Marekani bado shughuli
ya kuhesabu kura inaendelea, lakini vyombo vya habari vya dunia vinaangazia
hatua za kisheria zilizochukuliwa na Donald Trump na kuendeleza mjadala wa
vurugu zinazokumba shughuli ya kuhesabu kura.
Tuanze na nchini Kenya
ambapo gazeti la The Standard kichwa chake cha habari kinasoma "Vurugu
hadi mwisho".
Gazeti la Punch nchini
Nigeria liliangazia taarifa yenye kichwa "wasiwasi na mvutano" Marekani.
Gazeti la China la
Global Times limesema kura zinazoendelea kuhesabiwa zimesababisha "mgawanyiko,
ghasia na machungu makali" nchini Marekani. China, inasema
uchaguzi huo umekuwa kama "burudani", "jamii iliyokumbwa na
ghasia", gazeti hilo limeongeza.
Kwengineko shirika la habari la Iran limeangazia ghasia
zilizotokea mitaani wakati shughuli ya kuhesabu kura inaendelea katika majimbo
kadhaa. Radio Iran (VIRI) imesema "Sintofahamu iliyokumba matokeo nchini Marekani,
huku ghasia za uchaguzi zikiongezeka".
Nchini Urusi, uchaguzi wa Marekani haukuwa tena gumzo
badala yake vituo vyote vilijikita katika matamshi ya Trump ya wizi wa kura
bila kutaja ushahidi wowote.
Na gazeti la Corriere della Sera nchini Italia limesema
uchaguzi wa mwaka huu ni "mtihani mkubwa sana kwa demokrasia”, na unaoonesha
"uimara na udhaifu wa mfumo wao wa upigaji kura" Marekani.