Christian Eriksen: Jose Mourinho afufua mgogoro na mkufunzi Antonio Conte

Iliyochapishwa

Mkufunzi wa Tottenham Jose Mourinho amefufua upya mzozo kati yake na Antonio Conte baada ya mkufunzi huyo wa Inter Milan kuonyesha hamu hadharani ya kutaka kumsajili kiungo wa kati Christian Eriksen anayehusishwa na uhamisho wa klabu hiyo.

Raia huyo wa Denmark atakuwa mchezaji huru mwisho wa msimu huu baada ya kandarasi yake na klabu yake kumalizika huku ripoti zikisema kwamba anatarajiwa kuelekea Serie A.

''Antonio amezungumza hadharani kuhusu Eriksen'', alisema Mourinho.

''Nadhani sisi makocha tunafaa kuwa na tabia inayofanana wakati wa uhamisho. Nadhani hatufai kusema kitu hadi pale uhamisho utakapofanyika''.

Pia unaweza kusoma:

Mkufunzi huyo wa Spurs aliongezea: Unaponiuliza mimi kuhusu mchezaji huyu ama yule kama wakati nilipoulizwa kuhusu wachezaji watatu, ninawezaje kuzungumzia kuhusu wachezaji watatu ambao sio wachezaji wangu?

''Nadhani ni muhimu kuwalinda wachezaji. Sio kama ninavyowaona watu wenye majukumu makuu wakizungumzia kuhusu Eriksen... Nadhani hatufai kuzungumzia kuhusu wachezaji kutoka klabu nyengine hadi pale watakapokuwa wachezaji wetu''.

Akizungumza na vyombo vya habari vya Itali, Mkufunzi wa Inter Milan alikuwa amesema: Eriksen? ni vyema kuwafuatilia wachezaji ambao wanakaribia kumaliza kandarasi zao.

Spurs haijapokea ombi la uhamisho la Eriksen na kiungo huyo wa kati atashiriki katika mechi dhidi ya Watford siku ya Jumamosi kulingana na Mourinho.

Wakufunzi hao wawili walikuwa na uhusiano mbaya wakati Mourinho alipokuwa akiifunza Man United huku Conte akiisimamia Chelsea.

Mzozo wao ulianza msimu wa 2017-18 , wakati Mourinho aliposema kwamba hatopigwa marufuku kwa kushiriki katika udanganyifu wa mechi , akitaja marufuku ya Conte ya miezi minne aliyeshindwa kuelezea udanganyifu wa mechi akiifunza Juventus, baada ya kumuita Mourinho 'mcheshi', Conte alijibu kwa kumuita Mourinho ''Mtu mdogo''.

Mourinho anajaribu kuongeza wachezaji katika kikosi chake

Spurs itakosa huduma za mshambuliaji wa England Harry Kane, ambaye anauguza jeraha la paja na anatarajiwa kurudi katikati ya mwezi Aprili.

Mourinho amesema kwamba klabu hiyo italazimika kusaini mchezaji atakayechukua nafasi yake mwezi huu iwapo mchezaji anayelengwa atapatikana.

''Majina kadhaa yamewasilishwa na mengi yameletwa na maajenti wa wachezaji hao, na watu ambao wanataka kuweka majina ya wachezaji katika soko'', alisema mkufunzi huyo mwenye umri wa miaka 56.

Je tunahitaji mshambuliaji? Ndio iwapo itawezekana. Lakini ni sharti awe mchezaji ambaye atatusaidia .

Hatahivyo Mourinho amesema kwamba Tottenham ina washambuliaji mbadala kupitia Son heung-min, Lucas Moura, Erik Lamela, Giovani lo Celso na Dele Alli.

''Ni kweli kwamba wote ni wachezaji wazuri lakini tunamkosa mshambuliaji wetu nyota'', alisema.

''Tunajaribu kila njia, sio rahisi lakini tunajaribu kuongeza wachezaji katika kikosi''.

Tottenham tayari imemsajili kiungo wa kati Gedson Fernandes kwa mkopo kutoka Benfica kwa miezi 18 wakiwa na uwezo wa kumnunua mwisho wa kandrasi yake.