Jeshi la Sudan latuhumiwa kuwaua raia 24 katika shambulio la droni
Takribani watu 24, wengi wao wanawake na watoto, wanaripotiwa kuuawa katika shambulio la ndege isiyo na rubani katika kijiji cha Sharshar katika eneo la West Bara, jimbo la Kordofan Kaskazini, kulingana na shirika la kutetea haki za binadamu la Darfur Victims Advocacy.
Shirika hilo liliwanukuu mashuhuda walioeleza kuwa ndege isiyo na rubani inayohusishwa na Jeshi la Sudan (SAF) ilifanya shambulio hilo mnamo tarehe 29 Julai, ikilenga eneo la Sharshar mwendo wa saa saba unusu kwa saa za Sudan.
Kundi hilo lilisema linawajibisha jeshi kikamilifu kwa uhalifu huo. Muungano wa Sudan Founding Alliance, ambao ni muungano wa kisiasa na kijeshi unaoungwa mkono na kundi la wanamgambo la Rapid Support Forces (RSF), pia lililituhumu jeshi kwa kufanya shambulio hilo, likisema kuwa nyumba za raia na miundombinu zililengwa.
Jeshi la Sudan (SAF) halijatoa tamko lolote kuhusiana na madai hayo.
BBC haijathibitisha madai yaliyotolewa kuhusu shambulio hilo.
Shambulio hilo liliripotiwa siku chache baada ya jeshi na vikosi washirika kutangaza kulomboa mji muhimu wa kimkakati wa Bara kutoka mikononi mwa RSF.
Mji huo, ulioko Kordofan Kaskazini, ni muhimu kutokana na eneo lake katika njia zinazounganisha Sudan ya Kati na eneo la Darfur.
Udhibiti wa Kordofan Kaskazini umekuwa eneo muhimu katika vita vya Sudan, huku pande zote mbili, SAF na RSF, zikigombea ushawishi katika eneo hilo linalounganisha maeneo muhimu.






























