Hii ni tovuti ya maandishi pekee ambayo inatumia data kidogo. Tazama toleo kuu la tovuti likijumuisha picha na video zote.
Pata maelezo zaidi kuhusu toleo hili la linalotumia kiasi kidogo cha data
Mwanamuziki Bobi Wine aachiwa kwa dhamana
Mahakama moja mashariki mwa Uganda imemshtaki mgombea urais wa chama cha upinzani Robert Kyagulanyi maarufu kama Bobi Wine, kwa makosa ya kutenda kitendo chenye uwezekano wa kusambaza ugonjwa wa kuambukiza.
Moja kwa moja
Asha Juma
Habari za hivi punde, Uchaguzi wa Uganda 2021:Mwanamuziki Bobi Wine aachiwa kwa dhamana
Mahakama moja mashariki mwa Uganda imemshtaki mgombea urais wa chama cha upinzani Robert Kyagulanyi maarufu kama Bobi Wine, kwa makosa ya kutenda kitendo chenye uwezekano wa kusambaza ugonjwa wa kuambukiza.
Bobi Wine alikamatwa katika mkutano wa kampeni Jumatano akishtumiwa kwa kukiuka miongozo ya kudhibiti ugonjwa wa virusi vya corona kwenye mkusanyiko wa hadhara.
Hata hivyo Bobi Wine amepewa dhamana.
Wakati huohuo, jeshi la Uganda limeongeza wanajeshi wake katika mji wa Kampala na miji mingine kukabiliana na maandamano yanayoendelea kuibuka.
Hadi kufikia sasa watu 28 wamethibitishwa kufariki dunia kote nchini humo wakati wa maandamano yaliyokuwa yakidai kuachiliwa huru kwa Bobi Wine huku wengine zaidi ya 500 wakikamatwa, kulingana na jeshi la polisi.
Maandamano hayo ya kudai kuachiliwa huru kwa Bobi Wine, yalisambaratishwa kwa kutumia vitoza machozi na wakati mwingine risasi zilitumiwa.
Awali, naibu msemaji wa jeshi, Kanali Deo Akiiki aliviambia vyombo vya habari kuwa wanajeshi watapelekwa katika barabara zote kuu zinazoingia mjini.
Januari 2021, Uganda itakuwa na uchaguzi mkuu wa urais lakini wiki za kwanza za kampeni tayari zimekubwa na vurugu na ghasia.
Pia unaweza kusoma:
Mwanasheria wa Trump aitaja Tanzania katika shutuma ya wizi wa kura Marekani
Wakili wa Donald Trump ameitajaTanzania wakati wa mkutano na wanahabari siku ya Alhamisi, akilenga kuungwa mkono katika madai ya wizi wa kura kwenye uchaguzi wa urais uliofanyika Novemba 3 nchini Marekani.
"Kila jimbo, karibu kila nchi yenye demokrasia ikiwemo Tanzania, na maeneo ambayo hata huwezi kuyafikiria, wana sheria za uangalizi hasa kwa kura zinazopigwa kwa njia ya posta," Rudy Guliani amewaambia wanahabari Alhamisi.
Joe Biden ndio rais mteule lakini Bwana Trump bado hajakiri kushindwa kwa madai kwamba kulikuwa na udanganyifu ambako kulimpendelea Bwana Biden.
Rais wa Tanzania John Magufuli alishinda awamu ya pili madarakani mwezi uliopita.
Bwana Giuliani alitumia dhana ya uwepo wa njama na kukosoa jinsi madai ya timu yake ya kampeni ya kupinga uchaguzi yalivyo angaziwa, akisema kuwa vyombo vya habari vimeonesha "chuki kwa rais".
Soma habari zaidi:
Somali yamfuta kazi waziri wa mambo ya nje juu ya mgogoro wa Ethiopia
Waziri mkuu wa Somali Mohamed Hussein Roble amemfuta kazi waziri wa mambo ya nje Ahmed Isse Awad, saa chache baada ya kuibuka kwa mtafaruki juu ya msimamo wa Somali katika mgogoro wa Ethiopia unaoendelea.
"Katika agizo lilitolewana ofisi ya Waziri Mkuu wa Somali, Mohamed Abdirizak Mohamud Abubakar ameteuliwa kuwa waziri wa mambo ya nje na kuchukua nafasi ya mtangulizi wake," Tovuti ya radio inayomilikiwa na serikali imeonesha.
Hata hivyo waziri aliyepigwa kalamu ametajwa kama balozi, ripoti hiyo inasema.
Hapo jana, Bwana Awad alituma ujumbe katika akaunti yake ya Twitter akikanusha madai kuwa ametoa taarifa rasmi kuu ya mzozo wa Ethiopia.
Awali, Waziri wa mambo ya nje alikuwa ametoa taarifa akionesha “kuunga mkono kwa umoja wa Ethiopia".
“Somali imeonesha mshikamano wake kwa serikali ya Ethiopia chini ya uongozi wa Waziri mkuu Abiy Ahmed katika utekelezaji wa katiba na kuheshimu mipaka ya Ethiopia," Wizara ya mambo ya nje imesema kuwa taarifa hiyo iliondolewa baadaye.
Soma zaidi:
Jinsi wanawake wanavyoshughulika na uvuvi Rwanda
Maelezo kuhusu taarifa - Author, Yves Bucyana
- Nafasi, BBC Swahili
Huko magharibi mwa Rwanda kama ilivyo kwenye maeneo mengine mengi, uvuvi ni shughuli maalum kwa wanaume tu, Mariana alibadili dhana hiyo katika kisiwa cha Nkombo kilichopo ndani ya ziwa Kivu.
Mariana Nyiranizeyimana, mwenye umri wa miaka 48, ndiye mwanamke wa kwanza katika kisiwa hicho kufanya kazi ya uvuvi wa samaki.
Mwanzoni alihangaika kubadili mtazamo wa kwamba uvuvi ni kazi ambayo inahitaji nguvu ya mwili ikiwa inafanywa usiku kwenye historia hapa ni haswa kazi ya wanaume.
Mwanzoni mume wake alikuwa na wasiwasi juu ya mtazamo wa umma kuhusu mkewe, aliyefanya kazi iliyochukuliwa na wengine kama mwiko.
"Lakini alipoona faida niliyokuwa nikipata, alihisi kuwa haijalishi kwake...Mume wangu ndiye ambaye angefanya nishindwe kuifanya, lakini kwa sababu nilikuwa na nia nzuri...alihisi kuwa hakuna sababu ya kunizuia..." Nyiranizeyimana alisema.
Mapinduzi katika uvuvi yalimvutia Mukamuli Immaculata mwenye umri wa miaka 55, alijiunga na kazi ya uvuvi wa samaki baada ya kuona ushujaa wa Mariana aliyechangamkia kazi ya wanaume.
“Tulikuwa tunafanya biashara ya kuuza viazi vitamu hapa kwenye ziwa Kivu na tukaona Mariana anazidi kustawi, alinunua timu yake, akamnunulia mumewe timu nyingine. "tukamwendea kumuomba ushauri baadae alitufundisha pole pole ...ndipo tuliingia katika kazi ya uvuvi’’ Timu anayozungumzia ni vifaa vya uvuvi vikiwemo mashua maalumu .
Wanawake hao wanasema biashara ya samaki huko Kivu inawaruhusu kupata pesa, kulipia bima ya afya, na kuwa na afya bora kwa ujumla.
Mmoja wao alisema, "sasa ninamsaidia mume wangu kushughulikia maswala ya nyumbani, aliwekeza nguvu zake na mimi ninawekeza katika uvuvi na sasa nina shamba ambalo naweza kumpa mtoto kama urithi akajenga nyumba yake."
Mariana aliongeza kusema kwamba: "Wavulana wangu ni wahitimu wa vyuo vikuu, na wasichana wako sekondari. Sina kazi nyingine isipokuwa uvuvi tu,ndio inaonisaidia kulipia masomo yao.
Serikali kugharamia matibabu ya waliojeruhiwa katika maandamano ya Bobi Wine
Waziri anayehusika na masuala ya Afya Dr. Joyce Moriku Kaducu ametangaza kuwa serikali itachukua jukumu la kutibu waliojeruhiwa katika maandamano ya kudai Bobi Wine aachiwe huru.
Vurugu zilianza kutokea katika mji wa Kampala pamoja na miji mingine ya nchi hiyo Jumatano na tangu wakati huo vikosi vya usalama vimekuwa vikiwafyatulia risasi waandamanaji na kutmia vitoza machozi ili kudhibiti hali.
Akizungumza na wanahabari katika hospitali Kuu ya Mulago, Dr. Kaducu alisema hakuna aliyejuruhiwa anayestahili kulipa chochote kwasababu serikali imechukua jukumu la kugharamia matibabu.
“Gharama ya matibabu ni bure. Kama serikali, tunataka kusema, na liko wazi, hakuna raia atakayelipa pesa za matibabu wala hakuna atakayelipa pesa za matibabu ya upasuaji wowote. Serikali imechukua jukumu hilo,” Dr. Kaducu amesema.
Kulingana na gazeti la Nile Post, kuna wadi maalum iliyotengwa kwa ajili ya kushughulikia waliojeruhiwa katika jengo jipya la hospitali ya Mulago.
Bobi Wine alikamatwa Jumatano hatua iliyosababisha mauaji na majeruhi zaidi ya 60 huku wengine 321 kushikiliwa na polisi.
Bobi Wine anatarajiwa kufikishwa mahakamani hii leo.
Soma zaidi:
Uchaguzi wa Marekani 2020: Biden amshinda Trump baada ya kura kuhesabiwa tena Georgia
Rais mteule wa Marekani Joe Biden aibuka na ushindi Georgia baada ya kura kuhesabiwa tena huku juhudi za kuchukua mkondo wa kisheria za Donald Trump zikiendelea katika majimbo matatu zikiendela.
Chama cha Democratic kimeshinda chama pinzani cha Republican huko Georgia kwa kura 12,284 kama inavyohitajika katika sheria ya kuhesabu kura tena.
Bwana Biden amesema Bwana Trump alijua kuwa hatashinda na alionesha "kutowajibika kwa kiwango cha juu" kutokiri kuwa ameshindwa.
Rais wa chama cha Democratic amejipanga kuchukua nafasi Januari kama rais wa 46 wa Marekani.
Ushindi wa Bwana Biden katika wingi wa kura hadi kufikia sasa ni milioni 5.9.
Katika kura za majimbo ambazo ni lazima kushinda ili kuwa rais wa Marekani, Biden alipata kura 306 dhidi ya Trump aliyepata kura 232 akiwa amepita zile zinazohitajika.
Soma zaidi:
Msumbiji yasema China haiwezi kuchukuwa mali yake
Waziri wa mambo ya nje wa Msumbiji, Adriano Maleiane, ametupilia mbali hofu kuwa China inaweza kuchukua mali za nchi hiyo ikiwa itashindwa kulipa mikopo yake.
Waziri huyo amewaambia wabunge Alhamisi kuwa hofu hiyo haina msingi wowote.
“Hakuna ishara yoyote ya kutokea kwa hilo”, alisema.
Amesema kuwa madeni ambayo Msumbiji imeomba kwa China hadi kufikia sasa inaendelea kulipwa kwa makubaliano yaliofikiwa kati ya nchi hizo mbili.
Bwana Maleiane amesema kuwa jumla ya deni la Msumbiji kwa China ni takriban dola bilioni 2.
Kiasi kikubwa cha deni hilo takriban dola bilioni 1.97 ni kutoka kwa benki ya China ya Exim Bank, ambayo inafadhili miradi mikubwa ya miundo mbinu, ikiwemo barabara ya Maputo Ring na ujenzi wa daraja katika ghuba ya Maputo uliositishwa.
Waziri huyo amesema hatimaye miradi hiyo itajilipa yenyewe.
Pia uanweza kusoma:
Nabii Bushiri milionea anayetafutwa na Afrika Kusini aachiwa huru Malawi
Nabii milionea wa Malawi Shepherd Bushiri na mke wake wameachiwa bila masharti yoyote na mahakama moja mjini Lilongwe nchini Malawi baada ya kujisalimisha kwa polisi Jumatano.
Afrika Kusini inataka ikabidhiwe wawili hao kwa kukiuka masharti ya dhamani nchini humo.
Bushiri na mke wake wameshtakiwa nchini Afrika Kusini walikokuwa wanaishi kwa makosa ya utakatishaji wa fedha na ulaghai.
Hata hivyo wawili hao wamekanusha mashtaka hayo.
Wakili wao, Wapona Kita, aliitaka mahakama iwaachilie wawili hao bila masharti yoyote akisema kuwa kukamatwa kwao ni kinyume na sheria.
Mwendesha mashtaka aliomba mahakama kuruhusu polisi kuendelea kuwashikilia wanandoa hao kwa siku 30 zaidi ili kuwezesha Afrika Kusini kuwasilisha rasmi ombi lao la kutaka wakabidhiwe kwa nchi hiyo.
Bwana Kita alisema ni kinyume cha sheria kumzuilia mtu wakati Afrika Kusini haijawasilisha ombi rasmi.
Soma zaidi:
Tanzania yashtakiwa kwa sheria inayopiga marufuku wasichana wajawazito shuleni
Taasisi ya kimataifa ya kutetea haki za wanawake, Equality Now ikishirikiana na washirika wake nchini Tanzania, wamewasilisha kesi dhidi ya serikali ya Tanzania katika mahakama moja ya Afrika inayoshughulikia masuala ya kibinadamu na haki baada ya nchi hiyo kuweka marufuku kwa wasichana wajawazito kuhudhuria shule au wasirejee mara wanapojifungua.
Katika taarifa yake, taasisi hiyo imesema kuwa kwenda mahakamani ilikuwa ndio uamuzi wa mwisho uliosalia baada ya kuishawishi serikali kwa miaka kadhaa, kubatilisha uamuzi huo bila mafanikio.
Serikali ya Tanzania bado haijatoa tamko rasmi tangu kushtakiwa.
Kwa mujibu wa sheria iliyopitishwa mwaka 2002, wasichana wajawazito wanaruhusiwa kufukuzwa shuleni.
Sheria hiyo inasema wasichana wanaweza kufukuzwa na kuondolewa kabisa shule kwa "makosa ya ukosefu wa 'maadili na "ndoa'.
Makundi ya kutetea haki za wanawake yamekuwa yakisihi serikali ya Tanzania kubadilisha sheria hiyo.
Wasichana 8,000 nchini Tanzania hulazimika kuacha shule kila mwaka kwasababu ya kupata ujauzito, kulingana na ripoti ya Shirika la Human Rights Watch.
Shirika la Equality Now, limesema kuwa marufuku hiyo ilikuwa ya kibaguzi na wengi wanaoathirika ni wasichana kutoka jamii maskini ambao huwa katika hatari nyingine ya ukiukaji wa haki za binadamu kama vile ukeketwaji.
Pia unaweza kusoma:
Uchaguzi wa Uganda 2021: Rais Yoweri Museveni alaani vikali wanasiasa wanaovunja masharti ya kudhibiti corona
Rais Yoweri Museveni wa Uganda ashtumu vikali wanasiasa wanovunja masharti ya kudhibiti virusi vya corona wakati huu wa kampeni za uchaguzi wa rais.
Kauli hiyo imetolewa na mgombea huyo wa urais wa chama cha NRM, ikiwa leo ni siku ya tatu tangu mpinzani wake Robert Kyagulanyi, maarufu kama Bobi Wine alipokamatwa na jeshi la polisi kwa kufanya mkutano wa hadhara wa kampeni.
Rais Yoweri Museveni amesema hayo katika mkutano wa kampeni alipokutana na viongozi wa chama tawala mkoa wa Karamoja, Kaskazini Mashariki mwa Uganda wakati anatetea kiti chake cha urais kwa muhula wa sita.
‘’Tayari tumepoteza watu wengi wakiwemo wabunge wawili, tumepoteza wanasayansi hivyo ni uhalifu kwa mtu ambaye anavunja masharti. Kila mtu ni lazima afuate masharti yaliyowekwa na wizara ya afya’’, amesema Museveni.
Aidha, rais Museveni amesema wanasiasa hao wanaungwa mkono na watu kutoka nje wenye dhamira mbaya wasiopenda amani na utawala bora nchini Uganda.
Rais Museveni amesema hayo wakati mpinzani wake Bobi Wine, mgombea urais kupitia chama cha NUP akiwa amekamatwa polisi mjini Jinja kwa kosa la kukiuka masharti dhidi ya corona.
Kukamatwa kwa Bobi Wine kumesababisha zaidi ya mauaji ya raia 16 , majeruhi 60 na wengine 321 kushikiliwa na polisi wakati wa makabiliana na polisi wakitaka mgombea wao kuachiwa huru.
Pia unaweza kusoma:
Hujambo na karibu katika matangazo yetu ya moja kwa moja hii leo ikiwa ni tarehe 20/11/2020.