Nani kucheka, kulia upepo mkali wa Rais Samia Tanzania?

    • Author, Florian Kaijage
    • Nafasi, BBC Swahili
  • Iliyochapishwa

Tanzania bado ipo katika mjadala mkali kufuatia matamshi mazito ya Rais wa nchi hiyo, Samia Suluhu Hassan kuwa anakusudia kufanya mabadiliko ya baraza la mawaziri hivi karibuni, ili kuwaondoa wale wote wanaojishughukisha zaidi na siasa za uchaguzi wa 2025 hivyo kudumaza utendaji wa serikali yake.

Rais Samia pia ameonesha dhahiri kwa mara nyingine kukerwa na ukosoaji wa Spika wa Bunge Job Ndugai juu ya mikopo ya serikali kutoka maeneo mbalimbali duniani zikiwemo shilingi trilioni 1.3 kutoka Shirika la Fedha Duniani (IMF).

Tayari Spika Ndugai aliomba radhi akisema "Nimekosa, nimekosa mimi, nimekosa sana" lakini sasa ni dhahiri kuwa Rais Samia hajaipokea kwa uzito radhi hiyo pamoja na kusema tu "wasameheni"

Mitandao ya kijami, na vyombo mbalimbali vya habari kunaendelea mjadala juu ya jambo hilo huku yakiangaliwa yanayoweza kutokea siku chachae zijazo. Je ni athari zipi za moja kwa moja za hali hii kwa siasa za Tanzania na utendaji mzima wa serikali?

Kwanza kuna watu binafsi watapoteza nafasi baada ya mabadiliko ya baraza la mawaziri ambayo yatakuwa ya pili tangu Rais Samia alipotangaza baraza lake Machi 2021, kufuatia kifo cha mtangulizi wake, Rais John Magufuli Machi 17.

Watakaotupwa nje ya baraza ni dhahiri watajiona wametendewa hivyo kwa sababu za siasa za uchaguzi wa 2025 (hata kama zipo sababu zingine), hivyo itawapa fursa ya kujimwaga kwa uhuru na pengine kwa uwazi zaidi katika ziasa na kufanya matayarisho ya kutosha kwa kutafuta uungwaji mkono ndani na nje ya Chama cha Mapinduzi (CCM).

Hali hii inaweza kuchangamsha mijadala na harakati za kisiasa za Tanzania ikingali mapema zaidi kuliko ilivyozoeleka.

Mustakabali wa nafasi ya Spika ni athari nyingine ya moja kwa moja inayotarajiwa kujionesha.

Pamoja na kwamba Rais hakumtaja jina Spika wa Bunge Job Ndugai - bado haipo wazi iwapo aliacha kumtaja jina kwa makusudi au la-pengine kuepusha kulifanya jambo hilo la binafsi, kitendo cha kutaja msimamizi wa mhimiri wa Bunge, inaondoa shaka kuwa anayezungumzwa ni Spika Job Ndugai.

Ni dhahiri sasa kuna wingu nene juu ya nafasi ya Spika kwa kuwa haivi chungu kimoja na Mkuu wa serikali.

Mjadala unaoendelea hasa mitandaoni kwa ujumla unaonesha Spika Ndugai hayuko salama kisiasa.

Maswali ya msingi ni Je anaweza kujiuzulu kwa hiari yake ili kwa kiwango fulani kulinda heshima yake kwa kuwajibika juu ya matamshi yake yaliyoiletea ukakasi serikali na hasa Rais?

Je atajadiliwa ndani ya chama cha CCM na pengine akionekana kuw ana hatia avuliwe uanachama, hivyo kukosa sifa za kuwa Spika kwa kutokuwa na udhamini wa chama cha siasa?

Je atajitokeza mbunge kuwasilisha hoja ya kutokuwa na imani na Spika ili ufuatwe utaratibu wa kumuondoa madarakani kwa kufuata taratibu zilizowekwa kikanuni ikiwemo kupitia Kamati ya Bunge ya Haki, Maadili na Madaraka ya Bunge kuandaa mashtaka yatakayowasilishwa bungeni na kisha zipigwe kura zisizopungua theluthi mbili?

Je Shinikizo lililoanza katika maeneo mbalimbali ya nchi likiwemo jimbo la uchaguzi la Ilala, Dar es Salaam na wabunge kadhaa binafsi litatosha kumsukuma Spika Ndugai kujiuzulu?

Ifahamike kuwa iwapo hili la kuondoka kwa Spika kwa kujiuzulu au kuondolewa litatokea litakuwa la kwanza tangu Tanganyika kupata Uhuru 1961 kabla ya 1964 kuungana na Zanzibar kuunda Tanzania. Maspika wote wa awali waliondoka kwa sababu tofauti ikiwemo ikiwemo kustaafu au kutoteuliwa na Chama kuwa wagombea lakini si kwa kuachia ngazi wakiwa bado madarakani.

Jambo lingine ambalo linaonekana kuwa na athari ni kutajwa kwa Waziri Mkuu Kassim Majaliwa kuwa yupo katika bunge ambalo kulisikika matamshi ya serikali ya mpito anayoiongoza Rais Samia.

Izingatiwe kuwa kwa wadhifa wake Waziri Mkuu Majaliwa, aliyeteuliwa mara mbili na Rais wa awamu ya tano, Magufuli, ndiye msimamizi mkuu wa shughuli za serikali bungeni na ndiye mwenyekiti wa wabunge wa CCM ambao ni zaidi ya asilimia 90 bungeni.

Hivyo, kutajwa kwake katika hoja ambayo kwa tafsiri ya Rais Samia ni upotoshaji wa Katiba ya nchi, kwa upande mmoja linaweza kutafsiriwa kuwa Majaliwa hayuko salama sana katika nafasi yake.

Hata hivyo bado hakuna ushahidi wa wazi na wenye mashiko mbele ya umma wa kumhusisha Majaliwa na 'Homa' ya 2025-kama alivyoiita Rais Samia, dhidi ya Rais isipokuwa minong'ono tu.

Mwisho huu 2022 ni mwaka wa uchaguzi wa ndani ya Chama kwa ngazi zote kuanzia shina hadi Taifa.

Kwa hiyo kauli ya Rais kuwa kuna watu ndani ya CCM ambayo pia ni mwenyekiti wake wa Taifa wanaomkwamisha ni angalizo zito kuwa kutakuwa na mabadiliko makubwa ya ndani ili kuondoa vimelea vyote vinavyoleta upinzani na ukinzani wa ndani ya Chama na kuikwamisha serikali.

Yote hayo ni mchakato na si ya siku moja, nani mwishowe atacheka au kulia katika huu upepo mpya wa Rais Samia Suluhu Hassan? Ni suala la kungoja na kuona. Lakini jambo moja la dhahiri ni kuwa siasa za Tanzania zinachngamka tena na kuna uwezekano mkubwa zikachangamka zaidi.