Mzozo wa Libya: Viongozi wa mataifa yenye uwezo mkubwa wana nia ya kuweka amani, asema Guterrez

Iliyochapishwa

Katibu mkuu wa Umoja wa Mataifa Antonio Guterres amesema kuwa mataifa yenye uwezo mkubwa duniani yamejitolea kuhakikisha kuwa kuna suluhu ya amani nchini Libya baada ya mkutano nchini Ujerumani.

Viongozi hao wameahidi kutoingilia vita vya wenyewe kwa wenyewe nchini humo mbali na kuheshimu vikwazo vilivyowekwa na Umoja wa mataifa.

Mzozo huo ni kati ya jenerali Khalifa Hiftar dhidi ya serikali inayoungwa mkono na Umoja wa Mataifa GNA.

Licha ya pande zote zinazozozana kushiriki katika mkutano huo hazikukutana.

Kansela wa Ujerumani Angela Merkel alisema kwamba pande hizo mbili zilielezewa na kushauriwa na vyama vingine.

Pamoja na bi Merkel , waliohudhuria mkutano huo ni rais wa Urusi Vladimir Putin, rais wa Uturuki Recep Tayyip Erdogan , rais wa Ufaransa Emmanuel Macron na waziri mkuu wa Uingereza Boris Johnson.

Kabla ya mkutano , bwana Johnson alisema kwamba lengo la mkutano huo ilikuwa kusitisha wale wanaopigania nyadhfa. Raia wa Libya wameteseka kwa muda mrefu , alisema alipowasili siku ya Jumapili ni wakati wa taifa hilo kusonga mbele.

Ni nini kilichotokea mjini Berlin?

Viongozi kutoka kwa Muungano wa Ulaya , Urusi na Uturuki walikuwa miongoni mwa wale walioahidi kumaliza hatua ya mataifa ya kigeni kuingilia kati mgogoro huo mbali na kuheshimu vikwazo vya Umoja wa mataifa.

Baada ya mkutano huo kiongozi wa Ujerumani bi Merkel alisisitiza kwamba hakuna njia ya kijeshi itakayomaliza mzozo huo isipokuwa suluhu ya kisiasa pekee.

Bwana Guterres wakati huohuo alisema kwamba mataifa yote yenye uwezo mkubwa yaliokuwepo yalikubaliana kuhusu uamuzi wa kuzuia vita zaidi.

Hatahivyo alisema kwamba alikuwa na wasiwasi mkubwa kuhusu ripoti kwamba majeshi yanayomtii Jenerali Haftar yalikuwa yamefunga bandari na bomba muhimu la kusafirisha mafuta nchini humo.

Waziri wa maswala ya kigeni nchini Urusi Sergei Lavrov pia aliwasilisha wasiwasi wake .

Alisema baadaye kwamba mataifa yenye uwezo mkubwa duniani hayajafanikiwa katika kuanzisha mazungumzo thabiti kati ya pande zinazozozana.

Na kulikuwa na maswali kuhusu iwapo kutakuwa na amani ya kudumu na jinsi wazo hilo litakavyoendelezwa . Hatahivyo bwana Lavrov alisema kwamba pande zote zimepiga hatua mbele.

Uwezekano wa kusitisha mapigano hauko karibu kuafikiwa

Na mwandishi Rana Jawad

Ahadi ya mataifa ya kigeni katika mggoro huo ikiwemo Urusi, Misri na Uturuki kuheshimu vikwazo vya UN yataheshimiwa iwapo baraza la usalama la Umoja wa mataifa litachukua hatua dhidi ya ukiukwaji huo.

Hiki ni kitu ambacho baraza hilo limeshindwa kufanya katika miaka mingi ya mzozo huo.

Kwa hatua zozote kuafikiwa katika kipindi cha muda mrefu , pande zinazopigana Libya zitalazimika kusitisha vita hatua ambayo haionekani kuafikiwa karibuni.

Iwapo kutakuwa na makubaliano ya kusitisha vita, itaruhusu UN kurudi katika meza ya kisiasa hatua ambayo iliifutiliwa mbali katika kipindi cha mwaka mmoja kutokana na mgawanyiko wake kuhusu suluhu.

Ni nini kinachoendelea Libya?

Kama ilivyotokea kwa Syria, ilianza tu kwa maandamano ya wakati wa vuguvugu la mapinduzi ya Arabuni 2011.

Vikosi vinavyoungwa mkono na Nato vilipindua utawala wa muda mrefu wa Muammar Gaddafi mwaka huo, huku raia wakiwa na matumaini mengi tu si raia wa Libya pekee balii hata jamii ya kimataifa.

Tangu wakati huo, nchi hiyo imekuwa katika vita vya wenywe kwa wenyewe.

Baada ya miaka kadhaa ya mapigano, Umoja wa Mataifa ulisaidia kuanzishwa kwa utawala ulioongozwa na waziri mkuu Serraj.

Serikali yake ya Muungano wa Kitaifa ilikuwa mjini Tripoli na ilitarajiwa kuunganisha nchi hiyo.

Japo sio kila mmoja aliyeunga mkono makubaliano hayo na Jenerali Haftar alitaka kuwa nguvu zaidi ya madaraka.

Aliunda jeshi lake la taifa mashariki mwa nchi hiyo kwa kuzingatia miji ya Tobruk na Benghazi.

Pia alidai kwamba anaweza kurejesha usalama na kupiga vita kile alichokiita ugaidi wa makundi ya kiislamu.

Vikosi vya Jenerali Haftar vimekuwa vikiingia kuelekea mji mkuu wa Tripoli tangu April 2019. Mwezi huu, vilifanikiwa kuteka mji wa kimkakati wa pwani wa Sirte.

Lakini ili kuchanganya mambo zaidi, wanamgambo wapo katika miji mbalimbali, wakipigana vita vyao na wakati hayo yakiendelea, kundi linalojiita Islamic State limejitokeza na kuendeleza shughuli zake katika maeneo mbalimbali ya jagwani.

Mataifa ya kigeni yanahusikaje katika mgogoro huo?

Mataifa ya kigeni katika mgogoro huu yameanza kuhusishwa katika miezi ya hivi karibuni, haswa Uturuki ambayo ikidaiwa kusaidia kwa kutoa silaha ili kusidia serikali ya Libya kuendelea na mapigano.

Jenerali Haftar wa kikosi cha wapiganaji anaungwa mkono na Urusi, Misri, Saudi Arabia, Jumuiya ya Mataifa ya kiarabu na Jordan.

Siku ya Jumamosi, kikosi maalum cha Umoja wa mataifa kilitaka mataifa makubwa duniani kuacha kuvisaidia vikosi vya wapiganaji kwa kuwapa silaha, fedha na msaada wa kijeshi.

Aliiambia BBC kuwa hatua zinapaswa kuchukuliwa ili kusitisha mapigano hayo ambayo yanawagawa Walibya.

Bwana Salamé aliiambia BBC kuwa suluhisho la kisiasa katika mgogoro huu lilikuwa muhimu kwa pande zote kushiriki katika mkutano huo ili wapate suluhisho la pamoja, kutokana na ukanda waliotoka, nguvu wanayotumia, madhara yanayosababishwa kwa wananchi wa Libya, uharibifu wa miudombinu na ugumu wa taifa hilo kuendelea.