Mwalimu aliyestaafu Kasara Mnaku amemkumbuka aliyekuwa
mwanafunzi mwenzake – Hayati mzee John Magufuli, ambaye amefariki dunia akiwa
na umri wa miaka 61.
Katika mahojiano na mwandishi wa BBC Aboubakar Famau,
Bwana Mnaku amesema:
''Tuliishi katika
kijiji kimoja. Tulikuwa darasa moja na tukaketi dawati moja. Katika maisha yake
ya awali, hadi alipokuwa rais, tulikuwa pamoja na alikuwa rafiki yangu. Kila
alipohitaji ushauri angenipigia simu na tungezungumza''.
Bw Mnaku Aliongeza: ''Tulipokuwa
watoto tulikuwa na uhusiano wa karibu kweli na kusaidiana na tulipenda mno
kusoma.Hili lilitusaidia kufika
tulipofika, Nikawa mwalimu na yeye pia akawa mwalimu lakini hatimaye akaamua
kuacha taaluma hiyo na kuhudumia nchi."
Mwanafunzi mwingine
aliyesoma naye, Elias Kwaswahili, amesema:
''Tuliishi
kijiji kimoja cha Rubambangwe na sote tulisomea katika shule ya msingi ya Chato. Na
baadaye tukakutana katika shule ya sekondari ya Lake Mwanza''.
Elias Kwaswahili: ''Alikuwa mwanafunzi mzuri sana
darasani hasa katika sayansi. Tuliona masomo ya sayansi yakiwa magumu hasa
hisabati. Lakini alikuwa mzuri sana katika hesabu na hili ndili lililo msukuma
kufanya masomo ya sayanasi. Hivyo ndivyo nilivyo mfahamu".
Bwana Magufuli alikuwa na shahada ya uzamili ya kemia
na aliwahi kufanya kazi kama mwalimu wa sayansi na hisabati. Alikuwa mbunge
mwaka 1995 na kupanda cheo hadi kuwa rais mwaka 2015.
Serikali imesema Bwana
Magufuli amefariki dunia kutokana na maradhi ya moyo.