Hii ni tovuti ya maandishi pekee ambayo inatumia data kidogo. Tazama toleo kuu la tovuti likijumuisha picha na video zote.
Pata maelezo zaidi kuhusu toleo hili la linalotumia kiasi kidogo cha data
Yoweri Museveni: 'Afrika ilishindwa kuisaidia Libya ilipovamiwa '
Rais Yoweri Museveni wa Uganda amesema kwamba bara la Afrika lina uwezo wa kuzuia mataifa ya magharibi kuingilia kati ama hata kuvamia mataifa ya Afrika kiholela.
Museveni ambaye alikuwa akizungumza na BBC amesema kwamba ilikuwa makosa kwa mataifa ya magharibi kuivamia Libya na kumng'oa kiongozi wake Muammar Gaddafi bila ya Afrika kuzuia kitendo hicho.
Amesema kwamba viongozi wa Afrika walitumia diplomasia kutatua mzozo huo lakini badala yake wangetumia jeshi lake kukabiliana na wavamizi.
Kiongozi huyo wa Uganda anasema kwamba bara la Afrika lina uwezo mkubwa wa kuweza kuwakabili waliovamia Libya ambayo hadi sada inakumbwa na mzozo wa wenye kwa wenyewe.
''Nawaza Afrika ingeingilia kati na kumpatia mtu funzo, hapo ndipo tulipofeli'', alisema rais huyo anayedaiwa kuwa miongoni mwa viongozi wa Afrika waliokalia madaraka kwa kipindi kirefu kufikia sasa.
Bw. Museveni amesema: ''Lilikuwa shambulio la uvamizi kwani hata mimi mwenyewe sikudhania kwamba mtu anaweza kuwa na mawazo ya kipuzi na kuvamia taifa la Afrika kama walivyofanya''.
''Tatizo ni kwamba tulipatikana wakati mbaya ambapo tulikuwa tumetawanyika hatuakuwa tumejiandaa'', aliongezea.
Amesema kwamba bara la Afrika lina uwezo ambao haujutumika wa kukabiliana na uvamizi wowote kutoka kwa mataifa ya magharibi.
''Iwapo tunataka kuwafurusha wavamizi tunaweza, tuliwafukuza na kuwashinda Wareno na Boers wakati wa ukolini wa mwisho wa karne ya 17 licha ya wao kusaidiwa na mataifa mengi ya kigeni.
Museveni anasema licha ya kukabiliana na wanajeshi wa Muamar Gaddaffi mara mbili nchini Uganda, anasema kwamba kiongozi huyo alikuwa na matatizo yake lakini jinsi alivyotendewa na mataifa ya magharibi ilikuwa makosa makubwa.
Anasema kwamba kulikuwa na njia chungu nzima za kukabiliana na kiongozi huyo na kwamba nguvu zilizotumika dhidi yake zilikuwa mbaya kwa kiongozi wa Afrika aliyekuwa na haiba kama yake.
Kuhusu mazungumzo yanayoendelea kuhusu Libya, Museveni anasema kwamba bara la Afrika lingechukua jukumu la kuangazia maswala yake badala ya kutegemea mataifa ya nje kutafuta suluhu Afrika.
Swala hilo linajiri wakati ambapo Ethiopia na Misri pia zimeamua kuwasilisha tatizo lao la matumizi ya mto Nile Marekani badala ya Muungano wa Afrika.
Mzozo wa Mto Nile
Taarifa ya pamoja iliyotolewa na nchi tatu, pamoja na Marekani na Benki ya Dunia, ilisema kwamba washiriki wanaojadiliana wamekubaliana kujaza bwawa la Grand Renaissance linalojengwa Ethiopia wakati wa msimu wa mvua kati ya miezi ya Julai na Agosti.
Hata hivyo taarifa hiyo haikusema lolote kuhusu masuala ya msingi yanayozunguka mgogoro huo ambayo ni kasi ya kujaza bwawa hilo.
Ethiopia inataka kujaza bawa la Grand Renaissance kwa miaka 6 lakini Misri imependekeza angalau mradi huo uchukue kipindi cha miaka 10 - kwa kuhofia kwamba kuchukua kipindi kifupi kutaathiri mtiririko wa maji ya mto Nile ambayo inategemea asilimia 90 .
Makubaliano ya mwisho yatatiwa saini Januari 28-29, wakati ambapo mawaziri kutoka nchi tatu watakuwa wanakutana Washington.
Museveni amesema kwamba huo ndio udhoofu wa Afrika kutumia ''mwalimu mkuu'' kutatua matatizo yake .
Hatahivyo amesema kwamba juhudi kama hizo zitakwisha na mataifa husika yatarudi katika meza ya mazungumzo iwapo ''Mwalimu mkuu'' huyo atashindwa kutoa suluhu ya kudumu.
Amesema kwamba tayari amewasilisha maoni yake kuhusu mzozo huo kwa AU.
Nini kilichosababisha vita vya wenyewe kwa wenyewe Libya?
Kama ilivyotokea kwa Syria, ilianza tu kwa maandamano ya wakati wa vuguvugu la mapinduzi ya Arabuni 2011.
Vikosi vinavyoungwa mkono na Nato vilipindua utawala wa muda mrefu wa Muammar Gaddafimwaka huo, huku raia wakiwa na matumaini mengi tu si raia wa Libya pekee badi hata jamii ya kimataifa.
Tangu wakati huo, nchi hiyo imekuwa katika vita vya wenywe kwa wenyewe.
Baada ya miaka kadhaa ya mapigano, Umoja wa Mataifa ulisaidia kuanzishwa kwa utawala ulioongozwa na waziri mkuu Serraj.
Serikali yake ya Muungano wa Kitaifa ilikuwa mjini Tripoli na ilitarajiwa kuunganisha nchi hiyo.
Japo siyo kila mmoja aliyeunga mkono makubaliano hayo na Jenerali Haftar alitaka kuwa na nguvu zaidi ya madaraka.
Aliunda jeshi lake la taifa mashariki mwa nchi hiyo kwa kuzingatia miji ya Tobruk na Benghazi.
Pia alidai kwamba anaweza kurejesha usalama na kupiga vita kile alichokiita ugaidi wa makundi ya kiislamu.
Vikosi vya Jenerali Haftar vimekuwa vikiingia kuelekea mji mkuu wa Tripoli tangu April 2019. Mwezi huu, vilifanikiwa kuteka mji wa kimkakati wa pwani wa Sirte.
Lakini ili kuchanganya mambo zaidi, wanamgambo wapo katika miji mbalimbali, wakipigana vita vyao na wakati hayo yakiendelea, kundi linalojiita Islamic State limejitokeza na kuendeleza shughuli zake katika maeneo mbalimbali ya jagwani.
Kina nani wanaochochea vita
Vita vya Libya kwa kiasi kikubwa vinafanana na vile vya Syria: Makundi hasimu hayatokei tu nchini Libya.
Pande zote za mgogoro wa Libya zimevutia washirika wenye nguvu wa kieneo na kimataifa.
Umoja wa Falme za Kiarabu,UAE na Saudi Arabia wanasema kwamba wanataka kumaliza makundi ya Kiislam katika eneo hilo. Kwa kujitokeza kama adui wa makundi ya Kiislamu yenye msimamo mkali, Jenerali Haftar alifanikiwa kuvutia nchi hizi upande wake.
Pamoja na Jordan, UAE imekuwa ikitoa silaha na usaidizi wa anga kwa Jeshi la taifa la Libya, na Umoja wa Mataifa umelaumu UAE kwa kusambaza silaha za kijeshi ambazo zimesababisha mauaji ya raia wengi wakati Jenerali Haftar alipofanya mashambulizi.
Misri, majirani wa Libya upande wa mashariki, wanamuunga mkono Jenerali Haftar na pia imekuwa ikiisaidia kwa masuala ya usafiri.
Na kwa wakati huu Urusi ambayo pia inatafuta kuwa na ushawishi pia imeingia kwenye vita hivyo. Inasemekana kwamba mamluki wa Urusi wamekuwa wakipigana na vikosi vya Jenerali Haftar ingawa Urusi imekanusha madai hayo.
Upande mwengine Uturuki, imetuma vikosi vyake kumuunga mkono waziri mkuu Serraj.
Kama ilivyo kwa Urusi, Uturuki pia inataka kuwa na ushawishi siku zijazo na kuonekana kama yenye nguvu katika eneo hilo. Serikali ya Uturuki imesema kwamba vikosi vyake vimepelekwa Tripoli kutoa mafunzo na ushauri.
Lakini chanzo katika serikali ya Haftar kimeithibitishia BBC kwamba vikosi vya Uturuki ni pamoja na wapiganaji wa waasi wa Syria wanaoungwa mkono na Uturuki.
Kulingana na mwanahabari wa BBC Jonathan Marcus, nia ya Uturuki huenda ikawa inataka raslimali za baharini.