Mwanaume wa Israel auawa katika shambulio la ndege isiyo na rubani huko Tel Aviv

Chanzo cha picha, Reuters
Mtu mmoja ameuawa na takriban watu wanane kujeruhiwa katika shambulio la ndege isiyo na rubani katikati mwa Tel Aviv, Israel.
Sehemu ya ghorofa ilishambuliwa na kile afisa wa kijeshi wa Israel alisema kuwa ni ndege ya anga iliyotengenezwa na Iran (UAV), ambayo ilikuwa imefanyiwa marekebisho ili kuruka umbali mrefu.
Wapiganaji Wahouthi nchini Yemen - zaidi ya maili 1,000 (1,600km) - walisema walifanya shambulio hilo, na kuapa kufanya zaidi.
Msemaji wa jeshi la Israel Rear Admiral Daniel Hagari alisema uchunguzi wa awali uliashiria shambulio hilo lilianzia Yemen.
Iwapo wapiganaji wa Houthi watahusika, itaashiria ongezeko kubwa la mashambulizi yao dhidi ya Israel ambayo yalianza baada ya mashambulizi ya kijeshi ya Israel huko Gaza, ambayo yalichochewa na shambulio la Hamas dhidi ya Israel tarehe 7 Oktoba.
Hadi sasa, karibu makombora yote ya Houthi na ndege zisizo na rubani zilizorushwa kuelekea Israel zimenaswa. Hakuna kombora linalojulikana anayejulikana kufika Tel Aviv.
Afisa huyo wa jeshi la Israel alisema vikosi vyake vya ulinzi vimegundua ndege hiyo isiyo na rubani iliyokuwa ikiingia lakini hawakujaribu kuitungua kwa sababu ya "makosa ya kibinadamu".
















