Kizza
Besigye, kiongozi wa upinzani nchini Uganda, amelazwa katika chumba cha
wagonjwa mahututi (ICU) katika mji mkuu Kampala baada ya kuanguka na kupoteza
fahamu wakati wa kusikilizwa kwa kesi yake ya uhaini.
Besigye,
mwenye umri wa miaka 70, amekuwa kizuizini tangu mwezi Novemba 2024.
Wakili
wake mkuu alikamatwa mwezi uliopita na kushtakiwa kwa madai ya kushindwa
kuripoti vitendo vya uhaini na
anazuiliwa na polisi hadi sasa.
Besigye ambaye hali yake ya afya inaonekana
kuwa dhaifu, alikuwa akipinga uamuzi wa mawakili wa serikali kuteuliwa
kumwakilisha mahakamani, kabla ya kuanguka na kupoteza fahamu. Walinzi wa
gereza walimkimbiza hospitalini.
“Bado amepoteza fahamu. Hawezi
kuzungumza, na haitikii hata akidungwa
sindano ili kupima mwitikio wa maumivu,” mkewe, Winnie Byanyima, ambaye
anaongoza shirika la Umoja wa Mataifa linalopambana ugonjwa wa UKIMWI (UNAIDS), amechapisha kwenye mtandao wa X.
Siku ya Jumatano
katika Mahakama Kuu ya Kampala, mashahidi waliokuwa mahakamani walisema Besigye
alipaza sauti mara kadhaa akisema “wacheni” kuhusu suala la uwakilishi wake wa kisheria kabla ya kuanguka.
Besigye
alipelekwa katika
Hospitali ya Taifa ya Rufaa ya Mulago, hospitali kubwa zaidi ya umma nchini
Uganda, lakini alikataa kutibiwa na wahudumu wa afya wa serikali.
Mkewe Byanyima alisema kupitia X kuwa “Hatutaruhusu afisa yeyote wa
serikali kumgusa.”
Mkewe
anataka Besigye aruhusiwe kupata matibabu
kutoka kwa daktari wake binafsi katika kliniki ya kibinafsi, badala ya kutibiwa
katika kituo cha afya cha serikali.
Kitengo
cha ICU ambako Besigye anatibiwa, kimezingirwa na maafisa wa usalama . Ripoti
zinaeleza kuwa dada yake, ambaye pia ni daktari wake binafsi, ameweza kuruhusiwa kumwona.
Wakili
mkuu wa Besigye, Erias Lukwago, yuko gerezani baada ya kukamatwa na jeshi mwezi
uliopita.
Wakili
wake mwingine Martha Karua kutoka
nchini Kenya, alizuiwa kuingia nchini Uganda baada ya kusafiri kwenda huko
mwezi uliopita kumwakilisha Besigye.
Mwanawe
Besigye, Adam Ampa, amemwomba Rais Yoweri Museveni na mwanawe, Jenerali Muhoozi
Kainerugaba, ambaye ni mkuu wa jeshi la Uganda, kuwa na huruma na kumuachilia baba yake kwa misingi
ya kibinadamu.
Besigye,
ambaye amewania urais dhidi ya Rais Yoweri
Museveni mara nne, alitekwa nyara nchini Kenya mwaka wa 2024.