Hii ni tovuti ya maandishi pekee ambayo inatumia data kidogo. Tazama toleo kuu la tovuti likijumuisha picha na video zote.

Bofya kuelekea tovuti kuu

Pata maelezo zaidi kuhusu toleo hili la linalotumia kiasi kidogo cha data

Mahakama kuu ya Umoja wa Mataifa yasema uvamizi wa Israel katika maeneo ya Wapalestina ni kinyume cha sheria

Mahakama hiyo ya Kimataifa ya Haki (ICJ) imesema Israel inapaswa kusimamisha shughuli za makazi katika Ukingo wa Magharibi na Jerusalem Mashariki inayokaliwa na kukomesha uvamizi wake "haramu" wa maeneo hayo na Ukanda wa Gaza haraka iwezekanavyo.

Muhtasari

  • Mahakama kuu ya Umoja wa Mataifa yasema uvamizi wa Israel katika maeneo ya Wapalestina ni kinyume cha sheria
  • Maandamano Kenya: Serikali yafichua mashirika ya Kenya yanayodaiwa kudhaminiwa na Wakfu wa Ford
  • Maandamano Kenya: Kanisa lawaambia vijana ‘wampe muda Ruto’
  • Urusi yamfunga jela mwandishi wa habari wa Marekani makosa ya ujasusi
  • Nitawafukuza wahamiaji kwa namna ambayo haijawahi kutokea katika historia ya Marekani - Trump
  • Zelensky aomba tena ruhusa ya kurusha makombora ya Magharibi ndani ya Urusi
  • Ulaya inapaswa kuwa tayari kwa miaka kumi ya vita katika Ukraine - Katibu mkuu wa Nato
  • Korea Kusini yamteua aliyeiasi Korea Kaskazini kuwa waziri msaidizi
  • Ripoti zataja Crowdstrike kama sababu inayowezekana ya hitilifu inayoshuhudiwa
  • Usafiri wa ndege wasitishwa baada ya hitilifu ya kiteknolojia kuathiri mashirika ya ndege, vyombo vya habari na benki duniani kote
  • Bangladesh yatoa tahadhari ya usalama huku maandamano mabaya yakiongezeka
  • Trump: 'Nitamaliza kila mgogoro wa kimataifa'
  • Hatua za haraka zahitajika kuchukuliwa kwa vimelea vilivyokuwa sugu kwa tiba ya malaria
  • Babake mshambuliaji wa Trump alipigia simu polisi kuhusu mwanawe kabla ya shambulio
  • 'Mungu alikuwa upande wangu' - Trump aelezea jaribio la kumuua anapokubali uteuzi wa chama cha Republican
  • Mwandishi wa habari atakiwa kumfidia Waziri Mkuu wa Italia kwa kufanyia mzaha kimo chake
  • Zelesnky: Ni kibarua 'kigumu' kufanya kazi na Trump lakini sisi ni wachapakazi

Moja kwa moja

Na Asha Juma, Yusuf Jumah, Dinah Gahamanyi & Seif Abdalla

  1. Mwanaume wa Israel auawa katika shambulio la ndege isiyo na rubani huko Tel Aviv

    Mtu mmoja ameuawa na takriban watu wanane kujeruhiwa katika shambulio la ndege isiyo na rubani katikati mwa Tel Aviv, Israel.

    Sehemu ya ghorofa ilishambuliwa na kile afisa wa kijeshi wa Israel alisema kuwa ni ndege ya anga iliyotengenezwa na Iran (UAV), ambayo ilikuwa imefanyiwa marekebisho ili kuruka umbali mrefu.

    Wapiganaji Wahouthi nchini Yemen - zaidi ya maili 1,000 (1,600km) - walisema walifanya shambulio hilo, na kuapa kufanya zaidi.

    Msemaji wa jeshi la Israel Rear Admiral Daniel Hagari alisema uchunguzi wa awali uliashiria shambulio hilo lilianzia Yemen.

    Iwapo wapiganaji wa Houthi watahusika, itaashiria ongezeko kubwa la mashambulizi yao dhidi ya Israel ambayo yalianza baada ya mashambulizi ya kijeshi ya Israel huko Gaza, ambayo yalichochewa na shambulio la Hamas dhidi ya Israel tarehe 7 Oktoba.

    Hadi sasa, karibu makombora yote ya Houthi na ndege zisizo na rubani zilizorushwa kuelekea Israel zimenaswa. Hakuna kombora linalojulikana anayejulikana kufika Tel Aviv.

    Afisa huyo wa jeshi la Israel alisema vikosi vyake vya ulinzi vimegundua ndege hiyo isiyo na rubani iliyokuwa ikiingia lakini hawakujaribu kuitungua kwa sababu ya "makosa ya kibinadamu".

  2. Na mpaka hapo ndio tunafikia mwisho wa matangazo yetu ya moja kwa moja kwa leo tukutane tena hapo kesho.

  3. Mahakama kuu ya Umoja wa Mataifa yasema uvamizi wa Israel katika maeneo ya Wapalestina ni kinyume cha sheria

    Mahakama ya juu ya Umoja wa Mataifa imesema uvamizi wa Israel katika maeneo ya Wapalestina ni kinyume cha sheria za kimataifa.

    Mahakama hiyo ya Kimataifa ya Haki (ICJ) imesema Israel inapaswa kusimamisha shughuli za makazi katika Ukingo wa Magharibi na Jerusalem Mashariki inayokaliwa na kukomesha uvamizi wake "haramu" wa maeneo hayo na Ukanda wa Gaza haraka iwezekanavyo.

    Agizo hilo la ushauri la mahakama sio la lazima kisheria lakini bado lina uzito mkubwa wa kisiasa. Ni mara ya kwanza kwa ICJ kutoa msimamo wake kuhusu uhalali wa kisheria wa ujenzi wa makazi hayo uliodumu kwa miaka 57.

    Mahakama ya ICJ yenye makao yake makuu The Hague nchini Uholanzi, imekuwa ikichunguza suala hilo tangu mwanzoni mwa mwaka jana, kwa ombi la Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa.

    Unaweza pia kusoma:

  4. Maandamano Kenya: Serikali yafichua mashirika ya Kenya yanayodaiwa kudhaminiwa na Wakfu wa Ford

    Serikali ya Kenya imeliandikia rasmi shirika la Ford Foundation ikieleza wasiwasi mkubwa kuhusu shughuli za hivi majuzi za ufadhili za shirika hilo la Marekani nchini humo.

    Katika barua iliyotumwa kwa Bw. Darren Walker, Rais wa Wakfu wa Ford, serikali ya Kenya, kupitia katibu wa kudumu wa masuala ya kigeni Korir Sing'Oei , inasema kwamba baadhi ya wafadhili wa taasisi hiyo wanaweza kuchochea maandamano yanayoendelea nchini.

    Aidha iliwashutumu baadhi ya mashirika hayo kwa kujihusisha katika shughuli zinazokiuka sheria za Kenya, ikiwa ni pamoja na uchochezi, matamshi ya chuki, na uhamasishaji kwa kutumia taarifa potofu, ambazo zinaweza kukiuka Sera ya ya Wakfu wa Ford.

    "Ingawa tunatambua umuhimu wa kudumisha nafasi ya wazi ya kiraia na heshima kwa kanuni za serikali iliyo wazi ambayo sisi sote tunashiriki, vitendo vya baadhi ya mashirika munayofadhili nchini vinakiuka sheria za Kenya, ikiwa ni pamoja na kupiga marufuku uchochezi, matamshi ya chuki, uasi na uhamasishaji kwa kutumia taarifa potofu.

    "Matendo yao pia yanapingana na Sera ya Wakfu ya Ford ya kuuliza swali kiwapo Wakfu wako umeachana na sera hii na sasa una nia ya kuathiri vibaya michakato ya kisiasa na sera ndani ya Jamhuri ya Kenya," barua hiyo inaongeza.

  5. Maandamano Kenya: Kanisa lawaambia vijana ‘wampe muda Ruto’

    Kanisa la Kianglikana nchini Kenya (ACK) limewataka vijana wa Kenya wanaopinga serikali kusitisha mara moja maandamano na kumpa Rais William Ruto muda wa kushughulikia malalamishi yao.

    Wakiongozwa na Askofu Mkuu wa kanisa hilo Joseph Ole Sapit, makasisi waliwapongeza waandamanaji, kutokana na athari kubwa ya maandamano yaokwa utawala wa Kenya Kwanza, ikiwa ni pamoja na kutimuliwa kwa Baraza la Mawaziri na baadaye kubadilishwa kwa aliyekuwa Inspekta Jenerali wa Polisi Japhet Koome.

    Askofu Mkuu, hata hivyo, amesema kuwa Ruto anahitaji muda zaidi kushughulikia malalamishi ya ziada yaliyotolewa wakati wa maandamano.

  6. Urusi yamfunga jela mwandishi wa habari wa Marekani makosa ya ujasusi

    Mwandishi wa habari wa Marekani Evan Gershkovich amehukumiwa na mahakama ya Urusi kifungo cha miaka 16 katika gereza lenye ulinzi mkali kwa makosa ya ujasusi, baada ya kesi ya siri iliyokanushwa kuwa "uzushi" na mwajiri wake.

    Mwandihi huyo wa Wall Street Journal (WSJ) alikamatwa kwa mara ya kwanza Machi mwaka jana akiwa katika safari ya kuripoti katika jiji la Yekaterinburg, takriban kilomita 1,600 (maili 1,000) mashariki mwa Moscow, na vyombo vya usalama.

    Waendesha mashtaka wamemshutumu kwa kufanyia kazi na Shirika la Ujasusi (CIA), shutuma ambazo Bw Gershkovich, WSJ na Marekani wamezikanusha vikali.

    Hii ni mara ya kwanza kuhukumiwa kwa mwandishi wa habari wa Marekani kwa ujasusi nchini Urusi tangu Vita Baridi kumalizika zaidi ya miaka 30 iliyopita.

  7. Nitawafukuza wahamiaji kwa namna ambayo haijawahi kutokea katika historia ya Marekani - Trump

    Rais wa zamani wa Marekani, Donald Trump amesema iwapo atakuwa rais tena, atawafukuza wageni kwa namna ambayo hakijawahi kushuhudiwa katika historia ya nchi hiyo.

    Trump aliyasema hayo wakati akitoa hotuba ya kuthibitisha nia ya chama chake cha Republican katika uchaguzi wa urais mwezi Novemba, katika mkutano wa chama hicho ulioingia siku ya nne na ya mwisho mjini Milwaukee.

    Rais huyo wa zamani aliahidi kupunguza mfumuko wa bei na kukomesha uingiaji wa wahamiaji nchini, ambapo aliahidi kukamilisha ukuta aliouanzisha utakaotenganisha Marekani na Mexico, ambako wahamiaji mara nyingi huingilia.

    Alisema atakomesha uhamiaji mara moja siku ya kwanza kwa kufunga mpaka.

    Donald Trump, ambaye alitumia zaidi ya saa moja kuwasilisha hotuba yake, ambayo ilizungumzwa zaidi badala ya hotuba iliyoandikwa.

    Unaweza pia kusoma

  8. Zelensky aomba tena ruhusa ya kurusha makombora ya Magharibi ndani ya Urusi

    Katika mkutano na Waziri Mkuu wa Uingereza Keir Starmer na baraza lake la mawaziri, Rais wa Ukraine Vladimir Zelensky kwa mara nyingine tena, ametoa wito kwa washirika kuiruhusu Ukraine kurusha silaha za Magharibi katika ardhi ya Urusi.

    "Muhimu kwa hili ni silaha za masafa marefu. Tafadhali washawishi washirika wetu wengine kuondoa vizuizi, "Zelensky alimueleza Bw Starmer, akimaanisha kuruhusu mashambulizi ya kulipiza kisasi kwa silaha za Magharibi kwenye eneo linalotambuliwa la Urusi bila vizuizi.

    Alipopokelewa na mwenyeji wake katika makazi ya Waziri mkuu wa Uingereza katika 10 Downing Street, Rais wa Ukraine Vladimir Zelensky aliishukuru Uingereza kwa msaada na mshikamano wake na Ukraine.

    “Asante kwa mwaliko na kunipa heshima ya kuwa hapa. Asante kwa umoja huu. Tunahisi msaada huu, na maamuzi yako mazito yalisaidia kulinda uhuru na demokrasia nchini Ukraine na kuwasaidia sana watu wa Ukraine’’ , amesema na kuongeza kuwa "Pia nataka kujadili na wewe leo maamuzi mazito ambayo yanaweza kutusaidia katika vita hivi," Zelensky aliongeza.

    Rais wa Ukraine amekuwa mgeni wa kwanza wa kigeni katika Downing Street tangu Starmer achaguliwe kama waziri mkuu mpya. Zelensky anatarajiwa kuhutubia mkutano usio wa kawaida wa serikali ya Uingereza.

    Vita vya Ukraine - soma zaidi:

  9. Ulaya inapaswa kuwa tayari kwa miaka kumi ya vita katika Ukraine - Katibu mkuu wa Nato

    Katibu Mkuu wa muungano wa nchi za magharibi NATO anayemaliza muda wake Jens Stoltenberg, amesea Ulaya na NATO zinatakiwa kujiandaa tayari kwa ajili ya vita vya Ukraine kwa miaka kumi .

    Anasema kadiri washirika wa Magharibi wanavyodhihirisha kwa uthabiti zaidi utayari kwa vita virefu, ndivyo vinavyoweza kumalizika kwa haraka

    Alipoulizwa katika mahojiano na BBC ikiwa nchi za NATO zinapaswa kuwa tayari kwa vita vya Ukraine kwa zaidi ya miaka kumi, Stoltenberg alijibu: "Ndiyo."

    “Lakini jambo kuu hapa ni kwamba kadiri tunavyoiunga mkono Ukraine na kadri tunavyokuwa tayari kuiunga mkono, ndivyo vita inavyoweza kuisha kwa haraka.

    Kitendawili ni kwamba Rais Putin sasa anaamini kwamba anaweza kuketi nasi. Ndio maana vita vinaendelea," Jens Stoltenberg alisema.

    "Na tunapoonyesha wazi kwamba tuko hapa kwa muda mrefu, kwamba tumejitolea kuisaidia Ukraine kwa muda mrefu, basi tunaweka mazingira ya utatuzi wa mzozo ambapo Ukraine itaweza kujitawala kama nchi huru, ” Katibu Mkuu wa NATO aliendelea.

    Jens Stoltenberg amehudumu kama Katibu Mkuu wa NATO kwa miaka 10 na atajiuzulu wadhifa huu Oktoba mwaka huu. Nafasi yake itachukuliwa na Waziri Mkuu wa zamani wa Uholanzi Mark Rutte.

    Vita vya Ukraine -soma zaidi:

  10. Korea Kusini yamteua aliyeiasi Korea Kaskazini kuwa waziri msaidizi

    Mwanadiplomasia wa zamani wa Korea Kaskazini Tae Yong-ho ameteuliwa kuwa kiongozi mpya wa baraza la ushauri la rais wa Korea Kusini kuhusu muungano.

    Hili linamfanya kuwa mtu wa kwanza aliyeiasinchini yake kushika nafasi ya cheo cha juu zaidi kati ya maelfu ambao wamehamia Kusini - na wa kwanza kupewa kazi katika ofisi ya makamu wa waziri.

    Tae, 62, alikuwa naibu balozi wa Pyongyang nchini Uingereza kabla ya kukimbilia Korea Kusini mwaka wa 2016.

    Pyongyang imemshutumu kama "mtu muovu" na aliyehusika kwenye ubadhirifu wa fedha za serikali na uhalifu mwingine.

    Bw Tae amekuwa Mkorea wa Kaskazini wa kwanza kushinda kiti katika Bunge la Kitaifa la Korea Kusini 2020.

    Alishindwa kupata muhula wa pili katika uchaguzi wa bunge mwezi Aprili, lakini katika jukumu lake jipya, atakuwa akiishauri ofisi ya Rais wa Korea Kusini Yoon Suk Yeol kuhusu muungano wa amani wa Korea.

    "Yeye ndiye mtu anayefaa kusaidia kuanzisha sera ya umoja ya amani kwa msingi wa demokrasi yenye uhuru na kupata uungwaji mkono kutoka ndani na nje ya nchi," ofisi ya rais ilisema siku ya Alhamisi.

    Alizaliwa Pyongyang mwaka wa 1962, Bw Tae aliingia katika utumishi wa masuala ya nchi za kigeni akiwa na umri wa miaka 27 na alitumia karibu miaka 30 kufanya kazi chini ya vizazi vitatu vya utawala wa Kim.

    Pia unaweza kusoma:

  11. Ripoti zataja Crowdstrike kama sababu inayowezekana ya hitilifu inayoshuhudiwa

    Kumekuwa na ripoti zinazopendekeza kwamba kampuni ya usalama wa mtandao iitwayo Crowdstrike, ambayo hutengeneza programu ya kuzuia virusi, ilitoa sasisho la programu ambalo limeenda vibaya sana na linavuruga kompyuta za Windows - na kusababisha kinachojulikana kama "skrini ya bluu ya kifo" kwenye Kompyuta.

    Sasa, kama masuala haya mawili ni kitu kimoja, au kama ni dhoruba kamili ya mambo mawili makubwa yanayotokea kwa wakati mmoja -bado haijulikani Hakika inaonekana kama itasababisha uharibifu mkubwa.

    Tumewasiliana na Crowdstrike ili kupata jibu lakini bado hatujajibiwa.

    Na Zoe KleinmanMhariri wa Teknolojia

  12. Habari za hivi punde, Usafiri wa ndege wasitishwa baada ya hitilifu ya kiteknolojia kuathiri mashirika ya ndege, vyombo vya habari na benki duniani kote

    Benki kuu, vyombo vya habari na mashirika ya ndege kwa sasa yanakabiliwa na hitilafu kubwa za IT.

    Safari za ndege zimesimamishwa katika uwanja wa ndege wa Sydney, United Airlines imeacha kupaa angani , na jukwaa soko la hisa la London Stock Exchange linakabiliwa na hitilafu .

    Hitilafu ya IT : Nini kinatokea?

    • Ripoti za kukatika kwa IT zinakuja kutoka kote ulimwenguni
    • Mashirika ya ndege, mashirika ya utangazaji na benki zimeathirika - ikiwa ni pamoja na Sky News nchini Uingereza, ambayo haipo hewani
    • Viwanja vingi vya ndege nchini Uingereza na duniani kote vinaripoti kuchelewa, na baadhi ya safari za ndege zimesitishwa
    • Nchini Marekani, mashirika makubwa ya ndege yakiwemo United na Delta yamesimamisha safari za ndege
    • Nchini Australia, viwanja vya ndege, maduka na mawasiliano vimeathirika, Mratibu wa Kitaifa wa Usalama wa Mtandao wa Australia akielezea kama "kukatika kwa huduma za kiufundi kwa kiasi kikubwa"
    • Kampuni za reli nchini Uingereza zinaripoti ucheleweshaji
    • Microsoft inasema inaendelea kukabiliana na "athari zinazoendelea" za kukatika kwa huduma za kiteknolojia
  13. Bangladesh yatoa tahadhari ya usalama huku maandamano mabaya yakiongezeka

    Tahadhari ya Usalama wa Hali ya Juu imetolewa kwa kote nchini Bangladesh, huku ghasia mbaya kati ya wanafunzi na polisi yakiendelea.

    Mji mkuu wa Dhaka unakumbwa na ukosefu wa mtandao na laini za simu pia hazifanyikazi.

    Siku ya Alhamisi jioni, maelfu ya waandamanaji walivamia kituo cha utangazaji cha serikali BTV, na kuharibu samani, kuvunja madirisha na taa na kuchoma moto baadhi ya jengo hilo la utangazaji.

    Waziri wa habari wa Bangladesh aliambia BBC kuwa matangazo yamesitishwa na wafanyikazi wengi walikuwa wameondoka kwenye jengo hilo lililopo mji mkuu.

    Ujumbe kwenye ukurasa rasmi wa mtandao wa Facebook wa BTV awali ulikuwa umesema "wengi" walikuwa wamekwama ndani ya jengo hilo, na kuomba msaada kutoka kwa zima moto ili kuzima moto huo.

    Mwandishi wa habari mkuu wa BTV ambaye hakutaka jina lake litajwe, aliambia BBC: "Hali ilikuwa mbaya sana hatukuwa na chaguo jingine ila kuondoka mahali hapo. Baadhi ya wenzetu walikuwa wamekwama ndani ya jengo. Sijui nini kilichowatokea."

    Pia unaweza kusoma:

  14. Trump: 'Nitamaliza kila mgogoro wa kimataifa'

    Donald Trump amehutubia hadhira katika mkutano wa Kitaifa wa chama cha Republican akikubali kupeperusha bendera ya chama hicho kwenye kinyang’anyiro cha kuingia Ikulu.

    "Ni wakati wa mabadiliko," rais huyo wa zamani wa Marekani aliambia mkutano huo kabla ya kuzindua mfululizo wa ahadi kwa watu wa Marekani.

    Trump aliahidi kupunguza mfumuko wa bei, kumaliza uhamiaji haramu na kukomesha vita ambavyo anasema havingetokea kama angekuwa Ikulu.

    Trump awasifu 'wazalendo' wa kihistoria

    Alirejelea vita kuu vya historia ya Marekani, na kupendekeza vinawakilisha umoja kwa nchi.

    “Njia yetu ya maisha ilipotishwa, wazalendo Wamarekani waliandamana hadi vitani, wakikimbilia katika ngome za adui, na kutazama kifo kwa macho ili kudumisha uhuru…," Trump alisema.

    "Kama mababu zetu, ni lazima sasa tuje pamoja, tutupilie mbali tofauti zetu na mizozo ya siku za nyuma, na kusonga mbele kwa umoja, kama watu wamoja, na taifa moja," aliongeza.

    Trump amalizia hotuba yake kwa kugusia ‘Marekani iliyosahaulika’

    Chama cha Republican ambacho kinaelezea misimamo ya sera za chama, huanza na kujitolea kwa "Wamarekani waliosahaulika".

    Na Trump alipomaliza hotuba yake, aliunga mkono kujitolea kwa hilo.

    "Kwa wanaume na wanawake wote waliosahaulika ambao wamepuuzwa, kutelekezwa, na kuachwa nyuma, hamtasahaulika tena," alisema.

    Soma zaidi:

  15. Hatua za haraka zahitajika kuchukuliwa kwa vimelea vilivyokuwa sugu kwa tiba ya malaria

    Mamilioni ya maisha ya watu yako hatarini isipokuwa labda hatua za haraka na kali zichukuliwe kukomesha ugonjwa wa malaria sugu barani Afrika, wanasayansi wanaonya.

    Viwango vya dawa kutofanyakazi sasa vimeongezeka katika baadhi ya maeneo kutoka chini ya 1% hadi zaidi ya 20% katika muda wa miaka mitatu.

    Dawa kutofanyakazi mara ya mwisho dhidi ya malaria barani Afrika kulisababisha kuongezeka mara tatu kwa idadi ya watoto wanaofariki dunia.

    Wanasayansi 28 wanaoongoza katika utafiti wa kukabiliana na malaria kutoka nchi 10 wametoa mwito wa hatua kuchukuliwa katika jarida la Sayansi.

    Artemisinin huua vimelea vya malaria na ndio msingi wa matibabu.

    Vimelea vinavyoweza kuwa sugu kwa dawa zenye artemisinin viliibuka kwa mara ya kwanza barani Afrika nchini Rwanda, na kisha nchini Uganda na Eritrea.

    Vimelea hawa sugu wameenea ndani ya nchi zao na kuvuka mipaka.

    Sasa, zaidi ya 10% ya maambukizi ya malaria husababishwa na vimelea sugu nchini Ethiopia, Eritrea, Rwanda, Uganda na Tanzania.

    "Sasa ni wakati wa kuchukua hatua kabla ya mamilioni ya watu kufariki dunia kwa sababu ya tiba za malaria zisizo na ufanisi," alisema Prof Olugbenga Mokuolu, kutoka idara ya watoto katika Chuo Kikuu cha Ilorin nchini Nigeria.

    Mnamo 2016, aina sugu ya vilemea vilikugunduliwa kaskazini mwa Uganda. Kufikia 2019, zaidi ya 20% ya vimelea vilivyojaribiwa vilikuwa sugu katika mikoa kadhaa.

    Soma zaidi:

  16. Babake mshambuliaji wa Trump alipigia simu polisi kuhusu mwanawe kabla ya shambulio

    Baba yake mshambuliaji aliyejaribu kumuua Donald Trump alipiga simu polisi kabla ya shambulizi la Jumamosi kwa sababu alikuwa na wasiwasi kuhusu mtoto wake, kulingana na ripoti za vyombo vya habari.

    Simu hiyo ni mojawapo ya vilivyofichuliwa kusababisha wasiwasi katika siku za hivi majuzi vilivyoripotiwa kwa vyombo vya sheria kabla ya milio ya risasi kusikika katika mkutano wa Trump wa Pennsylvania Jumamosi.

    Utekelezaji wa sheria - haswa Huduma Maalum ya Usalama Marekani - imekabiliwa na maswali mengi kuhusu usalama huku baadhi ya wabunge wakitoa wito mkuu wa shirika hilo kujiuzulu.

    Babake Matthew Crooks alipiga simu polisi kwa sababu alikuwa na wasiwasi kuhusu mtoto wake mahali alipo, chanzo cha sheria kiliambia mshirika wa BBC, CBS. Haijulikani ni lini simu hiyo ilipigwa lakini ilikuwa kabla ya tukio la Trump kupigwa risasi.

    Fox News iliripoti kwamba wazazi wa Crooks, Mary na Matthew, waliwaambia maafisa kuwa "walikuwa na wasiwasi" kuhusu mtoto wao na kwamba aliondoka nyumbani bila kujulikana alipokwenda.

    Wazazi wake wote wanatoa ushirikiana katika uchunguzi, FBI imesema.

    Vyanzo vya utekelezaji wa sheria vimeviambia vyombo vya habari vya Marekani kwamba mtu huyo aliyekuwa na silaha alikuwa amefanya uchunguzi mtandaoni kuhusu tatizo kubwa la mfadhaiko na Kongamano la Kitaifa la chama cha Democratic lililopangwa kufanyika Agosti.

    Pia alikuwa amehifadhi picha za Trump, Rais Joe Biden, Mwanasheria Mkuu Merrick Garland, Mkurugenzi wa FBI Chris Wray na mmoja wa Familia ya Kifalme ya Uingereza, kulingana na ripoti kutoka Washington Post na Associated Press.

    Wachunguzi bado wanajaribu kufuatilia chanzo cha kijana huyo mwenye umri wa miaka 20, ambaye aliuawa kwa kupigwa risasi na mwanajeshi mlengaji shabaha baada ya kufyatua risasi.

    Shambulio lake lilisababisha kifo cha mwanachama wa Republican mmoja na wengine kadhaa kujeruhiwa.

    Uchunguzi wa awali umegundua kuwa Crooks alipanda juu ya paa la jengo la karibu nje ya mkutano huo kwenye eneo lenye viyoyozi, afisa ambaye hakutajwa jina aliiambia CBS.

    Soma zaidi:

  17. 'Mungu alikuwa upande wangu' - Trump aelezea jaribio la kumuua anapokubali uteuzi wa chama cha Republican

    "Kulikuwa na damu iliyomwagika kila mahali, na hata hivyo, kwa namna fulani nilijisikia salama sana, kwa sababu nilikuwa na Mungu upande wangu," Trump anasema, wakati anaendelea kuelezea kilichotokea wakati wa shambulio dhidi yake.

    "Kama singesogeza kichwa changu mara ya mwisho, risasi ya muuaji ingefikia lengo lake , na nisingekuwa nanyi usiku wa leo."

    "Sitakiwi kuwa hapa usiku wa leo," anasema. “Nasimama mbele yenu katika uwanja huu tu kwa neema ya Mwenyezi Mungu. Watu wengi wanasema ilikuwa wakati mzuri."

    Tumesikia baadhi ya marejeleo ya kuingilia kati kwa Mungu katika kongamano la wiki hii wakati wazungumzaji wamekuwa wakijadili jaribio la kumuua rais huyo wa zamani , na Trump anagusia mada hiyo tena

    Unaweza pia kusoma

  18. Mwandishi wa habari atakiwa kumfidia Waziri Mkuu wa Italia kwa kufanyia mzaha kimo chake

    Mwanahabari wa Italia ameagizwa kumlipa Waziri Mkuu Giorgia Meloni fidia ya €5,000 (£4,210) kutokana na machapisho ya mitandao ya kijamii yanayodhihaki urefu wake.

    Jaji aliamua kwamba jumbe mbili za Giulia Cortese katika mtandao wa kijamii wa X ambaye pia alipewa faini atakayolipa baadaye ya €1,200, zilikuwa za kumchafulia jina Waziri mkuu na zilidhamiria ‘kumuaibisha’ kwa sababu ya mwili wake.

    Ilifuatia mazungumzo ambayo Bi Cortese alimtaja Bi Meloni kama "mwanamke mdogo" na kumwambia: "Siwezi hata kukuona."

    Akijibu uamuzi huo, Bi Cortese alisema serikali ya Italia ina "tatizo kubwa la uhuru wa kujieleza na upinzani wa waandishi wa habari".

    Wawili hao waligombana kwa mara ya kwanza mnamo Oktoba 2021, wakati chama cha Bibi Meloni cha Mrengo wa kulia cha Brothers of Italy kilikuwa bado katika upinzani, baada ya Bi Cortese kuchapisha picha ya dhihaka ya Bi Meloni kwenye X, ambayo zamani ilikuwa Twitter.

    Bi Meloni alionekana kwenye picha akiwa amesimama mbele ya rafu ya vitabu ambapo picha ya dikteta wa kifashisti Benito Mussolini ilikuwa imeongezwa kwa njia ya bandia.

    Katika chapisho kwenye Facebook , Bi Meloni alisema picha hiyo ilikuwa ya "dhamira mbaya" na kwamba atachukua hatua za kisheria.

    Baadaye siku hiyo hiyo, Bw Cortese alisema kuwa alikuwa ameifuta picha hiyo baada ya kugundua kuwa ilikuwa ya uwongo.

    Baadaye alisema katika chapisho tofauti : "Hunitishi, Giorgia Meloni. Baada ya yote, una urefu wa 1.2m [3ft 9in] tu. Siwezi hata kukuona."

    Urefu wa Bi Meloni unaripotiwa katika vyombo vya habari vya Italia kuwa 1.63m (5ft 3in).

  19. Zelensky: Ni kibarua 'kigumu' kufanya kazi na Trump lakini sisi ni wachapakazi

    Rais wa Ukraine Volodymyr Zelensky amesema kufanya kazi na Donald Trump iwapo atachaguliwa tena kuwa rais wa Marekani itakuwa "kibarua kigumu, lakini sisi pia ni wachapakazi".

    Katika mahojiano ya kipekee na BBC mjini London, Bw Zelensky alisema yuko tayari kufanya kazi na yeyote aliye madarakani nchini Marekani.

    Siku chache zilizopita, Trump alimtangaza Seneta wa Ohio JD Vance kama mgombea mwenza wake katika uchaguzi wa Novemba. Vance mwenye umri wa miaka 39 hapo awali alisema kwa njia moja au nyingine "hajali kinachotokea Ukraine".

    Uteuzi huo umeibua upya hofu kwamba ahadi ya Marekani kwa Ukraine inaweza isitimie iwapo Trump atarejeshwa Ikulu katika uchaguzi wa Novemba.

    "Labda haelewi kinachoendelea Ukraine, hivyo basi inabidi tushirikiane na Marekani," Bw Zelensky aliambia BBC.

    Kiongozi huyo wa Ukraine yuko nchini Uingereza kuhudhuria mkutano wa Jumuiya ya Kisiasa ya Ulaya (EPC), ambapo alitoa hotuba yake Alhamisi mchana.

    EPC, ambayo inajumuisha wanachama 27 wa Umoja wa Ulaya pamoja na wasio wanachama 20 kama Uingereza, ni jukwaa la ushirikiano usio rasmi.

    Bw Zelensky hapo awali alikutana na Waziri Mkuu wa Uingereza Keir Starmer, ambaye ameapa kusimama na Ukraine kwa "muda wote ambao tutahitajika kufanya hivyo "na amejitolea kutumia £3bn kama msaada kwa nchi hiyo.

    Alisema anatumai muda wa Bw Starmer ungeashiria enzi "maalum" katika sera za kigeni za Uingereza.

    "Sidhani msimamo wa Uingereza ungebadilika," Bw Zelensky aliambia BBC. "Lakini ningependa Waziri Mkuu Starmer awe wa kipekee - akizungumza kuhusu siasa za kimataifa, kulinda usalama wa dunia, na vita vya Ukraine."

    Aliongeza kuwa Ukraine "haihitaji tu ukurasa mpya, tunahitaji nguvu kubadilisha simulizi hili".

    Soma zaidi:

  20. Hujambo na karibu katika matangazo yetu mubashara ikiwa ni tarehe 19/7/2024