AFCON 2019: Nani kuibuka mbabe Nigeria vs Afrika Kusini?

Iliyochapishwa

Tayari tambo za mashabiki wa Afrika Kusini na Nigeria zimeshaanza mitandaoni, huku kila upande ukivutia upande wake na kupachika majina upande pinzani.

Leo usiku timu hizo zitashuka dimbani katika mechi ya robo fainali ya pili ya michuano ya Kombe la Mataifa ya Afrika (AFCON) jijini Cairo.

Mechi ya kwanza itazikutanisha Senegal dhidi ya Benin.

Japo Benin waliwatoa Morocco kwenye hatua ya mtoano kwa mikwaju ya penati, wachambuzi wengi wanaamini itakuwa ni kazi ngumu kwao kuwatoa Senegali.

Hivyo ni mawazo ya wengi kuwa Senegali (ambayo imezifunga timu tatu za Afrika Mashariki) itasonga mbele mpaka hatua ya nusu fainali.

Upinzani mkali unatarajiwa kuwa baina ya Nigeria na Afrika Kusini.

Mashabiki wa timu hizo tayari wameshabadili majina ya utani ya timu pinzani.

Afrika Kusini ni maarufu kwa jina la Bafana Bafana, neno bafana kwa lugha ya Kizulu linamaanisha wavulana kwa Kiswahili, lakini mashabiki wa Nigeria wameligeuza na kuwa 'Banana Banana', banana kwa maana ya ndizi.

Nigeria wao ni maarufu kwa jina la Super Eagles, lenye maana ya Tai Wakubwa, lakini mashabiki wa Bafana sasa wanawaita wapinzani wao 'Super Egos'.

Ego ni neno la Kingereza lenye maana ya ubinafsi, hivyo 'Super Egos' inaweza kutafsiriwa 'wabinafsi wakubwa'.

Timu zote hizo ni mabingwa wa zamani wa kombe hilo, japo Nigeria amekuwa na historia nzuri na kiwango cha juu zaidi ya Afrika Kusini.

Hata hivyo timu hizo mbili zilipangwa kwenye kundi moja katika mbio za kufuzu kwenye mashindano hayo.

Mechi yao ya kwanza iliisha kwa Nigeria kukubali kichapo cha 2-0 na mechi ya marudiano ikamalizika kwa sare ya 1-1.

Hata hivyo, mshambuliaji kinara wa Nigeria Odion Ighalo amewaonya Afrika Kusini kuwa wasitegemee kuwa mambo yatakuwa kama kwenye mbio za kufuzu: "Tupo tayari, na tutalidhihirisha hilo kesho (leo). Mechi hii ni tofauti kabisa na zile mechi za hatua ya kufuzu. Tunajua itakuwa ni mechi ngumu, lakini tupo tayari kuwapa furaha Wanaigeria."

Nigeria imetinga robo fainali baada ya kuwafunga waliokuwa mabingwa watetezi Cameroon 3-2.

Afrika Kusini yenyewe iliwashangaza wengi baada ya kuwafunga wenyeji Misri goli 1-0 na kusababisha kocha wa Misri kutimuliwa na raisi wa chama cha mpira cha nchi hiyo kujiuzulu.

Je nani kati yao kuibuka mbabe hii leo? Bofya hapa na ubashiri matokeo ya mchezo huo.