Marekani bingwa wa soka la wanawake, Brazil watwaa Copa Amerika

Iliyochapishwa

Huu ni ushindi uliotarajiwa, na uthibitisho kuwa Marekani ni miamba ya mpira wa miguu kwa upande wa wananwake.

Timu ya Taifa ya Wanawake ya Marekani imeicharaza Uholanzi 2-0 na kutetea ubingwa wa dunia.

Nyota wa Marekani katika michuano hiyo, Megan Rapinoe alifungua ukurasa wa ushindi kwa goli lake katika dakika ya 61 kupitia mkwaju wa penati, dakika nane baadae Rose Ravelle.

Rapinoe, amefunga jumla ya magoli 6 katika mechi 5 alizocheza kwenye fainali hizo zilizofanyika nchini Ufaransa.

Mchezaji huyo pia alitoa pasi 2 zilizozaa magoli.

Kutokana na kiwango hicho, Rapinoe ameshinda kiatu cha dhahabu kama mfungaji bora wa mashindano na mpira wa dhahabu kama mchezaji alieonesha kiwango bora zaidi.

Rapinoe tayari ameshasema hatokanyaga Ikulu ya White House endapo timu hiyo itaalikwa kusherehekea na Rais Donald Trump.

Rapinoe amejitangaza kuwa ni mpenzi wa jinsia moja na mkosoaji wa sera za Trump.

Marekani pia ilishinda ubingwa huo miaka minne iliyopita nchini Canada.

Brazil yashinda Copa America

Hatimaye timu ya taifa ya wanaume ya Brazil imenyakua ubingwa wa kandanda wa bara la Amerika ya Kusini baada ya kusubiri kwa miaka 12.

Brazil imeichapa Peru 3-1 na kutawazwa mabingwa wapya wa Amerika Kusini.

Sousa Soares aliitanguliza Brazil katika dakika ya 15 kabla ya Guarrero kuisawazishia Peru katika dakika ya 44 kupitia mkwaju wa penati.

Gabriel Jesus aliirudisha Brazil mbele kwa goli la pili katika dakika za nyongeza za kipindi cha kwanza (45+3).

Jesus alitolewa kwa kadi nyekundu katika dakika ya 70 ya mchezo, na akatoka kwa hasira akipiga teke chupa ya maji na kusukuma mashini ya usaidizi ya mwamuzi (VAR).

Richarlson alipigilia msumari wa mwisho kwenye jeneza la Peru katika dakika ya 90 kwa kufunga mkwaju wa penati.

Huu ni ubingwa wa tisa wa Copa America kwa Brazil, na ushindi wao mkubwa wa kwanza toka mwaka 2016 waliposhinda fainali ya Olimpiki na kunyakua medali ya dhahabu.

Baada ya filimbi ya mwisho, Jesus aliomba radhi kwa vitendo vyake baada ya kuoneshwa kadi nyekundu.

"Nataka kuomba radhi," alisema. "Ningeweza kujizuia, na inanihtaji nikue kwa haraka."