Israel yaonya vita na Hamas vinaweza kuchukua 'miezi kadhaa' zaidi

Wapiganaji 70 walikamatwa katika hospitali ya Gaza; Hamas yasema huduma ya matibabu imezuiwa

Moja kwa moja

Ambia Hirsi, Yusuf Jumah and Asha Juma

  1. Na kufikia hapo ndio tunakamilisha matangazo yetu ya moja kwa moja kwa leo. Kwaheri!

  2. Israel yasema wapiganaji 70 wa Hamas "walijisalimisha na silaha zao" kaskazini mwa Gaza

    .

    Chanzo cha picha, Getty Images

    Jeshi la Israel linasema limewakamata zaidi ya wanachama 70 wa Hamas katika hospitali moja kaskazini mwa Gaza, huku maafisa wa afya katika eneo hilo wakishutumu vikosi vya Israel kwa kuwazuia wahudumu wa afya kutoa huduma.

    Msemaji wa Jeshi la Ulinzi la Israel, Avichay Adraee, alisema wapiganaji hao "wamejisalimisha na silaha zao" katika hospitali ya Kamal Adwan.

    Akiandika kwenye mtandao wa X, pia aliweka mfululizo wa picha zinazoonyesha wanaume waliovuliwa nguo hadi kiunoni wakitoa kile kinachoonekana kuwa bunduki.

    Msemaji wa wizara ya afya inayoendeshwa na Hamas alishutumu vikosi vya Israel kwa kuwazuia wahudumu wa afya kutoa huduma kwa watu 10 waliojeruhiwa katika hospitali hiyo, ikiripotiwa kusababisha wawili kati yao kufariki. Hata hivyo, Adraee

    Inawadia baada ya Umoja wa Mataifa kuripoti kuwa hospitali hiyo "imezingirwa na wanajeshi wa Israel na vifaru kwa siku kadhaa, huku mapigano ya kivita yakiripotiwa katika maeneo ya karibu".

    Tangu vita vilipoanza tarehe 7 Oktoba, Israel imeishutumu Hamas kwa kutumia hospitali kwa madhumuni ya kijeshi.

    Mamia ya maelfu ya watu wamekimbia kaskazini mwa Gaza, ambayo ilikuwa lengo la awali la vita.

    Soma zaidi:

  3. Tanzania: Mahakama yafuta uamuzi wa kuwavua uanachama wabunge 19

    .

    Mahakama Kuu ya Tanzania imefuta uamuzi wa chama cha upinzani cha Chadema wa kuwafuta uanachama wabunge 19 wa viti maalumu kwa sababu chama hicho kilikiuka kanuni ya kawaida wakati wa kuwafukuza uanachama mwaka 2021.

    Jaji aliyesikiiza shauri hilo, Cyprian Mkeha ametoa uamuzi muda mfupi uliopita kuwa, wajumbe wa Kamati Kuu ya chadema kuwa wajumbe wa Baraza Kuu lililopaswa kufanya kazi ya kimahakama, ni wazi kuwa wasingeweza kutenda bila Upendeleo.

    Kwa sababu hiyo, Jaji amesema anaona Kwamba, Baraza Kuu la chadema lilikwenda kinyume na kanuni ya kawaida ya kutokupendelea, hivyo kukubaliana na maombiya wabungekuwa yamezingatia hoja za msingi za ufanisi wa chombo cha maamuzi.

    Kufutwa kwa uamuzi wa baraza kuu la Chadema kunamaanisha kuwa wabunge 19 bado ni wanachama halali wa chama hicho, hivyo wataendelea kuwa wabunge kwa sababu moja ya sifa za msingi za mtu kuwa mbunge nchini Tanzania ni kuwa mwanachama wa chama cha siasa.

    Kamati Kuu ya chadema iliwavua uanachama wabunge 19 Novemba 27, 2020 baada ya kuapishwa jijini Dodoma na Spika wa Bunge la Tanzania wa wakati huo, Job Ndugai.

    Baadaye mwaka 2021 Baraza Kuu la chadema lilibariki uamuzi wa Kamati Kuudhidi ya wabunge hao wakiongozwa na aliyewahi kuwa mbunge a Kawe, pia mwenyekiti wa baraza la wanawake wa Chadema (Bawacha), Halima Mdee.

    Kwa mujibu wa maelezo ya Katibu Mkuu wa Chadema, John Mnyika wabunge hao hawakupewa idhini ya kuapishwa wala yeye hakuwasilisha majina yao tume ya Uchaguzi kama ulivyo utaratibu. Hata hivyo, maelezo hayo yalipingwa na viongozi mbalimbali wa serikali na Spika wa Job Ndugai na mrithi wake Tulia Ackson ambaye ni Spika wa sasa.

  4. Waziri wa ulinzi wa Israel asema kuiangamiza Hamas itachukua miezi kadhaa

    Mshauri wa usalama wa taifa wa Marekani Jake Sullivan amefanya mazungumzo na waziri mkuu wa Israel na waziri wa ulinzi, Yoav Gallant.

    Kulingana na taarifa kutoka kwa serikali ya Israel, Gallant alimwambia Sullivan kwamba kuiangamiza Hamas kutahitaji "zaidi ya miezi kadhaa".

    Gallant alimshukuru Sullivan kwa ziara yake, akimwambia haikuwa rahisi kuharibu miundombinu iliyojengwa na Hamas huko Gaza.

    "Itahitaji muda - itachukua zaidi ya miezi kadhaa, lakini tutashinda na tutawaangamiza," alisema.

    Ziara ya Mmarekani huyo nchini Israel inakuja huku kukiwa na shinikizo la kimataifa kuhusu ongezeko la vifo na kuzorota kwa hali ya kibinadamu huko Gaza.

    Soma zaidi:

  5. Mshauri wa usalama wa Marekani akutana na Netanyahu Israel ikiendeleza mashambulizi dhidi ya Hamas

    .

    Chanzo cha picha, Amos Ben Gershom /GPO

    Mkutano kati ya Waziri Mkuu wa Israel Benjamin Netanyahu na mshauri wa usalama wa taifa wa Marekani Jake Sullivan umefanyika mjini Tel Aviv.

    Sullivan aliwasili Israel kwa mazungumzo na maafisa wakuu, huku vikosi vya Israel vikiendelea na mashambulizi dhidi ya Hamas huko Gaza na kutoelewana na Marekani kukizidi.

    Jana, Netanyahu alisema hakuna kitakachozuia vita hivyo, akimaanisha kuongezeka kwa shinikizo la kimataifa la kusitishwa kwa mapigano huku kukiwa na ongezeko la vifo vya raia na mzozo mkubwa wa kibinadamu.

    Ziara hiyo inafanyika siku chache baada ya Rais Joe Biden kutoa maoni yake makali zaidi kuhusu mwenendo wa kijeshi wa Israel, akisema Israel inaanza kupoteza uungwaji mkono kimataifa na "mashambulizi ya kiholela" ya Gaza, jambo ambalo limekataliwa na Israeli.

    Tofauti zinazidi kuongezeka kuhusu nani atawale Gaza baada ya vita. Marekani inaunga mkono maoni kwamba Mamlaka ya Palestina, ambayo kwa sasa inasimamia baadhi ya maeneo ya Ukingo wa Magharibi unaokaliwa na Israel, ichukue udhibiti wa Gaza - jambo ambalo Netanyahu amelikataa kwa sasa.

    Baadhi ya vyombo vya habari vya Israel vinapendekeza kwamba Netanyahu, kwa kutokubaliana waziwazi na utawala wa Biden, anajaribu kuvutia mrengo wake wa kulia.

    Netanyahu, ambaye anakabiliwa na mashtaka ya rushwa, yuko chini ya shinikizo kwa kushindwa kwa usalama ambayo haikuzuia mashambulizi ya Hamas tarehe 7 Oktoba.

  6. Mwanamke wa Australia ashtakiwa kwa kuiba gari lililokuwa limebeba donati 10,000

    .

    Chanzo cha picha, Getty Images

    Mwanamke mmoja nchini Australia ameshtakiwa kwa kuiba gari la kubebea mizigo lililokuwa na donati 10,000 za Krispy Kreme.

    Gari hilo lilitoweka kwenye kituo cha petroli katika kitongoji cha Sydney saa za mapema tarehe 29 Novemba.

    Polisi walipata gari hilo likiwa limetelekezwa wiki moja baadaye - pamoja na maelfu ya donati zilizoharibika - kwenye maegesho ya magari.

    Walimkamata mwanamke huyo, 28, siku ya Alhamisi. Alinyimwa dhamana na anakabiliwa na mashtaka ikiwa ni pamoja na wizi wa gari na kuendesha gari licha ya kukosa leseni.

    Picha za CCTV za tukio hilo zinadaiwa kumuonyesha mwanamke huyo akiwa kwenye kituo cha huduma mwendo wa saa 04:00 kwa saa za eneo (17:00 GMT mnamo 28 Novemba) kabla ya kuingia ndani ya gari hilo la kusafirisha bidhaa ambalo halikuwa na mtuna kuanza kuliendesha.

    Haijulikani ikiwa alijua gari hilo lilikuwa na donati 10,000 ikiwa ni pamoja na zenye mapambo ya Krismasi.

  7. Mama aliyefungwa jela kwa miaka 20 aondolewa mashtaka ya mauaji ya watoto

    .

    Chanzo cha picha, EPA

    Mwanamke aliyepewa jina "mama mbaya zaidi wa Australia" aliyehukumiwa kwa kuwaua watoto wake wanne amefutiwa hukumu hiyo.

    Mahakama ya Juu ya New South Wales iliamua Alhamisi kwamba ushahidi uliotumiwa awali kumfunga jela Kathleen Folbigg "haukuwa wa kutegemewa".

    Mama huyo mwenye umri wa miaka 56 alisamehewa na kuachiliwa na serikali mwezi Juni, baada ya kukaa jela kwa miaka 20.

    Bi Folbigg alifurahishwa na habari za hivi punde lakini akasema uthibitisho wa kutokuwa na hatia "umepuuzwa na kufutiliwa mbali" kwa miongo kadhaa.

    "Mfumo ulipendelea kunilaumu badala ya kukubali kwamba wakati mwingine watoto wanaweza kufariki ghafla na bila kutarajia na kwa kuhuzunisha," alisema nje ya mahakama siku ya Alhamisi.

    Kesi ya Bi Folbigg imeelezwa kuwa mojawapo ya makosa makubwa zaidi ya haki nchini Australia.

    Ilihusu vifo vya watoto wake wachanga wanne Caleb, Patrick, Sarah, na Laura - ambao kila mmoja wao alifariki ghafla kati ya 1989 na 1999, wenye umri wa kati ya siku 19 na miezi 18. Waendesha mashtaka katika kesi yake walidai kuwa alikuwa amewachoma moto.

    Kesi hiyo ilitegemea ushahidi wa kimazingira, kwa kutumia shajara za Bi Folbigg - ambazo hazikuwahi kuchunguzwa na wanasaikolojia au wataalamu wa magonjwa ya akili - kumchora kama mama asiye na msimamo, anayekabiliwa na hasira.

    Mnamo 2003, alihukumiwa kifungo cha miaka 40 jela kwa mauaji ya Sarah, Patrick na Laura, na mauaji ya Kalebu.

    Baadaye ilipunguzwa hadi miaka 30 baada ya kukata rufaa, lakini Bi Folbigg alipoteza msururu wa changamoto za kisheria ambazo zilitaka kubatilisha hukumu yake.

    Mapema mwaka huu, uchunguzi wa kihistoria katika kesi yake ulihitimisha kuwa kulikuwa na shaka juu ya hatia yake, kutokana na matokeo ya kisayansi kwamba watoto wake wangeweza kufa kwa sababu za kawaida kwa sababu ya mabadiliko ya nadra sana ya jeni.

  8. Putin aiambia Urusi malengo yake ya vita hayajabadilika

    ,

    Chanzo cha picha, Reuters

    Rais wa Urusi Vladimir Putin amewaambia Warusi kwamba amani na Ukraine itafanyika tu "tutakapofikia malengo yetu".

    Anafanya mkutano wake mkuu wa kwanza wa habari tangu alipozindua uvamizi wake wa kwanza kamili wa Ukraine mnamo Februari 2022.

    Tukio hilo la kila mwaka halikufanyika mwaka jana.

    Sehemu ya kwanza ya hafla hii imelenga kile Bw Putin anachokiita "operesheni maalum ya kijeshi nchini Ukraine".

    Mawazo yake ya awali yalishughulikia umuhimu wa uhuru wa Urusi. "Kuwepo kwa nchi yetu bila uhuru haiwezekani. Haitakuwepo," aliambia mtangazaji wa Channel One inayodhibitiwa na serikali Yekaterina Berezovskaya.

    Bw Putin alisema uchumi wa Urusi ulikuwa imara wakati wa vita na mada ya mazungumzo haraka ikahamia Ukraine.

    Soma zaidi:

  9. Balozi wa Israel nchini Uingereza asema Israel haitakubali suluhisho la mataifa mawili

    .

    Chanzo cha picha, Getty Images

    Balozi wa Israel nchini Uingereza amesema nchi hiyo haitakubali suluhu ya mataifa mawili baada ya vita vya Gaza kumalizika.

    Alipoulizwa kuhusu matarajio ya Wapalestina kuwa na taifa lao, Tzipi Hotovely aliiambia Sky News: "Hapana kabisa."

    Suluhu ya mataifa mawili ni wazo kwamba kuanzisha Palestina huru pamoja na Israel kungetengeneza njia kwa watu hao wawili kuishi pamoja kwa amani.

    Sera hiyo inaungwa mkono na mshirika wa karibu wa Israel Marekani na mataifa mengine ya Magharibi.

    Alipoulizwa kuhusu jinsi gani kunaweza kuwa na amani katika eneo hilo bila suluhu ya mataifa mawili, Hotovely alisema "ulimwengu unapaswa kujua sasa kwamba Wapalestina hawakutaka kamwe kuwa na taifa karibu na Israel".

    Soma zaidi:

  10. Mkuu wa polisi wa Haiti yuko nchini Kenya kabla ya mpango wa kuisadia kupambana na magenge kuanza rasmi

    .

    Chanzo cha picha, Getty Images

    Maelezo ya picha, Kikosi cha kwanza kimepangwa kutumwa ifikapo Februari mwaka ujao,

    Mkuu wa polisi wa Haiti Frantz Elbe yuko nchini Kenya kwa ziara ya siku tatu kabla ya mipango ya kupeleka polisi kusaidia kupambana na ghasia za magenge katika nchi hiyo ya Caribbean.

    Bw Elbe na ujumbe wake Jumatano walikutana na mkuu wa polisi wa Kenya Japhet Koome na maafisa wengine wakuu wa usalama kwa ajili ya "majadiliano ya usalama wa nchi mbili", Huduma ya Polisi ya Kitaifa ya Kenya ilisema.

    Ziara hiyo ni sehemu ya maandalizi ya kutumwa kwa zaidi ya maafisa wa polisi 1,000 kutoka Kenya kwa ajili ya Ujumbe wa Kimataifa wa Kusaidia Usalama (MSS), Umoja wa Mataifa uliidhinisha miezi miwili iliyopita, kulingana na vyombo vya habari vya Kenya.

    Kikosi cha kwanza cha maafisa wapatao 300 kimepangwa kutumwa ifikapo Februari mwaka ujao, kulingana na gazeti la kibinafsi la The Star.

    Mwezi uliopita, bunge la Kenya liliidhinisha kutumwa kwa wanajeshi hao, lakini mahakama kuu ilirefusha amri ya kuzuia hatua hiyo, ikisubiri matokeo ya pingamizi la kisheria katika mpango huo.

    Mpango huo umekabiliwa na ukosoaji mkubwa, hasa kutokana na rekodi mbaya ya hatua za awali nchini Haiti na rekodi ya ukiukwaji wa haki na polisi wa Kenya.

    Kiongozi mkuu wa upinzani nchini Kenya, Raila Odinga, amelaani mpango huo lakini Rais William Ruto ameutetea akisema kuwa “Afrika ina nia ya kuchangia uhuru na usalama wa Haiti”.

    Karibu magenge 300 yanafanya kazi kote Haiti na 80% ya mji mkuu, Port-au-Prince, iko chini ya udhibiti wa magenge.

    Pia unaweza kusoma:

  11. Smyllum Park: Watawa na mlezi wapatikana na hatia ya kuwanyanyasa watoto yatima

    h

    Chanzo cha picha, PRESSTEAM

    Maelezo ya picha, Eileen Igoe na Sarah McDermott walipatikana na hatia katika Mahakama ya Airdrie Sheriff

    Watawa wawili na mfanyakazi wa kuwatunza watoto yatima wamepatikana na hatia ya kuwadhulumu vijana walio katika mazingira magumu katika kituo cha watoto yatima cha Uskochi.

    Sista McDermott, 79, Sista Eileen Igoe, 79, na mlezi Margaret Hughes, 76, waliwatesa watoto katika kituo cha malezi ya watoto yatima cha Smyllum Park, Lanark Uskochi kuanzia 1969 hadi 1981 kituo hicho kilipofungwa.

    Nyumba ya watoto yatima imekuwa katika mzozo wa madai ya unyanyasaji wa kihistoria.

    Mahakama ilisikiliza ushahidi kwamba watoto waliokuwa chini ya uangalizi wao walifanyiwa matukio kadhaa "ya kikatili na yasiyo ya kawaida".

    Tahadhari- maelezo haya yana maudhui ya kutatanisha

    Mwanamke mmoja aliiambia mahakama kuwa alipigwa na McDermott baada ya kuripoti kushuhudia kaka yake akidhulumiwa kingono kwenye choo katika kituo hicho cha watoto yatima.

    Alisema mfanyakazi wa kujitolea Brian Dailey, ambaye baadaye alifungwa jela miaka 15 kwa kuwadhulumu vijana, alimmyanyasa mtoto huyo wa miaka mitatu kwenye jumba moja.

    Badala ya kuchunguza unyanyasaji huo, McDermott alimpiga msichana huyo kofi na kumwambia kwamba alikuwa akimletea "tabia chafu za nyumbani katika sehemu nzuri ya Kikatoliki".

    Pia unaweza kusoma:

  12. Kampuni ya Kenya Power yatangaza kuanza kutoa umeme kwa mgao

    xx

    Chanzo cha picha, AFP

    Kampuni ya Kenya Power itaanza kutoa umeme kwa mgao, ikilenga eneo maeneo tofauti nchini ili kupunguza shinikizo dhidi ya miundombinu ya umeme iliyozeeka ambayo inatatizika kukidhi ongezeko la ghafla la mahitaji.

    Katika taarifa,kampuni hiyo imesema kuwa mpango wa kutoa umeme kwa mgao utaathiri kaunti za Kiambu, Machakos, Kajiado, Embu, Nyeri, Uasin Gishu, Nandi, Kisii, Migori na Kilifi. Maeneo hayo yatakuwa bila umeme kuanzia saa mbili asubuhi hadi saa moja usiku.

    Haya yanajiri baada ya Wizara ya Kawi kutangaza msururu wa hatua zinazokusudiwa kupunguza matatizo ya mara kwa mara ya umeme nchini, kisa cha hivi punde zaidi kikiwa Jumapili usiku.

    Mapema wiki hii, Waziri wa Kawi Davis Chirchir alisema usambazaji wa kawaida wa umeme ulisababishwa na mahitaji makubwa ya umeme, ambayo yalisababisha njia ya ugavi wa umeme katika eneo la magharibi mwa kenya kukatika.

    Waziri Chirchir alihusisha changamoto hiyo na ukosefu wa uwekezaji katika uzalishaji wa umeme na usambazaji wake.

  13. Wanaume washtakiwa kuwaua ndege 3,600 wakiwemo tai

    k

    Chanzo cha picha, Getty Images

    Maelezo ya picha, Tai mwenye upara aliwahi kutajwa kuwa katika hatarini katika maeneo mengi ya Marekani, lakini amerejea tena

    Wanaume wawili wa Marekani wameshtakiwa kwa kuwaua ndege wapatao 3,600 kinyume cha sheria, wakiwemo tai wenye vipara na wenye rangi ya dhahabu.

    Simon Paul na Travis John Branson wanadaiwa kuwapiga risasi ndege hao kwa miaka kadhaa na kuuza sehemu na manyoya kwenye soko haramu.

    Walishtakiwa kwa kula njama, kukiuka Sheria ya Ulinzi wa Tai na kufanya ulanguzi wa ndege hao kwa njia haramu.

    Wanaume hao wawili waliamriwa kufika mahakamani mwezi Januari.

    Mashtaka yaliyotolewa hadharani siku ya Jumatano yanadai kuwa waliwaua ndege kwenye Hifadhi ya Wahindi ya Flathead magharibi mwa Montana na kwingineko.

    Shtaka lilisema Bw Branson alituma jumbe za kujisifu kuhusu "kufanya uhalifu" na "kutekeleza mauaji", na kwamba wawili hao waliuza ndege na manyoya yao kwa "kiasi kikubwa cha pesa".

    Wakati fulani, wanaume hao waliweka mzoga wa kunguru ili kuvutia kundi la ndege kwenye eneo kabla ya kuwapiga risasi.

    Hati ya mashtaka inaorodhesha matukio 13 tofauti ya madai ya ukiukaji wa Sheria ya Ulinzi wa Tai, lakini waendesha mashtaka hawakubainisha ni aina gani nyingine za ndege ambao wanaume waliua au ikiwa wengi walikuwa wachache au walikuwa hatarini.

    Waendesha mashtaka walikataa kutoa maelezo zaidi walipotafutwa Jumatano

  14. Waandishi wa habari 17 waliuawa wakiripoti kuhusu vita vya Israel na Hamas

    Waandishi wa habari 17 wameuawa wakifuatilia vita vilivyoanza kati ya Israel na Hamas vilivyozuka tarehe 7 Oktoba, kulingana na shirika lisilo la kiserikali la Reporters Without Borders (RWB).

    13 kati yao waliuawa katika Ukanda wa Gaza, RWB inasema

    Lakini ikiwa utajumuisha waandishi wa habari waliouawa katika "mazingira ambayo hayajathibitishwa kuwa yanahusiana na majukumu yao", jumla ya wanahabari 63 wameuawa katika vita hivyo.

    Data ilikuwa sahihi kufikia tarehe 1 Desemba.

    xx

    Chanzo cha picha, Reuters

    Mapema mwezi huu, mashirika ya kutetea haki za binadamu yalisema Israel inapaswa kuchunguzwa kwani kuna uwezekano inatekeleza uhalifu wa kivita kutokana na kifo cha mwandishi habari nchini Lebanon mwezi Oktoba.

    Mwandishi wa habari wa Reuters Issam Abdallah, 37, alifariki katika shambulio la roketi la Israel kwenye mpaka wa Israel-Lebanon. Watu wengine sita walijeruhiwa.

    Mashirika ya kutetea haki za binadamu ya Amnesty International na Human Rights Watch yalisema uchunguzi umeonyesha kuwa waandishi wa habari huenda walishambuliwakimakusudi na wanajeshi wa Israel.

    Israel inakanusha kuwalenga waandishi.

  15. Mamia ya wapiganaji wa ADF wameuawa katika mashambulizi Uganda - Museveni

    Rais Yoweri Museveni anasema mashambulizi zaidi dhidi ya ADF yamefanywa tangu mauaji ya Septemba

    Chanzo cha picha, Reuters

    Maelezo ya picha, Rais Yoweri Museveni anasema mashambulizi zaidi dhidi ya ADF yamefanywa tangu mauaji ya Septemba

    Wanajeshi wa Uganda waliwauwa wapiganaji 200 wa ADF katika Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo, wakati operesheni za kijeshi za kuwaondoa wanamgambo wa kundi la Islamic State zikiendelea, rais wa Uganda alisema.

    "Tumekuwa tukifanya mashambulizi ya anga dhidi ya magaidi nchini Congo," Rais Yoweri Museveni alisema kwenye mtandao wa X, zamani wa Twitter, akiongeza kuwa karibu "200 kati yao waliuawa" katika mashambulizi yaliyofanywa tarehe 16 Septemba.

    Mashambulizi zaidi dhidi ya wapiganaji hao yametekelezwa tangu wakati huo, Bw Museveni aliongeza, bila kutoa maelezo zaidi.

    Msemaji wa jeshi la Uganda Felix Kulayigye ameliambia shirika la habari la AFP kwamba rais alikuwa akimaanisha wapiganaji wa kijihadi wa kundi la ADF.

    Mnamo mwaka wa 2021, Uganda na DR Congo zilianzisha mashambulizi ya pamoja ya kijeshi dhidi ya ADF mashariki mwa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo, lakini kundi hilo bado linafanya mashambulizi katika nchi zote mbili.

    Mnamo Oktoba, watalii wawili, mwanamume wa Uingereza na mwanamke wa Afrika Kusini kwenye fungate yao, pamoja na kiongozi wao, waliuawa walipokuwa safarini katika Mbuga ya Kitaifa ya Malkia Elizabeth nchini Uganda.

    Kundi la Islamic State lilidai kuhusika na shambulio hilo. Mwezi Juni, watu 42, wakiwemo wanafunzi 37, waliuawa katika shambulio dhidi ya shule ya sekondari magharibi mwa Uganda, ambalo pia lilihusishwa na ADF.

    Maelezo zaidi:

  16. Somalia yasherehekea kusamehewa deni la dola bilioni 4.5

    Waziri Mkuu Hamza Abdi Barre anasema afueni hiyo itaiwezesha Somalia kuwekeza katika maendeleo na kufufua uchumi

    Chanzo cha picha, Somalia Office of the Prime Minister/X

    Maelezo ya picha, Waziri Mkuu Hamza Abdi Barre anasema afueni hiyo itaiwezesha Somalia kuwekeza katika maendeleo na kufufua uchumi

    Serikali ya Somalia siku ya Jumatano ilifanya sherehe katika mji mkuu, Mogadishu, baada ya Shirika la Fedha Duniani (IMF) na Benki ya Dunia kutangaza msamaha wa deni wa dola bilioni 4.5 kwa nchi hiyo.

    Waziri Mkuu Hamza Abdi Barre anasema kwamba afueni hiyo ni "sawa na kumuondolea kila Msomali deni la zaidi ya dola 300".

    "Huu ni ushahidi kwamba nchi yetu na watu wetu wana uwezo wa kifedha, na kuvutia wawekezaji kutoka nje, na hatuko tena kwenye minyororo ya madeni," anaongeza.

    Mashirika hayo yalisamehe deni la Somalia chini ya mpango wa Nchi Maskini Wenye Madeni Mengi (HIPC), ambao uliundwa mwaka 1996 kusaidia nchi maskini zinazokabiliwa na mzigo wa madeni usioweza kurekebishwa.

    Msamaha wa deni wa $4.5bn pia unajumuisha msamaha wa wadai wengine wa kimataifa, wa nchi mbili na wa kibiashara.

    "Deni la nje la Somalia limeshuka kutoka asilimia 64 ya Pato la Taifa mwaka 2018 hadi chini ya asilimia 6 ya Pato la Taifa kufikia mwisho wa 2023," taasisi hizo zilisema katika taarifa yake ya pamoja.

    Waziri Mkuu Barre anasema afueni hiyo ni kubwa kwani itairuhusu Somalia kuwekeza katika mipango ya maendeleo, kufufua uchumi na kukopa pesa kutoka kwa taasisi za kimataifa zinazotoa mikopo.

  17. Kiongozi wa Hamas: Gaza bila Hamas baada ya vita ni 'udanganyifu'

    xx

    Chanzo cha picha, Reuters

    Hapo awali tumeangazia msimamo wa Israel kuhusu mpango wake wa Gaza baada ya mapigano.

    Kujibu kauli zilizotolewa na Israel, Ismail Haniyeh - ambaye anachukuliwa kuwa kiongozi wa kundi hilo ameonya mpango wowote wa baada ya vita huko Gaza bila Hamas ni "udanganyifu", alisema katika hotuba ya televisheni.

    "Tuko tayari kujadili mawazo au mipango yoyote ambayo inaweza kukomesha uchokozi wa [Israel] na kufungua ukurasa mpya wa kujadili uongozi wa Palestina katika Ukingo wa Magharibi na Ukanda wa Gaza," Haniyeh aliongeza, katika maoni yaliyotafsiriwa na shirika la habari la Reuters.

    Serikali ya Israel inasema moja ya malengo yake ya vita ni kuwaondoa kikamilifu Hamas.

    Hamas imeorodheshwa kama shirika la kigaidi katika nchi kadhaa, ikiwa ni pamoja na Marekani na Uingereza.

    Pia unaweza kusoma:

    • Je, Israel itaweza kuharibu mahandaki ya Hamas huko Gaza?
    • Chombo cha habari cha Hamas: Tunachojua kumhusu Abu Ubaida
    • Je, kuna vikundi vingapi vyenye silaha huko Gaza na ni nani?
    • Kwa nini vita vya sasa vya Gaza ni tofauti na vita vilivyopita?
  18. Mshauri wa usalama wa taifa wa Marekani afanya mazungumzo Saudi Arabia

    Jake Sullivan

    Chanzo cha picha, EPA

    Mshauri wa usalama wa taifa wa Marekani Jake Sullivan amefanya mazungumzo na Mwanamfalme wa Saudia Mohammed bin Salman alipotembelea Saudi Arabia.

    Majadiliano yalilenga kuhusu vita vya Israel-Gaza na masuala mengine ya kikanda, ikiwa ni pamoja na juhudi za kuzuia mashambulizi ya Houthi dhidi ya meli za kibiashara katika Bahari Nyekundu.

    Shirika la habari la Reuters linamnukuu afisa mmoja akisema wawili hao walijadili juhudi za "kudumisha utulivu katika eneo lote na kuzuia mzozo wa Israel na Hamas kuenea".

    Afisa huyo anaongeza kuwa Sullivan alilenga kuendeleza kazi ambayo tayari inaendelea ili kujaribu kuleta amani endelevu kati ya Waisraeli na Wapalestina.

    Mshauri huyo wa usalama wa taifa sasa anatarajiwa kusafiri hadi Israel, ambako atarajiwa kufanya mazungumzo na Waziri Mkuu wa Israel Benjamin Netanyahu na wajumbe wa baraza la mawaziri la vita.

  19. Tazama: Wakati tembo alipovunja dirisha la gari akitafuta chakula nchini Sri Lanka

    Maelezo ya video, Tazama tembo alivyovunja dirisha la gari akitafuta chakula nchini Sri Lanka

    Huu ndio wakati ambapo familia moja iliachwa na mshangao baada ya tembo kushambulia gari lao na kuvunja dirisha akitafuta chakula, walipokuwa likizoni nchini Sri Lanka.

    Video inaonyesha mnyama huyo akitoka kwenye miti katika Hifadhi ya Kitaifa ya Yala, kabla ya kukimbia ghafla kuelekea alipokuwa Kasun Basnayake na familia yake kwenye gari walilokuwa wamekodisha.

    Kisha alitumia pembe zake kuvunja dirisha la dereva na kufika ndani ya gari huku mkonga wake ukitafuta chakula. Kasun, kutoka Perth, Australia Magharibi, aliiambia BBC: "Alianza kunusa ,kuzunguka miguu yetu kwa ajili ya chakula na dereva akatuambia tumpe chochote tulichokuwa nacho kwa hiyo nikamlisha sandwichi iliyobaki ya mwanangu."

    "Aliniambia nivitupe vingine dirishani ndivyo nilivyofanya na dereva kisha akafanikiwa kuondoka kwa kasi... Mikate hiyo ya sandwish na vibanzi pengine ziliokoa maisha yetu."

    Hakuna aliyejeruhiwa katika tukio hilo

  20. Israel yasema vita vya Gaza vitaendelea 'ikiwa itapata au kukosa’ uungwaji mkono wa kimataifa

    Benjamin Netanyahu

    Chanzo cha picha, EPA

    Maelezo ya picha, Waziri Mkuu wa Israel Benjamin Netanyahu

    Hakuna kitakachozuia Israel kuendelea na vita dhidi ya Hamas, ikiwa ni pamoja na "shinikizo la kimataifa", Waziri Mkuu Benjamin Netanyahu anasema, katika video iliyotumwa kwenye mtandao wa X (zamani Twitter).

    Akizungumza na wanajeshi katika kambi ya kijeshi kusini mwa Israel, anasema Israel "itaendelea hadi mwisho, hadi ushindi, hadi kuondolewa kwa Hamas".

    Netanyahu anaongeza: "Nataka kuweka bayana kile nilichosema hivi punde kwa kamanda uwanjani - tutaendelea na vita hadi mwisho.

    "Hakuna mjadala kuhusiana na hilo hata kidogo. Nasema hivi pia nikizingatia maumivu makubwa [ya askari waliouawa], lakini pia katika kukabiliana na shinikizo la kimataifa.

    "Hakuna kitakachotuzuia, tutaenda hadi mwisho, mpaka ushindi upatikane."

    Maelezo zaidi: