Hii ni tovuti ya maandishi pekee ambayo inatumia data kidogo. Tazama toleo kuu la tovuti likijumuisha picha na video zote.

Bofya kuelekea tovuti kuu

Pata maelezo zaidi kuhusu toleo hili la linalotumia kiasi kidogo cha data

Moja kwa moja, Trump: Tutaishambulia Iran tena ikibidi

Trump pia amesema kuwa licha ya kile kinachoangaziwa kwenye vyombo vya habari, Marekani ndiyo inayodhibiti Mlango-Bahari wa Hormuz.

Muhtasari

Moja kwa moja

Na Ambia Hirsi & Beldeen Waliaula

  1. Tutajibu vikwazo vya kiuchumi vya Marekani - Iran

    Iran imesema itajibu vikali vitisho vipya kutoka Marekani, baada ya Marekani kusema inapania kuweka vikwazo vikali Zaidi vya kifedha dhidi ya Iran, vitakavyoporomosha utawala wa taifa hilo.

    Rais wa Marekani Donald Trump pia alionya kuchukua hatua za kiuchumi dhidi ya nchi yoyote itakayotoa msaada kwa Iran.

    Mkuu wa Majeshi ya Iran, Meja Jenerali Ali Abdollahi, amesema jibu la Jamhuri ya Kiislamu litakuwa pana na la kuamua.

    “Kwa kuwa tumejiandaa kikamilifu ardhini, baharini, angani, katika ulinzi wa anga na kwenye anga ya mtandao, majeshi ya Iran yatajibu vitisho vipya vya adui kwa mashambulizi makali, ya kuangamiza,” vyombo vya habari vya Iran vilimnukuu mkuu huyo wa majeshi.

    Spika wa Bunge la Iran, Mohammad Baqer Qalibaf, ambaye ni mwakilishi mkuu wa nchi hiyo katika mazungumzo kati ya Iran na Marekani, amesema Washington inaonekana kufikia hitimisho kwamba haiwezi kushinda katika makabiliano ya moja kwa moja ya kijeshi.

    “Lazima tufanye mipango ya kukabiliana na vikwazo visivyo vya haki ili tuweze kuvishinda,”Qalibaf alisema akiwa nchini Iraq, huku akiishutumu Marekani na Israel kwa kutumia kile alichokiita vita vya kiuchumi na kisaikolojia kuidhulumu Iran.

    Soma pia:

  2. Raia wawili wa Mexico wakamatwa Afrika Kusini katika maabara ya dawa ya kulevya

    Raia wawili wa Mexico wamekamatwa nchini Afrika Kusini baada ya polisi kugundua maabara ya kutengeneza dawa za kulevya aina ya crystal methamphetamine yenye thamani ya mamilioni ya dola kaskazini mwa nchi hiyo.

    Maabara hiyo ilivamiwa usiku katika shamba lililoko karibu na mji wa Musina, katika mkoa wa Limpopo, karibu na mpaka wa Afrika Kusini na Zimbabwe. Raia wawili wa Zimbabwe na raia mmoja wa Malawi pia walikamatwa.

    Dawa za kulevya na vifaa vyenye thamani ya takriban dolla million 37 vilikamatwa, pamoja na kiasi cha fedha taslimu ambacho hakikutajwa.

    Soma pia:

  3. Iran haiwezi kuendelea ikiwa wananchi wake wana njaa - Ghalibaf

    Spika wa Bunge la Iran, Mohammad Baqer Ghalibaf, amesema serikali ya taifa hilo lazima ijipange kukabiliana na vitisho vya kiuchumi kutoka kwa Marekani, la sivyo serikali hiyo haitadumu kwa muda mrefu.

    Ghalibaf, ambaye yuko nchini Iraq, amesema kuwa “haijalishi tuna nguvu kiasi gani kijeshi, ikiwa wananchi wana njaa na hatuna mzunguko wa fedha, ukuaji wa uchumi na uzalishaji wa ndani, hatutaweza kuendelea kuishi.”

    Ghalibaf, ambaye amekuwa mmoja wa viongozi wakuu wa Iran katika mazungumzo na Marekani, amesema ni lazima Iran iweke mipango ya kukabiliana na vikwazo vya kiuchumi anavyovita vya “ukandamizaji”, ili iweze kushinda vita hivyo.

    Ghalibaf amehoji kuwa sarafu za kitaifa za Iran na Iraq zitumike katika biashara ya nchi hizo mbili ili kupunguza matumizi ya dola ya Marekani.

    Waziri wa fedha wa Marekani, Scott Bessent, amesema vikwazo vipya vya Washington dhidi ya Iran “vitawatenga pakubwa kiuchumi na huenda ikaporomosha utawala wa Iran”

    Soma pia:

  4. Polisi Zambia wamtaka kiongozi wa upinzani kuhojiwa kuhusu madai yake ya wizi wa kura

    Polisi nchini Zambia wanamtaka kiongozi wa upinzani Brian Mundubile kuhojiwa baada yakudai kuwa kulikuwa na wizi wa kura katika uchaguzi uliokamilika wiki iliyopita.

    Kiongozi huyo alishikilia nafasi ya pili baada ya Rais Hakainde Hichilema kushinda uchaguzi huo na kuanza kuhudumu muhula wake wa pili.

    Hichilema, ambaye amekuwa madarakani tangu mwaka wa 2021 katika taifa hilo lenye utajiri wa madini, amekanusha madai kwamba uchaguzi huo ulikumbwa na udanganyifu.

    Aidha awali Mundubile alisema atakwenda mahakamani kupinga matokeo hayo.

    Katika taarifa iliyotolewa na idara ya polisi, imesema kuwa wanataka kumhoji Mundubile pamoja na mgombea mwenza wake, Makebi Zulu, kama sehemu ya uchunguzi kuhusu madai ya kutishia usalama wa taifa.

    Mgombea huyo wa urais wa upinzani amekuwa mafichoni baada ya polisi kufanya msako muda mfupi baada ya uchaguzi wa Agosti 13, ambapo viongozi kadhaa wa upinzani walikamatwa na mmoja wao, aliyekuwa waziri Mutotwe Kafwaya, kuuawa kwa kupigwa risasi wakati wa majibizano ya risasi.

    Taarifa ya polisi pia ilisema imetuma barua kwa mawakili wa viongozi hao wa upinzani wakitaka Mundubile na Zulu kujiwasilisha katika kituo cha polisi.

    Soma pia:

  5. Kepler: Ni meli saba pekee zilipitia lango la Hormuz Alhamisi

    Data ya awali ya kampuni ya Kepler inayofuatilia usafiri wa majini inaonyesha kuwa idadi ya meli zilizopitia Mlango-Bahari wa Hormuz ilipungua siku Alhamisi ikilinganishwa na siku zingine.

    Usafiri kupitia Hormuz umeathiriwa na hali ya wasiwasi unaoongezeka katika eneo hilo na huku mazungumzo ya amani kati ya Iran na Marekani yakiendelea kugubikwa na hali ya sintofahamu.

    Kulingana na Reuters, data kutoka kwa kampuni ya ufuatiliaji wa safari za baharini ya Kepler inaonyesha kuwa ni meli saba pekee za mizigo zilizopita katika Mlango - Bahari wa Hormuz siku ya Alhamisi.

    Kulingana na takwimu za Kepler, idadi hii ni sawa na nusu ya meli zilizopita katika eneo hilo siku ya Jumatano.

    Kati ya meli hizo saba, nne ziliingia katika Mlango-Bahari wa Hormuz na tatu ziliondoka.

    Kulingana na Kepler, hakuna hata moja kati ya meli hizo iliyokuwa meli za mafuta au meli za gesi.

    Rais wa Marekani Donald Trump amekuwa akisisitiza mara kwa mara kwamba Marekani inadhibiti wa mlango-bahari.

    Soma pia:

  6. Marekani yawataka washirika wake kuitenga Iran kiuchumi

    Marekani imetoa wito kwa washirika wake na China kujiunga na kampeni mpya ya Rais Donald Trump ya kuitenga kiuchumi Iran.

    Rais wa China, Xi Jinping, anatarajiwa kuzuru Marekani tarehe 24 Septemba.

    Iran imetaja vitisho vya Marekani dhidi yake kuwa "ugaidi wa kiuchumi" na kuongeza kuwa haitababaishwa na hatua hiyo.

    Bw. Trump ameapa kuendesha operesheni ya kiuchumi "yenye madhara makubwa zaidi" katika historia ya Iran.

    Waziri wa Fedha wa Marekani, Scott Besant, ameunga mkono msimamo wa rais na kusisitiza umuhimu wa kuimarisha shinikizo la kiuchumi dhidi ya Tehran.

    Bw. Trump na Waziri wa Fedha bado hawajatangaza maelezo ya hatua wanazopanga kuchukua dhidi ya Iran.

    Besant alisema atatoa maelezo zaidi kuhusu suala hilo katika mkutano na waandishi wa habari Jumatatu ijayo.

    Soma zaidi:

  7. Mohammed bin Salman kuzuru Ufaransa kwa mazungumzo kuhusu migogoro inayoendelea Mashariki ya Kati

    Ofisi ya Rais wa Ufaransa ilitangaza kuwa Emmanuel Macron atampokea Mrithi wa Ufalme wa Saudi Arabia, Mohammed bin Salman, arehe 23 na 24 Agosti, na viongozi hao wawili wanatarajiwa kujadili mivutano inayoendelea Mashariki ya Kati.

    Ofisi ya Macron pia imesema kuwa viongozi hao wawili wangejadili masuala na mada muhimu zaidi za kikanda.

    Mazungumzo hayo yatafanyika katika mfumo wa ushirikiano wa karibu kati ya Ufaransa na washirika wake katika eneo la Ghuba, kwa lengo la kuunga mkono utulivu na amani Mashariki ya Kati.

    Ziara ya Mohammed bin Salman jijini Paris inafanyika wakati viongozi wa nchi za Magharibi na Mashariki ya Kati wakijaribu kutatua mzozo na Iran pamoja na mgogoro unaoendelea kati ya Israel na Wapalestina.

  8. Trump: Tutaishambulia Iran tena ikibidi

    Rais wa Marekani Donald Trump amesema hatasita kuishambulia tena Iran akilazimika kufanya hivyo, ili kuizuia mpango wake wa nyuklia.

    Katika mahojiano na kituo cha WBBC77, Bw. Trump alisema kuwa kama si hatua alizochukua, Israel na Mashariki ya Kati zingekuwa zimeshaangamizwa kufikia sasa.

    Katika mahojiano hayo, alikiri kuwa aliamuru shambulio dhidi ya vituo vya nyuklia vya Iran wakati nchi hiyo ilipokuwa imesalia na wiki mbili tu kabla ya kutengeneza silaha ya nyuklia.

    Bw. Trump alisema kuwa licha ya kile kinachoripotiwa kwenye vyombo vya habari, Marekani ndiyo inayodhibiti Mlango-bahari wa Hormuz.

    Alisisitiza tena kuwa uwezo wa Iran wa makombora na ndege zisizo na rubani (droni) umedhoofishwa sana na uchumi wake uko ukingoni mwa kuporomoka.

    Bw. Trump alilitaja makubaliano ya JCPOA kuwa "janga" na kuongeza kuwa kujiondoa katika makubaliano hayo ni jambo la lazima ili kuizuia Iran kupata silaha ya nyuklia.

    Aliiita Iran kuwa "mdhalimu wa Mashariki ya Kati" na kusema: "Kama tulivyoona, Iran iliwahi kushambulia hata nchi kama Qatar, Bahrain, Kuwait, na UAE ambazo zilikuwa na uungaji mkono mdogo kwa Iran."

    Rais wa Marekani alisisitiza kuwa kama Marekani isingechukua hatua za kijeshi, Iran ingeziharibu nchi hizo zote na ingekuwa ikijiandaa kushambulia Marekani.

    Pia unaweza kusoma:

  9. FBI yamkamata mwanamke aliyepanga kulipua jengo la bunge Marekani

    Shirika la Upelelezi la Marekani FBI limemkamata mwanamke mmoja wa New York ambaye inadaiwa alipanga kulipua jengo la Bunge ili kuwaua wabunge.

    Waendesha mashtaka wanasema Jessica Bowie, 35, alikuwa mfuasi wa kundi la Islamic State.

    Bi. Bowie pia anashtakiwa kwa kutoa msaada wa vifaa au rasilimali kwa shirika la kigaidi la kigeni.

    Waendesha mashtaka wanasema Bi. Bowie "alifuatilia matukio katika jengo la Bunge mara kadhaa" na alikuwa amebeba bomu bandia na silaha isiyofanya kazi vizuri aliyopewa na maajenti wa FBI waliofichwa.

    Kulingana na mashataka ya jinai, Bi. Bowie aliwaambia maafisa: "Nataka kuharibu sehemu kubwa ya jengo iwezekanavyo na kuwaua maseneta."

    Haijabainika ikiwa ana mpango wa kujitetea dhidi ya mashtaka hayo.

    Bi. Bowie, mkazi wa eneo la Albany kaskazini mwa New York, alidaiwa kufichua mipango yake na watoa habari wa FBI na alikuwa na maajenti walioifanya wanachama wa ISIS kwa wiki kadhaa.

    Waendesha mashtaka wanasema alichagua jengo la Bunge jijini New York katika eneo la Albany kwa sababu alidhani ingekuwa lengo rahisi zaidi kuliko White House.

    Aliwaambia maafisa, "Nataka hili liathiri mfumo wa Marekani." Waendesha mashitaka wanasema alitembelea jengo hilo takribani mara tano katika misheni ya upelelezi kabla ya shambulio.

    Soma pia:

  10. Makumi ya watu wafariki dunia baada ya boti kuzama kaskazini-magharibi mwa Nigeria

    Takriban watu 46 wamefariki dunia nchini Nigeria baada ya boti kuzama katika jimbo la Sokoto, kaskazini-magharibi mwa nchi hiyo.

    Maafisa wanasema boti hiyo iliaminika kubeba zaidi ya watu 70, wengi wao wakiwa watoto, na operesheni ya uokoaji inaendelea.

    Msemaji wa polisi, Ahmad Rufai, ameimbia BBC siku ya Alhamisi kuwa miili 46 imepatikana karibu na Gorau katika eneo la Gorony.

    Watu 16 wameokolewa, huku 15 wakiwa bado hawajapatikana. Eneo hilo ni gumu kufikika, na vyombo vya usalama pamoja na huduma za dharura vinaelekea eneo la tukio, Rufai aliongeza.

    Mashuhuda mmoja aliambia shirika la habari la Reuters kuwa anaamini watoto waliokuwemo ndani ya boti hiyo walikuwa wakisafiri na wamiliki wa mashamba pamoja na vibarua waliokuwa wakielekea kufanya kazi ya kuvuna mpunga.

  11. Waziri Mkuu wa zamani wa Pakistan, Imran Khan apelekwa hospitalini kwa matibabu

    Aliyekuwa Waziri Mkuu wa Pakistan Imran Khan, amewasili katika hospitali moja jijini Islamabad baada ya Mahakama ya Juu kuamuru kuwa aruhusiwe kutoka gerezani kwa ajili ya kufanyiwa uchunguzi wa kimatibabu.

    Kulikuwa na ulinzi mkali wa polisi huko Rawalpindi, ambako Bwana Khan amekuwa akishikiliwa kwa miaka mitatu.

    Hii ndiyo nafuu kubwa zaidi ambayo Khan ameipata kutoka mahakamani tangu afungwe gerezani mwaka wa 2023 kwa tuhuma za ufisadi, ambazo anadai kuwa zilitokana na sababu za kisiasa.

    Mbali na kuhamishiwa hospitalini, agizo hili la mahakama pia liliagiza kuwa Khan aruhusiwe kuonana na familia yake, jambo ambalo hajaliweza kulifanya kwa miezi kadhaa.

    Usiku wa Jumanne, dada yake alimtembelea gerezani. Chama cha kisiasa cha Khan, Tehreek-e-Insaf (PTI), kwa kawaida huwa cha kwanza kudai kuwa maamuzi ya mahakama yanayomkabili yamechochewa na siasa.

    Hata hivyo, chama hicho hakijajihusisha hadharani na dhana kwamba uamuzi wa Mahakama ya Juu unaashiria kuwepo kwa hila za kisiasa nyuma ya pazia.

    Khan alipatikana na hatia katika mashtaka ya ufisadi, ambayo anasema yalichochewa kisiasa.

    Soma pia:

  12. Nchi za Magharibi zalaani mpango wa Israel wa kujenga makazi ya Walowezi Ukingo wa Magharibi

    Mipango ya Israel ya kufungua zabuni za ujenzi wa takriban nyumba 1,200 za walowezi katika eneo lenye umuhimu wa kimkakati katika Ukingo wa Magharibi unaokaliwa kwa mabavu imelaaniwa vikali na mataifa kadhaa ya Magharibi.

    Katika taarifa ya pamoja, Uingereza, Ufaransa, Ujerumani, Italia, na Canada zilitaja uamuzi huo kuwa ''usiokubalika" na kuionya Israel kubatilisha mipango hiyo mara moja.

    Makazi yote ya Walowezi ni haramu chini ya sheria za kimataifa na kutokana na shinikizo la kimataifa,

    Israel ilisitisha kwa miongo kadhaa mipango ya kujenga makazi ya Walowezi katika eneo lijulikanalo E1 upande wa mashariki mwa Jerusalem.

    Washirika wake wengi na Wapalestina walidai kuwa ujenzi huo ungedidimiza kwa kiasi kikubwa matumaini ya kufikiwa suluhisho la mataifa mawili, na kimsingi kuugawanya Ukingo wa Magharibi vipande viwili na kuitenga Jerusalem Mashariki.

    Taarifa hiyo kutoka kwa washirika wa Israel wa Ulaya na Canada iliyochapishwa jana Alhamisi imesema "Wakati huu wa kukosekana kwa utulivu mkubwa katika Ukingo wa Magharibi kukiwa na viwango ambavyo havijawahi kushuhudiwa vya vurugu zinazofanywa na walowezi dhidi ya raia, na vizuizi vikubwa kwa uchumi wa Palestina, uamuzi huo wa kutaka kujenga makazi ya walowezi unatia wasiwasi mkubwa zaidi.

    Katika taarifa tofauti, Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa pia alisema mpango huo unaleta "tishio la uwepo" kwa taifa linaloungana la Palestina. Msemaji wake Stephane Dujarric, amesema Katibu mkuu anatiwa wasiwasi mkubwa na hatua ya Israel.

    "Katibu Mkuu amesikitishwa sana na ripoti za kuwepo makazi mapya haramu ya walowezi wa Israeli katika Ukingo wa Magharibi, ikiwa ni pamoja na zabuni mpya, zikiwemo za eneo la E1. Anatiwa wasiwasi mno na mipango hiyo ya kujengwa makazi eneo la E1, ambayo yatakata kabisa uhusiano kati ya kaskazini na kusini mwa Ukingo wa Magharibi.

    Hali hiyo itakuwa na madhara makubwa kwa uhuru wa kujitawala katika maeneo ya Palestina na kutishia uwezekano wa kuwepo suluhisho la mataifa mawili''.

    Mapema hapo jana, Waziri wa Mambo ya Nje wa Uingereza, Ed Miliband pia alilaani vikali mpango huo wa Israel,mtizamo ambao ulimkera Waziri wa Mambo ya Nje wa Israel.

    Wizara ya nyumba ya Israel siku ya Jumatano wiki hii, ilitoa zabuni kwa ajili ya ujenzi wa nyumba 1,234 kati ya nyumba 3,401 zilizoidhinishwa na serikali ya Israel mnamo Agosti iliyopita. Inachukua takriban kilomita za mraba 12 kati ya Jerusalem Mashariki na makazi ya Maale Adumim.

    Wakati wa kuzinduliwa kwake, Waziri wa Fedha Bezalel Smotrich,mwanasiasa mwenye misimamo mikali na mlowezi,alisema wazo la kuwepo taifa la Palestina linafutwa.

    Mwisho wa kupokea zabuni ni tarehe 19 Oktoba, siku chache tu kabla ya uchaguzi mkuu wa Israel unaotarajiwa kufanyika tarehe 27 Oktoba,hatua inayoonekana kufanya iwe vigumu zaidi kwa serikali yoyote ya baadaye kubatilisha zabuni zilizotolewa.

    Israel imejenga takriban makazi 160 yanayohifadhi Wayahudi laki saba tangu ilipokalia kwa mabavu Ukingo wa Magharibi na Jerusalem Mashariki, ardhi ambayo Wapalestina wanaitaka, pamoja na Gaza, kwa ajili ya taifa la baadaye linalotarajiwa.

    Inakadiriwa kuwa Wapalestina milioni 3.3 wamelazimika kuishi sambamba na Wayahudi hao. Licha ya upinzani mkali wa kimataifa, serikali ya Israel imeruhusu makazi hayo kukua.

    Maelezo zaidi:

  13. Natumai hujambo.