Hii ni tovuti ya maandishi pekee ambayo inatumia data kidogo. Tazama toleo kuu la tovuti likijumuisha picha na video zote.

Bofya kuelekea tovuti kuu

Pata maelezo zaidi kuhusu toleo hili la linalotumia kiasi kidogo cha data

Rais Samia: 'Urais ni taasisi sio mtu'

Rais wa Tanzania Samia Suluhu Hassan amewataka mawaziri na naibu mawaziri kuheshimu taasisi ya urais na mamlaka yake bila ya kujali nani anaiongoza taasisi hiyo kwani mamlaka na uongozi hutoka kwa mungu

Moja kwa moja

  1. Na kufikia hapo tunakamilisha matangazo haya ya moja kwa moja kwa leo. Hadi kesho Kwaheri.

  2. Bodi ya Tuzo ya Nobel inamtaka Abiy kukomesha vita vya Ethiopia

    Kamati ya Nobel ya Norway imeungana jamii ya kimataifa kumtaka Waziri Mkuu wa Ethiopia kumaliza vita vya wenyewe kwa wenyewe vilivyodumu kwa miezi 14 nchini humo.

    Katika taarifa kwa shirika la habari la AFP ilisema Abiy Ahmed - ambaye alishinda Tuzo ya Amani ya Nobel mwaka 2019 - alikuwa na jukumu maalum la kukomesha umwagaji damu.

    Mwaka mmoja tu baada ya kupata tuzo kwa kumaliza mzozo wa muda mrefu kati ya nchi yake na Eritrea, Bw Abiy alituma wanajeshi kupigana na waasi katika eneo la kaskazini la Tigray.

    Vita hivyo vimewalazimisha mamilioni ya watu kutoka makwao. Serikali imekuwa ikilaumiwa kwa kuzuia misaada na kumekuwa na tuhuma nyingi za ukatili unaofanywa na pande zote mbili.

    Msemaji wa Bw Abiy Billene Seyoum hapo awali alisema kuwa Tuzo ya Amani ya Nobel haikuwa "kifungo cha kutochukua hatua wakati nchi inatishiwa".

    Wito wa Kamati hiyo unatarajiwa kuongeza shinikizo la kutafuta suluhisho la amani katika vita hivyo.

  3. Wiliam Lukuvi atwikwa majukumu mapya

    Rais Samia Suluhu Hassan ametangaza nafasi mpya ya Lukuvi siku ya Alhamisi Januari 13, wakati wa mkutano maalum na mawaziri na manaibu mawaziri walioteuliwa hivi karibuni uliofanyika katika ukumbi wa mikutano wa Hazina mjini Dodoma.

    Samia alisema ni sekta chache ambazo zina athari za moja kwa moja kwa wananchi na hivyo ni lazima zipewe kipaumbele na uratibu wa karibu.

    Mkuu huyo wa nchi alizitaja sekta hizo kuwa ni, elimu, afya, maji, umeme vijijini na nyingine zinazogusa moja kwa moja kwa wananchi.

    "Kwa wale ambao wamewahi kuwa mawaziri na manaibu waziri siku za nyuma wanafahamu kwamba kulikuwa na ukosefu wa uratibu na ushirikiano kati ya sekta za serikali, kila mtu alikuwa akifanya yake," "Hii ilisababisha kutofikia malengo ambayo yalipaswa kufikiwa kwa sababu ukiuliza matokeo ya mradi fulani, kila mmoja anawasilisha sehemu yake ya mradi," alisema.

    Aidha, Samia alisema Lukuvi atasaidia katika kuratibu utendaji wa ngazi za juu za mawaziri ambapo makatibu wakuu bado watakuwa chini ya Ofisi ya Katibu Mkuu Kiongozi.

  4. 'Fungua vitabu na ufunge miguu yako,' waziri anawaambia wasichana

    Waziri wa afya wa Limpopo nchini Afrika Kusini anakosolewa kwa ujumbe wake wa elimu ya ngono kwa wasichana wakati wa ziara ya shule.

    Phophi Ramathuba aliwaambia wasichana "kufungua vitabu na kufunga miguu yao" - wa uwazi kama njia ya kuwahimiza wajiepushe na maambukizi ya virusi vya Ukwimwi (VVU/UKIMWI).

    Alisema wasichana hao walikuwa wakishawishiwa na wanaume wazee kwa kutumia vitu vya bei ghali kama vile wigi za bei ghali na simu za kisasa.

    Ujumbe wake hatahivyo umekosolewa kwa kuwatwika wasichana hao pekee mzigo wa kuwajibikia vitendo vya kingono, huku baadhi ya watu katika mitandao ya kijamii wakisema pia ni jukumu la wavulana na wanaume kukomesha mienendo ya kushawishi wasichana kingono.

    Waziri huyo alitetea ujumbe wake, akisema ulitolewa nje ya muktadha na kwamba pia aliwashauri wavulana kutojihusisha na ngono, liliripoti gazeti la Times Live.

    Takwimu katika majimbo ya Afrika Kusini mwaka jana zilionyesha kumekuwa na ongezeko kubwa la idadi ya mimba za utotoni wakati wa janga hilo.

    Utekelezaji wa programu za elimu ya ngono katika baadhi ya shule ulisitishwa baada ya pingamizi kutoka kwa wazazi.

    Sheria ya uhalifu wa kingono nchini Afrika Kusini imewekwa kuwachukulia hatua wahalifu na sajili ya wahalifu inapatikana kwa taasisi, lakini waathiriwa wengi wanaogopa kuripoti uhalifu huu.

  5. Emirates yarejesha safari za ndege kwenda nchi tano za Afrika

    Safari za ndege kwenda na kutoka Ghana, Guinea, Angola, Ivory Coast na Uganda sasa zimerejelewa katika Shirika la Ndege la Emirates - baada ya kampuni hiyo kubatilisha marufuku iliyoweka mwezi uliopita.

    Taarifa kutoka kwa shirika hilo la ndege inasema wasafiri kutoka Dubai lazima wafuate mwongozo mpya wa kuzuia maambukizi ya virusi vya corona:

    • Wasafiri wanaowasili kutoka Guinea,Uganda ama Ghana lazima wawe wamefanyiwa kipimo hasi cha PCR ndani ya saa 48 kuonesha hawana virusi, kipimo hasi cha saa 6 cha Rapid PCR na kipimo hasi cha PCR wanapowasili.
    • Wasafiri kutoka Angola au I vory Coast lazima waonyeshe kipimo hasi cha PCR cha saa 72, na kipimo kingine hasi cha PCR wanapowasili.

    Mnamo Desemba, nchi hiyo alipiga marufuku safari za ndege kutoka nchi 10 za Afrika ikiwa ni pamoja na Ghana, hatua inayoaminika kuwa juu ya wasiwasi wa Covid-19. Ijapokuwa shughuli za nje kutoka Dubai hadi nchi 10 ziliendelea, abiria waliokuwa kwenye usafiri au walio na Dubai kama kituo cha mwisho hawakuruhusiwa kusafiri.

    Emirates ilikuwa tayari imesimamisha safari za ndege kwenda Nigeria kufuatia agizo lililowekwa hivi majuzi la kuwawekea kikomo kwa safari moja kwa wiki . Mvutano kati ya shirika hilo la ndege na serikali ya Nigeria uliendelea hadi mwaka mpya bila dalili zozote za kupatikana kwa suluhu.

    Vile vile serikali ya Kenya ilisimamisha safari zote za ndege za abiria zinazoingia na kutoka Umoja wa Falme za Kiarabu (UAE), kwa siku saba, kuanzia tarehe 10 Januari.

    Mamlaka inasema ilichukua uamuzi huo wa kurudisha marufuku ya safari za ndege za abiria za Kenya kwenda UAE Desemba mwaka jana kufuatia madai ya abiria wa Kenya kukutwa na virusi vya corona walipofika Dubai, licha ya kuwa na vipimo vya PCR vilivyotoka Kenya.

  6. Rais Samia: Urais ni taasisi sio mtu

    Rais wa Tanzania Samia Suluhu Hassan amewataka mawaziri na naibu mawaziri kuheshimu taasisi ya urais na mamlaka yake bila ya kujali nani anaiongoza taasisi hiyo kwani mamlaka na uongozi hutoka kwa Mungu.

    Akizungumza wakati wa mkutano kati ya mawaziri na naibu mawaziri, Samia anasisitiza kuwa kama humpendi anayeiongoza taasisi hiyo basi ipende nchi yako.

    "Urais ni taasisi na sio mtu, kwa hiyo yoyote anayekuwa yuko pale anafanyia kazi taasisi ya urais, sasa kama humpendi aliyoko penda nchi yako" alisema Samia.

    "Tunaambiwa kwamba mamlaka na uongozi wowote unatoka kwa mungu si ndio? na sisi sote hapa tuna dini zetu na tunaamini mungu si ndio?, sasa kama humpendi aliyepo muheshimu mungu wako", aliongeza.

    Wakati huohuo amewaasa mawaziri na naibu mawaziri hao kupunguza migogoro na migongano baina yao ikiwemo kugombania Safari hivyo kuwataka kila mtu afanye majukumu katika eneo lake.

    "Waziri na naibu wake migongano, mnagombaniana safari, ooh safari ilikuwa yangu anakwenda yeye mimi hanipi, wakati sekta ni kubwa, kila mtu akashike eneo lake mkafanye kazi, migongano yenu siielewi" alisema Samia.

    Vilevile amewataka kudumisha umoja na kuijenga nchi ikiwa ni pamoja na kuheshimu kiapo cha maadili kwani wengi hawakifuati kiapo walichoapa.

    "Tukifuatana mmoja mmoja wengi wetu kile kiapo hatukifuati, nina faili hapa la assessment la kila mmoja wenu mnapishana tu viwango vya makosa lakini kila mtu anadosari zake" Januari 8, 2022.

    Rais Samia alifanya mabadiliko katika baraza la mawaziri ambapo Januari 10 aliwaapisha mawaziri wapya.

    Hii leo amekutana na viongozi hao kuwakumbusha miongozo na majukumu ya kazi zao.

  7. Hoda Muthana: Mwanamke aliyeolewa na Islamic State apoteza rufaa ya kurudi Marekani

    Mahakama ya kilele nchini Marekani imekataa kusikiliza kesi ya rufaa ya mwanamke raia wa Marekani ambaye alijiunga na Islamic State na sasa anataka kurudi nchi mwake.

    Hoda Muthana alikulia katika jimbo la Alabama na kusafiri hadi Syria kujiungana na IS 2014.

    Wakati alipokuwa ughaibuni , mamlaka iliamuru kwamba bi Muthana ambaye kwasasa ana umri wa iaka 27 sio raia wa Marekani na kuifuta pasipoti yake.

    Mwaka 2019, babake bi Muthana alikata rufaa dhidi ya mahakama ya kijimbo ambayo ilimzuia kuingia nchini humo. Siku ya Jumatano, mahakama hiyo ilikataa kesi hiyo bila jibu.

    Bi Muthana, mtoto wa kike wa mwanadiplomasia wa Yemen , alizaliwa Marekani. Lakini chini ya sheria za kijimbo, Watoto wa wanadiplomasia waliozaliwa nchini Marekani hawapatiwi uraia wa moja kwa moja.

    Katika malalamishi yake , Ahmed Ali Muthanaanasema kwamba familia yake ilifutilia mbali fursa yao ya kidiplomasia kabla ya mwana wao wa kike kuzaliwa , hatua iliomfanya kuwa raia.

    Ilisisitiza kuwa bi Muthana awali alitambulika na wizara ya masuala ya kigenina kupatiwa pasipoti ya Marekani 2004.

  8. El Classico: Real Madrid yailaza Barcelona na kufuzu Fainali

    El Classico: Real Madrid yailaza Barcelona kufuzu Fainali

    Real Madrid imefuzu kuingia fainali ya kombe la Super Cup nchini Uhispania baada ya kuwalaza wapinzani wao wa jadi Barcelona katika muda wa ziada.

    Federico Valverde alifunga bao la ushindi baada ya mshambuliaji wa Barcelona Ansu Fati kusawazisha katika dakika za lala salama na kulazimisha mechi hiyo kuendelea katika muda wa ziada nchini Saudia.

    Katika mechi ya kuvutia ya El Clasicco , Real Madrid ilichukua uongozi mara tatu , huku Barca ikitoka nyuma mara mbili kabla ya Valverde kufunga bao la tatu la ushindi.

    Mshambuliaji wa Real Madrid Karim Benzema alipata bao katika muda wa kawaida , lakini Luuk de Jong na Fati walifunga katika kila kipindi cha mchezo.

  9. Mchekeshaji wa Nigeria akamatwa katika operesheni dhidi ya dawa za kulevya

    Mchekeshaji maarufu wa Nigeria ambaye hutengeza maigizo mafupi ya mitandaoni amekamatwa wakati wa uvamizi uliofanywa na shirika la kupambana na dawa za kulevya.

    Sunday Joshua maarufu kama De General alipatikana na Tramadol - dawa iliyozuiliwa inayotumika kutibu maumivu - na bangi.

    Alikuwa akirusha mbashara kwenye akaunti yake ya Instagram - ambayo ina wafuasi zaidi ya 700,000 - wakati wa uvamizi huo.

    De General hajazungumza lolote kuhusu kukamatwa kwake lakini taarifa ya shirika hilo ilisema alikiri kumiliki dawa hizo zilizokutwa nyumbani kwake.

    Marafiki zake hata hivyo wameambia vyombo vya habari vya ndani kwamba alikuwa amefanyiwa njama ya kusingiziwa.

  10. Boris Johnson: Viongozi wakuu wa chama cha Tory wamtaka Waziri Mkuu kujiuzulu

    Boris Johnson anakabiliwa na wito kutoka kwa wanachama wakuu wa tories kujiuzulu kama waziri mkuu baada ya kukiri kuhudhuria karamu ya vinywaji wakati wa vikwazo vikali vya kutotoka nje wakati wa janga la Corona .

    Waziri Mkuu aliomba msamaha kwa jinsi alivyoshughulikia hafla hiyo katika bustani ya Downing Street mnamo 2020 na akasema anaelewa "hasira" ya umma juu yake.

    Mawaziri akiwemo naibu Waziri Mkuu Dominic Raab wanamuunga mkono Bw Johnson.Lakini kiongozi wa Scotland wa chama cha Tory Douglas Ross na wabunge William Wragg, Caroline Nokes na Roger Gale wanamtaka aende.

    Bw Ross, mbunge, alisema alikuwa na "mazungumzo magumu" na Bw Johnson baada ya Waziri Mkuu kuomba msamaha mapema Jumatano katika bunge la House of Commons.

    Alisema ataiandikia Kamati ya 1922 - ambayo inapanga mashindano ya uongozi wa Tory - kusajili kutokuwa na imani kwake na PM.

    “Yeye ni waziri mkuu, ni serikali yake ndiyo iliyoweka sheria hizi, na inabidi awajibike kwa vitendo vyake,” alisema.

  11. Prince Andrew kukabiliwa na kesi ya unyanyasaji wa kijinsia baada ya uamuzi wa korti Marekani

    Prince Andrew atakabiliwa na kesi nchini Marekani kwa madai kwamba alimnyanyasa mwanamke mmoja kingono alipokuwa na umri wa miaka 17.

    Virginia Giuffre anamshtaki mwana mfalme huyo, akidai kuwa alimnyanyasa mwaka wa 2001.

    Mawakili wake walisema malalamiko hayo yanapaswa kutupiliwa mbali, akitoa mfano wa makubaliano ya 2009 ambayo alitia saini na mtuhumiwa kwa dhulma za ngono aliyehukumiwa Jeffrey Epstein. Lakini hakimu wa New York aliamua kesi hiyo kuendelea.

    Mwanamfalme Andrew amekuwa akikana madai hayo mara kwa mara.

    Kasri ya Buckingham ilisema haitatoa maoni yoyote juu ya suala la kisheria linaloendelea.

    Hoja ya kutupilia mbali kesi hiyo iliainishwa katika uamuzi wa kurasa 46 wa Jaji Lewis A Kaplan wa Mahakama ya Wilaya ya Marekani katika Wilaya ya Kusini ya New York.

    Inamaanisha kuwa kesi dhidi ya Duke wa York, 61, inaweza kusikilizwa mahakamani baadaye mwaka huu.Jaji Kaplan alisema uamuzi wake haukubainisha "ukweli au uwongo" wa malalamiko ya Bi Giuffre.

  12. Mhadhiri Morocco afungwa jela kuitisha ngono ili kupeana alama za juu

    Profesa wa chuo kikuu cha Morocco anayeshutumiwa kwa kuwapa wanafunzi alama nzuri kama malipo ya upendeleo wa ngono amefungwa jela kwa miaka miwili.

    Ni hukumu ya kwanza katika msururu wa kesi za unyanyasaji wa kijinsia maarufu katika vyuo vikuu nchini Morocco.

    Mhadhiri huyo wa masuala ya uchumi katika Chuo Kikuu cha Hassan I, karibu na Casablanca, alipatikana na hatia ya tabia chafu miongoni mwa mashtaka mengine.

    Wasomi wengine wanne watafikishwa mahakamani siku ya Alhamisi kama sehemu ya kashfa hiyo.

    Kesi hizo ziliangaziwa na vyombo vya habari vya Morocco mwaka jana baada ya wanahabari kuchukua jumbe zilizoripotiwa kuwa kati ya wanafunzi na wahadhiri.

    Wanaharakati wanasema ni nadra kwa kesi za unyanyasaji wa kijinsia kufikishwa mahakamani.

  13. Kiti cha rais wa Ghana kinachobebwa na gari la kifahari chazua gumzo mitandaoni

    Mitandao ya kijamiii nchini Ghana imekuwa na gumzo kuhusu mipango ya safari ya Rais Nana Akufo Addo. Kuna madai kuwa kiti cha kifahari cha ngozi ya rangi kahawia - kinachotumiwa na rais kwa matumizi yake binafsi kina gari lake la kukisafirisha popote anapokwenda.

    Kulikuwa na ripoti kwamba gari la Toyota V8 ndilo ambalo hutumiwa kukisafirisha kiti hichoambacho kina dereva wake maalum na maafisa wa ulinzi

    Waliotoa maoni yao kuhusu Habari hizo walisema ni jambo la kushangaza kuzitumia raslimaliza umma kwa njia hiyo .

    Aliyekuwa rais wan chi hiyo John Mahama alisema yeye mwenyewe amewahi kushuhudia kiti hicho kikisafirishwa kwa njia hiyo wakati rais Nana alipokuwa akihudhuria mazishi ya jaji mmoja .

  14. Hujambo na karibu kwa matangazo yetu ya moja kwa moja hivi leo Alhamisi tarehe 13 Januari 2022