Hii ni tovuti ya maandishi pekee ambayo inatumia data kidogo. Tazama toleo kuu la tovuti likijumuisha picha na video zote.
Pata maelezo zaidi kuhusu toleo hili la linalotumia kiasi kidogo cha data
Mahakama ya Kenya yaondoa marufuku ya polisi kuhusu maandamano
Mahakama ya Kenya imesitisha hatua ya polisi kupiga marufuku maandamano katika mji mkuu, Nairobi, na maeneo jirani "hadi taarifa zaidi" [itakapotolewa].
Muhtasari
- Serikali ya Kenya yatahadharisha kuhusu dawa gushi za kisukari baada tahadhari ya Interpol
- Mwana mfalme wa Saudia azungumza na rais wa Urusi
- Namibia yakataa kumuongezea muda wa visa mfalme wa Uganda
- Maelfu ya mayai ya ndege adimu yenye thamani ya $500,000 yanaswa Australia
- Kasisi wa Ufaransa ashtakiwa kwa unyanyasaji wa kijinsia miaka 17 baada ya kifo chake
- JD Vance: Mgombea mwenza wa Trump aapa kuwapigania Wamarekani 'waliosahaulika'
- Ujerumani inapanga kupunguza nusu ya msaada wa kijeshi kwa Ukraine
- Binti mfalme wa Dubai atangaza kumtalaki mume wake kupitia Instagram
- Mshambuliaji wa Trump alionekana kama tishio kabla ya kufyatua risasi lakini alipotea kwenye umati
- Makubaliano ya kusitisha mapigano yarefushwa DR Congo
- Biden akutwa na virusi vya Covid - Ikulu
- Polisi yapiga marufuku maandamano katikati mwa Nairobi
Moja kwa moja
Asha Juma & Dinah Gahamanyi & Seif Abdalla
Mahakama ya Kenya yaondoa marufuku ya polisi kuhusu maandamano
Mahakama ya Kenya imesitisha hatua ya polisi kupiga marufuku maandamano katika mji mkuu, Nairobi, na maeneo jirani "hadi taarifa zaidi" [itakapotolewa].
Mnamo Jumatano polisi ilitoa agizo hilo likielezea hali ya maandamano hayo kutokuwa na kiongozi ambayo imefanya kuwa vigumu kwa maafisa wa usalama kulinda salama, na kuongeza kuwa maandamano "yameingiliwa na wahalifu".
Hii ni baada ya mwezi mmoja wa maandamano dhidi ya serikali ambapo watu wengi wameuawa.
Maandamano zaidi yalikuwa yamepangwa kufanyika Alhamisi katika jiji hilo lakini hayakufanyika.
Katikati ya jiji la Nairobi kumekuwa kitovu cha maandamano yanayoongozwa na vijana, ambayo pia yamefanyika kote nchini.
Maandamano hayo yalianza kwa lengo la kupinga nyongeza ya ushuru lakini baada ya kuondolewa kwa nyongeza hiyo yameonekana kupanuka zaidi na kujumuisha matakwa ya kumtaka Rais William Ruto ajiuzulu.
Soma zaidi:
Aubameyang ajiunga na klabu ya Al Qadsiah nchini Saudia
Klabu mpya iliyopandishwa daraja katika ligi ya Saudi ya Pro League, Al Qadsiah imemsajili mshambuliaji wa Marseille Pierre Emerick Aubameyang kwa mkataba wa miaka miwili.
Mshambuliaji huyo wa Gabon mwenye umri wa miaka 35 aliichezea timu hiyo ya Ufaransa msimu mmoja akifungia mabao 30 katika mechi 51.
Aubameyang alijiunga na Marseille baada ya kuhangaika Chelsea, ambapo alifunga mabao matatu pekee katika mechi 21 baada ya kuhama kutoka Barcelona.
Anamfuata beki wa zamani wa Real Madrid Nacho katika klabu ya Al Qadsiah msimu huu wa joto, ambao walimaliza kileleni mwa Ligi ya Daraja la Kwanza la Saudi msimu uliopita na kupandishwa daraja hadi ligi kuu ya Saudia.
Aubameyang anajiunga na wachezaji kadhaa wa hadhi ya juu wanaocheza Saudi Arabia, ambao ni pamoja na fowadi wa Brazil Neymar na mshindi wa tuzo ya Ballon d'Or Karim Benzema na Cristiano Ronaldo.
Ikulu ya Kenya yatahadharisha kuhusu kukwama kwa shughuli zake
Ikulu ya Kenya inaonya kwamba shughuli zake zinaweza kusitishwa baada ya kupunguzwa kwa bajeti kwa sababu ya kukataliwa kwa Mswada wa Fedha wa 2024/2025.
Kulingana na msimamizi wa Ikulu, Katoo Ole Metito, bajeti ya Ikulu imepunguzwa kwa 54%, kutoka Shilingi za Kenya bilioni 9.496 bilioni hadi Ksh.4.382 bilioni, kiasi ambacho kitakuwa na athari kubwa katika uendeshaji wa shughuli za Ikulu.
Akizungumza mbele ya Kamati ya Utawala na Usalama wa Ndani, siku ya Alhamisi, Bw. Katoo aliisihi kamati hiyo kufikiria upya kupunguzwa kwa kiasi hicho kikubwa cha fedha.
Wafanyakazi katika Ofisi ya Mke wa Rais na washauri wake ndio watakaoathirika zaidi, kwani shilingi milioni 547 zilizokuwa zimetengwa kwa ajili ya mishahara yao zimepunguzwa kufuatia tamko la rais kwamba ofisi hiyo imeondolewa.
Serikali ya Kenya yatoa tahadhari kuhusu dawa gushi za kisukari baada tahadhari ya Interpol
Bodi ya Famasia na Sumu nchini Kenya (PPB) imeelezea wasi wasi wake kuhusu kalamu gushi za Ozempic ambazo hutumiwa kuingiza dawa mwilini kwa watu wazima walio na kisukari cha aina ya 2.
Katika taarifa iliyotolewa Alhamisi, Mkurugenzi mtendaji wa PPB Dk. Fred Siyoi amewatahadharisha Wakenya kufuatia tahadhari ya polisi ya kimataifa (Interpol) kuhusiana na matumizi ya chupa gushi za Ozempic.
Kulingana na Interpol, kalamu za Apidra Solostar, ambazo hutumiwa kutibu kisukari cha aina ya 1 na 2, zinawekewa lebo gushi za chupa za Ozempic katika masoko mbalimbali
Mwana mfalme wa Saudia azungumza na rais wa Urusi - kunani?
Mwanamfalme wa Saudia, Mohammed bin Salman,amefanya mazungumzo na rais wa Urusi, Vladimir Putin, kwa njia ya simu.
Gazeti la Saudia limeripoti kuwa viongozi hao wawili walijadili jinsi ya kurahisisha uhusiano kati ya nchi hizo mbili, na jinsi ya kusaidiana kuboresha maendeleo ya nchi hizo katika maeneo tofauti.
Urusi na Saudi Arabia ni miongoni mwa nchi tajiri zaidi duniani.
Rais wa Urusi Vradimir Putin anajaribu kujenga ushirikiano na nchi za eneo la Asia, baada ya kuvunjika kwa uhusiano mkubwa kati ya nchi yake na nchi za Magharibi kufuatia vita vya Ukraine.
Namibia yakataa kumuongezea muda wa visa mfalme wa Uganda
Serikali ya Namibia imekataa ombi la kuongeza muda wa visa kwa mfalme wa Uganda ambaye amekuwa akipata matibabu nchini humo tangu mwezi Aprili.
Mfalme Mutebi II wa Buganda amekuwa akipokea matibabu kwa hali ya kiafya ambayo haijatajwa. Kituo ambacho amekuwa akiishi kiliomba kuongezewa visa kwa mfalme huyo mapema mwezi huu.
Lakini katika kujibu, wizara ya mahusiano ya kimataifa sheria ya uhamiaji ya Namibia inatoa ukomo wa kukaa nchini humo siku 90 tu kwa mwaka kwa raia wa kigeni.
Haya yanajiri wiki kadhaa baada ya mamlaka kuripotiwa kutofurahishwa na maandamano ya wanaharakati wa Uganda katika ubalozi za Namibia.
"Baada ya kukagua rekodi, ningependa kukujulisha kuwa ombi la kuongezewa muda limekataliwa,'' shirika la utangazaji la serikali NBC lilimnukuu afisa wa wizara akisema.
Balozi wa Uganda nchini Afrika Kusini alisema hivi karibuni kwamba mamlaka ya Namibia haikufurahishwa na unyanyasaji wa maafisa wao wa kidiplomasia kuhusu kuendelea kubaki nchini kwa mfalme.
Mwezi Mei kulikuwa na maandamano katika Ubalozi wa Namibia nchini Uingereza, huku waandamanaji wa Uganda wakidai uwazi kuhusu kuwepo kwa mfalme huyo kwa muda mrefu nchini Namibia.
Walitaka Namibia kufichua habari kuhusu aliko mfalme huyo ili kusitisha shutuma kwamba alikuwa ametekwa nyara.
Serikali ya Namibia iliwasilisha suala hilo kwa mamlaka ya jadi ya Buganda.
Maelfu ya mayai ya ndege adimu yenye thamani ya $500,000 yanaswa Australia
Takriban mayai 3,404 yamenaswa nchini Australia baada ya operesheni dhidi ya biashara haramu ya ndege barani Ulaya.
Wachunguzi waligundua mzigo huo - unaoaminika kuwa wa thamani ya $400,000 hadi $500,000 (£207,000 - £259,000) - katika jumba moja huko Granton, Tasmania mwezi Julai tarehe 9.
Mzee mmoja wa miaka 62 alikuwa anachunguzwa lakini hakuna mtu aliyekamatwa, kulingana na maafisa.
Uhalifu wa kimazingira na wanyamapori umekuwa mojawapo ya sekta kubwa za uhalifu na zenye faida zaidi duniani zinazoendelea kukua huku ukisukuma spishi nyingi kwenye ukingo wa kuangamia Inatarajiwa kwamba mshukiwa huyo kutoka nchini Australia atafikishwa mahakamani baadaye kwa makosa ya kukiuka Sheria ya Ulinzi.
"Mtu huyoanadaiwa kuhusika katika ukusanyaji na uvunaji wa mayai ya ndege wa porini na kuuza mayai hayo ya ndege asili wa Australia wanaotambuliwa na shirika la CITES na watu kutoka ughaibuni," msemaji wa Idara ya Shirika la Mabadiliko ya Tabianchi, Nishati, Mazingira na Maji (DCCEEW) lilisema.
Kutambuliwa na CITES- kunamaanisha kuingia Mkataba wa Biashara ya Kimataifa ya Wanyama na Mimea ilio Hatarini Kutoweka (CITES), makubaliano ya kimataifa kati ya serikali ambayo inalenga kulinda mimea na wanyama walio hatarini kutoweka dhidi ya biashara ya kimataifa.
Kasisi wa Ufaransa ashtakiwa kwa unyanyasaji wa kijinsia miaka 17 baada ya kifo chake
Kasisi wa Kanisa Katoliki la Ufaransa, Abbe Pierre, anayekumbukwa kama mtetezi wa watu wasio na makazi, ameshtakiwa kwa unyanyasaji wa kijinsia miaka 17 baada ya kifo chake.
Akiwa mmoja wa watu wanaoheshimika sana nchini Ufaransa, Abbé Pierre alifariki Januari 2007, akiwa na umri wa miaka 94.Lakini sasa nchi imeshtushwa na madai kwamba aliwanyanyasa kingono wanawake saba kati ya 1970 na 2005.
Habari hiyo ilitolewa kwa mara ya kwanza na vuguvugu la kupambana na umaskini la Emmaus alilolianzisha.
Shirika hilo lilisema limesikia ushuhuda kutoka kwa wanawake hao saba na liliwaamini."Ufichuzi huo umetikisa mashirika yetu, ambapo Abbé Pierre amekuwa na jukumu kubwa," shirika hilo la misaada lilisema katika taarifa yake kwenye tovuti yake."Sote tunajua habari yake na ujumbe wake.
Vitendo hivi vinabadilisha sana jinsi tunavyomchukulia mtu huyu, ambaye alijulikana zaidi kwa mapambano yake dhidi ya ufukara na upweke.Kashfa hiyo inawakilisha anguko la ajabu baada ya kifo cha kasisi huyo, ambaye mara kwa mara aliongoza kura za umaarufu wa kitaifa wakati wa uhai wake.
Harakati zake zilikuwa na athari za kimataifa, na nyumba za kulala za Emmaus katika nchi kadhaa.
Alipofariki mwaka wa 2007, rais wakati huo, Jacques Chirac, alisema kwamba Ufaransa ilikuwa imepoteza "mtu muhimu na mwenye dhamira njema‘’.
JD Vance: Mgombea mwenza wa Trump aapa kuwapigania Wamarekani 'waliosahaulika'
Mgombea mwenza aliyeteuliwa na Donald Trump aliapa katika hotuba yake ya kwanza kuwapigania Wamarekani wa tabaka la wafanyakazi ambao alidai kuwa "wamewekwa pembeni na kusahauliwa" na Wanademocrats.
Akijitambulisha kwa mamilioni ya Wamarekani waliokuwa wakitazama kupitia runinga wakiwa majumbani, seneta huyo wa Ohio kwa unyenyekevu kutoka Midwest alishambulia kwa maneno wale ambao "siasa ndio kazi zao" kama Rais Joe Biden.
Alihoji katika hotuba yake kwenye Kongamano la Kitaifa la Republican huko Milwaukee, Wisconsin, kwamba Trump alikuwa "tumaini bora la mwisho" kwa Wamarekani.
Trump na mgombea mwenza wake wataingia kwenye kinyang’anyiro cha kutafuta tikiti ya kuingia Ikulu, wakishindana na mgombea wa Democratic ambaye kwa sasa ni Bw Biden na makamu wake, Kamala Harris, katika uchaguzi wa Novemba.
Akaunti ya Bw Biden kwenye mtandao wa X, ilimjibu Bw Vance Jumatano usiku, kuhusu misimamo yake katika masuala ya uavyaji mimba na Ukraine.
Bw Vance, 39, anatumai kuwa mmoja wa makamu wa rais wachanga zaidi katika historia ya Marekani.
Soma zaidi:
Ujerumani inapanga kupunguza nusu ya msaada wa kijeshi kwa Ukraine
Ujerumani inapanga kupunguza nusu ya msaada wa kijeshi kwa Ukraine mwaka ujao, kutoka karibu €8bn (£6.7bn; $8.7bn) hadi karibu €4bn, kulingana na rasimu ya bajeti iliyoidhinishwa na serikali.
Waziri wa Fedha Christian Lindner alisema ufadhili wa Ukraine ulikuwa "salama kwa mustakabali wa baadaye" kutokana na mpango wa kundi la G7 la mataifa tajiri wa kupata $50bn kutokana na riba ya mali ya Urusi iliyozuiliwa.
Ujerumani ni mfadhili mkuu wa pili wa kijeshi wa Ukraine baada ya Marekani. Mnamo 2024, bajeti ya Berlin kwa Kyiv imepangiwa kuwa karibu € 7.5bn.
Kupunguzwa kwa misaada iliyopangwa kunawadia huku kukiwa na hofu nchini Ukraine na kwa washirika wake wa Ulaya kwamba ufadhili wa Marekani unaweza kupunguzwa au hata kusimamishwa ikiwa Donald Trump atashinda urais katika uchaguzi wa Novemba.
Rais wa Urusi Vladimir Putin alianzisha uvamizi dhidi ya Ukraine mnamo Februari 2022.
Soma zaidi:
Binti mfalme wa Dubai atangaza kumtaliki mume wake kupitia Instagram
Binti wa mtawala wa Dubai ametangaza kumtalaki mume wake kupitia mtandao ya kijamii.
Ujumbe kutoka kwa akaunti ya Instagram iliyothibitishwa ya Sheikha Mahra bint Mohammed bin Rashid Al Maktoum ulisema anakatisha ndoa yake kwa kuandika: "Mimi natangaza talaka yetu."
BBC imewasiliana na maafisa nchini humo ili kupata ufafanuzi kuhusu suala hilo.
Hadi kufikia sasa, sio mume wake Sheikha Mahra, Sheikh Mana bin Mohammed bin Rashid bin Mana Al Maktoum, wala baba yake, ambaye ametoa maoni kuhusu suala hilo kwa umma.
Ujumbe huo, ambao ulianza kwa kusema "Mume wangu Mpendwa", ulihitimishwa na maneno - "Ninakupa talaka, ninakupa talaka, na ninakupa talaka," ukionekana kutumia desturi ya Kiislamu inayojulikana kama talaka tatu.
Kitendo hicho kimepigwa marufuku katika nchi nyingi, lakini kwa kawaida huwaruhusu waume kuwataliki wake zao haraka kwa kusema “Ninakupa talaka” mara tatu.
"Kila la kheri. Mke wako wa zamani," ujumbe huo wa kwenye Instagram uliandikwa.
Picha zote za mume wa Sheikha Mahra zinaonekana kuwa zimefutwa kwenye akaunti yake.
Vile vile, akaunti ya Sheikh Mana inaonyesha picha za mke wake zimefutwa.
Wenzi hao walioana mnamo Aprili 2023 katika sherehe ya kifahari, na mtoto wao wa kwanza alizaliwa miezi miwili iliyopita.
Baadhi ya maoni kutoka kwa watumiaji wa Instagram wanakisia kuwa akaunti ya Sheikha Mahra inaweza kuwa imedukuliwa lakini hakujakuwa na dalili au usemi rasmi juu ya hilo.
Wakati ujumbe huo wa kumtalaki mume wake unaonekana ulionyesha kuwa umekuwepo kwa siku moja.
Serikali ya Dubai na Ubalozi wa UAE mjini London hawakujibu mara moja maombi ya kupata maoni yao.
Pia unaweza kusoma:
Mshambuliaji wa Trump alionekana kama tishio kabla ya kufyatua risasi lakini alipotea kwenye umati
Mtu ambaye angemwua Donald Trump aliripotiwa kama mwenye "kutiliwa mashaka" na Huduma Maalum ya Usalama hadi saa moja kabla ya kuanza kumfyatulia risasi Trump lakini akapotea kwenye umati wa watu, wabunge wamearifiwa na maafisa wa usalama.
Maafisa wa usalama pamoja na Huduma Maalum ya Usalama walitoa taarifa kidogo kwa Bunge na Seneti ya kile kilichotokea wakati wa shambulizi hilo lililotokea kwenye mkutano wa Trump huko Pennsylvania.
Seneta wa Wyoming John Barrasso alisema Huduma Maalum ya Usalama iliwaambia kwamba walimwona mshambuliaji saa moja kabla ya shambulio hilo, lakini akawapotea machoni.
"Alitambuliwa kama anayetiliwa mashaka kwa sababu [alikuwa na] chombo cha kukadiria umbali wa kitu hasa kwa matumizi na kamera au bunduki na mkoba mgongoni. Na hii ilikuwa zaidi ya saa moja kabla ya ufyatuaji wa risasi kutokea," aliiambia Fox News.
"Kwa hiyo, unaweza kutafakari, kwa muda wa saa nzima, usimpoteze mtu huyo machoni."
Ilifichuliwa wakati wa kikao hicho kwamba mtu huyo alikuwa ametembelea eneo alilotekeleza shambulizi kabla ya mkutano na pia, aliwahi kutafuta kwenye simu yake, dalili za ugonjwa wa mfadhaiko, afisa mwingine aliiambia CBS News, mshirika wa habari wa BBC.
Aidha, mshambuliaji huyo aliwahi kutumia simu yake kutafuta picha za Donald Trump na Joe Biden.
Soma zaidi:
Makubaliano ya kusitisha mapigano yarefushwa DR Congo
Marekani imesema makubaliano ya kusitisha mapigano ili misaada ya kibinadamu iweze kufikishwa mashariki mwa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo yamerefushwa kwa siku kumi na tano zijazo hadi mapema mwezi Agosti.
Marekani imesema inafurahishwa na uamuzi huo wa kusitishwa mapigano.
Mashirika ya kutoa misaada Congo yameitaja hali ya kibinadamu mashariki mwa nchi hiyo kuwa janga na kuonya huenda mzozo wa Congo ukasambaa na kuziathiri pia nchi jirani.
Uasi wa kundi la M23 katika jimbo la Kivu Kaskazini umesababisha zaidi ya watu milioni tatu kuachwa bila ya makazi.
Soma zaidi:
Biden akutwa na virusi vya Covid - Ikulu
Rais Joe Biden wa Marekani ameambukizwa virusi vya Covid-19 na ana dalili ambazo sio kali sana, Ikulu ya Marekani ilisema.
Karine Jean-Pierre, mkuu wake wa vyombo vya habari, alisema rais wa Marekani alipewa chanjo pamoja na ile ya nyongeza.
Biden, alipimwa na kukutwa na Covid mara mbili hapo awali.
Bw Biden, 81, alionekana mapema Jumatano akiwatembelea wafuasi wa chama chake huko Las Vegas na kuzungumza katika hafla iliyokuwa imeandaliwa. Lakini alifuta hotuba ya kampeni baadaye usiku.
Ugonjwa huo unajulikana huku akikabiliwa na shinikizo kubwa la kujiondoa kwenye kinyang’anyiro cha kugombea urais kwa sababu ya umri wake.
Vyombo vya habari vya Marekani vinaripoti kwamba Kiongozi wa walio Wengi katika Seneti Chuck Schumer na Kiongozi wa walio Wengi katika Bunge Hakeem Jefferies - Wanademokrasia wawili wakuu katika Bunge la Marekani - walikutana na Bw Biden kwa faragha na nyakati tofauti na kueleza kwamba kuna wasiwasi mkubwa kuwa mgombea wake anaweza kuathiri vibaya ushindani katika Bunge na Seneti.
Bi Jean-Pierre alisema rais alipanga kujitenga nyumbani kwake huko Delaware huku akitekeleza "majukumu yake yote kikamilifu wakati huo".
Daktari wa rais, Kevin O'Connor, alisema Bw Biden alikuwa na dalili za matatizo ya kupumua, ikiwa ni pamoja na mafua na kikohozi na alipewa dozi yake ya kwanza ya Paxlovid.
Alijisikia vizuri wakati wa hafla yake ya kwanza ya siku hiyo, lakini baadaye akapatikana kuwa na maambukizi, Dk O'Connor alisema.
Bwana Biden baadaye alitumia mtandao wa X ambao zamani ulijulikana kama Twitter kumshukuru kila mtu kwa "kumtakia mema" na akasema "atahakikisha kazi inafanyika kwa watu wa Marekani" wakati anaendelea kupona.
Soma zaidi:
Polisi yapiga marufuku maandamano katikati mwa Nairobi
Idara ya Huduma ya Polisi nchini Kenya imepiga marufuku maandamano katika mwa mji wa Nairobi na viunga vyake na kutoa hakikisho la usalama katika eneo hilo.
Katika taarifa yake iliyotolea Julai, 17, 2024, imekumbusha umma jukumu muhimu la idara hiyo katika usalama wa nchi kulingana na katiba.
Hayo yamejiri huku Kenya ikiendelea kushuhudia maandamano ambayo yalianza tangu mwezi Juni, kupinga Mswada wa Fedha 2024.
‘’Nchi yetu imekuwa ikishuhudia hasara kubwa, watu wamejeruhiwa, kupoteza maisha, mali na biashara zimeharibiwa,’’ taarifa ya Idara ya Huduma ya Polisi ilisema.
Iliendelea kusema kuwa imepokea taarifa kwamba baadhi ya makundi ya kihalifu yanapanga kutumia vibaya maandamano ya siku ya Alhamisi, Julai 18, 2024 kutekeleza mashambulizi na uhalifu.
Idara hiyo ilielezea ukosefu wa uongozi kuwa imefanya kuwa vigumu kufanyika kwa maandamano ya amani katika siku zilizopita.
"Kukosekana kwa uongozi katika maandamano yaliyopita kumefanya kuwa vigumu kuhakikisha itifaki za usalama zinafuatwa. Kwa sababu hiyo, hakuna maandamano yataruhusiwa katika eneo la kibiashara katikati ya mji wa Nairobi na viunga vyake kwenda mbele kuhakikisha usalama wa raia," polisi ilisema.
Raia waliombwa kuwa makini katika maeneo yenye watu wengi, kushirikiana na polisi na kutoa taarifa zozote ambazo zinaweza kusaidia kubaini uhalifu.
Soma zaidi:
Hujambo na karibu katika matangazo yetu mubashara ikiwa ni tarehe 18/7/2024