Hii ni tovuti ya maandishi pekee ambayo inatumia data kidogo. Tazama toleo kuu la tovuti likijumuisha picha na video zote.
Pata maelezo zaidi kuhusu toleo hili la linalotumia kiasi kidogo cha data
Je wanaompinga rais Samia ndani ya CCM kujitokeza kuelekea uchaguzi wa urais 2025?
- Author, Rashid Abdallah
- Nafasi, Mchambuzi, Tanzania
- Iliyochapishwa
Kuna takribani miaka minne hadi uchaguzi mkuu wa Tanzania wa 2025. Ni muda mrefu kwa hakika. Wakati vyama vya upinzani havijawaza hata kuwasaka wagombea wao wa urais, Chama cha Mapinduzi (CCM) kinaonekana tayari kimekwishakumfahamu nani ataipeperusha bendera yao katika mwaka huo.
Hali hii inakuja baada ya kile kinachoweza kuitwa taarifa ya uzushi iliyoandikwa na gazeti kongwe la Uhuru, linalomilikiwa na CCM, likieleza Rais Samia hana nia ya kuwania kiti cha urais katika uchaguzi mkuu ujao. Sasa Rais mwenyewe ameibuka na kuweka bayana nia ya kutaka muhula wa pili.
"Wameanza kutuchokoza kuandika kwenye vigazeti Samia hatasimama nani kawaambia?....
Kauli yake ni ya kisiasa zaidi, imebeba maneno yenye kuashiria kana kwamba ana uhakika na ushindi. Ingawa hilo ni kawaida panapohusika tambo za kisiasa. Hatima ya tambo hizo huwa ni kura kisandukuni.
Sheria zinasemaje?
"Sasa ndugu zangu Rais mwanamke tutamuweka 2025, tukifanya vitu vyetu vizuri tukishikamana tukimweka rais wetu tutakutana hapa kwa furaha kubwa sana, wameaanza kutuchokoza, kuandika kwenye vigazeti Samia hatasimama nani kawaambia?"
Ni kauli ya Rais Samia wakati akizungumza na wanawake tarehe 15 Septemba, katika Ukumbi wa Diamond Jubilee, Dar Es Salaam. Ndio kauli ya kwanza ya wazi kuhusu mwelekeo wake baada ya muhula huu kuisha.
Msingi wa katiba ya nchi umamruhusu Rais huyo kugombea muhula wa pili itakapofika 2025. Baada ya kifo cha John Pombe Magufuli ataiongoza nchi kwa zaidi ya miaka mitatu, na huo utahesabika ni muhula wake wa kwanza.
Kikatiba, Tanzania haina mfumo wa kuruhusu mgombea huru, ambaye hatokani na chama chochote. Kwa mantiki hiyo, Rais Samia akiendelea kutumia tiketi ya CCM, atakuwa na uwezo utakaomruhusu kuchuana na wagombea wa upinzani ikiwa pumzi zitamruhusu.
Je, watajitokeza CCM wa kuchuana naye?
Kwa hakika haileti ukakasi wowote pindi Rais aliye madarakani kutokea Chama tawala, akitangaza nia ya kugombea muhula wa pili kuelekea kuisha ule wa kwanza. Vigogo na wafuasi wa CCM hawapati taabu na tangazo la aina hiyo, hata kama muda wa huo uchaguzi ungali mbali.
Kwa jicho jingine ni kauli yenye umuhimu mkubwa katika medani za siasa za ushindani. Mwenyekiti wa chama kusimama na kuutangazia umma wakiwemo wapinzani wake kisiasa, kwamba hana mpango wa kubwaga manyanga hivi karibuni.
Tatizo huja ikiwa mtu mwingine kutoka chama tawala atatangaza nia wakati Mwenyekiti wao tayari ameshaweka azma. Yakitokea mazingira kama hayo, ndipo magazeti huandika kwa anuani kubwa, "mgogoro ndani ya CCM."
Moja ya mfano wa karibuni zaidi CCM kufika katika mazingira hayo, ni wakati wa joto la uchaguzi wa 2020. Pale Waziri wa zamani wa mambo ya nje, Bernard Membe alipoonesha nia ya kutaka kupambana na Magufuli katika uchaguzi wa ndani wa chama.
Aliyekuwa Katibu Mkuu wa CCM, Dkt. Bashiru Ally, alipata kutamka hadharani kumtuhumu Membe kuwa anasuka mipango ya chini chini kuomba ridhaa ya kugombea urais ndani ya CCM ifikapo mwaka 2020.
Kuanzisha kampeni nzito za kushindana na mgombea wa kiti cha urais katika uchaguzi wa ndani kuelekea muhula wa pili hutafsriwa kwamba unakigawa chama na kuwaweka wanachama wake katika mafungu.
Ukweli ni kwamba utamaduni wa chama ni kumpitisha mgombea wao anayehudumu katika kiti cha urais ili agombee muhula mwingine bila kukumbana na kizingiti chochote kutoka ndani ya chama chake.
Historia inaonesha kuwa Membe amewahi kuadhibiwa na CCM mwaka 2014 kwa makosa ya utovu wa nidhamu na kukiuka taratibu kwa kuanza kampeni za urais ndani ya chama kabla ya wakati kuelekea uchaguzi mkuu wa mwaka 2015.
Wengine waliowahi kuadhibiwa na CCM kwa kosa la kuanza kampeni mapema ni Mawaziri Wakuu wa zamani, Edward Lowassa na ndugu Frederick Sumaye. Pia katika kundi hilo walikuwemo January Makamba, Stephen Wasira, na William Ngeleja.
Kwa utamaduni huo wa chama ambao haumtaki mwanachama akae mbele ya Mwenyekiti na wala asijitokeze kwa kutangaza nia kabla ya muda. Ni kielelezo tosha, hakutakuwa na mwanachama wa CCM atakayejitokeza kushindana na Rais Samia. Na hata akijitokeza atashughulikiwa mara moja.
Utata wa zuio la mikutano ya kisiasa
Mbali ya uharamu wa marufuku ya mikutano ya kisiasa. Kasoro nyingine kubwa ndani ya marufuku hiyo, ni mwasisi wa marufuku hayati Magufuli na mrithi wake Rais Samia, kutojiona kuwa na wao ni wanasiasa ambao marufuku hiyo ilipaswa kuwahusu.
Rais Samia na mtangulizi wake wamefanya mambo yanayofanana; kuzuia mikutano ya upinzani lakini wakiwa majukwaani kuna nyakati wanahubiri siasa za ushindani waziwazi, wakati huo huo wamewazuia wapinzani wao kufanya yale wanayowafanya wao.
Kwa mazingira ya uwanja wa siasa ulivyo sasa, si rahisi kwa mwanasiasa wa upinzani kusimama mbele ya watu na kujitengenezea njia kuelekea uchaguzi wa 2025, kama alivyofanya Rais Samia. Kwa sababu CCM imeamua kuweka uwanja wa siasa usio sawa.
Kauli iliyobeba dhamira ya kukitaka tena kiti cha urais, aliitoa Septemba 15, siku ya Demokrasia Duniani. Isivyo bahati, uhuru wa kisiasa ndani ya Tanzania hauakisi kile kinachopaswa kuadhimishwa katika siku hiyo hivyo kuna mambo ya kurekebishwa ili kikidhi vigezo vya demokrasia inayofahamika kote duniani ikiwemo mazingira sawa ya ushindani kisiasa.
Ujumbe wake una maana gani katika siasa?
Kauli ya Rais Samia itawarudisha nyuma wanachama wa CCM ambao walikuwa wanaimezea mate nafasi ya urais, huku wakisubiri Rais Samia aseme hatagombea tena. Kwa hesabu za haraka watapaswa kusubiri hadi 2030.
Kwa upande wa vyama vya upinzani, kauli ya Rais Samia imewapa mwanga wa mapema juu ya nani wanapaswa kumtazama kama mshindani wao hapo 2025.
Itawasaidia kujiandaa kikamilifu dhidi yake. Kwa kuendelea kurekodi upungufu na yale yanayofeli katika utawala wake ili baadaye yatumike katika ajenda za kupambana kisiasa wakati wa kampeni rasmi utakapowadia.
Hii ni kwa sababu sehemu kubwa ya kampeni ni kueleza utakayofanya na kurusha vijembe dhidi ya mpinzani wako huku ukisema kwa yakini maeneo ambayo amekengeuka au kufanya makosa ya dhahiri.