la viazi ambalo munaweza kunifanyia chochote.
''Nataka kuwa mahali ambapo nahitajika na kuheshimika . Kama ni hapa nitafurahia na iwapo ni mahala pengine basi ni mimi nitakayeamua na sio mtu mwengine''.
Barcelona kwa sasa ipo pointi mbili juu katika jedwali la La Liga , lakini Rakitic amehusika kidogo katika kampeni ya mwaka huu , akianzishwa mara 10 katika mechi 27 za Barcelona .
''Mwaka uliopita ulikuwa mwaka mzuri kati ya miaka sita nilioichezea Barcelona na nilichukizwa na jinsi nilivyochukuliwa . Nilishangaa na sikuelewa hata kidogo''.
''Matokeo yake hayakuwa mazuri na sijachezeshwa sana, hio ndio sababu nilikasirika'', alisema.
Kandarasi ya Rakitic katika klabu ya Barcelona inakamilika 2021, na yuko tayari kuhakikisha kuwa anaikamilisha.
''Nilikuwa na vipindi vibaya vya kipindi cha kwanza msimu huu , sikufurahia na nilishangazwa sana. lakini natumai nitakamilisha mwaka wa mwisho wa kandarasi yangu'' , alisema.
Vyovyote vile, matamshi ya Rakitic sio ya kushangaza .Mifano mingine ya kuchekesha katika historia inajitokeza.
Mwezi February , Jose Mourinho alituchekesha wengi wetu kuhusu mfano wake wa ngazi za kupanda katika nyumba akijibu jeraha la Son Heung -min.

Ama Matamshi ya Pochettino kuhusu ng'ombe ,treni na mechi za klabu bingwa Ulaya kutoka 2018.
Na hio ni bila kutaja mifano mizuri - kwa mafano Rafa Benitez akijibu ukosoaji kutoka kwa Roy Hodgson 2018 kwamba baadhi ya watu hawawezi kuwaona wahubiri katika mlima wa sukari .
Ama Eric Cantona , wakati aliposema kwamba ndege wa baharini hufuata boti ya kuvua samaki, wakidhania kwamba dagaa watatupwa.

Eric Cantona alizungumza kuhusu ndege wa baharini, Mauricio Pochettino akazungumzia kuhusu ng'ombe wake na sasa Ivan Rakitic amezungumzia kuhusu gunia lake la viazi.















