Iran yakamata 'majasusi' 21 wa Israel

Kwa mujibu wa wizara hiyo, watu hao wanadaiwa kukusanya taarifa kuhusu maeneo nyeti na ya siri ya kijeshi pamoja na mifumo ya ulinzi wa anga, kisha kuzifikisha kwenye shirika la ujasusi la Israel,Mossad.

Muhtasari

Moja kwa moja

Abdalla Seif Dzungu & Beldeen Waliaula

  1. Kufikia hapo tunatamatisha matangazo yetu ya moja kwa moja. Kwaheri.

  2. Bunge la Uganda laidhinisha kutumwa kwa wanajeshi Gaza

    .

    Chanzo cha picha, Getty Images

    Bunge la Uganda limeidhinisha pendekezo la serikali kuruhusu kutumwa kwa wanajeshi wa nchi hiyo Ukanda wa Gaza, kufuatia mwaliko wa Marekani chini ya mpango wa Board of Peace unaoongozwa na Rais Donald Trump.

    Pendekezo hilo liliwasilishwa bungeni na Waziri wa Ulinzi wa Uganda, Kiryowa Kiwanuka, ambaye aliwaambia wabunge kuwa Jeshi la Ulinzi la Wananchi wa Uganda (UPDF) lina uzoefu na uwezo wa kushiriki katika operesheni za kimataifa za kudumisha amani.

    Uamuzi huo ni ishara kuwa Uganda iko tayari kuwatuma wanajeshi wake kujiunga na kikosi cha kimataifa cha kudumish amani eneo la Gaza.

    Mwezi Julai, gazeti la serikali la New Vision, likinukuu vyanzo vya kijeshi, liliripoti kuwa Rais wa Marekani Donald Trump alimwomba Rais wa Uganda Yoweri Museveni, kutoa msaada wa kijeshi kupitia mpango wa Board of Peace, unaolenga kuunda kikosi cha kimataifa kitakachosaidia kudumisha usalama Ukanda wa Gaza.

    Akiwasilisha pendekezo hilo bungeni, Kiwanuka alisema kutumwa kwa wanajeshi hao kunazingatia mfumo wa Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa baada ya mazungumzo ya kidiplomasia kati ya Trump na Museveni.

    Aliongeza kuwa wanajeshi wa Uganda watafanya kazi kwa kuzingatia sheria za kimataifa na viwango vya kibinadamu.

    "Uganda ina jeshi imara lenye muundo mzuri wa uongozi ambao umeiwezesha kufanikisha operesheni za kulinda amani nchini Somalia, Sudan Kusini, Jamhuri ya Afrika ya Kati (CAR), pamoja na misheni mbalimbali za Umoja wa Mataifa," alisema Kiwanuka.

    Soma pia:

  3. Trump akanusha madai ya kuwa Marekani ina upungufu wa silaha, wanaoeneza uvumi watakamatwa

    .

    Chanzo cha picha, Getty Images

    Maelezo ya picha, Picha ya Donald Trump

    Rais wa Marekani Donald Trump amekanusha taarifa kuwa Marekani inakabiliwa na upungufu wa silaha na risasi za kijeshi, huku akiahidi kwamba utawala wake utatafuta "hukumu za muda mrefu gerezani" kwa watu watakaobainika kuvuja taarifa za siri.

    "Marekani ina akiba kubwa ya silaha na risasi. Zaidi ya hayo,tunaendelea kutengeneza huku zingine zikiletwa nchini kulingana na mahitaji yetu.” Trump aliandika kwenye mitandao ya kijamii mapema leo.

    Kauli hiyo ya Trump inajiri wakati vita kati ya Marekani na Iran vinaingia mwezi wa sita, huku Trump na Wizara ya Ulinzi ya Marekani wakikabiliwa na maswali kuhusu akiba ya silaha za jeshi la Marekani.

    Licha ya kusitishwa kwa mapigano mara kadhaa, Marekani na Iran zimeendelea kushambuliana, huku makubaliano ya kumaliza kabisa vita hivyo ikiwa bado haijaafikiwa

    Shirika la habari la CBS News, limeripoti kuwa Marekani imetumia sehemu kubwa ya akiba yake ya kimataifa ya makombora ya masafa marefu katika vita hivyo.

    Gazeti la Washington Post liliripoti siku ya Jumatano jioni kwamba Trump alimhoji Waziri wa Ulinzi Pete Hegseth wiki iliyopita kuhusu uwezekano wa kuwepo kwa upungufu wa silaha, gazeti hilo lilikinukuu vyanzo ambavyo havikutajwa majina.

    Soma pia:

  4. Boti yenye abiria 255 yawekwa karantini DRC baada ya vifo vya watu watano

    .

    Chanzo cha picha, Reuters

    Mamlaka nchini Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo (DRC) zinafanya uchunguzi wa ugonjwa wa Ebola na kipindupindu kwa abiria 255 waliokuwa ndani ya boti moja iliyozuiliwa katika Mto Congo.

    Boti hiyo, Yingfeng 2, inayomilikiwa na kampuni ya China, ilisimamishwa karibu na bandari ya Bende Bende, takriban kilomita 65 kutoka mji mkuu, Kinshasa.

    Waziri wa Afya wa DRC, Roger Kamba, amesema uchunguzi huo unafanyika kama tahadhari, baada ya abiria mmoja aliyekuwa na homa na kuendesha, ambaye alikuwa ameshuka katika kituo cha awali, kufariki akiwa hospitalini. Watu wengine wawili, mtoto wa miaka mitatu na mtoto mchanga pia wamefariki.

    Timu kutoka Wizara ya Afya ya DRC na Shirika la Afya Duniani (WHO) zimeanza kufanya uchunguzi.

    "Kwa sasa hakuna aliyebainika kuwa na Ebola, na kuna uwezekano mkubwa kwamba hakuna atakayepatikana na maambukizi baada ya kipindi cha siku 21 cha ufuatiliaji kukamilika," Kamba aliwaambia waandishi wa habari.

    Kwa mujibu wa taarifa hizo, boti hiyo iliondoka Kisangani, mji wa tatu kwa ukubwa nchini DRC, takriban wiki mbili zilizopita.

    Hivi karibuni, Kisangani imeripoti visa vya Ebola vilivyosababisha vifo vya angalau watu wanne.

    Kamba pia alisema hakujawa na visa vya Ebola katika jimbo la Mongala, ambako abiria aliyefariki alishuka, akikanusha taarifa za awali zilizodai kuwa kulikuwa na maambukizi huko.

    Boti hiyo ilisafiri zaidi ya kilomita 1,700 kuelekea Kinshasa kabla ya kuzuiliwa.

    Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo imekuwa ikikabiliana na mlipuko wake wa 17 wa Ebola tangu tarehe 15 Mei.

    Mlipuko huo unasababishwa na aina adimu ya virusi vya Ebola ya Bundibugyo.

    Soma pia:

  5. Iran yakamata wanaodaiwa 'majasusi' 21 wa Israel

    .

    Chanzo cha picha, Getty Images

    Wizara ya Ujasusi ya Iran imesema imewakamata watu 21 wanaodaiwa kuwa na uhusiano na shirika la ujasusi la Israel, Mossad, katika jimbo la Kerman, kusini mwa nchi hiyo.

    Katika taarifa iliyotolewa leo Alhamisi, wizara hiyo ilisema watuhumiwa hao walikamatwa wakati wa operesheni za kiintelijensia zilizolenga kile ilichokiita "mawakala wanaohusishwa na huduma ya ujasusi na ugaidi ya utawala wa Kizayuni (Mossad)."

    Kwa mujibu wa wizara hiyo, watu hao wanadaiwa kukusanya taarifa kuhusu maeneo nyeti na ya siri ya kijeshi pamoja na mifumo ya ulinzi wa anga, kisha kuzifikisha kwa Mossad.

    Iran haikutoa ushahidi wa madai hayo, huku Israel ikiwa haijatoa tamko lolote kuhusu tuhuma hizo.

  6. Raia wa Uganda waombeleza kifo cha nahodha wa timu ya Uganda baada ya kushambuliwa na genge la majambazi

    .

    Chanzo cha picha, SC Villa

    Raia wa Uganda wanaomboleza kifo cha mmoja wa wachezaaji wa soka maarufu nchini humo, David Owori, aliyefariki akiwa na umri wa miaka 27, baada ya kushambuliwa na majambazi wanaoshukiwa kuwa walikuwa wakitaka kumuibia karibu na nyumbani kwake, jijini Kampala.

    Polisi nchini Uganda wamesema Owori aliuawa baada ya kupigwa vibaya alipojaribu kupinga jaribio la kuibiwa simu yake ya mkononi na mali nyingine.

    Tukio hilo limezua majonzi makubwa na kuchochea hasira za umma kuhusu ongezeko la uhalifu nchini Uganda.

    Owori alikuwa nahodha wa klabu ya SC Villa, mabingwa wa Ligi Kuu ya Uganda, ambako alicheza kama beki wa kulia na kiungo wa kati. Pia aliwahi kuichezea timu ya taifa ya Uganda, The Cranes.

    "Tumepoteza zaidi ya mchezaji tumepoteza kiongozi, ndugu na rafiki," klabu ya SC Villa ilisema katika taarifa.

    Walioshuhudia tukio hilo wamesema kundi hilo la wezi lilimpiga Owori kwa mawe usiku wa Jumanne kabla ya kumpora mali zake na kutoroka, na kumuacha akiwa amepoteza fahamu.

    Owori alifariki kutokana na majeraha aliyopata katika hospitali moja Jijini Kampala.

    Soma pia:

  7. Iran yatishia kushambulia nchi za Ghuba iwapo Marekani itaishambulia tena

    .

    Chanzo cha picha, Reuters

    Iran imezionya nchi za Ghuba kwamba shambulio lolote jipya la Marekani dhidi ya ardhi yake itachochea mashambulizi ya kulipiza kisasi dhidi ya miundombinu muhimu ya nishati katika eneo hilo

    Tehran iko tayari kuchukua hatua yoyote ya kijeshi dhidi ya washirika wa Marekani katika eneo hilo.

    Maafisa wawili wa ngazi ya juu wa Iran, vyanzo viwili kutoka nchi za Ghuba na mwanadiplomasia mmoja wa ngazi ya juu wa kikanda walisema Waziri wa Mambo ya Kigeni wa Iran, Abbas Araqchi, alizungumza kwa simu na mawaziri wenzake wa Saudi Arabia, Uturuki na Qatar, pamoja na mkuu wa jeshi la Pakistan.

    Araqchi alizitaka nchi ambazo ni washirika wa Marekani eneo la Ghuba kutumia ushawishi wao kwa Rais Trump ili kumshawishi aepuke kuanzisha mashambulizi mapya dhidi ya Iran. Alionya kuwa shambulio lolote dhidi ya Iran litasababisha mashambulizi ya kulipiza kisasi dhidi ya mali za Marekani na miundombinu ya nishati katika eneo la Ghuba.

    Araqchi alisema ujumbe wa Iran ulikuwa ule ule katika mazungumzo yote "Tuko tayari kulipiza kisasi, lakini suluhisho la kidiplomasia ndilo njia bora ya kuepuka kutanuka kwa mzozo na uharibifu wa mali."

    Soma pia:

  8. DR Congo yapiga marufuku usafirishaji wa madini ya shaba na kobalti nje ya nchi

    .

    Chanzo cha picha, Reuters

    Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo (DRC) imepiga marufuku usafirishaji wa madini ya shaba na kobalti nje ya nchi, katika hatua kubwa ya kuhakikisha madini hayo yanaboreshwa ndani ya nchi hiyo na taifa la DRC linanufaika zaidi na rasilimali zake za madini.

    Katika amri ya serikali ya iliyotolewa mwezi tarehe 29 mwezi Juni, marufuku hiyo imetiwa saini na Waziri wa Madini Louis Kabamba Watum, Waziri wa Biashara ya Nje Julien Paluku Kahongya na Waziri wa Uchumi Daniel Mukoko Samba.

    Amri hiyo inaeleza kuwa: "Usafirishaji wa shaba na kobalti nje ya nchi imepigwa marufuku."

    DR Congo ndiyo mzalishaji mkubwa zaidi wa kobalti duniani na msambazaji wa pili kwa ukubwa wa shaba.

    Marufuku hiyo imeanza kutekelezwa mara moja, huku mfumo mpya wa ushuru wa madini ulioanzishwa ukipewa kipindi cha mpito cha miezi mitatu kabla ya kuanza kutumika kikamilifu.

    Hata hivyo, amri hiyo inampa Waziri wa Madini mamlaka ya kutoa kibali cha mwaka mmoja cha kusafirisha madini hayo nje ya nchi endapo kutakuwa na mazingira yanayoelezwa kuwa ya "kimkakati."

    Soma pia:

  9. Reuters: Makubaliano kati ya Iran na Oman kuipa Tehran udhibiti wa meli zinazoingia Ghuba ya Uajemi

    .

    Chanzo cha picha, Getty Images

    Makubaliano yaliyopendekezwa kati ya Iran na Oman yanayolenga kumaliza vita vya miezi mitano kati ya Iran na Marekani inaweza kuipa Tehran mamlaka ya kudhibiti meli zinazoingia katika Ghuba ya Uajemi kupitia Mlango Bahari wa Hormuz.

    Kulingana na vyanzo vya shirika la habari la Reuters nchini Iran,haya ni makubaliano makubwa yaliyoridhiwa na Iran.

    Marekani bado haijatoa kauli rasmi kuhusu pendekezo hilo.

    Rais Donald Trump amesema makubaliano ya kufungua tena Mlango Bahari wa Hormuz yako karibu kufikiwa, lakini maafisa wa Marekani wamesisitiza mara kadhaa kwamba hawatakubali Iran kuwa na udhibiti wa njia hiyo muhimu ya usafirishaji wa nishati duniani.

    Reuters inasema iwapo makubaliano hayo yatakamilika na kuruhusu Iran kudhibiti meli zinazopita katika mlango huo, vita vilivyoanzishwa na Marekani na Israel mwezi Februari vitakuwa vimesababisha mabadiliko makubwa ya mizani ya nguvu katika eneo hilo kwa manufaa ya Tehran.

    Kabla ya vita hivyo, Mlango Bahari wa Hormuz ulikuwa wazi kwa meli zote bila kutozwa ushuru wa kupita.

    Iran na Oman zimekuwa zikifanya mazungumzo ya pande mbili kama sehemu ya juhudi za kidiplomasia za kikanda kuhusu Mlango Bahari wa Hormuz, ambao njia zake za kaskazini na kusini ziko ndani ya maji ya nchi hizo mbili.

    Iran imesema mazungumzo hayo yamepiga hatua kubwa.

    Soma pia:

  10. Habari za hivi punde, Ukraine yashambulia viwanda viwili vya kusafisha mafuta vya Urusi - Zelensky

    .

    Chanzo cha picha, Getty Images

    Maelezo ya picha, Rais Zelensky

    Rais Volodymyr Zelensky amesema kuwa Ukraine imeshambulia viwanda viwili vya kusafisha mafuta nchini Urusi.

    Katika ujumbe kwenye mitandao ya kijamii, ameandika kuwa Vikosi vya Ulinzi vya Ukraine vilishambulia kiwanda cha kusafisha mafuta cha Slavneft-Yanos huko Yaroslavl na kiwanda cha Bashneft-Novoil huko Bashkortostan.

    Awali, tuliripoti kuwa moshi mweusi ulikuwa ukifuka kutoka upande wa kiwanda cha kusafisha mafuta cha Yaroslavl kufuatia mashambulizi ya ndege zisizo na rubani za Ukraine.

    Gavana wa Yaroslavl, Mikhail Evraev, anasema ndege hizo zisizo na rubani za Ukraine zilizoshambulia eneo hilo zimeharibiwa, lakini vipande vilivyoanguka chini vilisababisha nyumba tatu kuungua moto.

    Zelensky anasema pia walishambulia boti mbili za doria za kijeshi na meli kutoka kwenye kundi la meli za siri za Urusi katika Bahari Nyeusi.

  11. Wachezaji wawili wa soka wa kike kutoka Iran wapewa uraia wa Australia baada ya kuomba hifadhi

    .

    Chanzo cha picha, Jactran

    Wachezaji wawili wa zamani wa soka wa kike kutoka Iran wamesema wanajivunia kupata uraia wa Australia.

    Atefeh Ramezanizadeh na Fatemeh Pasandideh walikuwa miongoni mwa wachezaji saba wa timu ya taifa ya soka ya wanawake ya Iran waliokataa kuimba wimbo wa taifa katika mechi ya kwanza ya Kombe la Asia nchini Australia; hatua iliyosababisha baadhi ya watu nchini Iran kuwaita "wasaliti wa wakati wa vita."

    Kati ya wachezaji na wafanyakazi walioondolewa kwenye kambi ya timu ya taifa baada ya tukio hilo, ni hao wawili pekee walioamua kubaki Australia baada ya kupata msaada wa kibinadamu, na jana walikabidhiwa uraia wa Australia katika hafla iliyohudhuriwa na Tony Burke, Waziri wa Mambo ya Ndani wa Australia.

    Bi. Ramazanizadeh alisema katika ujumbe wake: "Jana ilikuwa siku ya kipekee na isiyosahaulika kwangu. Ninajivunia sana na ninashukuru kwa kuwa raia wa Australia."

    Bi. Pasandideh pia alisema katika ujumbe kwenye ukurasa wake wa Instagram: "Baada ya kupitia siku ngumu na zenye changamoto, leo ni mwanzo wa sura mpya kwangu. Ninawashukuru sana Australia na jamii ya Wa-Iran walioandamana nasi katika safari hii na kufanya kila waliloweza."

  12. Meneja wa timu ya Uganda hajui sababu ya mabondia wa nchi hiyo kutoweka

    .

    Chanzo cha picha, Getty Images

    Meneja wa timu ya Michezo ya Jumuiya ya Madola ya Uganda ameiambia BBC Scotland News kwamba hajui ni kwa nini mabondia wanne wa timu hiyo wametoweka.

    Wanaume wawili na wanawake wawili walioshindania Uganda kwenye Michezo hiyo walishindwa kujitokeza kwa safari zao za ndege zilizopangwa kurudi nyumbani na tangu wakati huo wamezima simu zao.

    Ripoti za vyombo vya habari nchini Uganda, nje zilionyesha kuwa wanne hao wanaweza kuwa wanatafuta hifadhi, lakini mpishi mkuu wa Uganda Godwin Kayangwe alisema anatumai wanariadha hao watarudi nyumbani kabla ya visa yao kumalizika mwezi Oktoba.

    Polisi wanasema uchunguzi unaendelea kuhusu wanariadha kadhaa wa Jumuiya ya Madola ambao wameshindwa kujitokeza kwa safari za ndege za kurudi nyumbani, lakini inaeleweka kuwa hakuna kitakachofanyika hadi visa yao itakavyoisha.

    Bondia hao wanne, Ibrahim Kemis mwenye miaka 20, Nuhu Batte 22, Emily Nakalema 32, na Angel Katushabe 21, walikuwa wanatarajiwa kurjea Uganda siku ya Ijumaa.

    Kayangwe alisema hana taarifa zozote kuhusu sababu ya wao kutoweka, lakini anahisi kuwa "huenda bado wako Glasgow au mahali fulani barani Ulaya."

    "Sijui chochote kuhusu sababu iliyowafanya waamue kutorejea nyumbani, lakini najua waliwasiliana na meneja wa timu yao na kusema kuwa watarudi.

    "Lakini baada ya hapo simu zao hazikupatikana, hivyo bila shaka wamekiuka kanuni za kambi kwa sababu hakuna mwanamichezo anayeruhusiwa kuondoka bila idhini.

    "Visa zao bado ni halali hadi mwezi Oktoba, kwa hivyo tunatumai kuwa huenda watarejea nchini mwao."

    Alipoulizwa ni kwa nini huenda wanariadha hao wanataka kuomba hifadhi, meneja wa timu alisema hajui.

  13. UN yashangazwa na ongezeko la mauaji ya watu Iran

    .

    Chanzo cha picha, LightRocket via Getty Images

    Mkuu wa haki za binadamu katika Umoja wa Matafa amesema ameshangazwa na ongezeko la mauaji Iran, huku adhabu kali ikiendelea kutekelezwa, kuwatia hofu watu na kukandamiza upinzani.

    Volker Türk alisema kuwa takriban watu 56 wameuawa kwa kunyongwa kutokana na mashtaka yanayohusiana na usalama wa taifa tangu tarehe 19 Machi, wakiwemo watu 27 katika kesi zilizohusishwa na maandamano ya nchi nzima dhidi ya serikali yaliyofanyika mwezi Januari.

    Aliongeza kuwa zaidi ya watu wengine 100 wako katika hatari ya kunyongwa kwa mashtaka kama hayo, huku mauaji ya kisheria kwa makosa yanayohusiana na dawa za kulevya pia yakiendelea kwa kasi ya kutisha.

    Iran inaaminika kuwa nchi ya pili duniani kwa idadi kubwa zaidi ya utekelezaji wa hukumu za kifo baada ya China. Mwaka jana, ilitekeleza hukumu ya kifo kwa angalau watu 2,159, kulingana na shirika la Amnesty International.

    Shirika hilo la haki za binadamu lilisema kuwa hiyo ndiyo idadi kubwa zaidi kuwahi kurekodiwa tangu mwaka 1981, na ilijumuisha mauaji ya watu 45 waliotuhumiwa kuwa wapinzani wa serikali kwa makosa yanayohusiana na usalama wa taifa.

    Wanaharakati wameonya kuwa mamalaka za Iran zitatumia zaidi hukumu ya kifo dhidi ya wapinzani kufuatia maanadamano ya Januari, ambapo maelfuya waandamanji waliuawa na makumi ya maelfu kukamatwa.

    Mkuu wa haki za binadamu katika Umoja wa Matafa amesema ameshangazwa na ongezeko la mauaji Iran, huku adhabu kali ikiendelea kutekelezwa, kuwatia hofu watu na kukandamiza upinzani.

    Volker Türk alisema kuwa takriban watu 56 wameuawa kwa kunyongwa kutokana na mashtaka yanayohusiana na usalama wa taifa tangu tarehe 19 Machi, wakiwemo watu 27 katika kesi zilizohusishwa na maandamano ya nchi nzima dhidi ya serikali yaliyofanyika mwezi Januari.

    Aliongeza kuwa zaidi ya watu wengine 100 wako katika hatari ya kunyongwa kwa mashtaka kama hayo, huku mauaji ya kisheria kwa makosa yanayohusiana na dawa za kulevya pia yakiendelea kwa kasi ya kutisha.

    Iran inaaminika kuwa nchi ya pili duniani kwa idadi kubwa zaidi ya utekelezaji wa hukumu za kifo baada ya China. Mwaka jana, ilitekeleza hukumu ya kifo kwa angalau watu 2,159, kulingana na shirika la Amnesty International.

    Shirika hilo la haki za binadamu lilisema kuwa hiyo ndiyo idadi kubwa zaidi kuwahi kurekodiwa tangu mwaka 1981, na ilijumuisha mauaji ya watu 45 waliotuhumiwa kuwa wapinzani wa serikali kwa makosa yanayohusiana na usalama wa taifa.

    Wanaharakati wameonya kuwa mamalaka za Iran zitatumia zaidi hukumu ya kifo dhidi ya wapinzani kufuatia maanadamano ya Januari, ambapo maelfuya waandamanji waliuawa na makumi ya maelfu kukamatwa.

  14. Maelfu ya watu wamiminika katika kijiji cha West Pokot Kenya kufuatia ripoti ya ugunduzi wa dhahabu

    .

    Ripoti kuhusu ugunduzi wa dhahabu katika kijiji cha Cheparor, eneo bunge la Kapenguria kaunti ya West Pokot, nchini Kenya imesababisha wimbi kubwa la watu wanaotafuta utajiri kumiminika katika eneo hilo.

    Video zilizotazamwa zilionyesha umati mkubwa wa watu ukiwa ametapakaa katika eneo la wazi, wakichimba kwa kutumia zana duni huku wengine wakikusanya udongo kwenye mabakuli na magunia kabla ya kuondoka nao.

    Picha hizo zilionyesha wanaume na wanawake wakifanya kazi pamoja; baadhi wakichimba mashimo madogo huku wengine wakipanga foleni kuchukua udongo uliochimbwa, wakionekana kuwa na nia ya kuuchunguza zaidi mahali pengine ili kuona kama una chembechembe za madini hayo ya thamani.

    Kulingana na taarifa zinazosambaa mtandaoni, harakati hizo zilianza baada ya wavulana wawili kudaiwa kugundua kitu kilichoaminika kuwa dhahabu katika eneo hilo.

    Hata hivyo, bado haijafahamika wazi iwapo ugunduzi huo ulikuwa wa kitu kimoja tu au iwapo eneo hilo lina akiba ya dhahabu inayoweza kuchimbwa kibiashara.

    Mamlaka husika hazikuwa zimethibitisha ripoti hizo.

    Video hiyo pia ilionyesha watu wakifika kutoka pande mbalimbali, huku baadhi ya ripoti zikidai kuwa watu wanaotafuta utajiri walisafiri kutoka nchi jirani ya Uganda na sehemu nyingine za Kenya baada ya habari za ugunduzi huo kusambaa.

  15. Mshawishi maarufu wa Mexico apigwa risasi na kuuawa wakati wa matangazo ya moja kwa moja

    .

    Chanzo cha picha, Instagram/César Gastélum

    Mshawishi mashuhuri wa Mexico, César Gastélum, amepigwa risasi na kuuawa alipokuwa akirusha matangazo ya moja kwa moja kwenye mitandao ya kijamii.

    Gastélum alikuwa akirekodi filamu na marafiki wawili nje ya mgahawa mmoja huko Tres Ríos, katika jiji la kaskazini la Culiacán, Jumanne jioni wakati wanaume wawili waliokuwa kwenye pikipiki walipomsogelea na mmoja akampiga risasi karibu.

    Alikuwa na wafuasi zaidi ya nusu milioni kwenye TikTok na zaidi alipakia video za vichekesho.

    Sio mara ya kwanza kwa mshawishi maarufu wa mitandao ya kijamii kuuawa nchini Mexico. Mwaka jana, Valeria Márquez mwenye umri wa miaka 23 alipigwa risasi na kuuawa katika saluni ya urembo alipokuwa akirusha matangazo ya moja kwa moja kwenye TikTok.

    Katika matangazo ya moja kwa moja, Gastélum na marafiki zake walikuwa wamevaa makoti ya rangi ya chungwa angavu na mifuko ambayo kwa kawaida hutumiwa na madereva wa usafirishaji.

    Vyombo vya habari vya ndani viliripoti kwamba mavazi yao hapo awali yaliwafanya polisi kuamini kwamba mwathiriwa alikuwa dereva wa usafirishaji, lakini maafisa baadaye waliarifiwa kuhusu utambulisho wake.

    Polisi na wataalamu wa uchunguzi wa mauaji walizingira eneo hilo na wanachunguza vifuniko vya risasi na picha za CCTV kwa dalili zozote.

    Hakuna mtu aliyekamatwa hadi sasa na watu wawili waliokuwa kwenye pikipiki walitoroka eneo la tukio.

  16. Timu ya wanawake ya Afghanistan yaungana tena uhamishoni

    .

    Chanzo cha picha, Phil Walter/Getty Images

    Baada ya kupigwa marufuku kushiriki soka nchini mwao, timu ya wanawake ya Afghanistan inaungana tena ikiwa umbali wa maili 8,000.

    Chumba cha kubadilisha nguo kina shughuli nyingi huku wachezaji soka, wakifanya maandalizi yao kabla ya mechi. Wengine wananyoosha viungo wakifunga kamba za viatu vyao, huku wengine wakikumbatiana.

    "Muwe imara kama kawaida kwa sababu tunawakilisha wanawake wa Afghanistan," anasema kiungo Fatima Haidari akiwaambia wenzake wa timu ya Afghan Women United.

    Makofi yanapigwa ndani ya chumba hicho ambamo bendera ya Afghanistan imetundikwa na wimbo wa kizalendo unachezwa.

    Wanawake hao wanapoimba pamoja, baadhi yao wanajitahidi kuzuia machozi.

    Kuna mkusanyiko wa mwisho wa timu ambapo wanapata maneno ya kutia moyo kutoka kwa kocha wao kabla ya kuelekea uwanjani,mahali ambapo kwa miaka mingi waliambiwa hawastahili kuwepo.

    Kikosi hicho cha wachezaji 23, kilichochaguliwa kutoka miongoni mwa wachezaji wa Afghanistan wanaoishi nje ya nchi, kimesafiri hadi New Zealand kwa ajili ya kambi ya mazoezi na kucheza mechi mbili za kirafiki zisizo rasmi dhidi ya Cook Islands.

    Hii ni mara ya kwanza kwao kuwa pamoja tangu shirikisho la soka duniani, FIFA, lilipoamua mwezi Aprili kwamba wanaweza kuiwakilisha nchi yao katika mashindano rasmi.

    Awali wangehitaji idhini kutoka shirikisho la soka la Afghanstan. Hili halingewezekana chini ya uongozi wa Taliban, waliorejea madarakani mwezi Agosti 2021, na kuweka vikwazo dhidi ya wananwake na wasichana, ikiwa ni Pamoja na kuwazuia kwenda shule ya sekondari na vyuo vikuu, kufanya kazi katika taaluma nyingi, na kushiriki michezo.

  17. Droni yenye vilipuzi yapatikana katika uwanja wa ndege wa Ujerumani - Polisi

    .

    Chanzo cha picha, Jens Schlueter/Getty Images

    Polisi wanasema ndege isiyo na rubani iliyobeba kifaa cha kulipuka imepatikana katika uwanja wa ndege wa Ujerumani.

    Roboti ilitumwa katika Uwanja wa Ndege wa Leipzig/Halle baada ya kifaa hicho kuonekana na mfanyakazi karibu na ndege za mizigo za Ukraine usiku kucha, kulingana na polisi wa Saxony.

    Kitu cha pili kisichojulikana pia kiligongana na ndege ya mizigo karibu na uwanja huo huo wa ndege. Kilitua Hanover kikiwa na uharibifu mdogo.

    Waziri wa mambo ya ndani wa Ujerumani alisema matukio hayo yalionyesha "kiwango kipya cha tishio".

    Viwanja vya ndege vya Ujerumani viko macho kufuatia safari kadhaa za ndege zisizo na rubani ambazo hazijaidhinishwa katika miezi ya hivi karibuni juu ya kambi za kijeshi, viwanja vya ndege, vituo vya nishati, bandari na makampuni ya usafirishaji.

    Polisi wameonya kuhusu uwezekano wa kuhusika kwa Urusi ambayo Moscow imekanusha.

    Uwanja wa Ndege wa Leipzig/Halle mashariki mwa Ujerumani unatumiwa na jeshi la Ujerumani na washirika wa Nato kwa ajili ya usafirishaji wa bidhaa za kijeshi na pia hutumika kama kituo cha Shirika la Ndege la Antonov la Ukraine - ambalo hubeba mizigo mingi ya angani nchini humo.

    Pia ni kitovu kikubwa cha kundi la usafirishaji, DHL.

  18. JD Vance: Wairani ni watu wasumbufu sana

    .

    Chanzo cha picha, EPA

    Maelezo ya picha, JD Vance

    Katika mahojiano na kituo cha habari cha Fox News, makamu wa rais wa Donald Trump, J.D. Vance, alijibu hoja kuhusu kutoridhika kwa wananchi wa nchi yake na vita dhidi ya Iran, akisema kuwa mojawapo ya changamoto ni kwamba ndani ya serikali ya Iran kuna kundi linalotaka mazungumzo, huku kundi jingine lenye msimamo mkali likitaka vita viendelee.

    Bw. Vance, ambaye aliongoza timu ya mazungumzo ya Marekani wakati wa mazungumzo ya Islamabad, aliambia Fox News kuwa kwa mtazamo wake, mchakato wa mzozo na makabiliano na Iran una vipindi vya kupanda na kushuka, lakini anaamini kuwa hatimaye, "mambo yote yatatatuliwa kwa maslahi bora ya wananchi wa Marekani."

    Wakati huo huo, baadhi ya ripoti zimeashiria kuwa Mohammad Baqer Qalibaf huenda akaitembelea Pakistan katika siku chache zijazo.

    Iran haijatoa majibu rasmi kuhusiana na ripoti hizo. Bw. Qalibaf alikuwa mjumbe mkuu wa mazungumzo kwa upande wa Iran wakati wa mazungumzo kati ya Tehran na Washington yaliyoongozwa na Pakistan, ambayo hatimaye yalisababisha kusainiwa kwa Hati ya Makubaliano ya Islamabad; hata hivyo, hati hiyo ilipoteza nguvu yake punde tu baada ya nchi hizo mbili kurejelea uhasama.

  19. Rais wa Nigeria aagiza nyongeza ya mishahara ya asilimia 80 kwa askari wa vyeo vya chini

    .

    Chanzo cha picha, Getty Images

    Maelezo ya picha, Wanajeshi wa Nigeria wanapambana na maadui kadhaa, wakiwemo wanamgambo wa Kiislamu, makundi ya wanaotaka kujitenga na magenge yanayowateka nyara raia ili kudai fidia.

    Wanajeshi wa Nigeria wanatarajiwa kupata nyongeza ya mishahara ya hadi asilimia 80 – ikiwa ni mara ya pili kwa mishahara yao kuongezwa ndani ya mwezi mmoja – kutokana na kile ambacho Rais Bola Tinubu anakitaja kuwa ni "shukrani kubwa" ya serikali kwa wale wanaopambana na vitisho vikubwa vya usalama vinavyolikabili taifa.

    Mwezi Julai, Waziri wa Ulinzi aliongeza mishahara ya kila mwezi ya askari wa ngazi ya chini kabisa kutoka dola 36 (pauni 27) hadi dola 73.

    Kufuatia uamuzi wa Rais, sasa watapokea dola 132 kuanzia mwezi Septemba.

    Hatua hii ni sehemu ya juhudi za Tinubu za kudhibiti vurugu zinazosababishwa na makundi mbalimbali yenye silaha, yakiwemo makundi ya wapiganaji wa Kiislamu na magenge ya uhalifu yanayojihusisha na utekaji nyara, ambayo kwa ndani yanajulikana kama "majambazi".

    Mwezi uliopita, aliamuru kuajiriwa kwa wanajeshi wa ziada 28,000 na kuanzishwa kwa vikosi vipya vinne vya jeshi.

    Hali ya ukosefu wa usalama inayoendelea nchi nzima imekuwa suala kuu la kisiasa kuelekea uchaguzi wa mwaka 2027.

  20. Washington Post: Trump na waziri wake watofautiana huko Camp David kuhusu kupungua kwa akiba ya makombora

    .

    Chanzo cha picha, Reuters

    Maelezo ya picha, Rais Trump na waziri Hegseth

    Kwa mujibu wa gazeti la Washington Post, Rais wa Marekani Donald Trump na Waziri wa Ulinzi Pete Hegsett walitofautiana kuhusu kupungua kwa akiba ya makombora na risasi za jeshi la Marekani wakati wa mzozo na Iran, katika mkutano wa maafisa wakuu wa serikali uliofanyika wikendi huko Camp David.

    Kwa mujibu wa vyanzo hivyo, katika mkutano huo, Bw. Trump alimtaka Pete Hegsett kuelezea sababu ya kupungua kwa kasi kwa akiba ya silaha zenye usahihi wa hali ya juu na makombora ya masafa marefu, huku akionyesha wasiwasi kuhusu utayari wa kijeshi wa nchi hiyo kwa ajili ya mzozo unaoendelea.

    Ripoti hiyo inakuja baada ya vyombo vya habari vya CBS News na Reuters kuripoti hivi karibuni—vikinukuu vyanzo visivyotajwa majina—kwamba Marekani imetumia karibu akiba yake yote ya makombora ya masafa marefu yenye usahihi wa hali ya juu, ikiwemo mfumo wa makombora ya kimkakati ya jeshi la nchi kavu (ATCM) na makombora ya mashambulizi yenye usahihi wa hali ya juu, wakati wa operesheni yake ya kijeshi dhidi ya Iran iliyopewa jina la "Epic Fury."

    Ripoti hizo pia zinaonyesha kuwa akiba ya makombora ya kulinda anga aina ya Patriot na THAAD imepungua kwa kasi inayozidi uwezo wa uzalishaji wa viwanda vya ulinzi vya Marekani.

    Hata hivyo, maafisa wa serikali ya Marekani wamekanusha tathmini hizo. Sean Parnell, msemaji mkuu wa Wizara ya Ulinzi ya Marekani, amesema kuwa jeshi la Marekani "linaendelea kuwa na kila kitu kinachohitajika kutekeleza majukumu yake" na lina uwezo wa kutosha kulinda maslahi ya Marekani.

    Awali, Pete Hegsett alizitaja ripoti kuhusu kupungua kwa kutia wasiwasi kwa akiba ya silaha za Marekani kuwa "hadithi ya kubuni" na kusema kuwa akiba ya kijeshi ya nchi hiyo haijapungua, bali inaendelea kuimarishwa.

    Maafisa waliozungumza na Washington Post walidai kuwa sababu ya shambulio kubwa ambalo Bw. Trump alitishia kuifanyia Iran wiki iliyopita ilikuwa ni wasiwasi kuhusu uhaba huo wa akiba ya makombora..