Mkuu wa shirika la Kimataifa la madaktari
wasio na mipaka MSF amesema mashirika ya Umoja wa Mataifa na mashirika mengine
ya kimataifa ya kutoa misaada ya kibinadamu yanapaswa kurudi na kuwasaidia watu
wa Sudan.
Vita vililivyozuka mwezi Aprili mwaka jana nchini Sudan vimsababisha
mzozo unaotajwa na Umoja wa Mataifa kuwa mbaya zaidi duniani na taifa hilo
limetumbukia katika msukosuko mkubwa.
Mkuu wa MSF Christos Christou amesema
baada ya miezi kumi na tano ya vita vikali Sudan,takriban mtu mmoja kati ya
watatu waliojeruhiwa nchini humo ni mwanamke au mtoto wa chini ya umri wa miaka
kumi na kuongeza kuwa mashirika mengi yameuamua kuchukua msimamo wa kusubiri na
kuona jinsi mzozo huo utakavyokwenda.
Bwana Christou amesema MSF inazungumza na
pande zote mbili zinazozona kujaribu kupata ridhaa ya kupitishwa kwa misaada ya
kiutu kwa mamilioni ya wasudan wanaohitaji kwa dharura chakula,maji na makazi.
MSF inasisitiza mzozo wa kibinadamu
unaoikumba Sudan kuwa mkubwa zaidi duniani na kusema kuwa licha ya hali kuwa
ngumu na inayohusisha changamoto lukuki,hatua zaidi zinahitaji kuchukuliwa
kulisaidia taifa hilo na watu wake.
Wito huo unakuja huku wajumbe wa
pande zinazozozana Sudan wakifanya mazungumzo na mjumbe wa Umoja wa Mataifa
mjini Geneva tangu wiki iliyopita.
Sudan kwa sasa inakabiliwa na ukame
mkali,wengi nchini humo ambao wameachwa bila ya makazi wakiripoti kuwa hawana
uwezo wa kujikimu kimaisha kwani wameishiwa fedha,chakula na njia karibu zote
za kujipatia riziki.
Mashirika mengi ya kutoa misaada yamesitisha
shughuli zao kwa kuhofia usalama wa wafanyakazi wake,kushambuliwa kwa vituo
vyao,kuporwa kwa misaada,kunyimwa ruhusa ya kufikia maeneo yanayohitaji misaada
na kutopata ufadhili wa kutosha kutoka kwa jumuiya ya kimataifa.
Umoja wa Mataifa umezishutumu pande zote
mbili zinazopigana,jeshi la Sudan na kikosi maalumu cha wanamgambo RSF kwa
kuzuia kimakusudi misaada kufikishwa kwa waathiriwa,miongoni mwa visa vingine
chungunzima vya ukiukaji wa haki za binadamu.
Kwa mfano katika mji wa El Fasher,vituo vya
MSF vimeshambuliwa mara tisa tangu tarehe kumi mwezi Mei na karibu kila kona ya
Sudan,wahudumu wa afya wanatishwa,wagonjwa wanauawa na vituo vya afya
vinalipuliwa kwa mabomu. Inaripotiwa zaidi ya asilimia sabini ya vituo vya afya
nchini humo havifanyi kazi.
Mzozo
wa Sudan umesababisha mauaji ya maelfu ya watu na kuwaacha takribani watu
milioni kumi na moja bila ya makazi.
Zaidi ya nusu ya idadi, jumla ya wasudani milioni 48 hawana chakula cha kutosha na hali inabashiriwa kuwa itazidi
kuzorota.