Hii ni tovuti ya maandishi pekee ambayo inatumia data kidogo. Tazama toleo kuu la tovuti likijumuisha picha na video zote.

Bofya kuelekea tovuti kuu

Pata maelezo zaidi kuhusu toleo hili la linalotumia kiasi kidogo cha data

Rais Gotabaya Rajapaksa ajiuzulu baada ya kutoroka Sri Lanka

Gotabaya Rajapaksa amejiuzulu kama rais wa Sri Lanka baada ya kukimbilia Singapore kufuatia maandamano makubwa ya kupinga utawala wake.

Moja kwa moja

  1. Tunakomea hapo kwa leo hadi kesho kwaheri.

  2. Sri Lanka: Rais Gotabaya Rajapaksa ajiuzulu baada ya kutoroka Sri Lanka

    Gotabaya Rajapaksa amejiuzulu kama rais wa Sri Lanka baada ya kukimbilia Singapore kutokana na maandamano makubwa nyumbani kwake kupinga utawala wake.

    Inaaminika alitaka kuondoka Sri Lanka kabla ya kuachia ngazi ili kuepusha uwezekano wa kukamatwa chini ya utawala mpya.

    Aliwasili Singapore baada ya kwanza kuelekea Maldives Jumanne usiku. Taarifa zinasema ameandamana na mkewe na walinzi wawili.

    Katika mji mkuu wa Colombo, waandamanaji walipokea taarifa za kujiuzulu kwake kwa vifijo na nderemo.

    Serikali ya Singapore ilisema "aliruhusiwa kuingia kwa ziara ya kibinafsi".

    Haijabainika iwapo Bw Rajapaksa atasalia au atahamia mahali pengine.

    Gharama ya chakula, mafuta na bidhaa zingine za kimsingi imepanda na raia wa Sri Lanka wanakabiliw ana wakati mgumu.

    "Hajaomba hifadhi na wala hajapewa hifadhi yoyote. Singapore kwa ujumla haitoi maombi ya hifadhi," Wizara ya mambo ya nje ya Singapore ilisema, ikithibitisha kuwasili kwa kiongozi huyo nchini humo.

    Bw. Rajapaksa ambaye kama rais ana kinga ya kutoshtakiwa, inaaminika alitaka kuondoka Sri Lanka kabla ya kujiuzulu ili kuepusha uwezekano wa kukamatwa na utawala mpya.

    Kaimu Rais Ranil Wickremesinghe leo Alhamisi aliweka amri ya kutotoka nje kwa siku ya pili ili kuzima maandamano.

    Maelezo zaidi:

  3. Afrika yakabiliwa na ongezeko la magonjwa kati ya wanyama na binadamu - WHO

    Shirika la Afya Duniani linaonya kuwa Afrika inakabiliwa na hatari inayoongezeka ya milipuko ya magonjwa ambayo huenea kutoka kwa wanyama hadi kwa watu.

    Linasema milipuko ya magonjwa ya aina hiyo imeongezeka kwa zaidi ya 60% katika muongo uliopita na kiwango kikubwa kilirekodiwa tangu 2019.

    Visa vingi vimehusisha virusi vya Ebola, magonjwa mengine ya virusi ya kuvuja damu, homa ya dengue, kimeta na tumbili.

    Mkurugenzi wa WHO kanda ya Afrika Matshidiso Moeti alisema kuna haja ya kuchukua hatua sasa kukomesha Afrika kuwa kitovu cha magonjwa ya kuambukiza yanayoibuka.

    WHO inasema miongoni mwa sababu zinazochangia kuenea kwa magonjwa hayo ni ongezeko la kasi la watu, ongezeko la mahitaji ya chakula kinachotokana na wanyama na uvamizi wa makazi ya wanyamapori.

    Soma:

    • Jinsi wanyama wanavyohusishwa katika mlipuko wa magonjwa mapya
    • Virusi vya corona: Kuna hofu ya kuongezeka kwa magonjwa kutoka kwa wanyama hadi kwa wanadamu
  4. Upinzani washauri serikali ya Tanzania kuingilia kati kupanda kwa gharama ya maisha

      • Author, Aboubakar Famau
      • Nafasi, BBC News, Dodoma

    Chama cha upinzani nchini Tanzania Chadema, kimeishauri serikali ya nchi hiyo kuchukua hatua za kupunguza gharama za maisha hasa katika kipindi hiki ambacho bei za mafuta zimepanda.

    Mjumbe wa kamati kuu ya Chadema John Heche amesema, kupanda kwa bei za mafuta haisababishwi na vita vitavyoendelea kati ya Urusi na Ukraine

    Katika mkutano na waandishi wa habari ulifanyika hii leo jijini Dodoma, Bw. Heche, ameitaka serikali kuchukua hatua, kupunguza angalau shilingi 600 kwa kila lita ya mafuta.

    Heche pia, ameishauri serikali kupunguza baadhi ya matumizi ambayo sio ya lazima kama sehemu ya kupunguza gharama za maisha.

    ‘’Katika mojawapo ya hatua za kukabiliana na ongezeko la bei za mafuta hapa nchini, Serikali imetoa ruzuku ya Shilingi billioni 100 kwa mwezi Julai mwaka 2022 ambayo imeelekezwa katika udhibiti wa bei ya mafuta ya petroli na dizeli ili kukabiliana na mfumko wa bei,’’alisema.

    Kwa mujibu wa ofisi ya taifa ya takwimu Mfumko wa Bei wa Taifa kwa miezi kadhaa iliyopita, unaonekana kuongezeka hadi asilimia 3.8 kutoka asilimia 3.6.

    Maelezo zaidi:

  5. Ni rasmi - nyama choma inaingia kwenye kamusi

    Kutembelea Kenya bila kuonja ladha ya nyama choma basi safari yako haijakamilika, sasa unaweza kuitafuna nyama huku ukijua kwamba waandishi wa kamusi kutoka Oxford wameiweka katika kamusi yao ya Kiingereza ambayo maarufu duniani.

    Ni mojawapo ya maneno 200 mapya yaliyoongezwa kutoka katika Kiingereza cha Afrika Mashariki katika toleo lao lililoboreshwa la hivi karibuni la Kamusi ya Kiingereza ya Oxford (OED).

    Kamusi ya Oxford ni moja ya vyanzo vinavyoheshimiwa sana vya lugha.

    Maneno mengine ambayo sasa yanatambulika katika kamusi ni:

    chapo - chapati nyembamba

    chips mayai – kwa Tanzania na Kenya –viazi vya kukaanga vilivyochanganywa na mayai wakati wa kupika.

    katogo - jina la mlo wa kawaida ambao ni kifungua kinywa cha asubuhi nchini Uganda unaojumuisha matoke iliyochemshwa kwenye sufuria na viungo vingine mbalimbali.

    Mbali na hayo maeneo mengine ni kama, sambaza maana yake "kushirikisha au kutuma kitu" sasa iko kwenye kamusi hiyo ya Oxford pamoja na kuweka lami (tarmacking) ambayo ni "kitendo au mchakato wa kutembea mitaani kutafuta kazi".

    Kama unashirikiana kufanya kazi na mtu unaweza kuiita collabo kwa kujua kwamba ni Kiingereza sahihi. Na ikiwa ungependa kusherehekea kuingizwa kwa maneno haya basi unaweza kupiga kelele "oyee!" – neno ambalo kwa mujibu wa wataalam wa kamusi ni njia ya kueleza "kutia moyo au kuunga mkono”

  6. WHO yaishauri Tanzania kupeleka sampuli za ugonjwa usiojulikana ili uchunguzwe

    Shirika la Afya Duniani (WHO) limeishauri Tanzania kupeleka sampuli za ugonjwa ambao haukutajwa jina ulioripotiwa katika maeneo ya kusini mwa nchi hiyo kwenye maabara yake ya rufaa nchini Senegal kwa uchunguzi zaidi.

    Shirika la afya duniani linasema kuwa linafanya kazi kwa karibu na mamlaka ya Tanzania ili kubaini ugonjwa huo uliosababisha vifo 3 vya watu watatu mpaka sasa.

    Licha ya kuwa nchi hiyo kufanya vipimo vya virusi vya Marburg na Ebola lakini viwango vya WHO ni kwamba sampuli za kesi zinazoshukiwani lazima zipelekwe katika Maabara ya Pasteur nchini Senegal kwa uthibitisho kamili.

    Tanzania imeondoa magonjwa yote mawili ya virusi katika uchunguzi wake ingawa majaribio zaidi yatasaidia kuamua jibu linalohitajika ili kudhibiti kuenea zaidi.

    Uchunguzi mpya wa WHO umezidi kufichua kuwa Afrika inakabiliwa na tishio kubwa la magonjwa ambayo husambaa kutoka kwa wanyama hadi kwa wanadamu.

    WHO inasema kuna ongezeko la 63% la idadi ya milipuko ya zoonotic (magonjwa yanayosambaa kutoka kwa Wanyama had bindamu) katika eneo la Afrika katika kipindi cha mwaka 2012-2022 ikilinganishwa na miaka kumi iliyopita.

    Ebola na homa kama hizo zilichangia karibu 70% ya milipuko hii.

    Soma:

  7. Serikali ya Kenya yatangaza bei mpya ya mafuta

    Bei ya mafuta nchini Kenya haitaraiwi kubadilika katika siku 30 zijazo kufuatia agizo la Rais Uhuru Kenyatta.

    Katika taarifa ya Alhamisi, Julai 14, iliyotiwa saini na msemaji wa Ikulu, Kanze Dena, bei ya Super Petrol itasalia kuwa Ksh159.12 kwa lita.

    Dizeli itaendelea kuuzwa kwa shilingi 140 kwa lita huku Mafuta ya Taa ikiendelea kuuzwa kwa shilingi 127.94.

    Bei hizo hazijabadilika baada ya Rais Kenyatta kuidhinisha ruzuku ya mafuta ya shilingi bilioni 16.7.

    Maelezo zaidi:

    • Wazijua bidhaa tatu zilizopanda bei Tanzania, Kenya na Uganda?
    • Bei za vyakula Kenya: Kwa nini zimepanda sana?
    • 'Wakati mwingine tunashinda bila chakula '
  8. Habari za hivi punde, Asanteni kwa maombi yenu - Omanyala

    Mwanariadha mwenye kasi zaidi barani Afrika Mkenya Ferdinand Omanyala amethibitisha kwamba atakuwa njiani kwenda kushiriki Mashindano ya Riadha ya Dunia yatakayoanza Marekani siku ya Ijumaa.

    Hapo awali ilionekana kana kwamba Omanyala huenda asishiriki katika mbio za mita 100 kwani visa yake ilikuwa haijatolewa - lakini alipata hati hiyo dakika za mwisho na anatarajiwa kuwasili saa chache kabla ya kundi la kwanza.

    "Asanteni sana kwa maombi yenu," alisema kwenye Twitter.

    "Changamoto za Visa zinakabiliwa na Wakenya na watu wengine kila siku, haikuwa tofauti kwangu."

    Omanyala atasafiri kwa ndege kutoka Kenya saa kumi na mbili jioni ya leo na anatarajiwa kuwasili Eugene chini ya saa tatu kabla ya mbio za mita 100 za wanaume kuanza jioni siku ya kwanza ya Mashindano ya Dunia.

    Hata hivyo, Omanyala atahitaji kutumia forodha ya Marekani, kusafiri hadi uwanjani.

  9. Aliyekuwa mkuu wa ujasusi wa Gambia ahukumiwa kifo

    Jaji mmoja nchini Gambia amemhukumu kifo aliyekuwa mkuu wa upelelezi wa nchi hiyo, Yankuba Badjie, na maafisa wengine wanne wa usalama kwa mauaji ya mwaka 2016 ya mwanaharakati wa kisiasa katika siku za mwisho za utawala wa kikatili chini ya Rais wa zamani Yahya Jammeh.

    Mwanaharakati, Ebrima Solo Sandeng - kiongozi mkuu katika chama cha upinzani cha United Democratic Party - alikuwa amekamatwa wakati wa maandamano ya kuipinga serikali.

    Alikufa gerezani siku mbili baadaye, baada ya kupigwa na kuteswa.

    Kifo chake kilichochea wimbi la hasira ya wananchi ambayo hatimaye ilisababisha kuondolewa madarakani kwa Rais Jammeh baada ya miaka 22 madarakani.

    Bw Jammeh alikimbia mwaka wa 2017 hadi Equatorial Guinea, ambako bado yuko uhamishoni.

    Soma zaidi:

  10. Jeshi la Urusi lapoteza kasi huko Donbas - ujasusi wa Uingereza

    Wanajeshi wa Urusi wanaendelea kupiga roketi na mizinga katika eneo la Donbas.

    Katika baadhi ya maeneo, mashambulizi ya majaribio ya makampuni madogo hadi kwenye kikosi yanaendelea, Wizara ya Ulinzi ya Uingereza inaripoti.

    ‘’Walakini, katika saa 72 zilizopita, hawajafanya maendeleo makubwa na hatari ya kupoteza kasi waliyopata baada ya kuchukua eneo la Lysychansk,’’ taarifa inasema.

    Ujasusi wa Uingereza unasema kuwa magari, silaha na mbinu zilizopitwa na wakati za enzi ya Usovieti zinazotumiwa na vikosi vya Urusi haziwaruhusu kupona haraka au kupata kasi.

    Labda zitumiwe kwa idadi kubwa, ambayo Urusi haiwezi kufanya hivi sasa, ripoti inasema.

    ‘’Licha ya mazungumzo ya Julai 13 kati ya wajumbe wa Ukraine, Urusi, Uturuki na Umoja wa Mataifa juu ya usafirishaji wa nafaka nje ya nchi na mazungumzo ya hivi karibuni yaliyofaulu juu ya kubadilishana wafungwa, matarajio ya mazungumzo mapana juu ya kumaliza mzozo bado ni mdogo,’’ Wizara ya Ulinzi ya Uingereza inaamini.

    Soma zaidi:

  11. Roketi tisa zarushwa huko Mykolaiv, na kuharibu hoteli na kituo cha madukani

    Eneo la Mykolaiv limekabiliwa na moto mkubwa wa roketi asubuhi.

    Kulingana na habari ya awali, makombora 9 kutoka kwa mfumo wa makombora ya kupambana na ndege ya S-300 yalirushwa kwenye kituo cha eneo la Mykolaiv, OVA iliripoti.

    Hivi sasa, kinachojulikana ni kuhusu uharibifu wa taasisi mbili za elimu na kituo cha miundombinu ya usafiri na hoteli.

    Meya wa Mykolaiv, Oleksandr Sienkovych, alifafanua kuwa hoteli ‘’Mykolaiv’’ katikati mwa jiji imeharibiwa.

    Kituo cha ununuzi na burudani kilichopo mkabala pia kiliharibiwa na vifusi na vumbi.

    Inasemekana kwamba mtu mmoja alijeruhiwa, lakini hapakuwa na waathirika, OVA aliongeza.

    Wakati huo huo, watu 4 walifariki na 2 walijeruhiwa kwa sababu ya kushambuliwa kwa kijiji cha Novoselivka katika jamii ya Pervomaysk siku moja kabla.

    Soma zaidi:

  12. Habari za hivi punde, Mwanariadha mwenye kasi zaidi Afrika kutoshiriki mashindano ya Dunia

    Mwanariadha mwenye kasi zaidi barani Afrika Ferdinand Omanyala hatashiriki Mashindano yajayo ya Riadha ya Dunia huko Eugene, Oregon, kwa sababu hakupokea visa yake kwa wakati ili kusafiri hadi Marekani, msemaji wake alisema Alhamisi.

    Mwanariadha huyo wa Kenya alijumuishwa katika orodha ya watakaoingia kwenye mbio za mita 100 kwenye michuano hiyo itakayoanza Ijumaa.

    "Cha kusikitisha, sitashiriki mashindano ya mwaka huu ya dunia huko Oregon. Sikupata visa yangu kwa wakati kwa ajili ya kusafiri," Omanyala alisema kwenye taarifa kupitia msemaji wake.

  13. Maeneo ya Urusi yasajili watu wa kujitolea kushiriki katika vita

    Urusi inaweza kuwa iliamuru maeneo ya Urusi kusajili watu wakujitolea kupigana katika vita, badala ya kutangaza uhamasishaji wa sehemu au kamili nchini Urusi, wataalam katika Taasisi ya Marekani ya Utafiti wa Vita (ISW) wanaandika katika ripoti nyingine.

    Mwandishi wa habari wa vita wa Urusi na mwanablogu Maxim Fomin alisema kuwa ‘’uhamasishaji wa hiari’’ umeanza nchini Urusi, ambapo kila eneo lazima liunde angalau kikosi kimoja cha kujitolea.

    Neno ‘’kujitolea’’ labda linamaanisha kwamba Kremlin iliamuru maeneo 85 ya serikali, ikiwa ni pamoja na Sevastopol iliyokaliwa na Crimea, kusajili na kuwahamasisha kifedha watu wa kujitolea kuunda vikosi vipya, badala ya uhamasishaji wa jumla na kuandaa rasimu ya wanajeshi wa akiba.

    Kulingana na ripoti za vyombo vya habari vya Urusi, mamlaka za kikanda huajiri wanaume walio na umri wa chini ya miaka 50 (au 60 kwa taaluma fulani za kijeshi) kwa mkataba wa miezi sita na kutoa wastani wa mshahara wa rubles 220,000 hadi 350,000 kwa mwezi ($ 3,750-6,000).

    Wataalamu wa ISW wamehesabu kwamba ikiwa kila eneo litaunda angalau kitengo kimoja cha kijeshi cha watu 400, jumla ya idadi ya ‘’wajitolea’’ inaweza kufikia watu 34,000.

    Soma zaidi:

    Urusi naUkraine: Mengi zaidi

    • MOJA KWA MOJA:Biden amuonya Putin: ''Madikteta watagharamika
    • YA MSINGI:Mzozo wa Ukraine: Kwanini Urusi inaivamia Ukraine na Putin anataka nini?
    • UFAFANUZI:Mzozo wa Ukraine: Swift ni nini na kwa nini kuipiga marufuku Urusi ni muhimu sana?
    • UCHAMBUZI:Mzozo wa Ukraine: Putin humsikiliza nani?
    • KWENYE RAMANI:Uvamizi wa Ukraine: Shambulio la Urusi kwenye ramani
    • ZELENSKY:Volodymyr Zelensky: Mfahamu rais wa Ukraine aliyeacha umaarufu wake wa TV na kuingia kwenye siasa
    • PUTIN:Vladimir Putin: Rais wa Urusi aliyeagiza shambulio Ukraine
  14. Maafisa wakuu wa Fukushima waagizwa kulipa fidia ya $97bn

    Wakubwa wa zamani wendeshaji wa kinu cha nyuklia cha Fukushima wameagizwa kulipa yen trilioni 13 (£80bn) kwa kushindwa kuzuia maafa.

    Wakubwa hao kutoka Kampuni ya Nishati ya Umeme ya Tokyo (Tepco) walishtakiwa na washikadau kuhusu msukosuko wa 2011 ambao ulisababishwa na tsunami.

    Mahakama iliamua kwamba watendaji wangeweza kuzuia ajali hiyo ikiwa wangeendeleza uangalifu unaostahili.

    Tepco aliomba radhi lakini akakataa kuzungumzia kesi hiyo mahakamani.

    ‘’Tunaomba radhi kwa mzigo mkubwa na wasiwasi mkubwa kwa ajali iliyotokea katika Kituo cha Nguvu za Nyuklia cha Fukushima Daiichi cha Tepco Holdings kwa wakaazi wa eneo hilo na jamii kwa ujumla,’’ taarifa ilisema.

    Walalamikaji waliibuka kutoka kwa mahakama ya Tokyo wakiwa wameshikilia mabango yaliyosomeka ‘’washikadau wanashinda’’ na ‘’wajibu unatambuliwa’’.

    Mawakili wao walisema wanaamini kuwa hiyo ndiyo kiasi kikubwa zaidi cha fidia kuwahi kutolewa katika kesi ya madai nchini Japan.

    Soma zaidi:

  15. Uber yashtakiwa na wanawake 550 kwa madai ya unyanyasaji wa kijinsia

    Uber inashitakiwa nchini Marekani na wanawake 550 wanaodaiwa kushambuliwa na madereva kwenye jukwaa la kubebea abiria.

    Jalada hilo linajumuisha madai kuwa abiria wanawake "walitekwa nyara, kushambuliwa kingono, kupigwa kingono, kubakwa, kufungwa gerezani kwa madai ya uongo, kuviziwa, kunyanyaswa, au kushambuliwa vinginevyo na madereva wa Uber".

    Kesi hiyo iliwasilishwa katika Mahakama Kuu ya Kaunti ya San Francisco siku ya Jumatano.

    "Unyanyasaji wa kijinsia ni uhalifu wa kutisha na tunachukulia kila ripoti kwa uzito, "msemaji wa Uber aliiambia BBC.

    "Hakuna kitu muhimu zaidi kuliko usalama, ndiyo maana Uber imeunda vipengele vipya vya usalama, imeanzisha sera zinazowalenga waathirika, na kuwa wazi zaidi kuhusu matukio mazito. Ingawa hatuwezi kutoa maoni kuhusu kesi zinazosubiriwa, tutaendelea kuweka usalama kipaumbele katika kazi yetu," waliongeza.

    Malalamiko hayo, yaliyowasilishwa na mawakili katika kampuni ya mawakili ya Slater Slater Schulman, yalidai kuwa unyanyasaji huo wa kingono ulifanyika katika "majimbo mengi".

    Pia ilisema kwamba angalau kesi zingine 150 zinazowezekana "zinachunguzwa kikamilifu."

    Kesi hiyo inadai kuwa mapema mwaka wa 2014 Uber ilifahamu kuwa madereva wake walikuwa wakiwanyanyasa kingono na kuwabaka abiria wa kike.

    Lakini jalada linadai kuwa kampuni ilitanguliza "ukuaji kuliko usalama wa wateja".

    "Mtindo mzima wa biashara wa Uber unategemea kuwapa watu safari salama, lakini usalama wa wateja haukuwa jambo lao kamwe - ukuaji ulikuwa, kwa gharama ya usalama wa abiria wao," Adam Slater, mshirika mwanzilishi wa Slater Slater Schulman, alisema.

    Mwezi uliopita, Uber ilitoa Ripoti yake ya pili ya Usalama ya Marekani, ambayo ilionyesha kulikuwa na matukio 998 ya unyanyasaji wa kijinsia, ikiwa ni pamoja na ripoti za ubakaji 141, mwaka wa 2020.

  16. Mwanaume ashtakiwa kwa kumbaka msichana wa miaka 10 aliyekataliwa kutoa mimba

    Mwanamume mmoja katika jimbo la Ohio nchini Marekani ameshtakiwa kwa kumbaka msichana mwenye umri wa miaka 10 ambaye alilazimika kuvuka mipaka ya jimbo kwa ajili ya kutoa mimba baada ya jimbo lake kuzuia utaratibu huo.

    Gershon Fuentes, 27, alifikishwa mahakamani huko Columbus siku ya Jumatano.

    Masaibu ya msichana ambaye hakutajwa jina yamevuta hisia za kimataifa.

    Rais wa Marekani Joe Biden alitoa mfano huo katika Ikulu ya White House alipokuwa akipinga vizuizi vya utoaji mimba, lakini wakosoaji walikuwa wamehoji ikiwa ni uwongo.

    Mamilioni ya wanawake na wasichana walipoteza haki ya muda mrefu ya kikatiba ya kutoa mimba baada ya uamuzi wa Mahakama ya Juu ya Marekani mwezi Juni.

    Katika hotuba yake Ijumaa iliyopita kulaani uamuzi huo, Rais Biden alitoa ripoti ya kesi ya mtoto huyo, akisema kwa hasira: ‘’Fikiria kuwa msichana huyo mdogo!’’.

    Saa chache baada ya uamuzi wa Mahakama ya Juu, wabunge wa Ohio waliharamisha uavyaji mimba baada ya wiki sita, bila ubaguzi wowote kwa waathiriwa wa ubakaji au kulawitiwa.

    Mtoto huyo alikuwa na ujauzito wa wiki sita na siku tatu, kulingana na gazeti la Indianapolis Star.

    Akirejelewa na daktari wa unyanyasaji wa watoto huko Ohio, msichana huyo alitembelea kliniki huko Indianapolis, Indiana, kuavya mimba mnamo Juni 30.

    Ingawa juhudi zinaendelea ili kuzuia ufikiaji wa utoaji mimba katika jimbo jirani la Ohio, utaratibu bado unasalia kuwa halali huko.

    Kufuatia uamuzi wa Mahakama ya Juu, majimbo 26 ya Marekani yameweka vikwazo vikali vya utoaji mimba au yanatarajiwa kufanya hivyo katika wiki na miezi ijayo.

    Soma zaidi:

  17. Hujambo na karibu katika matangazo yetu ya moja kwa moja